Sura 5
Uhindu—Jitihada ya Kutafuta Kukombolewa
“Katika jamii ya Kihindu, ni desturi ya kidini, jambo la kwanza asubuhi, kuoga ndani ya mto ulio karibu au nyumbani ikiwa hakuna mto wala kijito karibu. Watu huamini kwamba hilo huwafanya watakatifu. Halafu, wakiwa bado hawajala, wanaenda kwenye hekalu la kwao na kutoa sadaka za maua na chakula kwa kijimungu cha kwao. Wengine huiosha sanamu hiyo na kuipamba kwa poda nyekundu na ya manjano.
“Karibu kila nyumba ina pembe au hata chumba cha kuabudia kijimungu kipendwacho cha familia hiyo. Kijimungu kipendwacho na wengi katika sehemu fulani ni Ganesa, kijimungu-tembo. Watu husali kwacho hasa kwa ajili ya jaha njema, kwani chajulikana kuwa ndicho kiondosha-vizuizi. Katika sehemu nyingine Krishna, Rama, Siva, Durga, au kiabudiwa fulani kingine huenda kikachukua mahali pa kwanza katika ujitoaji.”—Tara C., Kathmandu, Nepal.
1. (a) Eleza juu ya baadhi ya desturi za Kihindu. (b) Baadhi ya tofauti kati ya mtazamo wa nchi za Magharibi na mtazamo wa Kihindu ni zipi?
UHINDU ni nini? Je! ni kule tu kurahisishwa kwa wazo la nchi za Magharibi la kuheshimu mno wanyama, kuoga katika Ganges, na kugawanywa vitabaka-tabaka? Au kuna zaidi? Jibu: Kuna zaidi. Uhindu ni njia tofauti ya kuelewa uhai, ambayo kwayo viwango vya nchi za Magharibi ni vigeni kabisa. Watu wa nchi za Magharibi huelekea kuona uhai kuwa mfuatano wa orodha ya matukio katika historia. Wahindu huona uhai kuwa mzunguko unaojirudia ambao katika huo historia ya kibinadamu ina umaana mdogo.
2, 3. (a) Kwa nini ni vigumu kueleza kirefu juu ya Uhindu? (b) Mwandikaji mmoja Mhindi hufafanuaje Uhindu na ibada ya miungu mingi?
2 Si rahisi kueleza kirefu Uhindu, kwani hauna itikadi, jamii ya kikuhani, au wakala wenye kuongoza maalumu na dhahiri. Hata hivyo, una waswami (walimu) na waguru (viongozi wa kiroho). Maelezo marefu ya Uhindu yanayotolewa na kitabu kimoja cha historia hutoa taarifa kwamba huo ni “jumla yote ya imani na desturi ambazo zimekuwapo tangu wakati ambao maandiko yao ya kale (na yaliyo matakatifu zaidi), Vedas, yalipotungwa mpaka sasa.” Kwingine hutoa taarifa hii: “Labda tuseme kwamba Uhindu ni mshikamano au ibada ya vijimungu Vishnu, au Shiva [Siva], au kijimungu-kike Shakti, au kutwaa kwavyo maumbo mengine, sura, mume na mke, au uzao.” Hiyo yatia ndani vidhehebu vya Rama na Krishna (kutwaa maumbo mengine kwa Vishnu), Durga, Skanda, na Ganesa (wa kwanza mke Siva na kisha wanaofuata wana wake). yadaiwa kwamba Uhindu una vijimungu milioni 330, hata hivyo yasemekana Uhindu hauabudu miungu mingi. Yawezekanaje iwe hivyo?
3 Mwandikaji Mhindi A. Parthasarathy afafanua: “Wahindu hawaabudu miungu mingi. Uhindu husema juu ya Mungu mmoja . . . vijimungu na vijimungu-vike tofauti-tofauti vya jamii ya vijimungu vya Hindu ni viwakilisho tu vya nguvu na kazi za Mungu mmoja aliye mkuu katika ulimwengu uliodhihirishwa.”
4. Usemi “Uhindu” unatia nini ndani?
4 Mara nyingi Wahindu hurejezea imani yao kuwa sanatana dharma, kumaanisha sheria au agizo la milele. Uhindua kwa kweli ni usemi usio na kanuni unaoeleza dini na faraka (sampradayas) nyingi ambazo zimesitawi na kuvuvumuka kwa maelfu ya miaka iliyopita chini ya himaya ya mfumo tata wa ngano za kale za Kihindu. Mfumo huo wa ngano ni wenye kutatana sana hivi kwamba New Larousse Encyclopedia of Mythology hutoa taarifa hii: “Mfumo wa ngano za Kihindi ni pori lisilotanzulika la vikuzi vilivyovuvumuka. Unapoliingia unapoteza nuru ya mchana na hisi yote iliyo wazi ya mwelekezo.” Hata hivyo, sura hii itazungumza baadhi ya sehemu na mafundisho ya imani hiyo.
Mizizi ya Kale ya Uhindu
5. Uhindu umeenea kadiri gani?
5 Ingawa Uhindu huenda usiwe umeenea kama dini nyinginezo kubwa-kubwa, bado, ulikuwa na wafuasi karibu milioni 700 kufikia 1990, au karibu 1 kwa 8 (13%) ya watu ulimwenguni. Hata hivyo, sehemu kubwa yao inapatikana India. Kwa hiyo ni jambo la akili kuuliza, Ni jinsi gani na ni kwa nini Uhindu ulisongamana katika India?
6, 7. (a) Kulingana na wanahistoria fulani, Uhindu ulifikaje India? (b) Uhindu huelezaje hekaya yao ya furiko? (c) Kulingana na mwakiolojia Marshall, ni namna ya dini gani iliyozoewa katika Bonde Indus kabla ya Waaria kuwasili?
6 Wanahistoria fulani husema kwamba mizizi ya Uhindu ilikuwa imeanza miaka zaidi ya 3,500 iliyopita katika wimbi la uhamaji lililowasilisha kikundi cha watu wenye ngozi nyeupe-nyeupe wa Kiaria kutoka kaskazini-magharibi mpaka kwenye Bonde Indus, ambalo sasa liko hasa katika Pakistan na India. Kutoka huko walisambaa mpaka kwenye nyanda za Mto Ganges na kotekote India. Wataalamu fulani husema kwamba mawazo ya kidini ya wahamiaji hao yalitegemea mafundisho ya kale ya Kiiran na Kibabuloni. Uzi ule ule wa tamaduni nyingi na pia unaopatikana katika Uhindu ni hekaya ya furiko.—Ona kisanduku, ukurasa 120.
7 Lakini ni dini ya namna gani iliyozoewa katika Bonde Indus kabla ya Waaria kuwasili? Mtaalamu mmoja wa akiolojia, Sir John Marshall, husema juu ya “‘Mama Mkuu Mungu-mke’, viwakilisho fulani vikiwa vijiumbo vya kike vyenye mimba, vingi vyavyo vikiwa maumbo ya kike yaliyo uchi wa koa na kola zilizoinuka na kaya. . . . Halafu kuna ‘Mungu wa Kiume’, ‘anayetambulika mara moja kuwa kifananishi cha Siva wa kihistoria’, akiwa ameketi na matako ya nyayo zake yakigusana (mkao wa yoga), uume wake umesimama (kumbuka ibada ya lingam [uume]), amezungukwa na wanyama (kuonyesha jina la pili la Shiva, ‘Bwana wa Hayawani’). Viwakilisho vya uume na uke ni tele, . . . ambavyo huelekeza kwenye ibada ya lingam na yoni ya Shiva na mke wake.” (World Religions—From Ancient History to the Present) Mpaka wa leo Siva huheshimiwa mno kuwa kijimungu cha mrutubisho, kijimungu cha uume. Fahali Nandi ni mchukuzi wake.
8, 9. (a) Msomi mmoja Mhindu hukataaje nadharia yake Marshall? (b) Ni hoja gani za kupinga zinazotolewa kuhusu vitu vya Uhindu na “Ukristo” vinavyoheshimiwa mno? (c) Ni nini msingi wa maandishi matakatifu ya Uhindu?
8 Swami Sankarananda msomi Mhindu akataa fasiri yake Marshall, akitoa taarifa kwamba hapo awali mawe yenye kuheshimiwa mno, mengine yakijulikana kuwa Sivalinga, yalikuwa viwakilisho vya “moto wa anga au jua na moto wa jua, miale.” (The Rigvedic Culture of the Pre-Historic Indus) Yeye anasababu kwamba “kidhehebu cha ibada ya ngono . . . asili yacho haikuwa kidhehebu cha kidini. Ni zao la baadaye. Ni mpotoko wa kile cha awali. Watu ndio wanaoshusha wazo hilo wakilileta kwenye viwango vyao wenyewe, ambalo ni la juu mno wasiweze kulielewa.” Ikiwa hoja ya kupinga uchambuzi wa nchi za Magharibi kuhusu Uhindu, yeye asema kwamba, kwa kutegemea kuheshimiwa sana kwa msalaba wa Wakristo, ambao ni mfananisho wa kipagani wa uume, “Wakristo . . . ndio wateteaji wa kidhehebu cha ibada ya ngono.”
