Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Daudi na Goliathi
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
    • Daudi akimrushia Goliathi jiwe kwa kombeo

      SOMO LA 40

      Daudi na Goliathi

      Yehova alimwambia Samweli hivi: ‘Nenda kwenye nyumba ya Yese. Mmoja kati ya wanawe atakuwa mfalme wa Israeli anayefuata.’ Kwa hiyo, Samweli akaenda kwenye nyumba ya Yese. Alipomwona mwana mkubwa wa Yese, akawaza hivi: ‘Kijana huyu ndiye anayepaswa kuwa mfalme.’ Lakini Yehova akamwambia Samweli hakuwa amemchagua kijana huyo. Yehova akasema: ‘Mimi ninaona kilicho moyoni mwa mtu, si jinsi alivyo kwa nje tu.’

      Samweli akimtia Daudi mafuta

      Yese akawaleta watoto wake wengine sita mbele ya Samweli. Lakini Samweli akasema: ‘Yehova hajamchagua yeyote kati yao. Je, una wana wengine?’ Yese akasema: ‘Nina mwana mwingine mmoja, yule wa mwisho, Daudi. Yuko nje anachunga kondoo zangu.’ Daudi alipoingia, Yehova akamwambia Samweli: ‘Huyu ndiye!’ Samweli akamimina mafuta juu ya kichwa cha Daudi na kumtia mafuta kuonyesha kwamba atakuwa mfalme wa Israeli wakati ujao.

      Goliathi

      Muda fulani baada ya hapo, Waisraeli wakaenda kupigana na Wafilisti. Walikuwa na jitu shujaa lililowapigania lililoitwa Goliathi. Siku baada ya siku, Goliathi aliwadhihaki Waisraeli. Alisema hivi kwa sauti kubwa: ‘Leteni mwanamume apigane nami. Akishinda, sisi tutakuwa watumwa wenu. Lakini mimi nikishinda, ninyi mtakuwa watumwa wetu.’

      Daudi akaja kwenye kambi ya jeshi la Waisraeli kuwaletea ndugu zake chakula. Ndugu zake walikuwa askari-jeshi. Aliposikia maneno ya Goliathi, Daudi akasema: ‘Mimi nitapigana naye!’ Mfalme Sauli akamwambia hivi: ‘Wewe ni mvulana tu.’ Daudi akamjibu: ‘Yehova atanisaidia.’

      Sauli akajaribu kumvisha mavazi yake ya vita, lakini Daudi akasema: ‘Siwezi kupigana nikiwa nimevaa mavazi haya ya vita.’ Daudi akachukua kombeo lake na kwenda mtoni. Akachagua mawe matano laini na kuyatia ndani ya mfuko. Kisha Daudi akakimbia kumwelekea Goliathi. Jitu hilo likasema hivi kwa sauti: ‘Njoo hapa wewe mvulana. Nitawapa nyama yako ndege wa mbinguni na wanyama wa mwituni.’ Daudi hakuogopa. Akajibu kwa sauti: ‘Unakuja ukiwa na upanga na mkuki, lakini mimi ninakuja kwa jina la Yehova. Wewe hupigani nasi; unapigana na Mungu. Kila mtu hapa ataona kwamba Yehova ni mwenye nguvu kuliko upanga au mkuki. Yeye atawatia ninyi nyote mkononi mwetu.’

      Daudi akatia jiwe katika kombeo lake na kulitupa kwa nguvu zake zote. Kwa msaada wa Yehova, jiwe likampiga Goliathi kwenye paji la uso wake na kupenya ndani. Jitu hilo likaanguka chini kwa kishindo likiwa limekufa. Kisha Wafilisti wakakimbia ili wasiuawe. Je, wewe unamtegemea Yehova, kama Daudi alivyofanya?

      “Kwa wanadamu haiwezekani, lakini sivyo ilivyo kwa Mungu, kwa maana mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”—Marko 10:27

      Maswali: Yehova alimchagua nani awe mfalme wa Israeli aliyefuata? Daudi alimshindaje Goliathi?

      1 Samweli 16:1-13; 17:1-54

  • Daudi na Sauli
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
    • Daudi akizungumza kwa sauti akiwa juu ya mlima umbali fulani kutoka kwenye kambi ya Sauli

      SOMO LA 41

      Daudi na Sauli

      Baada ya Daudi kumuua Goliathi, Mfalme Sauli alimweka Daudi asimamie jeshi lake. Daudi alishinda vita vingi, naye alijulikana na kusifiwa na watu wengi. Wakati wowote ambapo Daudi alirudi nyumbani, wanawake wangetoka nje wakicheza dansi na kuimba: ‘Sauli amepiga maelfu yake, na Daudi amepiga makumi ya maelfu yake!’ Sauli alianza kumwonea Daudi wivu na akataka kumuua.

