Imani ya Joshua—Ushindi kwa Haki za Watoto
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KANADA
“ULIKUWA wakati wa kwanza ile kanuni ya kutumiwa kwa mtoto mkomavu kufikiriwa kwenye kiwango cha mahakama ya rufani. Na watu fulani walisema hukumu huweka miongozo iliyo wazi si tu kwa madaktari na mahospitali katika New Brunswick lakini pia, labda, kwingineko katika Kanada.”—Canadian Medical Association Journal.
Jarida hilo lililo juu larejezea kisa kilichohusisha New Brunswick’s Consent of Minors Act (Idhini ya Kitiba ya New Brunswick Kuhusu Fungu la Watoto), isemayo kwamba ikiwa madaktari wawili watangaza mtoto aliye chini ya miaka 16 kuwa mkomavu na kwamba anafahamu maradhi yake na matibabu yanayokusudiwa, ana haki ya kisheria kukubali au kukataa matibabu ya kitiba, kama mtu mzima yeyote. Kuhusu Joshua Walker mwenye umri wa miaka 15, aliyekuwa na leukemia mbaya ya uboho, kwamba Hakimu Mkuu W. L. Hoyt wa Mahakama ya Rufani ya New Brunswick aliandika yafuatayo: “Hapa uthibitisho ni mwingi mno kwamba Joshua amekomaa vya kutosha na kwamba, katika hali hiyo, matibabu yaliyokusudiwa ni kwa faida yake na afya yake yenye kuendelea na hali njema. . . . Ni maoni yangu kwamba lile ombi [la kutangazwa kuwa mtoto mkomavu] halikuhitajika.” Hakimu Mkuu Hoyt katika uamuzi wake aliandika pia kwamba sheria ya umma ya Kanada “hutambua ile kanuni ya kutumiwa kwa mtoto mkomavu.”
Mmoja wa wanasheria wa Joshua, Daniel Pole, alisema kwamba uamuzi ulioandikwa wa Mahakama ya Rufani ‘utakuwa kesi iliyo kuu kotekote Kanada.’ Kwa sababu ilikuwa kesi isiyo ya kawaida, kikao cha mahakama kilikuwa na mahakimu watano badala ya wale watatu wa kawaida. “Katika hali za upeo,” Pole alisema, “mahakama itaketi kukiwa na benchi iliyojaa. Huenda ikawa kwamba walifikiria uamuzi huo kuwa wa maana kwa Kanada.” Alidokeza kwamba ule uamuzi wenye kuweka kanuni ufungue njia ili watoto wakomavu wawe wakijiamulia zaidi thamani iliyopanuka ya ushindi huu wa mahakama, Pole alitangaza hivi: “Ni uteteo mkubwa wa haki za watoto, wa wanaume vijana na wanawake vijana walio na uwezo wa kuamua wayatakayo kufanyiwa miilini mwao.”
Chini ya kichwa “Ushindi wa ‘Mdogo,’” tahariri fulani kwenye Telegraph Journal ilisema hivi: “Ule uamuzi wa Mahakama ya Rufani ya New Brunswick kwamba Joshua Walker aliye na umri wa miaka 15 ana haki ya kukubali au kukataa matibabu ya kitiba ni ushindi si kwa Mashahidi wa Yehova tu, bali kwa sisi sote. . . . Wakati fulani maamuzi yafanywayo na kila mmoja huenda yakaonekana magumu zaidi kwa jamii kumudu, magumu hasa ikiwa kinachohusika kwa kijana ni kufa na kupona. Lakini ile ambayo ingekuwa ngumu hata zaidi kuvumilia ni jamii ambayo kidesturi huingilia miili na nafsi za raia wake. Joshua Walker amefanya sehemu yake ili kutusalamisha na hayo.” wenyewe na kwamba “hakuna sababu yayo kurudi tena mahakamani. Imetimiza sehemu kubwa kwa ajili ya wachanga wengine.” Akikazia
Daktari Mjasiri
Tangu mwanzo wa ugonjwa wake, Joshua alichunguzwa na kutibiwa na Dakt. Mary Frances Scully, mtaalamu wa kufanyizwa kwa damu na vimbe za watoto. Kazi yake hutia ndani uchunguzi na utibabu wa kansa katika watoto.