9 Kadiri wakati ulivyokuwa ukipita, itikadi, ngano, na hekaya za India ziliandikwa, na leo ndiyo maandishi matakatifu ya Uhindu. Ijapokuwa maandishi hayo matakatifu ni ya kadiri kubwa, hayajaribu kupendekeza fundisho lenye umoja la Kihindu.
Maandishi Matakatifu ya Uhindu
10. Ni nini baadhi ya maandishi ya kale zaidi ya Uhindu?
10 Maandishi ya zamani zaidi ni Vedas, mkusanyo wa sala na nyimbo za kidini zinazojulikana kuwa Rig-Veda, Sama-Veda, Yajur-Veda, na Atharva-Veda. Yalitungwa wakati wa karne kadhaa na kukamilishwa karibu 900 K.W.K. Baadaye Vedas ziliongezewa maandishi mengine, kutia ndani Brahmanas na Upanishads.
11. (a) Ni nini tofauti kati ya Brahmanas na Upanishads? (b) Ni mafundisho gani yanayotolewa na Upanishads?
11 Brahmanas hutaja waziwazi jinsi sherehe za kiibada na dhabihu, za kinyumbani na za umma, zipasavyo kufanywa na hueleza kirefu sana maana yazo yenye kina. Ziliandikwa kuanzia yapata 300 K.W.K. au baadaye. Upanishads (kwa halisi, “vikao karibu na mwalimu”), zianazoitwa pia Vedanta na zilizoandikwa karibu 600-300 K.W.K., ni maandiko yanayoeleza sababu ya mawazo na matendo yote, kulingana na falsafa ya Kihindu. Mafundisho ya samsara (uhamaji wa nafsi) na Karma (itikadi ya kwamba vitendo vya maisha ya wakati uliotangulia ndivyo vinavyosababisha hali ya maisha ya mtu ya wakati huu) yalisemwa katika maandishi hayo.
12. Rama alikuwa nani, na hadithi yake yapatikana wapi?
12 Fungu jingine la maandishi ni Puranas, au hadithi-istiara ndefu zenye ngano nyingi za Kihindu juu ya vijimungu na vijimungu-vike na pia mashujaa Wahindu. Maandishi hayo ya Kihindu yenye kadiri kubwa yanatia ndani pia tenzi za Ramayana na Mahabharata. Utenzi wa kwanza ni hadithi ya “Bwana Rama . . . aliye mtukufu zaidi kati ya wahusika wote wanaopatikana katika fasihi ya kimaandiko,” kulingana na A. Parthasarathy. Ramayana ni moja ya maandishi yenye kupendwa zaidi kwa ajili ya Wahindu, yakiwa ya tarehe ya kuanzia yapata karne ya nne K.W.K. Ni hadithi ya shujaa Rama, au Ramachandra, anayeonwa na Wahindu kuwa kiolezo cha mwana, ndugu, na mume. Yeye hufikiriwa kuwa avatar (umbo jingine) la saba la Vishnu, na jina lake mara nyingi hutumiwa kuwa salamu.
13, 14. (a) Kulingana na chanzo kimoja cha Kihindu, Bhagavad Gita ni nini? (b) Sruti na Smriti vinamaanisha nini, na Manu Smriti ni nini?
13 Kulingana na Bhaktivedanta Swami Prabhupāda, mwanzilishi wa International Society for Krishna Consciousness, “Bhagavad-gītã [sehemu ya Mahabharata] ndiyo maagizo makuu ya adili. Maagizo ya Bhagavad-gītã huwa ndiyo utaratibu mkuu wa dini na utaratibu mkuu wa akili. . . . Agizo la mwisho la Gītã ndilo neno la mwisho la adili na dini: jisalimishe kwake Kṛs̩ṇa [Krishna].”—BG.
14 Bhagavad Gita (Wimbo wa Mbinguni), yanayoonwa na wengine kuwa “johari la hekima ya kiroho ya India,” ni mazungumzo kwenye uwanja wa pigano “kati ya Bwana Śrī Kṛṣṇa [Krishna], Nafsi Kuu ya Uungu, na Arjuna, rafiki wa karibu na sufii Wake, ambaye Humwagiza katika sayansi ya kujitambua.” Hata hivyo, Bhagavad Gita ni sehemu moja tu ya maandishi matakatifu ya Kihindu yenye kadiri kubwa. Baadhi ya maandishi hayo (Vedas, Brahmanas, na Upanishads) huonwa kuwa Sruti, au “yaliyosikiwa,” na kwa hiyo huchukuliwa kuwa hati takatifu iliyofunuliwa moja kwa moja. Mengine, kama tenzi na Puranas, ni Smriti, au “yaliyokumbukwa,” na hivyo yalitungwa na watungaji wa kibinadamu, ingawa yametokana na ufunuo. Kielelezo kimoja ni Manu Smriti, yanayoonyesha sheria ya kidini na kijamii ya Kihindu, kuongezea kufafanua msingi wa mfumo wa kitabaka. Ni nini baadhi ya itikadi ambazo zimezuka kutokana na maandishi hayo ya Kihindu?
Mafundisho na Mwenendo—Ahimsa na Varna
15. (a) Eleza kirefu juu ya ahimsa, na ufafanue jinsi wafuasi wa Dini ya Jaini wanavyoitumia. (b) Gandhi alikuwa na maoni gani juu ya ahimsa? (c) Wafuasi wa Dini ya Sikh hutofautianaje na Wahindu na wafuasi wa Dini ya Jaini?
15 Kama vile katika dini nyinginezo, katika Uhindu kuna mawazo fulani ya msingi yanayoongoza kufikiri na mwenendo wa kila siku. Moja lenye kutokeza ni lile la ahimsa (Sanskrit, ahinsa), au kutotumia jeuri, ambalo kwalo Mohandas Gandhi (1869-1948), aliyejulikana kuwa Mahatma, alikuwa maarufu sana. (Ona kisanduku, ukurasa 113.) Kwa msingi wa falsafa hiyo, Wahindu hawapaswi kuua au kufanya jeuri kwa viumbe vingine, hii ikiwa ndiyo moja ya sababu wao huheshimu sana wanyama, kama vile ng’ombe, nyoka, na nyani. Wateteaji thabiti zaidi wa fundisho hilo la ahimsa na staha kwa ajili ya uhai ni wafuasi wa Dini ya Jaini (iliyoanzishwa katika karne ya sita K.W.K.), ambao hutembea miguu mitupu na hata huvaa kifuniko cha uso ili wasimeze bila ya kukusudia mdudu yeyote. (Ona kisanduku, ukurasa 104, na picha, ukurasa 108.) Kinyume cha hilo, wafuasi wa Dini ya Sikh wanajulikana kwa ajili ya pokeo lao la upigaji vita, na Singh, ambalo ni jina lao wote la mwisho, humaanisha simba.—Ona kisanduku, kurasa 100-101.
16. (a) Wahindu walio wengi wana maoni gani juu ya mfumo wa kitabaka? (b) Gandhi alisema nini juu ya mfumo wa kitabaka?
16 Sehemu inayojulikana ulimwenguni pote ya Uhindu ni varna, au mfumo wa kitabaka, ambao hugawanya jamii katika matabaka magumu sana. (Ona kisanduku, ukurasa 113.) Mtu hakosi kuona kwamba jamii ya Kihindu ingali imegawanywa kitabaka-tabaka na mfumo huo, ingawa unakataliwa na wafuasi wa Dini ya Buddha na wa Jaini. Hata hivyo, sawa na vile ubaguzi wa rangi ungalipo katika United States na kwingineko, ndivyo mfumo wa kitabaka umeimarika katika akili ya Kihindi. Kwa njia fulani ni namna ya kuwa na fahamu ya kitabaka ambayo, kwa njia iyo hiyo, ingali yaweza kupatikana leo kwa kiwango cha chini katika jumuiya ya Uingereza na nchi nyinginezo. (Yakobo 2:1-9) Kwa hiyo, katika India mtu huzaliwa katika mfumo wa kitabaka ulio mgumu sana, na karibu hakuna njia ya kutokea. Zaidi ya hayo, Mhindu wa kawaida hatafuti njia ya kutoka humo. Yeye huona hilo kuwa liliamuliwa kimbele, fungu lisiloepukika maishani, matokeo ya vitendo vyake katika maisha yake ya awali, au Karma. Lakini mfumo huu wa kitabaka ulianzaje? Kwa mara nyingine ni lazima tugeukie ngano za Kihindu.
17, 18. Kulingana na ngano za Kihindu, mfumo wa kitabaka ulianzaje?
17 Kulingana na ngano za Kihindu, hapo awali kulikuwako matabaka manne makubwa yenye kutegemea sehemu za mwili wa Purusha, umbo-baba la awali la ainabinadamu. Nyimbo za kidini za Rig-Veda hutoa taarifa hii:
“Walipomgawanya Purusha walifanyiza visehemu vingapi?
Wanaitaje kinywa chake, mikono yake? Wanaitaje mapaja na miguu yake?
