Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 2/22 kur. 20-23
  • Nililindwa na Imani Katika Mungu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nililindwa na Imani Katika Mungu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Imani Yajaribiwa Katika Miaka Yangu ya Mapema
  • Maisha Katika Stutthof
  • Imani Yangu Yajaribiwa Kabisa
  • Imani Yangu Yaendelea Kutahiniwa
  • Kwa Msaada wa Yehova, Tuliokoka Serikali za Kimabavu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Imani Katika Mungu Ilinitegemeza
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Kungoja Ufalme Ambao Si “Sehemu ya Ulimwengu Huu”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Hakuna Kitu Kilicho Bora Kuliko Kweli
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 2/22 kur. 20-23

Nililindwa na Imani Katika Mungu

ULIKUWA mwezi wa Mei 1945, na Vita ya Ulimwengu 2 ilikuwa imetoka tu kwisha katika Ulaya. Nilikuwa nimefika nyumbani katika Chojnice, Poland, siku mbili tu zilizokuwa zimepita. Safari hiyo ilikuwa imechukua karibu miezi miwili, kwa sababu nililazimika kutembea kwa miguu na nilikuwa nikitua hapa na pale nikizuru watu. Nilikuwa katika kambi ya mateso ya Stutthof kwa miaka miwili iliyokuwa imepita, kambi hiyo ilikuwa karibu na Danzig (sasa ni Gdansk).

Tukiwa tumeketi katika sebule, mama, dada zangu wawili, na mimi tulikuwa tunafurahia ziara fulani. Mlango wa mbele ulibishwa, na Elaine, dada yangu mkubwa zaidi, akaomba radhi afungue mlango. Hatukufikiria sana mambo yaliyokuwa yakiendelea mlangoni mpaka tuliposikia nduru yake. Nikaruka mara moja kutoka kwa kiti na kukimbilia mlangoni. Wilhelm Scheider na Manfred Licnierski walikuwa wamesimama hapo, wale Wakristo wawili wenzetu niliodhani kwamba walikuwa wamekufa upesi baada ya kuwaona mara ya mwisho.

Baada ya kuwatazama kinywa kikiwa wazi kwa kutoamini macho yangu, Ndugu Scheider aliomba kuingia ndani. Tulitumia muda wote uliobaki mpaka usiku sana tukijuana tena na kukumbuka jinsi Yehova Mungu alikuwa ametulinda tulipokuwa tumefungwa. Kabla kusimulia baadhi ya maono hayo, acheni niwaeleze jinsi nilivyoenda katika kambi ya mateso.

Imani Yajaribiwa Katika Miaka Yangu ya Mapema

Wazazi wangu walikuja kuwa Wanafunzi wa Biblia (kama vile Mashahidi wa Yehova walivyokuwa wakiitwa wakati huo) karibu na wakati nilipozaliwa, katika 1923. Miaka ya kabla ya Vita ya Ulimwengu 2 haikuwa rahisi kwa Mashahidi. Dini ya Katoliki ilikuwa ikifunzwa shuleni, na Mashahidi walikuwa wakitendwa vibaya sana. Nilikuwa nikichokozwa na watoto wengine kila mara, na kwa kawaida mwalimu angeunga mkono watoto hao dhidi yangu. Kazi ya kuhubiri ilikuwa ngumu vilevile. Pindi moja tulipokuwa tukihubiri katika mji ulio karibu wa Kamien, wakazi wa mji huo wasiopungua mia moja walituzunguka sisi Mashahidi 20. Wanajeshi wa Poland walifika kwa wakati barabara na kutulinda dhidi ya umati huo.

Mnyanyaso uliongezeka sana Ujerumani ilipovamia Poland katika Septemba 1939. Hatimaye nilikamatwa na polisi wa Gestapo katika 1943 kwa sababu nilikataa kutumikia Jeshi la Ujerumani. Nilipokuwa nimeshikwa, polisi wa Gestapo walinihoji, wakijaribu kunilazimisha niwape majina ya Mashahidi wengine katika eneo hilo. Nilipokataa, polisi mmoja wa Gestapo aliniambia kwamba huenda nitakufa katika kambi ya mateso.

Kwanza, nilipelekwa katika jela Chojnice, ambako walinzi kadhaa walinipiga kwa fimbo za mpira, wakijaribu kuvunja azimio langu la kubaki mwaminifu-mshikamanifu kwa Yehova. Nilipigwa kwa muda wa dakika 15 au 20, na wakati huo wote nilikuwa nikisali kwa bidii sana. Kuelekea mwisho wa mapigo hayo, mmoja wa walinzi hao akalalamika kwamba alikuwa akichoka kabla nichoke kutokana mapigo.