Njia ya kawaida ya kutibu aina ya leukemia ya Joshua ni tibakemili na mitio ya damu mishipani. Familia ya Joshua ni Mashahidi wa Yehova na, kwa sababu za Kimaandiko, wao hukataa kutiwa damu mishipani. Kanuni ya kimungu kwa Wakristo ni: “Wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu.” (Matendo 15:20, 29) Joshua, tangu mwanzo, alichukua msimamo wenye azima ili kushikamana na sheria ya Yehova ya ‘kujiepusha na damu.’
Dakt. Scully aliandika kwenye chati ya hospitali kwamba Joshua alikuwa “asiyenyumbuka kabisa” kuhusu hili. Dakt. Dolan, mkuu wa idara ya hospitali ya uchunguzi wa vimbe za watu wazima, aliongea kibinafsi na Joshua. Wote wawili yeye na Dakt. Scully walikata shauri kwamba Joshua alikuwa mtoto mkomavu. Daktari wa familia ya Walker, Dakt. Lordon, pia alimwona Joshua kuwa mtoto mkomavu. Kukiwa na madaktari, si wale wawili tu watakwao, bali watatu walimtangaza Joshua kuwa mtoto mkomavu, alifuzu kabisa chini ya Idhini ya Kitiba Kuhusu Fungu la Watoto kujichagulia matibabu. Hakuna kesi ambayo ingalihitajiwa.
Kwa kusikitisha, hali haikubaki hivyo. Hospitali, tayari ikimwona Joshua kuwa mtoto mkomavu, ilitaka hili lithibitishwe na uamuzi wa kisheria ili kujilinda na lawama yoyote. Matokeo ya uchunguzi mrefu wa mahakama na wenye kujaribu yalikuwa kwamba hakimu aliamua kwamba Joshua hakuwa na haki ya kukataa matibabu. Uamuzi huu mara moja ulikatwa rufani kwenye mahakama kuu kukiwa na matokeo yaliyotajwa katika fungu letu la kwanza.
Wakati wote wa uguo la Joshua Dakt. Scully alishikamana na katao lake la kutotumia damu kwa Joshua chini ya hali zozote zile isipokuwa akibadili maoni yake kwa kukubali. Likiripoti msimamo wa mwanamke huyo, Canadian Medical Association Journal lilimnukuu kuwa akisema: “Hangaiko langu kubwa lilikuwa kwamba Joshua au familia yake wangekasirika kwamba wangerudi tu bila ya machaguo yoyote ya badala.” Makala hiyo yaendelea: “Wanatiba wengine baadaye walimwambia kwamba wao wangalikataa kabisa kumtibu [Joshua]. Hata hivyo, wazo hilo halikumjia akilini.” Msimamo wake wenye usababu na ulio bora ulikuwa wenye kutia moyo sana kwa Joshua na familia yake.
Joshua Alipenda Uhai na Aligusa Mioyo
Joshua Walker alipenda uhai; hakutaka kufa. Familia yake haikutaka afe. Katika mabara mengi, Mashahidi wa Yehova, ndugu zake wa kiroho, walitumaini kwamba angeweza kupata nafuu aishi. Joshua alikuwa na nia ya kukubali hali yake; imani yake katika Mungu ilimsadikisha angerudi kwenye ufufuo. Alipata utegemezo katika maneno ya Yesu: “Saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake [Mwana wa Mungu]. Nao watatoka.”—Yohana 5:25, 28, 29.