Brahman [tabaka la juu kabisa] lilikuwa ndilo kinywa chake, Rajanya lilifanyizwa kwa mikono yake miwili.
Mapaja yake yakawa Vaisya, kutoka kwa nyayo zake Sudra lilitokezwa.”—The Bible of the World.
18 Hivyo Wabrahma wa kikuhani, tabaka la juu kabisa, walidhaniwa kuwa walitokana n kinywa chake Purusha, sehemu yake ya juu kabisa. Tabaka lenye kuongoza, au la wapigaji vita, (Kshatriya au Rajanya) lilitoka kwenye mikono yake. Tabaka la wafanya biashara na wakulima, liitwalo Vaisya, au Vaishya, lilitokana na mapaja yake. Tabaka la kijamii la chini zaidi, Sudra, au Shudra, au tabaka la wafanya kazi ngumu, lilitokana na sehemu ya chini zaidi ya mwili, miguu yake.
19. Ni matabaka gani mengine yaliyokuja kutokea?
19 Karne zilivyopita hata matabaka ya chini zaidi yalitokea, matabaka ya walio nje na ya Wasiopasa Kuguswa, au kama Mahatma Gandhi alivyowaita kwa fadhili zaidi, Waharija, au “watu walio mali ya kijimungu Vishnu.” Ingawa sera ya wasiopasa kuguswa imekuwa haramu katika India tangu 1948, Wasiopasa Kuguswa wangali wana maisha magumu sana.
20. Ni sehemu gani nyingine za mfumo wa kitabaka?
20 Baada ya muda, matabaka hayo yaliongezeka yakalingana karibu na kila kazi na ufundi-stadi katika jumuiya ya Kihindi. Mfumo huu wa kale wa kitabaka, unaomweka kila mtu katika mahali pake pa kijamii, kwa halisi pia ni wa ubaguzi-rangi na “hutia ndani aina hususa za rangi kuanzia wanaojulikana kuwa Waaria [wenye rangi nyeupe-nyeupe] mpaka wazao wa kabla ya Dravidia [wenye rangi nyeus-nyeusi zaidi].” Varna, au tabaka, maana yake ni “rangi.” “Matabaka matatu ya kwanza ya kijamii yalikuwa Waaria, watu weupe zaidi; tabaka la nne, lenye kutia ndani waaborijini wenye ngozi nyeusi, halikuwa la Waaria.” (Myths and Legends Series—India, cha Donald A. Mackenzie) Ni wazi kwamba katika maisha ya India mfumo wa kitabaka, ukiwa umeimarishwa na fundisho la kidini la Karma, umefungia mamilioni ya watu katika umaskini na udhalimu wa kudumu.
Mrudio wa Maisha Wenye Kufadhaisha
21. Kulingana na Garuda Purana, Karma huathirije yatakayompata mtu hatimaye?
21 Imani nyingine ya msingi inayoathiri kanuni na mwenendo wa Kihindu, mojawapo muhimu zaidi, ni fundisho la Karma. Hii ni kanuni ya kwamba kila kitendo kina matokeo yake, mema au mabaya; huamua kila maisha ya nafsi iliyohama au ikatwaa umbo jingine. Ni kama ambavyo Garuda Purana hufafanua:
“Binadamu ndiye anayeumba ajali yake mwenyewe, na hata katika maisha yake akiwa kiini-tete yeye huathiriwa na kani za matendo yake ya maisha yake ya awali. Awe anaishi mahali salama mlimani au anatulia katika kifua cha bahari, awe yu salama pajani mwa mama yake au awe ameinuliwa juu ya kichwa chake, mwanadamu hawezi kupuruka atoke kwenye matokeo ya vitendo vyake mwenyewe vya wakati uliotangulia. . . . Chochote kitakachompata binadamu katika umri au wakati wowote ule kitamfikia wakati huo na mnamo tarehe hiyo.”
Garuda Purana huendelea hivi:
“Maarifa anayopata mtu katika uzawa wake wa awali, utajiri uliotolewa kuwa ufadhili katika maisha yake ya awali, na matendo aliyofanya katika maisha yake katika umbo lililotangulia, hutangulia nafsi yake katika safari yayo ya muda.”
22. (a) Kuna utofautiano gani kati ya hitiari za Kihindu na zile za Jumuiya ya Wakristo kwa ajili ya nafsi baada ya kifo? (b) Fundisho la Biblia juu ya nafsi ni nini?
22 Imani hiyo inategemea nini? Nafsi isiyoweza kufa ni ya muhimu kuhusiana na fundisho la Karma, na Karma ndiyo inayofanya maoni ya Kihindu ya nafsi yatofautiane na yale ya Jumuiya ya Wakristo. Mhindu huamini kwamba kila nafsi ya mtu pekee, ji̇̃va au prãn,b hupitia maisha yenye maumbo mengi na yawezekana kwenye “helo.” Ni lazima ijitahidi kuungana na “Nafsi Iliyo Kuu,” iitwayo pia Brahman, au Brahm (isieleweke makosa kuwa kijimungu cha Uhindu Brahma). Kwa upande ule mwingine, mafundisho ya Jumuiya ya Wakristo huipa nafsi chaguo la kwenda mbinguni, motoni, purgatori (toharani), au Limbo, ikitegemea sadikisho la kidini.—Mhubiri 9:5, 6, 10; Zaburi 146:4.
23. Karma huathirije maoni ya Kihindu juu ya uhai? (Linganisha Wagalatia 6:7-10.)
23 Kwa sababu ya Karma, Wahindu huelekea kuwa na imani ya ajali. Huamini kwamba hadhi na hali ya mtu ya wakati huu ni matokeo ya maisha ya wakati uliotangulia na kwa hiyo ni stahili, yawe ni mazuri au mabaya. Mhindu aweza kujaribu kufanya kumbukumbu nzuri zaidi ili kwamba maisha yake ya wakati ujao yawe afadhali zaidi. Hivyo, yeye hukubali kwa utayari zaidi fungu lake maishani kuliko mtu wa nchi za Magharibi. Kwa Mhindu yote hayo ni tendo la sheria ya kisababishi na tokeo kuhusiana na maisha yake ya wakati uliotangulia. Ni ile kanuni ya kuvuna ulichopanda katika yanayodhaniwa kuwa maisha ya wakati uliopita. Bila shaka, yote hayo hutegemea ile dhana ya kwamba mwanadamu ana nafsi isiyoweza kufa inayohama na kuingia katika uhai mwingine, uwe ni wa binadamu, au mnyama, au mboga.
24. Moksha ni nini, na Wahindu huamini inafikiwaje?
24 Kwa hiyo, ni nini shabaha ya upeo katika imani ya Kihindu? Kufikia moksha, maana yake ukombozi, au achilio, kutokana na gurudumu lenye kukandamiza la kuzaliwa tena na tena na kuishi maisha mengi tofauti-tofauti. Kwa hiyo, ni kuponyoka maisha ya mwilini, si mwili kuponyoka, bali “nafsi.” “Kwa kuwa moksha, au kufunguliwa kutoka kwa mifululizo mirefu ya maisha katika maumbo tofauti-tofauti, ndio mradi wa kila Mhindu, tukio kubwa zaidi maishani mwake kwa kweli ni kifo chake,” atoa taarifa mwelezaji mmoja. Moksha yaweza kufikiwa kwa kufuata margas, au njia tofauti-tofauti. (Ona kisanduku, ukurasa 110.) Lo! jinsi mafundisho mengi hayo ya kidini yanavyotegemea wazo la kale la Kibabuloni la nafsi isiyoweza kufa!
25. Maoni ya Kihindu juu ya uhai yatofautianaje na maoni ya Biblia?
25 Hata hivyo, kulingana na Biblia, dharau na kinaa hii ya uhai wa kimwili hupingana kabisa na kusudi la awali la Yehova Mungu kwa ajili ya ainabinadamu. Alipoumba wanadamu wawili wa kwanza, aliwapa mgawo wa kuwa na maisha ya kidunia yenye furaha na shangwe. Simulizi la Biblia latuambia:
“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. . . . Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana.” (Mwanzo 1:27-31)
Biblia hutoa unabii juu ya enzi iliyo karibu ya amani na haki kwa ajili ya dunia, enzi ambayo kila familia itakuwa na makao mazuri, na kwa umilele ainabinadamu itakuwa na afya na uhai kamili.—Isaya 65:17-25; 2 Petro 3:13; Ufunuo 21:1-4.
26. Ni swali gani linalohitaji jibu sasa?
26 Swali litakalofuata kujibiwa ni, Je! ni vijimungu gani ambavyo lazima Mhindu apendeze ili afikie Karma nzuri?
Jamii ya Vijimungu vya Kihindu
27, 28. (a) Ni vijimungu gani vinavyofanyiza Trimurti ya Kihindu? (b) Ni nani walio wake wavyo au waandamizi wavyo? (c) Taja baadhi ya vimjimungu na vijimungu-vike vingine vya Wahindu.