Ni ajabu kwamba baada ya mapigo machache ya kwanza, kwa kweli sikuyahisi tena. Badala ya hivyo, ilikuwa ni kana kwamba nawasikia wakipiga ngoma kwa umbali. Kwa hakika Yehova alinilinda na kujibu sala zangu. Upesi habari za kupigwa kwangu zilienea kotekote katika jela, na watu fulani wakaanza kuniita “mtu wa Mungu.” Muda mfupi baadaye, nilipelekwa katika makao makuu ya polisi wa Gestapo katika Danzig. Mwezi mmoja baadaye nilipelekwa katika kambi ya mateso ya Stutthof.

Maisha Katika Stutthof

Mara tu tulipofika tuliambiwa tupige mstari mbele za makao ya kulala. Kapo (mfungwa anayesimamia wafungwa wengine) alielekeza kwenye mabomba matatu ya moshi ya mahali pa kuchoma maiti na kutuambia kwamba kwa muda wa siku tatu tutakuwa pamoja na Mungu mbinguni. Nilijua kwamba Ndugu Bruski, kutoka kutaniko letu katika Chojnice, alikuwa amepelekwa Stutthof, kwa hiyo nilijaribu kumtafuta. Lakini, mfungwa mwenzangu akaniarifu kwamba huyo alikuwa amekufa karibu mwezi mmoja uliokuwa umepita. Nilishtuka sana hivi kwamba nilianguka chini. Nilihisi kwamba ikiwa Ndugu Bruski, Mkristo mwenye nguvu za kimwili na kiroho, alikuwa amekufa, hakika mimi ningekufa vilevile.

Wafungwa wengine walinisaidia kurudi makao ya kulala, na hapo ndipo nilipokutana na Ndugu Scheider kwa mara ya kwanza. Baadaye nilikuja kujua kwamba kabla ya vita alikuwa amekuwa mwangalizi wa ofisi ya tawi ya Poland. Aliongea nami kwa muda mrefu, akieleza kwamba nikipoteza imani katika Yehova, ningekufa! Nilihisi kwamba Yehova alikuwa amemtuma aniimarishe. Mithali isemayo hivi ni kweli kama nini: ‘Ndugu huzaliwa kwa siku ya taabu’!—Mithali 17:17.

Imani yangu ilikuwa imedhoofika wakati huo, na Ndugu Scheider alinionyesha Waebrania 12:1. Hapo Wakristo wanaambiwa wajihadhari na dhambi ile ituzingayo kwa upesi, yaani ukosefu wa imani. Alinisaidia kukumbuka watu waaminifu wanaotajwa katika Waebrania sura ya 11 na kuchanganua imani yangu kwa kulinganisha na yao. Nikawa karibu sana na Ndugu Scheider tangu wakati huo na kuendelea, na ingawa alinizidi umri kwa miaka 20, tulikuja kuwa marafiki wa karibu zaidi.

Pindi moja mtu mmoja mwenye mwili mkubwa aliyekuwa amevalia pembetatu ya kijani (iliyomaanisha kwamba alikuwa mhalifu) aliniambia nipande meza na kuhubiria wafungwa wengine juu ya Yehova. Nilipoanza kuhubiri, wafungwa wengine wakaanza kunidhihaki. Lakini mtu huyo mkubwa alienda na kuwanyamazisha—kila mtu alimwogopa. Tulipokutana kwa ajili ya mlo wakati wa adhuhuri na wakati wa jioni katika siku za juma lote lililobaki, mtu huyo mkubwa alikuwa akiniamuru nipande meza na kuhubiri.

Juma lililofuata baadhi ya wafungwa, pamoja na mimi, tulipelekwa katika makao tofauti. Mfungwa mwingine mwenye pembetatu ya kijani alinijia na kuniuliza mbona Mungu alikuwa amenipeleka kwenye “mateso hayo.” Nikajibu kwamba alinileta ili nihubirie wafungwa na kwamba kuwako kwangu huko kulitumika kutahini imani yangu. Nilipokuwa ningali na wafungwa hao, nilikubaliwa kusimama mbele yao na kuhubiri kila usiku kwa majuma mawili.

Siku moja kapo mmoja aliambia mfungwa mwenzangu anipige. Mfungwa huyo alikataa, akijihatarisha kupigwa yeye mwenyewe. Nilipomuuliza mbona hakunipiga, alisema kwamba alikuwa akipanga kujiua lakini alisikiliza mojapo hotuba zangu, na ilimfanya abadili maoni yake. Aliona kwamba niliokoa uhai wake na hangeweza kupiga mtu aliyekuwa ameokoa uhai wake.