Utegemezo ulimjia kutoka mahali kwingi. Evening Times Globe ilisema hivi: “Wazazi wote wawili walikazia jana kwamba hawamwachi Joshua. Walimleta kwenye Hospitali ya Kimkoa ili apate matibabu yaliyo bora yawezekanayo, bila damu. ‘Tungalimwacha nyumbani ikiwa tulitaka afe,’ baba akatoa hoja. ‘Hatutaki Joshua afe. Twafanya lolote kitiba ili kumweka hai. Na hilo ndilo yeyote angefanya kwa ajili ya yeyote wa wapendwa wao. Hatupo hapa ili kumtazama afe. Tupo hapa kumsaidia mvulana huyo apate nafuu, ili aweze kutoka na kurudia vigari-moshi vyake, arudi kwenye Jumba la Ufalme, kwenye mikutano yake na utumishi wake, na labda arudie kidogo mpira wa vikapu.’”
Hakika, familia yake kwa kweli walitaka kumsaidia na kumtegemeza. Gazeti moja liliandika hivi: “Huku mmoja wao akichukua zamu ya kuongea na Joshua, washiriki wengine wa familia walikusanyika karibu-karibu katika chumba kitulivu kidogo, wengine wao bado wakiwa wamevaa majoho pamoja na visetiri vya uso vilivyolegezwa vikiwa vinaning’inia shingoni mwao. Ni mandhari hiyohiyo ambayo imekuwa ikiendelea hapo tangu Machi 31, Joshua alipokuja kwanza [kwenye] hospitali. Kwa majuma matatu, Joshua hajatumia kipindi fulani bila mshiriki wa familia mwenye joho na kisetiri cha uso katika chumba chake cha hospitali. . . . Mara nyingi, wazazi wote wawili hukaa usiku kucha pamoja na Joshua, wakiwa wamelala katika kitanda kilicho kando ya mwana wao aliye mchanga zaidi. [Mama alisema,] ‘Twahitajiwa hapa, na ningefanya lolote kwa ajili ya Josh, kwa mtoto yeyote wangu.’ ‘Ningekaa nje kwenye mahali pa kuegesha magari ikiwa ingekuwa lazima,’ akasema baba.”
Usiri na Maongeo
Katika jioni ambazo mama au baba yake wamekuwa naye, kulikuwa na mazungumzo ya undani zaidi. Usiku mmoja alisema hivi: “Mama, tafadhali andika hili. Enyi nyote mlio vijana, tafadhali mkaribieni Yehova ili kwamba ikiwa jambo lolote litawapata, mdumishe uaminifu wenu wa maadili kwake. Nipatapo nafuu naahidi kufanya zaidi katika kutangaza jina la Yehova. Enyi vijana mlio na afya njema, fanyeni zaidi mkiweza.”
Usiku mmoja Josh alipokuwa hospitalini, alisema hivi: “Mama, mara nyingi uendapo kwenye bafu au kumchukua baba, madaktari huja na kusema: ‘Josh, wahitaji kutiwa damu mishipani. Bila ya hiyo utakufa. Twataka kukusaidia.’ Ndipo ningewajibu, ‘Basi tafadhali heshimuni mapendezi yangu kuhusu damu.’ Nilimwambia daktari mmoja aliyenijaribu ili nikubali kutiwa damu: ‘Huenda ukafikiri mimi nina kichaa, lakini nina nyezo zangu zote za kufikiri. Nataka tu kuishi kwa sheria ya Yehova juu ya damu. Yeye ajua kilicho bora kwa ajili yetu. Jambo lililo bora zaidi kwangu ni kuheshimu utakato wa uhai, na nikifa nitaishi tena.’”
Daktari mmoja, mkuu wa wanatiba wa watoto, Dakt. Garry, alisema kwa wazazi wa Josh hivi: “Mwoneeni fahari Josh. Ana imani ambayo maishani mwangu sijapata kamwe kuiona ikidhihirishwa.” Aliwakumbatia wote wawili na akasema hivi: “Nyinyi ni familia yenye moyo mkuu.”