27 Ingawa Uhindu waweza kudai kuwa na mamilioni ya vijimungu, katika zoea halisi kuna vijimungu fulani vipendwavyo zaidi ambavyo vimekuwa vya kukaziwa sana fikira na faraka mbalimbali za Kihindu. Vitatu vya vijimungu maarufu zaidi ni kutia ndani kile wakiitacho Wahindu, Trimurti, utatu, au utatu wa vijimungu.—Kwa ajili ya vijimungu vingine vya Kihindu, ona kisanduku, kurasa 116-17.
28 Ndani ya utatu mna Brahma aliye Muumba, Vishnu aliye Mhifadhi, na Siva aliye Mharabu, na kila mmoja ana angalau mke mmoja au mwandamizi. Brahma ameoa Saraswati, kijimungu-kike cha maarifa. Mke wa Vishnu ni Lakshmi, hali mke wa kwanza wa Siva alikuwa Sati, ambaye alijiua. Yeye alikuwa mwanamke wa kwanza kuingia kwenye moto wa kidhabihu, na hivyo akawa Suttee wa kwanza. Kwa kufuata kielelezo chake cha kingano, maelfu ya wajane Wahindu wakati wa karne nyingi wamejidhabihu wenyewe kwenye moto wa sherehe ya maziko ya mume wao, ingawa sasa zoea hili ni haramu. Siva pia yuna mke mwingine anayejulikana kwa majina na mitajo-rasmi kadhaa. Akiwa katika umbo lake la fadhili, yeye ni Parvati na Uma, na pia Gauri, Aliye wa Kidhahabu. Akiwa Durga au Kali, yeye ni kijimungu-kike cha kutisha.
29. Brahma huonwaje na Wahindu? (Linganisha Matendo 17:22-31.)
29 Brahma ajapokuwa kitovu cha ngano za Kihindu, yeye hana cheo cha maana katika ibada ya Mhindu wa wastani. Kwa kweli ni mahekalu machache yaliyowekwa wakfu kwake, hata ingawa aitwa Brahma aliye Muumba. Hata hivyo, ngano za Kihindu hupa mgawo wa kuumba ulimwengu unaoonekana mtu mkuu, chanzo, asili—Brahman, au Brahm, anayetambulishwa kwa silabi takatifu OM au AUM. Washiriki wote watatu wa utatu huo huonwa kuwa sehemu ya “Mtu” huyo, na vijimungu vinginevyo vyote huonwa kuwa midhihirisho tofauti-tofauti. Basi ikitegemea kijimungu chochote kinachoabudiwa kuwa kikuu, kiabudiwa hicho hufikiriwa kuwa wote watiwa ndani. Basi ingawa Wahindu huheshimu mno waziwazi mamilioni ya vijimungu, walio wengi hukiri Mungu mmoja tu wa kweli, ambaye aweza kutwaa maumbo mengi: ya kiume, ya kike, au hata ya mnyama. Kwa hiyo, wasomi Wahindu hufanya haraka kutaja kwamba Uhindu kwa kweli huabudu mungu mmoja, wala si miungu mingi. Hata hivyo, mawazo ya baadaye ya Veda, hutupilia mbali wazo la mtu fulani mkuu, na mahali pake kuweka kanuni ya kimungu au uhalisi usio na utu.
30. Ni zipi zilizo baadhi ya avatar za Vishnu?
30 Vishnu, kijimungu chenye kufadhili cha jua na ulimwengu, ndicho kitovu cha ibada kwa wafuasi wa Vaishnavism. Hicho huonekana chini ya maavatar kumi, maumbo mbalimbali, kutia ndani Rama, Krishna, na Buddha.c Avatari nyingine ni Vishnu Narayana, “linalowakilishwa katika umbo la kibinadamu likiwa limelala usingizi kwenye joka Shesha lililojipinda au Ananta, kikielea juu ya maji ya ulimwengu pamoja na mke wacho, kijimungu-kike Lakshmi, kilichoketi penye nyayo zake huku kijimungu Brahma kikiinuka kutoka yungiyungi inayomea kutoka kitovu cha Vishnu.”—The Encyclopedia of World Faiths.
31. Siva ni kijimungu cha aina gani?
31 Siva, ambacho huitwa na wote Mahesha (Bwana Mkuu) na Mahadeva (Mungu Mkubwa), ndicho kijimungu cha pili kwa ukubwa katika Uhindu, na ibada kinachopewa huitwa Usaivi. Hicho husimuliwa kuwa “mjinyimaji raha mkubwa, fundi wa yoga anayeketi akitafakari kwenye miteremko ya Himalayas, mwili wacho umepakwa majivu na kichwa chacho kimefunikwa nywele zilizosukwa.” Pia chajulikana “kwa ajili ya mahaba yacho, kuwa kileta mrutubisho na bwana mkuu wa uumbaji, Mahadeva.” (The Encyclopedia of World Faiths) Ibada hutolewa kwa Siva kupitia lingam, au kiwakilisho cha uume.—Ona picha, ukurasa 99.
32. (a) Kijimungu-kike Kali huchukua maumbo gani? (b) Neno moja la Kiingereza lilitokanaje na ibada yacho?
32 Sawa na dini nyinginezo za ulimwengu, Uhindu una kijimungu-kike kilicho kikuu, kinachoweza kuwa chenye kuvutia au chenye kutisha sana. Katika umbo lacho la kupendeza zaidi, chajulikana kuwa Parvati na Uma. Tabia yacho yenye kuogofya huonyeshwa kuwa Durga au Kali, kimungu-kike chenye kiu ya damu ambacho hufurahia dhabihu za damu. Akiwa Mungu-mke Mama, Kali Ma (Mama-Dunia Mweusi), ndicho kiabudiwa kikuu cha faraka la Shakti. Huonyeshwa kikiwa uchi kufikia nyongani na kimevaa mapambo ya maiti, nyoka, na mafuvu ya kichwa. Katika nyakati zilizopita, wahanga wa kibinadamu walionyongwa walitolewa sadaka kwacho na waumini walioitwa thugi, ambako neno la Kiingereza “thug” (jambazi) lilitoka.
Uhindu na Mto Ganges
33. Ni kwa nini Ganges ni mtakatifu kwa Wahindu?
33 Hatuwezi kuzungumza juu ya jamii ya vijimungu vya Uhindu bila kutaja mto wao ulio mtakatifu zaidi—Ganges. Nyingi za ngano za Kihindu zahusiana moja kwa moja na mto Ganges, au Ganga Ma (Mama Ganga), kama Wahindu wa kidini wanavyouita. (Ona ramani, ukurasa 123.) Wao huimba sala inayotia ndani majina tofauti-tofauti 108 kwa ajili ya mto huo. Ni kwa nini Ganges wastahiwa sana na Wahindu wenye moyo mweupe? Ni kwa sababu unashirikishwa karibu sana na maisha yao ya kila siku na hekaya zao za kale. Wao huitikadi kwamba hapo awali ulikuwako katika mbingu ukiwa ile Njia ya Kimaziwa. Basi ukawaje mto?
34. Kulingana na ngano za Kihindu, ni ufafanuzi gani mmoja juu ya jinsi mto Ganges ulivyopata kutokea?
34 Kukiwa na utofautiano fulani Wahindu walio wengi huufafanua hivi: Maharajah Sagara alikuwa na wana 60,000 waliouawa na moto wa Kapila, udhihirisho wa Vishnu. Nafsi zao zililaani kwenda kwenye helo isipokuwa kijimungu-kike Ganga kingeshuka kutoka mbinguni kizitakase na kuziachilia kutoka kwa laana hiyo. Bhagiratha, kitukuu cha Sagara, kiliteta na Brahma kiruhusu Ganga kitakatifu kishuke chini duniani. Simulizi fulani laendelea hivi: “Ganga kikajibu. ‘Mimi ni mvo mkubwa ningevunja-vunja misingi ya dunia.’ Basi baada ya [Bhagīratha] kutubu kwa miaka elfu, kikakiendea kijimungu Shiva, kikuu cha wajinyimaji raha wote, kikakishawishi kisimame juu ya dunia katikati ya mwamba na barafu ya Himalayas. Shiva kikaagiza nywele zilizosukwa zirundamane kichwani pacho, kikaruhusu Ganga kingurume kuteremka chini kutoka kwenye anga mpaka ndani ya mashungi yacho, yaliyomeza mtetemo wenye kutisha dunia. Ndipo Ganga kikachuruzika kwa ulaini kwenye dunia na kuteremka chini kutoka kwenye milima kuvuka nyanda, kikileta maji na kwa hiyo uhai kwenye dunia kavu.”—From the Ocean to the Sky, cha Sir Edmund Hillary.
35. Wafuasi wa Vishnu hufafanuaje mto huo ulivyopata kutokea?
35 Wafuasi wa Vishnu wana hadithi tofauti kidogo juu ya jinsi Ganges ulivyoanza. Kulingna na maandishi fulani ya kale, Vishnu Purana, hadithi yao ndiyo hii:
“Kutoka mkoa huu [kiti kitakatifu cha Vishnu] watoka mto Ganges, ambao huondoa dhambi yote . . . Hutoka kwenye ukucha wa kidole kikubwa cha mguu wa kushoto wa Vishnu.”