Imani Yangu Yajaribiwa Kabisa

Katika masika ya 1944, Warusi walikaribia Stutthof. Maofisa wa kambi Wajerumani waliamua kuhamisha wafungwa kabla ya Warusi kufika. Wajerumani wakaanza kutembeza wafungwa wapatao 1,900 kati yetu sisi kwenda Słupsk. Tulipofika katikati ya mwendo, ni watu wapatao 800 pekee kati yetu waliokuwa wamebaki. Tulikuwa tukisikia mifyatuo mingi ya risasi muda wote wa safari, inaonekana kwamba wengine wote walikuwa wamepigwa risasi au walikuwa wametoroka.

Kabla ya kuanza msafara, kila mmoja wetu alikuwa amepewa gramu 450 za mkate na gramu 220 za siagi. Wengi walikula mara hiyo chakula chote walichopewa. Hata hivyo, nilipima yangu kwa kadiri ambayo ningeweza, nikijua kwamba safari hiyo ingechukua muda wa karibu majuma mawili. Kulikuwa na Mashahidi karibu kumi pekee miongoni mwa wafungwa, na Ndugu Scheider nami tukawa tunatembea pamoja.

Katika siku ya pili ya safari hiyo, Ndugu Scheider akawa mgonjwa. Tangu wakati huo na kuendelea nililazimika kumbeba kihalisi, kwa sababu kama tungalisimama, tungalipigwa risasi. Ndugu Scheider aliniambia kwamba Yehova alikuwa amejibu sala zake kwa kunifanya niwe hapo ili nimsaidie. Katika siku ya tano, nilikuwa nimechoka sana na mwenye njaa sana hivi kwamba nikahisi nisingeweza kutembea tena, sembuse kumbeba Ndugu Scheider. Yeye pia alikuwa akidhoofika kwa kukosa chakula.

Katika wakati wa mapema wa alasiri hiyo, Ndugu Scheider aliniambia kwamba alitaka kwenda haja ndogo, kwa hiyo nikambeba hadi kwenye mti fulani. Nilikuwa nikitazama huko na huko kuhakikisha kwamba hatukuonwa na walinzi Wajerumani. Baada ya muda unaokaribia dakika moja, Ndugu Scheider aligeuka akiwa na mkate mkononi mwake. “Uliupata wapi?” nikauliza. “Ulikuwa ukining’inia kutoka kwenye mti ama vipi?”

Akasema kwamba nilipokuwa nimegeuka, mtu mmoja alimjia na kumpa mkate huo. Niliona tukio hilo kuwa jambo la kutokeza sana kwa sababu sikuona mtu yeyote. Wakati huo tulikuwa wenye njaa sana kiasi cha kwamba hatukuuliza maswali ya jinsi mkate huo ulivyoletwa. Lakini naweza kusema kwamba lile ombi ambalo Yesu alitufundisha la kuomba riziki ya kila siku lilikuwa lenye umaana zaidi baada ya hapo. (Mathayo 6:11) Hatungeokoka siku nyingine bila mkate huo. Nilifikiria pia maneno ya mtunga-zaburi: “Sijamwona mwenye haki ameachwa, wala mzao wake akiomba chakula.”—Zaburi 37:25.

Lakini baada ya karibu juma moja, tulipokaribia kabisa nusu ya mwendo wa kwenda Słupsk, tulisimama katika kambi ya Vijana wa Hitler. Hapo tungekutana na wafungwa kutoka kambi nyinginezo. Ndugu Licnierski alikuwa amepatwa na homa ya matumbo na alikuwa amewekwa katika kao la pekee pamoja na wafungwa wengine waliokuwa wagonjwa. Kila jioni ningejificha kutoka kao letu na kwenda kumwona Ndugu Licnierski. Ningalipigwa risasi kama ningalionekana, lakini ilikuwa ni jambo la muhimu sana kwangu kupoza homa yake kadiri niwezavyo. Ningetia kitambaa kwa maji na kuketi kando yake nikipangusa paji la uso wake. Kisha ningejificha tena na kurudi kao langu. Ndugu Scheider pia akapatwa na homa ya matumbo akawekwa katika kao moja na Ndugu Licnierski.

Tuliambiwa kwamba Wajerumani walikuwa na mpango wa kutupeleka hadi Bahari ya Baltiki, watuweke kwenye mashua, na kutupeleka hadi Denmark. Lakini, Warusi walikuwa wakikaribia zaidi na zaidi. Wajerumani walipoanza kuogopa na kuanza kutoroka, wafungwa nao walipata nafasi ya kutoroka. Wajerumani waliniamuru niondoke, lakini kwa vile Ndugu Scheider na Ndugu Licnierski walikuwa wagonjwa mno wasiweze kusafiri na singeweza kuwabeba, nilishindwa jambo la kufanya. Kwa hiyo, niliondoka nikiomba kwamba Yehova awalinde hao wenzi wangu wapendwa.