Jioni moja katika hospitali, baada ya habari fulani mbaya kupewa familia kuhusu hali ya Josh, ndugu yake Jeff na dada yake, Janice, walikuwa naye. Jeff alilia, na Josh akasema hivi: “Jeffrey, acha kulia. Mimi ni mshindi vyovyote vile. Usifadhaike kunihusu.” Jambo lake kuu lilikuwa kwamba ikiwa alipata nafuu kutokana na uguo lake, yeye alikuwa mshindi; ikiwa hakuweza na akafa na afufuliwe katika dunia iliyo Paradiso, basi bila shaka yeye alikuwa mshindi!
Kulipokuwa na mazungumzo ya kubadilisha uboho wa mfupa, ndugu yake Jerry alikuwa wa kwanza kutoa uboho wake wa mfupa. Wakati mmoja, ndugu zake John na Joe walikuwa wakimbusu Josh kwa heri ya kulala. Alipofika umri wa miaka 13, alieleza mama yake awaeleze wao alikuwa mkubwa mno kutendewa hivyo. Lakini wakati wa ugonjwa wake, ingawaje alikuwa na miaka 15, walipoianzisha tena na wakimkumbatia na kusali pamoja naye, Josh alimwambia mama yake wakati huo ilikuwa sawa—ilionyesha bado walimpenda.
Utegemezo wa Jumuiya
Jerry na Sandra, wazazi wa Joshua, wasema ule utegemezo kutoka kwa jumuiya umekuwa mwingi mno na uliosambaa. Mei 1994, gazeti moja lilisema hivi: “Kwa wastani, Joshua hupokea kadi 20 kwa siku. Hata zimetoka mbali kabisa kama Rumania na Mexico. Pia amepokea simu na faksi hospitalini kutoka mbali kama vile Alberta na Washington. Zaidi ya yote hayo, alitumiwa karibu nusu dazani ya vikapu vyenye matunda [na] madazani ya maua. . . . Takwimu zake za dalili . . . zilipoboreka, wauguzi walipanga msherehekeo wa luau ya Kihawaii kwa heshima yake. Walitengeneza skati za nyasi kutoka kwa masazo ya mifuko ya plastiki na kucheza hula wakizunguka chumbani mwake. ‘Alicheka sana, nilifikiri atalia,’ alisema Sandra.”
Jerry, baba yake Josh, aliongezea habari fulani zenye kupendeza: “Hatungeweza kuwaruhusu watoto wote waliomtembelea kutoka shuleni kuingia katika chumba cha hospitali. Kwa hiyo mkuu wa shule alikuwa akija kupata ripoti juu ya Josh. Wanafunzi walimpelekea Josh fumbo lenye sehemu 1,000 la picha za reli—Josh anapenda sana magari-moshi. Polisi walitaka kumpangia dansi ya kukusanya fedha ili kulipia gharama fulani, lakini hatukuwapa ruhusa yetu ili kuiendeleza. Darasa la masomo ya kijamii shuleni lilizungumza kuhusu haki za watu, na kila mmoja katika darasa hilo akimwandikia Josh kuhusu kuwatolea hotuba juu ya hilo, akiwapa maoni yake.”
Kwa wakati huu wote, ushughulikaji wa magazeti ulikuwa mkubwa sana—ripoti zikiwa na picha katika kurasa za kwanza katika magazeti kadhaa ya kila siku. Wakuu wa shule walipasha taarifa za habari juu ya afya ya Joshua. Alipata mialiko ya kuzungumza apatapo nafuu, na shule zilikuwa na vipindi kuhusu mambo ya kindani ya kisa hicho.