Au kama wasemavyo wafuasi wake Vishnu katika Sanskrit: “Visnu-padabja-sambhuta,” maana yake “Uliozaliwa na kutokana na mguu wa Vishnu ulio kama yungiyungi.”
36. Wahindu huamini nini juu ya nguvu za maji ya Ganges?
36 Wahindu huamini kwamba Ganges una nguvu za kuacha huru, kutakasa, kusafisha, na kuponya waumini. Vishnu Purana hutoa taarifa hii:
“Watakatifu, wanaotakaswa kwa kuoga katika maji ya mto huu, na ambao akili zao zimetolewa kwa ajili ya Kesava [Vishnu], hupata ukombozi wa mwisho kabisa. Mto huo mtakatifu, unaposikiwa, unapotamaniwa, unapoonwa, unapoguswa, unapoogewa ndani, au kuimbiwa, siku baada ya siku hutakasa watu. Na wale ambao wanaishi hata mbali . . . hupaaza sauti ‘Ganga na Ganga’ waondolewa dhambi walizofanya wakati wa maisha yao matatu yaliyopita.”
The Brahmandapurana hutoa taarifa hii:
“Wale wanaooga kwa ujitoaji mara hiyo katika mikondo yenye kutakata ya Ganga, makabila yao hulindwa na Yeye kutokana na mamia ya maelfu ya hatari. Maovu yaliyolimbika kwa vizazi vingi yanaangamizwa. Kwa kuoga tu ndani ya Ganga mtu hutakaswa mara hiyo.”
37, 38. Ni kwa nini mamilioni ya Wahindu humiminika kwenye Ganges?
37 Wahindi humiminika kwenye mto huo wakafanye puja, au ibada, kwa kutoa sadaka ya maua, wakiimba sala, na kupokea kutoka kwa kuhani tilak, doa la lahamu nyekundu au manjano kwenye kipaji cha uso. Ndipo wanapotembea ndani ya maji hayo wakaoge. Pia wengi huyanywa maji hayo, hata ingawa yamechafuliwa sana na takataka, kemikali, na mizoga. Lakini ndivyo Ganges unavyovutia kiroho hivi kwamba ni tamaa kubwa ya mamilioni ya Wahindi kuoga angalau mara moja katika ‘mto mtakatifu’ wao, uwe ni mchafu au la.
38 Wengine huleta miili ya wapendwa wao iteketezwe kwenye marundo ya vitu vya kuchomwa kando ya mto, ndipo majivu yanapotapanywa katika mto huo. Wanaamini kwamba hilo linatoa uhakikisho wa raha ya milele kwa ajili ya nafsi iliyoondoka. Wale walio maskini mno wasiweze kugharimia maziko ya kuchoma huutumbukiza tu mwili uliofungwa kwa sanda ndani ya mto huo, humo unashambuliwa na ndege wala mizoga au kuoza tu. Hilo latuleta kwenye swali, Kuongezea yale tuliyokwisha kuzungumza, Uhindu hufundisha nini juu ya maisha ya baada ya kifo?
Uhindu na Nafsi
39, 40. Msimulizi mmoja wa Kihindu husema nini juu ya nafsi?
39 Bhagavad Gita hutoa jibu kinaposema:
“Nafsi iliyomo ndani ya mwili inapoendelea kupita, katika huu mwili, tangu uvulana kuingia ujana, na halafu kuingia umri wa uzee, vivyo hivyo hiyo nafsi huingia ndani ya mwili mwingine wakati wa kifo.”—Sura 2, aya 13.
40 Maelezo fulani ya Kihindu juu ya aya hii hutoa taarifa hii: “Kwa kuwa kila kitu kilicho hai ni nafsi moja moja, kila kimoja hubadili mwili wacho kila dakika, nyakati nyingine kujidhihirisha kuwa mtoto, nyakati nyingine kuwa kijana, na nyakati nyingine kuwa mtu mzee—ijapokuwa nafsi ya roho ile ile ipo na haibadiliki vyovyote. Nafsi hii moja moja hatimaye hubadili mwili wenyewe, kwa kuhama kutoka mmoja mpaka mwingine, na kwa kuwa ina hakika kuwa na mwili mwingine katika uzawa utakaofuata—ama uonekanao au wa kiroho—hakukuwa na sababu ya Arjuna kuomboleza kwa ajili ya kifo.
41. Kulingana na Biblia, ni utofautisho gani kuhusu nafsi wapasa kufanywa?
41 Angalia kwamba maelezo hayo hutoa taarifa kwamba “kila kitu kilicho hai ni nafsi moja moja peke yake.” Basi taarifa hiyo yakubaliana na yale ambayo Biblia husema kwenye Mwanzo 2:7:
“BWANA [Yehova] Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.”
Lakini ni lazima utofautiano wa maana ufanywe: Je! mtu alifanyizwa kuwa nafsi hai pamoja na matendo na akili zake zote, au je! yeye yuna nafsi iliyo mbali na matendo yake ya kimwili? Je! binadamu ni nafsi, au je! yeye yuna nafsi? Nukuu lifuatalo laonyesha wazi wazo hilo la Kihindu.
42. Uhindu na Biblia hutofautianaje juu ya kuielewa nafsi?
42 Sura 2, aya 17, ya Bhagavad Gita hutoa taarifa hii:
“Kile kinachouenea mwili mzima wote hakiharibiki. Hakuna anayeweza kuharibu nafsi isiyoweza kuharibika.”
Ndipo aya hii hufafanuliwa hivi:
“Ndani ya kila mwili mna nafsi moja moja, na ishara ya kuwapo kwa hiyo nafsi huhisiwa kwa utambuzi wa mtu mmoja mmoja.”
Kwa hiyo, ingawa Biblia hutoa taarifa kwamba mwanadamu yu nafsi, fundisho la Kihindu hutoa taarifa kwamba yeye yuna nafsi. Na kuna tofauti kubwa sana hapo ambayo ina matokeo makubwa juu ya mafundisho ambayo yametokana na maoni hayo.—Mambo ya Walawi 24:17, 18, NW.
43. (a) Ni ni asili ya fundisho la nafsi isiyoweza kufa? (b) Matokeo yalo ni nini?
43 Fundisho la nafsi isiyoweza kufa chanzo chalo ni lile dimbwi tuli la maarifa ya kidini ya Babuloni ya kale. Kufikiri kuzuri huongoza ndani ya matokeo ya ‘uhai baada ya kifo’ yanayokazwia katika mafundisho ya dini nyingi mno—kuzaliwa upya kwa nafsi katika umbo jingine, mbingu, helo, purgatori (toharani), limbo, na kadhalika. Kwa Mhindu, mbingu na helo ni sehemu za kati na kati za kungojea kabla ya nafsi kuzaliwa upya katika umbo lile lifuatalo. Lenye kuvutia kipekee ni wazo la Kihindu juu ya helo.
Fundisho la Kihindu Juu ya Helo
44. Twajuaje kwamba Uhindu hufundisha kwamba kuna helo ya kuteseka mtu akiwa na fahamu?
44 Aya moja kutoka Bhagavad Gita hutoa taarifa hii:
“O Kṛịṣna [Krishna], mdumishaji wa watu, nimesikia kwa wenye mamlaka kwamba wale wanaoharibu mila za familia hukaa . . . katika helo.”—Sura 1, aya 43.
Maelezo fulani husema: “Wale walio watenda dhambi mno katika maisha yao ya kidunia lazima wapitie adhabu za aina tofauti-tofauti katika sayari za kihelo.” Hata hivyo, kuna tofauti moja na mateso ya milele ya moto wa helo ya Jumuiya ya Wakristo: “Adhabu hii . . . si ya milele.” Basi, mateso ya Kihindu ni nini hasa?
45. Mateso ya helo ya Kihindu yanaelezwaje?
45 Yafuatayo ni maelezo juu ya yanayompata mtenda dhambi, yametwaliwa kutoka Markandeya Purana:
“Kisha wajumbe wake Yama [kijimungu cha wafu] humfunga upesi kwa vitanzi vya kuogopesha na kumburuta mpaka kusini, akitetemeka kwa mpigo wa ufito. Kisha huburutwa na wajumbe wa Yama kupitia nyanja zenye mikwaruzo pamoja na [mmea] Kusa, miiba, na vichuguu, pini na mawe, yakiwaka moto sehemu fulani fulani, zilizofunikwa na mashimo, yenye mwako wa joto la jua na mteketeo wa miale yalo, akipiga mayowe mabaya. Akiwa anaburutwa na wajumbe hao wenye kuogopesha na kuliwa na mamia ya mbweha, mtu huyo mtenda dhambi huiendea nyumba yake Yama kupitia njia yenye kuhofisha. . . .
“Mwili wake unapoteketezwa hupata hisi kali ya kuchomeka; na mwili wake unapopigwa au kukatwa anahisi maumivu makali.
“Mwili wake ukiwa umeharibiwa hivyo, kiumbe, ajapotembea kuingia katika mwili mwingine, hupatwa na huzuni ya milele kwa sababu ya vitendo vyake vibaya. . . .
“Halafu ili dhambi zake zisafishwe hupelekwa kwenye helo nyingine inayofanana na hiyo. Akiisha kupitia helo zote hizo mtenda dhambi huyo hutwaa maisha ya hayawani. Halafu kupitia maisha ya mabuu, wadudu, na mainzi, hayawani wa mawindo, chawa, tembo, miti, farasi, ng’ombe, na kupitia maisha mengine mbalimbali ya dhambi na yenye huzuni, yeye, akirejea kwenye jamii ya binadamu, huzaliwa akiwa kibiongo, au mtu mwenye sura mbaya au mbilikimo au Chandala Pukkasa.”
46, 47. Biblia husema nini juu ya hali ya wafu, na twaweza kufikia mikataa gani?
46 Linganisha hayo na yale ambayo Biblia husema juu ya wafu:
“Kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa. Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lo lote lililofanyika chini ya jua. Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu [Sheoli, NW] uendako wewe.”—Mhubiri 9:5, 6, 10.
47 Bila shaka, ikiwa kama Biblia isemavyo, binadamu hana nafsi bali ni nafsi, basi hakuna maisha ya kuwa na fahamu baada ya kifo. Hakuna raha, wala hakuna mateso. Mitatanisho yote isiyo ya akili ya “maisha ya baada ya kifo” inakwisha.d
Mshindani wa Uhindu
48, 49. (a) Kwa kupitia, ni nini baadhi ya mafundisho ya Kihindu? (b) Ni kwa nini wengine wametilia shaka kufaa kwa Uhindu? (c) Ni nani aliyetokea kupinga wazo la Kihindu?
48 Mapitio hayo mafupi ya lazima kuhusu Uhindu yameonyesha kwamba huo ni dini ya kuabudu miungu mingi kwa kutegemea ibada ya mungu mmoja—imani katika Brahman, Aliye Mkuu, chanzo, au asili, akiwakilishwa na silabi OM au AUM, na akiwa na nyuso au midhihirisho mingi. Pia huo ni dini inayofundisha kuvumiliana na hutia moyo fadhili kuelekea wanyama.
49 Kwa upande mwingine, sehemu fulani za fundisho la Kihindu, kama vile Karma na udhalimu wa mfumo wa kitabaka, pamoja na ibada ya sanamu na mapingano ya ngano, zimefanya watu fulani wanaofikiri watilie shaka kufaa kwa imani hiyo. Mmoja mwenye kushuku hivyo alitokea katika India ya kaskazini-mashariki yapata mwaka 560 K.W.K. Yeye alikuwa Siddhārtha Gautama. Yeye alisimamisha imani mpya iliyoshindwa kusitawi katika India lakini ikafanikiwa kwingineko, kama sura yetu ifuatayo itakavyofafanua. Imani mpya hiyo ilikuwa ni Dini ya Buddha.
[Maelezo ya Chini]
a Jina Uhindu ni ubuni wa watu wa Ulaya.
b Katika Sanskrit, “nafsi” mara nyingi hutafsiriwa kutoka ãtma, au ãtman, lakini “roho” ni tafsiri sahihi zaidi.—Ona A Dictionary of Hinduism—Its Mythology, Folklore and Development 1500 B.C.-A.D. 1500, ukurasa 31, na kijitabu Victory Over Death—Is It Possible for You? kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., katika 1986.
c Avatari la kumi na la wakati ujao ni lile la Kalki Avatara “anayeonyeshwa kwa picha kuwa kijana wa kupendeza aliyepanda farasi mkubwa mweupe pamoja na upanga ulio kama kimondo akimimina kifo na uharibifu pande zote.” “Kuja kwake kutaimarisha tena uadilifu kwenye dunia, na kurudi kwa enzi ya usafi na hali ya kutokuwa na hatia.”—Religions of India; A Dictionary of Hinduism.—Linganisha Ufunuo 19:11-16.
d Fundisho la Biblia la ufufuo wa wafu halina uhusiano wowote na fundisho la nafsi isiyoweza kufa. Ona Sura 10.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 100, 101]
Dini ya Sikh—Dini ya Kimapinduzi
Dini ya Sikh, ikiwakilishwa na panga tatu na duara, ni dini ya watu zaidi ya milioni 17. Walio wengi huishi katika Punjab. Golden Temple la Dini ya Sikh, lililojengwa katikati ya ziwa lililofanyizwa na wanadamu, liko katika Amritsar, jiji takatifu la Dini ya Sikh. Wanaume wa Dini ya Sikh hutambulika vyepesi kwa sababu ya vilemba vyao vya buluu, vyeupe, au vyeusi, kuvivaa kukiwa ni sehemu ya lazima ya zoea lao la kidini, sawa na vile kuachilia nywele zao ziwe ndefu.
Neno sikh katika Kihindi humaanisha “mwanafunzi.” Wafuasi wa Dini ya Sikh ni wanafunzi wa mwanzilishi wao, Guru Nānak, na wafuasi wa mafundisho ya waguru kumi (Nānak na waandamizi tisa) ambao maandishi yao yamo ndani ya kitabu kitakatifu cha Dini ya Sikh, Guru Granth Sahib. Dini hiyo ilianza karne ya 16 mapema wakati Guru Nānak alipotaka kutwaa mambo yaliyo mazuri zaidi ya Uhindu na Uislamu na kuunda dini yenye umoja.
Utume wa Nānak waweza kuelezwa kwa sentensi moja: “Kwa kuwa kuna Mungu mmoja tu, na Yeye ndiye Baba yetu; kwa hiyo, lazima sisi sote tuwe ndugu.” Kama vile Waislamu, wafuasi wa Dini ya Sikh huamini Mungu mmoja na hukataza matumizi ya sanamu. (Zaburi 115:4-9; Mathayo 23:8, 9) Wao hufuata mila ya Kihindu ya kuamini katika nafsi isiyoweza kufa, kutwaa umbo jingine, na Karma. Mahali pa ibada pa wafuasi wa Dini ya Sikh huitwa gurdwara.—Linganisha Zaburi 103:12, 13; Matendo 24:15.
Moja ya amri kubwa za Guru Nānak ilikuwa: “Sikuzote mkumbuke Mungu, liseme tena jina Lake.” Mungu anasemwa kuwa “Yeye wa Kweli,” lakini hapewi jina. (Zaburi 83:16-18) Amri nyingine ilikuwa ni “Shiriki unachochuma pamoja na wale waliopungukiwa.” Kwa kupatana na hilo kuna langar, au jiko lisilo la malipo, katika kila hekalu la Dini ya Sikh, ambako watu wa aina zote waweza kula bure. Hata kuna vyumba visivyo vya malipo ambako wasafiri waweza kulala usiku.—Yakobo 2:14-17.
Guru wa mwisho, Gobind Singh (1666-1708), alianzisha shirika la udugu wa wafuasi wa Dini ya Sikh liitwalo Khalsa, wanaofuata zinazojulikana kuwa K tano, ambazo ni: kesh, nywele zisizonyolewa, zikifananisha ukiroho; kangha, kichanuo katika nywele, kikifananisha utaratibu na nidhamu; kirpan, upanga, ukifananisha adhama, moyo mkuu, na kujidhabihu; kara, kikuku cha chuma cha pua, kikifananisha umoja pamoja na Mungu; kachh, kaptura zinazovaliwa kuwa vazi la ndani, kutoa wazo la kiasi na huvaliwa kufananisha kizuizi cha kiadili.—Ona The Encyclopedia of World Faiths, ukurasa 269.
[Picha]
Golden Temple la Dini ya Sikh, Amritsar, Punjabi India
[Picha]
Kilemba cha buluu hufananisha akili iliyo pana kama anga, isiyoachia nafasi ya chuki isiyo na sababu
Kilemba cheupe humaanisha mtu mtakatifu anayeishi maisha yaliyo kielelezo chema
Kilemba cheusi ni kikumbusho cha kunyanyaswa kwa wafuasi wa Dini ya Sikh walikofanyiwa na Waingereza katika 1919
Rangi nyinginezo ni kutegemea ladha ya mtu
[Picha]
Katika wonyesho wa kisherehe kuhani wa Dini ya Sikh asimulia historia ya silaha takatifu
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 104]
Dini ya Jaini—Kujikana na Kutofanya Jeuri
Dini hii, pamoja na kifananishi chayo cha swastika cha India kilicho cha kale, ilianzishwa katika karne ya sita K.W.K. na mwana-mfalme Mhindi aliyekuwa tajiri Nataputta Vardhamāna, anayejulikana vizuri zaidi kuwa Vardhamana Mahāvīra (mtajo rasmi unaomaanisha “Mwanamume Mkubwa” au “Shujaa Mkubwa”). Aligeukia maisha ya kujikana na kujinyima raha. Alifunga safari akiwa uchi atafute maarifa “kupitia vijiji na nyanda za India ya kati akiwinda uhuru wa mrudio wa kuzaliwa, kifo, na kuzaliwa tena.” (Man’s Religions, cha John B. Noss) Yeye aliamini kwamba wokovu wa nafsi ungeweza kupatikana tu kupitia kujikana mno na kujitia nidhamu na kufuatia sana ahimsa, kutofanyia viumbe vyote jeuri. Alifuatia ahimsa mno kufikia kadiri ya kubeba ufagio mwororo ambao kwao angeweza kufagia polepole wadudu wowote ambao wangeweza kuwa katika njia yake. Staha yake kwa ajili ya uhai ilikuwa pia kulinda utakato na ukamilifu wa nafsi yake mwenyewe.
Wafuasi wake leo, katika jitihada ya kufanya Karma yao iwe bora zaidi, huishi maisha kama hayo ya kujikana na hustahi viumbe wengine wote. Mara tena twaona matokeo yenye nguvu kwenye maisha za kibinadamu kuhusu imani ya kutoweza kufa kwa nafsi ya kibinadamu.
Leo kuna waumini wa imani hii wachache zaidi ya milioni nne, na walio wengi wamo Bombay na maeneo ya Gujarati ya India.
[Picha]
Mfuasi wa Dini ya Jaini akiabudu kwenye miguu ya mfano wenye urefu wa meta 17 wa mtakatifu Gomateswara katika Karnataka, India
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 106, 107]
Kiongozi Sahili cha Istilahi za Kihindu
ahimsa (Sanskrit, ahinsa)—kutofanya jeuri; kutoumiza wala kuua chochote. Msingi wa Wahindu kula mboga na kuheshimu wanyama
ashram—kihekalu au mahali ambapo guru (kiongozi wa kiroho) hufundisha
ātman—roho; hushirikishwa na kile kisichoweza kufa. Mara nyingi hutafsiriwa kimakosa kuwa nafsi. Ona jīva
avatar—udhihirisho au maisha katika umbo jingine la kiabudiwa cha Kihindu
bhakti—ujitoaji kwa mungu fulani ambao huongoza kwenye wokovu
bindi—kidoa chekundu ambacho wanawake walioolewa hupaka kwenye kipaji cha uso
Brahman—daraja la kikuhani na la juu zaidi la kitabaka; pia Nafsi ya Upeo. Ona ukurasa 116
dharma—sheria ya upeo ya vitu vyote; kile kinachoamua uhaki au ukosa wa vitendo
ghat—njia ya ngazi ya jukwaa kando ya mto
guru—mfundishaji au kiongozi wa kiroho
Harijan—mshiriki wa tabaka la Wasiopasa Kuguswa; humaanisha “watu wa Mungu,” jina la huruma walilopewa na Mahatma Gandhi
japa—ibada ya Mungu kwa kurudia moja la majina yake; mala, au tasbihi ya shanga 108, hutumiwa kutunza hesabu
jīva (au prān, prāni)—nafsi ya kipekee au mtu
Karma—kanuni ya kwamba kila kitendo kina matokeo mema na mabaya kwa ajili ya maisha yatakayofuata ya nafsi iliyohama
Kshatriya—jamii tarazaki, yenye kuongoza, na ya wapigaji vita na daraja la pili la mfumo wa kitabaka
mahant—mwanamume mtakatifu au mfundishaji
mahatma—Mtakatifu Mhindu, kutoka kwa maha, wa juu au mkubwa, na ātman, roho
mantra—mbinu fulani takatifu, inayoaminiwa kuwa na nguvu za kimizungu, hutumiwa katika kwenda jando la faraka na hurudiwa katika sala na tabano
maya—ulimwengu ni hadaa
moksha, au mukti—achilio kutoka kwa mrudio wa kuzaliwa tena; mwisho wa safari ya nafsi. Hujulikana pia kuwa Nirvana, kuungana kwa mtu na Aliye Mkuu, Brahman
OM, AUM—kiwakilishi cha neno kinachowakilisha Brahman kinachotumiwa kwa ajili ya kutafakari; sauti inayoonwa kuwa mtetemo wa kifumbo; hutumiwa kuwa mantra takatifu
paramatman—Roho-ulimwengu, ātman ya ulimwengu wote mzima, au Brahman
puja—ibada
sadhu—mwanamume mtakatifu; mjinyimaji raha au mtu wa kutafakari
samsara—kuhama kwa nafsi ya milele, isiyopotea
Shakti—nguvu za kike au mke wa kijimungu fulani, hasa mwandamizi wake Siva
sraddha—sherehe za maana zinazofanywa kwa kuheshimu wazazi wa kale waliokufa na kusaidia nafsi zilizoondoka zifikie moksha
Sudra—mfanya kazi ngumu, tabaka la chini zaidi la yale manne.
swami—mfundishaji au daraja la juu zaidi la kiongozi wa kiroho
tilak—kialama kwenye kipaji cha uso kinachofananisha kutunza kumbukumbu la Bwana katika vitendo vyake vyote
Trimurti—Utatu wa Kihindi wa Brahma, Vishnu, na Siva
Upanishads—maandishi matakatifu ya kishairi ya mapema ya Uhindu. Pia yajulikana kuwa Vedanta, mwisho wa Vedas
Vaisya—jamii ya wafanya biashara na wakulima; kikundi cha tatu katika mfumo wa kitabaka
Vedas—maandishi matakatifu ya kishairi ya mapema zaidi ya Uhindu
Yoga—kutokana na shina yuj, kumaanisha kuunganisha au kufunga nira pamoja; lahusu kuunganisha binadamu na mtu wa kimungu wa ulimwengu wote mzima. Hujulikana na wengi kuwa ile nidhamu ya kutafakari inayohusu kudhibiti kikao cha mwili na upumuaji. Uhindu hutambua angalau Yoga au njia nne kubwa-kubwa. Ona ukurasa 110
[Picha]
Kutoka kushoto, mahant Mhindu; sadhu, amesimama akitafakari; guru kutoka Nepal
[Sanduku katika ukurasa wa 110]
Njia Nne za Kufikia Moksha
Imani ya Uhindu hutoa angalau njia nne za kufikia moksha, au kukombolewa kwa nafsi. Hizi zajulikana kuwa yogas au margas, vijia vya kufikia moksha.
1. Karma Yoga—“Njia ya tendo, au karma yoga, nidhamu ya kitendo. Kwa msingi, karma marga humaanisha mtu kutenda dharma yake kulingana na mahali pa mtu katika maisha. Watu wote watakwa kutimiza wajibu fulani, kama vile ahimsa na kujiepusha na kileo na nyama, lakini dharma hususa ya kila mtu hutegemea tabaka la mtu huyo na hatua ya maendeleo katika maisha yake.”—Great Asian Religions.
Karma hii hufanywa kwa kufuatia kabisa mipaka ya kitabaka. Utakato wa tabaka hudumishwa kwa kutofunga ndoa wala kula nje ya tabaka la mtu, lililoamuliwa na Karma ya mtu wakati wa maisha yaliyotangulia. Kwa hiyo tabaka la mtu halionwi kuwa udhalimu bali urithi kutoka maisha yaliyotangulia katika umbo jingine. Katika falsafa ya Kihindu wanaume na wanawake hawalingani. Wao hugawanywa na tabaka na jinsia na, kwa kweli, na rangi. Kwa kawaida kadiri ngozi ilivyo nyeupe zaidi, ndivyo tabaka linavyokuwa la ngazi ya juu zaidi.
2. Jnana Yoga—“Njia ya Maarifa, au jnana yoga, nidhamu ya maarifa. Kwa kutofautisha na njia ya tendo, karma marga, pamoja na wajibu wayo uliopendekezwa nalo kwa ajili ya kila pindi maishani, jnana marga hutokeza njia ya kifalsafa na ya kisaikolojia ya kujijua binafsi na ulimwengu wote mzima. Kuwapo, si kutofanya, ndiko ufunguo wa kufikia jnana marga. [Italiki ni zetu.] La maana zaidi, njia hii hufanya moksha iwezekane katika maisha haya kwa ajili ya wale wanaoizoea.” (Great Asian Religions) Inahusisha yoga ya kujielekezea fikira na kujitenga na ulimwengu na zoea la kujinyima raha. Ni wonyesho wa kujidhibiti na kujikana.
3. Bhakti Yoga—“Namna ya pokeo la Kihindu leo yenye kupendwa kabisa na wengi. Hii ndiyo njia ya ujitoaji, bhakti marga. Kwa kutofautisha na karma marga . . . njia hii ni rahisi zaidi, ya hiari zaidi, na yaweza kufuatwa na watu wa tabaka lolote, jinsia, au umri . . . . Huruhusu hisia-moyo na tamaa za kibinadamu zijidhihirishe badala ya kuzishinda kwa maisha ya yoga ya kujinyima raha . . . Hutia ndani kujitoa kabisa kwa watu wa kimungu.” Na kwa kawaida kuna milioni 330 wa kuheshimu mno. Kulingana na kawaida hiyo, kujua ni kupenda. Kwa kweli, bhakti humaanisha “ufungamano wa kihisia-moyo wa kijimungu chenye kuchaguliwa na mtu.”—Great Asian Religions.