      Daudi alijua kupiga kinubi vizuri sana. Siku moja Daudi alipokuwa akipiga kinubi, Sauli alimrushia mkuki. Daudi akakwepa kabla tu ya mkuki kumpata nao ukapiga ukuta. Baada ya hapo, Sauli akajaribu mara nyingi zaidi kumuua Daudi. Mwishowe, Daudi akakimbia na kujificha nyikani.

      Daudi akichukua mkuki wa Sauli huku Sauli akiwa amelala

      Sauli akachukua jeshi la watu 3,000 na kwenda kumwinda Daudi. Sauli akaingia ndani ya pango ambamo Daudi na wanaume wake walikuwa wakijificha. Wanaume hao wakamwambia Daudi kwa sauti ya chini: ‘Hii ndiyo nafasi yako ya kumuua Sauli.’ Daudi akamnyemelea Sauli na kukata koti lake. Sauli hakutambua. Baadaye, Daudi akahisi vibaya kwa sababu alikuwa amemvunjia heshima mfalme mtiwa-mafuta wa Yehova. Hakuwaruhusu wanaume wake wamshambulie Sauli. Hata alimwambia Sauli kwamba alikuwa amepata nafasi ya kumuua lakini hakufanya hivyo. Je, Sauli angebadili nia yake kumwelekea Daudi?

      Hapana. Sauli aliendelea kumwinda Daudi. Usiku mmoja Daudi na mpwa wake Abishai waliingia kimyakimya kwenye kambi ya Sauli. Hata Abneri, mlinzi wa Sauli, alikuwa amelala. Abishai akasema: ‘Hii ndiyo nafasi yetu! Niruhusu nimuue.’ Daudi akajibu: ‘Yehova atamwadhibu Sauli. Acha tuchukue mkuki wake na gudulia lake la maji tuondoke.’

      Daudi akapanda juu ya mlima uliokuwa karibu na kambi ya Sauli. Akasema kwa sauti kubwa: ‘Abneri, kwa nini hukumlinda mfalme? Uko wapi mkuki wa Sauli na gudulia lake la maji?’ Sauli akatambua sauti ya Daudi na kusema: ‘Ungeweza kuniua, lakini hukufanya hivyo. Ninajua kwamba utakuwa mfalme anayefuata wa Israeli.’ Sauli akarudi kwenye jumba lake la kifalme. Lakini si wote katika familia ya Sauli waliomchukia Daudi.

      “Ikiwezekana, kwa kadiri inavyowategemea ninyi, fanyeni amani na watu wote. Wapendwa, msijilipizie kisasi bali iachieni nafasi ghadhabu.”​—Waroma 12:18, 19

      Maswali: Kwa nini Sauli alitaka kumuua Daudi? Kwa nini Daudi alikataa kumuua Sauli?

      1 Samweli 16:14-23; 18:5-16; 19:9-12; 23:19-29; 24:1-15; 26:1-25

  • Yonathani Alikuwa jasiri na Mshikamanifu
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
    • Yonathani na mtumishi wake aliyembebea silaha

      SOMO LA 42

      Yonathani Alikuwa Hodari na Mshikamanifu

      Yonathani, mwana wa kwanza wa mfalme Sauli, alikuwa shujaa hodari wa vita. Daudi alisema kwamba Yonathani alikuwa na mbio kuliko tai na alikuwa na nguvu kuliko simba. Siku moja, Yonathani aliona wanajeshi Wafilisti 20 wakiwa juu ya mlima. Alimwambia hivi mtumishi aliyembebea silaha: ‘Tutawashambulia ikiwa tu Yehova atatupa ishara. Wafilisti wakituambia twende mahali walipo, hiyo itakuwa ishara kwamba tunapaswa kuwashambulia.’ Wafilisti wakapaaza sauti: ‘Njooni tupigane!’ Kwa hiyo, wanaume hao wawili wakapanda mlima huo na kuwashinda askari-jeshi hao.

      Yonathani akimpa Daudi baadhi vitu vyake

      Kwa kuwa Yonathani alikuwa mtoto wa kwanza wa Sauli, yeye ndiye aliyepaswa kuwa mfalme baada ya baba yake. Lakini Yonathani alijua kwamba Yehova alikuwa amemchagua Daudi kuwa mfalme wa Israeli anayefuata. Yonathani hakumwonea Daudi wivu. Yonathani na Daudi wakawa marafiki wa karibu. Waliahidi kulindana na kuteteana. Yonathani akampa Daudi koti, upanga, upinde, na mshipi wake kama ishara ya urafiki wao.

      Daudi alipokuwa akimkimbia Sauli, Yonathani alimwendea na kumwambia hivi: ‘Usiogope, uwe jasiri. Yehova amekuchagua kuwa mfalme. Hata baba yangu anajua jambo hilo.’ Je, ungependa kuwa na rafiki mzuri kama Yonathani?