“Je, mliona mabadiliko makubwa kwa Joshua maradhi haya yalipomkumba na kuhatarisha uhai wake?” likauliza Amkeni! Jerry, baba yake Josh, alieleza: “Kulikuwa na badiliko kubwa kwake, tena la ghafula. Mbeleni Josh alikuwa mtani, kivulana kisichojali mno, wakati mwingine akihitaji ushauri ambao wenye umri wa miaka 15 huhitaji. Nimekaa na kumtazama kwa mshangao. Ni kana kwamba alikua usiku kucha. Jioni moja mwanasheria wake alitaka kuongea naye, na Joshua akaniomba niondoke. Kabla ya kuwa mgonjwa alitenda kwa ucheshi; ghafula akawa mkomavu, akiongea na wanasheria na mahakimu. Dharura yaweza kuleta kutoka vilindi vya moyo mambo yasiyoshukiwa kamwe kuwako.”
Dakt. Scully alimshehenezea Joshua heshima ya kuvutia. Alisema kwa mama yake hivi: “Yeye kati ya wagonjwa wote ambao nimepata kutibu ndiye mwenye urafiki, mwenye kufikiria wengine sana, mwenye uungwana na mwenye huruma zaidi ambaye nimepata kukutana naye. Yeye ni mwenye moyo mkuu na mwanamume kijana ambaye hatutamsahau kamwe. Yeye ni mtu mwenye kupendeka sana. Waweza kumwonea fahari, Bi. Walker.”
Katika muda wa majuma machache, hiyo leukemia ilibadilika. Vile vipindi vifupi vya kuwa na nafuu vilikuwa vimepita; kansa ilirudi. Dakt. Scully aliiambia familia hiyo kwamba Josh huenda asiishi kwa muda mrefu zaidi—labda majuma kadhaa, yawezekana miezi kadhaa. Jioni iliyofuata, wazazi wa Joshua wakiwako, Dakt. Scully alimwambia Joshua kwamba kansa imerudi na huenda pia kufikia hapo ikawa tumboni. “La! haijarudi—una uhakika imerudi?” akasema Joshua. Dakt. Scully akasema hivi: “Josh, matokeo ya uchunguzi wa damu yako si mazuri sana.” Muda mfupi baadaye Jerry aliondoka chumbani, kisha Dakt. Scully.
Mioyo Miwili Yenye Kuuma Ikitafuta Amani
Mama ya Josh aeleza mandhari hiyo hivi: “Kulikuwa na kimya. Nilivuta kiti mpaka kando ya kitanda chake nikaushika mkono wake. Nilimuuliza kama alifadhaika au alishuka moyo kwa aliyoyasema daktari. Alijibu hivi: ‘Sikuwa nimefikiri kuhusu kufa na kuondoka karibuni hivyo. Lakini, mama usifadhaike. Siogopi kufa, wala siogopi kifo. Je, utakuwa nami nifapo? Sitaki kufa nikiwa peke yangu.’ Nilianza kulia na nikamkumbatia. Alilia pia, akasema hivi: ‘Mama, mimi nimo mikononi mwa Yehova.’ Kisha, ‘Nataka nyinyi nyote mbaki katika kweli ili mweze kunikaribisha kwenye ufufuo. Mama, naweza kukuambia nikiwa na uhakika wote hivi: Ninajua hakika Yehova atakuja kunirudisha kwenye ufufuo. Ameusoma moyo wangu, nami nampenda kwelikweli.’
“Nilianza kulia tena. Nilimwambia jinsi tulivyompenda sana na, kwa miaka hiyo 16 ambayo tumekuwa naye hapa, jinsi tumemwonea fahari—na zaidi ya yote, jinsi Yehova alivyomtazama kwa ukubali wenye furaha. Alisema, ‘Mama, ninajua.’ Nami nikamwambia hivi: ‘Josh, japo nachukia sana kukata tamaa, ungekuwa ubinafsi tu kwa upande wetu kukutaka uendelee kuishi.’ Alisema hivi: ‘Mama, najua, na kwa hakika ni kama hivi nimechoka kupigana.’”
Mipaka ya Kisheria
Daniel Pole, mmoja wa wanasheria wa Joshua, pamoja na mawakili wengine, walishughulikia masuala yaliyotokezwa na kisa cha Joshua Walker. Mtoto mkomavu ni nini chini ya Idhini ya Kitiba Kuhusu Fungu la Watoto? Je, idhini ya matibabu yatia ndani haki ya kuyakataa? Je, ile hoja ya parens patriae, ambayo katika hiyo serikali hutenda kwa ajili ya mtu fulani asiyejiweza kikamili, yatumika hapa? Je, mtu mmoja-mmoja ana haki ya kisheria kuamua linaloweza kufanyiwa mwili wake mwenyewe? Je, uhaki wake wa kuamua lipaswalo kufanywa na mwili wake ni usioweza kuvunjwa? Na vipi kuhusu sheria ya umma ya Kanada? Je, yatumika katika kesi kama hii? Hatimaye, je, kesi ya Joshua Walker ilihitaji kupelekwa mahakamani pale mwanzoni?
Je, maswali haya yalipata kusuluhishwa kwa uamuzi ulioandikwa na Mahakama ya Rufani? Ndiyo, yalisuluhishwa. Kufikia mwisho wa usikizi huo, ile mahakama yenye mahakimu watano ilienda faraghani na kisha baadaye wakarudi kwenye chumba cha mahakama na kutoa kwa mdomo uamuzi wa mahakimu wote, ulikuwa kama ifuatavyo:
“Rufani imekubaliwa. Uamuzi wa Turnbull, J. [hakimu wa mahakama ya chini] umebadilishwa. Joshua Walker ametangazwa kuwa mtoto mkomavu chini ya maandalizi ya Medical Consent of Minors Act na idhini ya wazazi wake kuhusu matibabu yake haihitajiwi. Suala la gharama za kesi litashughulikiwa katika uamuzi wetu ulioandikwa.”
Je, sheria ya umma ya Kanada yatumika katika kesi hii? Ndiyo. Ripoti iliyochapishwa ya usikizi huo yataarifu hivi: “Katika Kanada, sheria ya umma hung’amua ile kanuni ya mtoto mkomavu, yaani, mmoja aliye na uweza wa kufahamu hali na matokeo ya matibabu yanayokusudiwa. . . . New Brunswick imeratibisha ile sheria ya umma kufikia kiwango cha kwamba imedhihirishwa kwenye Medical Consent of Minors Act.”
Hatimaye, je, kesi ya Joshua ilipelekwa mahakamani ili kumfanya kisheria aweze kukataa mitio-damu mishipani? La. “Mradi yale maandalizi ya Act yatafuatwa, hakuna uhitaji wa kufanya ombi kama hilo.”
Hakimu Mkuu W. L. Hoyt alimalizia hivi: “Ombi hilo lilifanywa kwa nia nzuri pamoja na kwa utahadhari mwingi. Hata hivyo, matokeo ya ombi hilo yalikuwa kuhusisha Joshua na familia yake katika kesi ambayo haikuhitajiwa. Kwa sababu hiyo, kwa maoni yangu, Hospitali yapaswa igharimie.”
Joshua alikufa Oktoba 4, 1994.
[Blabu katika ukurasa wa 12]
“Hukumu huweka miongozo iliyo wazi . . . kwa madaktari na mahospitali.”—Canadian Medical Association Journal
[Blabu katika ukurasa wa 13]
“Ni ushindi si kwa Mashahidi wa Yehova tu, bali kwa sisi sote.”—Telegragh Journal
[Blabu katika ukurasa wa 14]
“Nataka tu kuishi kwa sheria ya Yehova juu ya damu.”—Joshua Walker
[Blabu katika ukurasa wa 15]
“Ana imani ambayo maishani mwangu sijapata kamwe kuiona ikidhihirishwa.”—Dakt. Garry