4. Raja Yoga—Mbinu fulani ya “vikao vya mwili maalumu, mbinu za kupumua, na kurudia sawasawa taratibu za kuwaza zinazofaa.” (Man’s Religions) Ina hatua nane.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 113]
Mahatma Gandhi na Mfumo wa Matabaka
“Kutotumia jeuri ndilo sharti la kwanza la imani yangu. Pia ndilo sharti la mwisho la kanuni yangu ya imani.”—Mahatma Gandhi, Machi 23, 1922.
Mahatma Gandhi, anayejulikana sana kwa ajili ya uongozi wake usio wa kutumia jeuri katika kupata uhuru wa India kutoka kwa Uingereza (ulitolewa katika 1947), pia alijishughulisha kufanya hali ya mamilioni ya Wahindu wenzake kuwa nafuu. Ni kama Profesa M. P. Rege Mhindi anavyofafanua: “Yeye alitangaza ahimsa (kutotumia jeuri) kuwa kanuni ya msingi ya kiadili, ambayo alifasiri kuwa kuhangaikia adhima na hali njema ya kila mtu. Yeye alikataa mamlaka ya maandiko ya Kihindu wakati fundisho layo lilipopingana na ahimsa, kwa ushujaa alijitahidi kukomesha sera ya mfumo wa matabaka ya viongozi wa kidini, akasitawisha usawa wa wanawake katika sehemu zote za maisha.”
Maoni ya Gandhi yalikuwa nini juu ya hali ya Wasiopasa Kuguswa? Katika barua aliyomwandikia Jawaharlal Nehru, ya tarehe 2, Mei, 1933, aliandika hivi: “Chama cha Harijan hakizuiwi na harakati ya majadiliano tu. Hakuna kitu kibaya zaidi ya hicho ulimwenguni. Na hali siwezi kuacha dini na kwa hivyo Uhindu. Maisha yangu yangekuwa ni mzigo kama Uhindu haungenifaa. Napenda Ukristo, Uislamu na imani nyingine nyingi kupitia Uhindu. . . . Lakini siwezi kuuvumilia ukiwa na [sera ya] wasiopasa kuguswa.”—The Essential Gandhi.
[Picha]
Mahatma Gandhi (1869-1948), kiongozi na mfundishaji Mhindu wa ahimsa mwenye kuheshimiwa mno
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 116, 117]
Uhindu—Baadhi ya Vijimungu na Vijimungu-Vike
Aditi—mama ya vijimungu; kijimungu-kike cha anga; Kisicho na Kikomo
Agni—kijimungu cha moto
Brahma—Mungu Muumba, kanuni ya uumbaji katika ulimwengu wote mzima. Mmoja wa vijimungu vya Trimurti (utatu)
Brahman, au Brahm—mtu aliye Mkuu Kabisa wa ulimwengu wote mzima, aliye kila mahali, anayewakilishwa na sauti OM au AUM. (Ona kiwakilishi juu.) Pia hurejezewa kuwa Atman. Wahindu fulani humwona Brahman kuwa Kanuni ya Kimungu isiyo na utu au Nafsi ya Upeo
Buddha—Gautama, mwanzilishi wa Dini ya Buddha; Wahindu humwona kuwa maisha ya Vishnu katika umbo jingine (avatar)
Durga—mke au Shakti wa Siva na hutambulishwa na Kali
Ganesa (Ganesha)—mungu-mwana wa Siva mwenye kichwa cha tembo, Bwana wa Vipingamizi, kijimungu cha bahati njema. Pia huitwa Ganapati na Gajanana
Ganga—kijimungu-kike, mmoja wa wake zake Siva na tashihishi ya mto Ganges
Hanuman—kijimungu-tumbili na kifuasi kilichojitoa cha Rama
Himalaya—makao ya theluji, baba ya Parvati
Kali—mwandamizi (Shakti) mweusi wa Siva na kijimungu-kike cha uharibifu chenye kiu ya damu. Mara nyingi huonyeshwa taswira kikiwa na ulimi mkubwa mwekundu unaoning’inia
Krishna—umbo la Vishnu la nane la michezo-michezo na kijimungu cha Bhagavad Gita. Wapenzi wacho walikuwa ni gopis, au wanawali wa maziwa
Lakshmi—kijimungu-kike cha urembo na bahati njema; kiandamizi cha Vishnu
Manasa—kijimungu-kike cha nyoka
Manu—mzazi wa kale wa jamii ya kibinadamu; aliyeokolewa na samaki mkubwa kutoka uharibifu wa furiko
Mitra—kijimungu cha nuru. Kwa Waroma kilijulikana kuwa Mithras
Nandi—fahali, mchukuzi wa Siva au kisafirishi chake
Nataraja—Siva kikiwa katika kikao cha kucheza dansi kimezungukwa na pete ya mialimoto
Parvati au Uma—kijimungu-kike kiandamizi cha Siva. Picha hutwaa umbo la Durga au Kali
Prajapati—Muumba wa ulimwengu wote mzima, Bwana wa Viumbe, baba ya vijimungu, mashetani, na viumbe vingine vyote. Baadaye chajulikana kuwa Brahma
Purusha—mtu wa ulimwengu. Yale matabaka makubwa manne yalifanyizwa kutokana na mwili wacho
Radha—kiandamizi cha Krishna
Rama, Ramachandra—umbo la saba la kijimungu Vishnu. Utenzi unaosimulia Ramayana hueleza hadithi ya Rama na mkeye Sita
Saraswati—kijimungu-kike cha maarifa na kiandamizi cha Brahma Muumba
Shashti—kijimungu-kike kinacholinda wanawake na watoto wakati wa kuzaa
Siva—kijimungu cha mrutubisho, kifo, na uharibifu; kishiriki cha Trimurti. Hufananishwa na mkuki wenye vyembe vitatu
Soma—kijimungu pia dawa ya kulevya; dawa ya kurefusha uhai
Vishnu—kijimungu kinachohifadhi uhai; kishiriki cha tatu cha Trimurti
[Hisani]
(Imetegemea mworodhesho katika Mythology—An Illustrated Encyclopedia)
[Picha]
Kutoka juu kushoto, kisaa, Nataraja (Siva mcheza dansi), Saraswati, Krishna, Durga (Kali)
[Sanduku katika ukurasa wa 120]
Hekaya ya Kihindu Juu ya Furiko
“Asubuhi walimletea Manu [mzazi wa kale wa ainabinadamu na mtoa-sheria wa kwanza] maji ya kuoga . . . Alipokuwa akikoga, samaki mmoja [Vishnu katika umbo lake akiwa Matsya] akaingia mikononi mwake.
“Akamwambia neno hili, ‘Nilee, mimi nitakuokoa wewe!’ ‘Utaniokoa mimi kutoka nini?’ ‘Furiko litafagia viumbe vyote hivi: mimi nitakuokoa wewe kwalo!’ ‘Nikuleeje?’”
Samaki huyo akamwagiza Manu jinsi ya kumtunza. “Kisha akasema, ‘Katika mwaka fulani na fulani furiko hilo litakuja. Ndipo wewe utanihudumia (kwa ushauri wangu) kwa kutayarisha merikebu; na furiko hilo likiisha tokea wewe utaingia ndani ya merikebu hiyo, nami nitakuokoa wewe kwalo.’”
Manu alifuata maagizo ya samaki huyo, na wakati wa furiko hilo samaki huyo akaiburuta merikebu hiyo mpaka kwenye “mlima wa kaskazini. Ndipo akasema, ‘Mimi nimekuokoa wewe. Tia nanga merikebu kwenye mti; lakini usiruhusu maji yakukatilie mbali, ukiwa ungali juu ya mlima. Maji yapunguapo, wewe waweza kuteremka polepole!’”—Satapatha-Brahmana; linganisha Mwanzo 6:9–8:22.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 123]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Ganges watiririka kilometa zaidi ya 2,400 kutoka Himalayas mpaka Calcutta na delta yao katika Bangladesh
INDIA
Calcutta
Mto Ganges
[Picha]
Ganga Ma, juu ya kichwa cha Siva, wateremka kupitia nywele zake
Wahindu waabudu kwenye kijia cha ngazi, wakioga katika Ganges kwenye Varanasi, au Benares
[Picha katika ukurasa wa 96]
Ganesa, kijimungu-kichwa-tembo cha Kihindu chenye jaha njema, mwana wake Siva na Parvati
[Picha katika ukurasa wa 99]
Lingam (viwakilisho vya uume) zinazoheshimiwa mno na Wahindu. Siva (kijimungu cha mrutubisho) kimo ndani ya lingam moja nacho kina vichwa vinne kuzunguka kimoja na chenzake
[Picha katika ukurasa wa 108]
Watawa wa kike wafuasi wa Dini ya Jaini wamevaa mukha-vastrika, au kiziba-kinywa, kinachozuia wadudu wasiingie na kuuawa
[Picha katika ukurasa wa 115]
Ibada ya nyoka, inayozoewa hasa katika Bengali. Manasa ndicho kijimungu-kike cha nyoka
[Picha katika ukurasa wa 118]
Vishnu, pamoja na mke wacho Lakshmi, juu ya mapindo ya joka Ananta pamoja na Brahma chenye vichwa vinne juu ya yungiyungi inayomea kutoka kitovu cha Vishnu