      Zaidi ya mara moja, Yonathani alihatarisha maisha yake ili kumsaidia rafiki yake. Alijua kwamba Mfalme Sauli alitaka kumuua Daudi, kwa hiyo akamwambia baba yake hivi: ‘Ukimuua Daudi utakuwa ukifanya dhambi; hajafanya kosa lolote.’ Sauli alimkasirikia Yonathani. Miaka michache baadaye, Sauli na Yonathani wakafa vitani.

      Baada ya Yonathani kufa, Daudi alimtafuta Mefiboshethi, mwana wa Yonathani. Daudi alipompata Mefiboshethi, alimwambia hivi: ‘Kwa sababu baba yako alikuwa rafiki yangu wa karibu, nitakutunza maisha yako yote. Utaishi katika nyumba yangu ya kifalme na utakula mezani pangu.’ Daudi hakumsahau kamwe rafiki yake Yonathani.

      “Mpendane kama vile nilivyowapenda. Hakuna mtu aliye na upendo mkuu kuliko huu, kwamba mtu atoe uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.”​—Yohana 15:12, 13

      Maswali: Yonathani alionyeshaje kwamba alikuwa jasiri? Yonathani alionyeshaje kwamba alikuwa mshikamanifu?

      1 Samweli 14:1-23; 18:1-4; 19:1-6; 20:32-42; 23:16-18; 31:1-7; 2 Samweli 1:23; 9:1-13

  • Dhambi ya Mfalme Daudi
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
    • Nabii Nathani akimshauri Mfalme Daudi

      SOMO LA 43

      Dhambi ya Mfalme Daudi

      Sauli alipokufa, Daudi akawa mfalme. Alikuwa na umri wa miaka 30. Baada ya kuwa mfalme kwa miaka kadhaa, usiku mmoja akiwa juu ya paa la nyumba ya mfalme alimwona mwanamke mrembo. Daudi akaambiwa kwamba mwanamke huyo anaitwa Bath-sheba na kwamba alikuwa mke wa mwanajeshi aliyeitwa Uria. Daudi akaagiza Bath-sheba aletwe kwenye nyumba yake ya kifalme. Akalala naye, na Bath-sheba akawa mja-mzito. Daudi alijaribu kuficha kile alichokuwa amefanya. Alimwambia mkuu wa jeshi lake amweke Uria kwenye mstari wa mbele wa vita kisha waondoke na kumwacha peke yake. Uria alipouawa vitani, Daudi akamwoa Bath-sheba.

      Mfalme Daudi akitoa sala ya kuomba msamaha

      Lakini Yehova aliona mambo yote mabaya yaliyotukia. Angefanya nini? Yehova alimtuma nabii Nathani aende kwa Daudi. Nathani akamwambia hivi: ‘Mwanamume fulani tajiri alikuwa na kondoo wengi, na mwanamume maskini alikuwa na mwana-kondoo mmoja mdogo ambaye alimpenda sana. Yule tajiri akamchukua mwana-kondoo wa yule mwanamume maskini.’ Daudi akakasirika na kusema: ‘Huyo mwanamume tajiri anastahili kufa!’ Ndipo Nathani akamwambia Daudi: ‘Wewe mwenyewe ndiye yule tajiri!’ Daudi akahuzunika sana, akamwambia Nathani waziwazi hivi: ‘Nimemtendea Yehova dhambi.’ Dhambi hiyo ilimletea Daudi na familia yake matatizo mengi sana. Yehova alimwadhibu Daudi, lakini akamwacha aendelee kuwa hai kwa sababu alikuwa mnyoofu na mnyenyekevu.

      Daudi alitaka kumjengea Yehova hekalu, lakini Yehova akamchagua Sulemani mwana wa Daudi alijenge. Daudi alianza kukusanya vitu kwa ajili ya Sulemani na kusema: ‘Hekalu la Yehova linapaswa kuwa lenye utukufu. Sulemani ni mchanga, lakini nitamfanyia matayarisho.’ Daudi alichangia pesa nyingi kwa ajili ya kazi hiyo ya ujenzi. Akatafuta wafanyakazi wenye ustadi. Akakusanya dhahabu na fedha, na akaleta mierezi kutoka Tiro na Sidoni. Alipokaribia kufa, Daudi akampa Sulemani ramani ya ujenzi wa hekalu. Akamwambia hivi: ‘Yehova aliniagiza niandike mambo haya yote kwa ajili yako. Yehova atakusaidia. Usiogope. Uwe mwenye nguvu na uanze kazi.’

      Daudi akizungumzia ramani ya ujenzi na kijana Sulemani

      “Anayefunika makosa yake hatafanikiwa, lakini yeyote anayeyaungama na kuyaacha ataonyeshwa rehema.”—Methali 28:13

      Maswali: Daudi alifanya dhambi gani? Daudi alifanya nini ili kumsaidia mwana wake Sulemani?

      2 Samweli 5:3, 4, 10; 7:1-16; 8:1-14; 11:1–12:14; 1 Mambo ya Nyakati 22:1-19; 28:11-21; Zaburi 51:1-19

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki