Je! Umepata Kujiuliza?
KUKIWA na mamia ya dini, madhehebu na vidhehebu ulimwenguni leo, waweza kutambuaje dini inayokubaliwa na Mungu? Huenda ionekane kama kutafuta sindano katika rundo la nyasi kavu. Lakini je, unahitaji kuchunguza rundo hilo la nyasi unyasi kwa unyasi? La. Waweza kutumia utaratibu wa uondoaji. Neno la Mungu, Biblia, hutenda kama sumaku ambayo hukusaidia kutambulisha hiyo “imani moja.”—Waefeso 4:5.
Katika toleo la awali la gazeti hili, chini ya kichwa “Je! Umepata Kujiuliza” (Januari 8, 1994 ukurasa 13), tulizungumzia lile swali la nafsi isiyoweza kufa. Kwa kutumia usababu wa Kibiblia, tulithibitisha kwamba mwanadamu hana nafsi isiyoweza kufa ambayo hubarikiwa au huteseka baada ya kifo. (Mhubiri 9:5, 10; Ezekieli 18:4) Tukiwa na kweli hiyo sahili, tunaweza kuondoa dini yoyote ambayo hufunza kwamba mwanadamu ana nafsi isiyoweza kufa. Hilo laacha dini chache mno katika utafutaji wetu wa ile dini inayokubaliwa na Mungu. Kwa hiyo acheni tutumie maswali kadhaa zaidi ambayo yaweza kutusaidia kupunguza orodha hata zaidi, kisahili, kwa kuangalia na kusababu juu ya Maandiko yaliyoonyeshwa chini.
1. Je, ibada ya kweli ingeweza kukweza, kutukuza, na kuheshimu kupita kiasi viongozi wa kidini wa kibinadamu, hata kwa kuwapa vyeo visivyo vya kimaandiko?—Zaburi 96:5-7; Mathayo 23:6-12; 1 Wakorintho 3:5-9.
2. Je, dini ya kweli yapaswa kuwa na kazi zenye kutokeza faida, hivi kwamba viongozi wayo wanaweza kuishi kwa anasa?—Mathayo 6:19-21; Yakobo 2:1-4; 5:1-3.
3. Je, dini ya kweli yapaswa kutambulishwa kutokana na fundisho moja (kama vile Baptisti, Pentekoste), kutokana na vyanzo vyayo ya kijiografia (kama vile Kiroma, la Kusini, Kanisa la Uingereza), kutokana na mwanzilishi wayo asiye mkamilifu (Luther, Calvin, Wesley) au kutokana na aina ya kanuni wanayotumia (kama vile Presbyterian, Episkopali, Congregational)?—Isaya 43:10, 12; Matendo 11:26.
4. Je, ibada ya kweli ingejaribu kuficha au kubadili jina la Mungu lililofunuliwa?—Isaya 12:4, 5; Mathayo 6:9; Yohana 17:26.
5. (a) Dini ya kweli yapaswa kuionaje Biblia? (Zaburi 119:105; Luka 24:44, 45; Warumi 15:4; 2 Timotheo 3:14-16) (b) Yapaswa kuyaonaje yale mafunuo yaitwayo eti ya baada ya Biblia?—Wagalatia 1:8, 9.
6. Waabudu wa kweli wanaelekeza uangalifu kwa ajili ya wokovu wao kwenye nini na kwa nani?—Zaburi 27:1; Mathayo 6:33; Warumi 16:25-27; 1 Wakorintho 15:27, 28; Ufunuo 11:15.
7. Ni mwenendo wa aina gani ambao dini ya kweli yapaswa kutokeza kama tokeo la mafundisho yayo?—Mathayo 22:37-40; Waefeso 4:23-29; linganisha Wagalatia 5:19-21 na 5:22, 23.
8. Je, udugu wa ulimwenguni pote wa waabudu wa kweli wa Mungu ungejihusisha katika siasa zenye kugawanya na utukuzo wa taifa?—Danieli 2:44; 7:14; Yohana 18:36; Warumi 16:17; 1 Wakorintho 1:10.
9. Je, ibada inayokubaliwa na Mungu ingeruhusu ushiriki katika vita na mauaji ya kijamii au ya kikabila?—Kutoka 20:13; Isaya 2:2-4; Yohana 13:34, 35.
10. Ni nani leo ulimwenguni pote waonyeshao upendo wa kweli wa Kikristo? Ambao hawagawanywi na siasa, jamii, au utukuzo wa taifa? Ambao hawatukuzi viongozi wa kibinadamu? Ambao hawatumii watu ili kupata utajiri au cheo? Ambao hawashiriki katika vita? Ambao wana jina la Kibiblia? Ambao wanatetea utawala wa Ufalme wa Mungu kuwa suluhisho lenye kudumu la matatizo ya wanadamu?—Isaya 43:10, 12.
Je! Umepata Kujiuliza? Majibu ya Biblia
Yafuatayo ni baadhi ya maandiko yaliyoorodheshwa na maswali yaliyo kwenye ukurasa 20:
1. “Hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi. Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.”—Mathayo 23:6-12.
2. “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu wala nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.” (Mathayo 6:19-21) “Haya basi, enyi matajiri! lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto.”—Yakobo 5:1-3.
3. “Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi wangu niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye.” (Isaya 43:10) “Ilikuwa kwanza katika Antiokia kwamba wanafunzi kwa uongozi wa kimungu waliitwa Wakristo.”—Matendo 11:26, New World Translation.
4. “Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake; yatangazeni matendo yake kati ya mataifa, litajeni jina lake kuwa limetukuka. . . . Yajulikane haya katika dunia yote.” (Isaya 12:4, 5) “Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe.”—Mathayo 6:9.
5. (a) “Tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki.” (2 Timotheo 3:15, 16) (b) “Ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe.”—Wagalatia 1:8.
6. “Basi, fulizeni kutafuta kwanza ufalme na uadilifu wake, na vitu vingine vyote hivi mtaongezwa.” (Mathayo 6:33, NW) “Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele.”—Ufunuo 11:15)
7. “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. . . . Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.” (Mathayo 22:37-40) “Matunda ya roho ni upendo, shangwe, amani, ustahimilivu, fadhili, wema, imani, upole, kujidhibiti. Dhidi ya mambo ya namna hiyo hakuna sheria yoyote.”—Wagalatia 5:22, 23, NW.
8. “Yesu akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.”—Yohana 18:36.
9. “Usiue.” (Kutoka 20:13) “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”—Yohana 13:34, 35.
10. “Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye. . . . Kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, nami ni Mungu.”—Isaya 43:10, 12.