Muda wa saa moja baada ya mimi kuondoka, Warusi waliingia kambini. Mwanajeshi mmoja aliwapata Ndugu Scheider na Ndugu Licnierski na kuamuru mwanamke Mjerumani aliyeishi katika shamba lililokuwa karibu awalishe supu ya kuku kila siku mpaka wapone. Mwanamke huyo aliambia mwanajeshi huyo kwamba Wajerumani walikuwa wamechukua kuku zake wote. Kisha mwanajeshi huyo akamwambia kwamba kama hawalishi watu hao, atamuua. Bila shaka, alipata kuku haraka, na ndugu hao wapendwa wakaanza kupata nafuu!

Imani Yangu Yaendelea Kutahiniwa

Tulipokuwa tungali katika sebule ya mama yangu, tuliongea juu ya mambo hayo na maono mengine hadi alfajiri. Ndugu hao walikaa kwa siku kadhaa na kisha wakaenda kwao. Ndugu Scheider alitumiwa sana na Yehova katika kupanga upya kazi katika Poland, akichukua tena mengi ya madaraka yake ya zamani. Hata hivyo, utendaji wa kuhubiri ukawa mgumu sana kwa sababu ya Wakomunisti kutwaa mamlaka.

Pindi kwa pindi Mashahidi walishikwa kwa sababu ya kuhubiri juu ya Ufalme wa Mungu. Mara nyingi nilikuwa miongoni mwa hao na nilikuwa nikihojiwa na walewale walionifungua kutoka kwa Wanazi. Kisha tukang’amua sababu iliyofanya wenye mamlaka wajue utendaji wetu vizuri sana. Wakomunisti walikuwa wameweka wapelelezi katika tengenezo wa kuturipoti. Kitendo hicho kilifanikiwa sana hivi kwamba katika usiku mmoja tu wa 1950, maelfu ya Mashahidi walikamatwa.

Hatimaye mke wangu Helena na familia yetu iliyokuwa ikiendelea kukua iliamua kuhamia United States. Tulifika katika 1966. Nilipokuwa nikizuru Brooklyn, New York, niliweza kutolea ndugu wenye madaraka katika makao makuu ya ulimwengu ya Mashahidi wa Yehova habari iliyowawezesha kutambua wale waliokuwa wamewekwa na Wakomunisti katika tengenezo.—Linganisha Matendo 20:29.

Sasa nina umri wa miaka 70 na naishi katika jimbo la Colorado, ambako ninatumikia nikiwa mzee katika kutaniko moja la hapo. Kwa sababu ya afya yangu inayodhoofika, sasa siwezi kufanya mambo kama nilivyoweza kufanya zamani. Lakini bado nafurahia sana kuongea na watu juu ya Ufalme wa Yehova. Ninapofanya kazi pamoja na vijana shambani, mimi huchukua fursa hiyo pia kuwasaidia kutambua kwamba hata magumu makali kadiri gani yawakabilipo, nyakati zote Yehova huwapo kuwasaidia wale ambao wana imani kamili kwake.

Ninapokumbuka maisha yangu ya mbeleni, ninathamini kwamba Yehova aliniokoa pamoja na marafiki wangu kutoka katika hali za hatari. Matukio hayo yamefanya imani yangu katika ulinzi wake kwa hakika iwe yenye nguvu zaidi. Sina shaka kabisa kwamba mfumo huu wa mambo utaisha upesi katika “dhiki ile iliyo kuu” inayokuja upesi sana na kwamba waokokaji watakuwa na matazamio mazuri ajabu ya kurudisha dunia kuwa paradiso ya ulimwenguni pote.—Ufunuo 7:14; 21:3, 4; Yohana 3:16; 2 Petro 3:13.

Ninatazamia kushiriki katika urudisho huo mtukufu wa kufanya dunia kuwa hali ya paradiso, na ndivyo wewe pia uwezavyo kutazamia ukifanya mapenzi ya Yehova kwa kadiri uwezavyo na kutumaini katika ahadi yake ya kwamba atalinda wale ambao wana imani kwake.—Kama ilivyosimuliwa na Feliks Borys.

[Picha katika ukurasa wa 20]

Mwaka mmoja baada ya kutoka katika kambi ya mateso

[Picha katika ukurasa wa 23]

Nikiwa na mke wangu, Helena

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki