Sanamu
Maana: Viwakilishi vinavyoonekana vya watu au vitu. Wale wanaoabudu sanamu mara nyingi husema kwamba wanamwabudu roho anayewakilishwa na sanamu hiyo. Dini nyingi zisizo za Kikristo hutumia sanamu. Kuhusu desturi ya Kanisa Katoliki, New Catholic Encyclopedia (1967, Buku la 7, uku. 372) husema hivi: “Kwa kuwa mtu anapoabudu sanamu huwa anamwabudu mtu anayewakilishwa na sanamu hiyo, vivyo hivyo ibada anayostahili mtu huyo inaweza kutolewa kwa sanamu inayomwakilisha.” Hilo si fundisho la Biblia.
Neno la Mungu husema nini kuhusu kutengeneza sanamu zinazoabudiwa?
Kut. 20:4, 5, UV: “Usijifanyie sanamu ya kuchongwa wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; [“usijiiname mbele yao kuzitumikia,” ZSB]. Kwa kuwa, mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.” (Italiki zimeongezwa.) (Ona kwamba walikatazwa kufanya sanamu na kuinama mbele yake.)
Law. 26:1, UV: “Msifanye sanamu yoyote, wala msijisimamishie sanamu ya kuchonga, wala mnara [“nguzo takatifu,” NW], wala msiweke jiwe lolote lililochorwa katika nchi yenu ili kulisujudia; kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.” (Sanamu yoyote ambayo watu wangeinama ili kuiabudu haikupaswa kusimamishwa kamwe.)
2 Kor. 6:16, UV: “Pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai.”
1 Yoh. 5:21, UV: “Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu [“sanamu,” ZSB; “sanamu za miungu,” BHN, VB; “miungu ya sanamu,” NAJ].”
Je, tunaweza kumwabudu Mungu wa kweli kupitia sanamu?
Yoh. 4:23, 24, UV: “Waabudu halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” (Wale wanaomwabudu Mungu kupitia sanamu hawamwabudu “katika roho” bali kupitia kitu wanachoweza kuona kwa macho yao.)
2 Kor. 5:7, UV: “Twaenenda kwa imani, si kwa kuona.”
Isa. 40:18, UV: “Mtamlinganisha Mungu na nani? Au mtamfananisha na mfano wa namna gani?”
Mdo. 17:29, UV: “Basi kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu.”
Isa 42:8, UV: “Mimi ni BWANA; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu [“sanamu ya kuchonga,” ZSB] sifa zangu.”
Je, “watakatifu” wanaweza kutuombea kwa Mungu, na je, tunaweza kutumia sanamu zao katika ibada yetu?
Mdo. 10:25, 26, UV: “Petro alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguuni, akamsujudia. Lakini Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu.” (Ikiwa Petro mwenyewe hakukubali kuabudiwa, je, angetutia moyo tupige magoti mbele ya sanamu yake? Ona pia Ufunuo 19:10.)
Yoh. 14:6, 14, UV: “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.” (Yesu anasema waziwazi kwamba tunaweza kumfikia Baba kupitia kwake tu na kwamba tunapaswa kuomba kwa jina lake.)
1 Tim. 2:5, UV: “Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Yesu Kristo.” (Wengine hawawezi kuwa wapatanishi kwa ajili ya washiriki wa kutaniko la Kristo.)
Ona pia kurasa 406, 407, chini ya kichwa “Watakatifu.”
Je, wanaotumia sanamu humwabudu mtu anayewakilishwa, au baadhi ya sanamu huonwa kuwa muhimu kuliko nyingine?
Ni muhimu kufikiria maoni ya waabudu. Kwa nini? Jinsi ambavyo sanamu hutumiwa ndiyo huamua iwapo ni ibada ya sanamu au la.
Akilini mwa mwenye kuabudu, je, sanamu moja ya mtu fulani ni muhimu kuliko sanamu nyingine ya mtu huyohuyo? Ikiwa ndivyo, sanamu hiyo ndiyo inayoabudiwa, wala si mtu anayewakilishwa. Kwa nini watu hufunga safari ndefu kwenda kuabudu katika mahekalu hususa? Je, sanamu zenyewe sizo zinazoonwa kuwa na nguvu za “kimwujiza”? Kwa mfano, katika kitabu Les Trois Notre-Dame de la Cathédrale de Chartres, cha mtawa Yves Delaporte, tunaambiwa hivi kuhusu sanamu za Maria katika kanisa kuu huko Chartres, Ufaransa: “Sanamu hizo, zilizochongwa, zilizochorwa au zinazoonekana katika madirisha ya vioo vyenye rangi mbalimbali, hazilingani kwa umaarufu. . . . Sanamu tatu tu ndizo huabudiwa hasa: Our Lady of the Crypt, Our Lady of the Pillar, na Our Lady of the ‘Belle Verriere.’” Lakini ikiwa waabudu wangekuwa wakimwabudu hasa mtu anayewakilishwa na sanamu hizo, hakungekuwa na tofauti yoyote kati ya sanamu hizo, sivyo?
Mungu anazionaje sanamu zinazoabudiwa?
Yer. 10:14, 15, VB: “Kila fundi anaona haya kwa ajili ya sanamu yake. Maana sanamu zake ni udanganyifu tu, hamuna pumzi ndani yake. Hazina maana, ni vitu vya kuchekesha.”
Isa. 44:13-19, UV: “Seremala hunyosha uzi; huiandika kwa kalamu ya mate; huitengeneza kwa randa, huiandika kwa bikari, huifanza kwa mfano wa mwanadamu, sawasawa na uzuri wa mwanadamu, ili ikae nyumbani. Yeye hujikatia mierezi, hutwaa mtiriza, na mwaloni, hujichagulia mti mmoja katika miti ya msituni; hupanda mvinje, mvua ikausitawisha. Kisha utamfaa mwanadamu kwa kuni; hutwaa kipande, akaota moto; naam, huuwasha moto, akaoka mkate; naam, huufanya mungu, akauabudu; huifanya sanamu ya kuchonga, akaisujudia. Sehemu moja huiteketeza; kwa sehemu nyingine hula nyama; huoka chakula kiokwacho, akashiba; naam, huota moto, akasema, Aha, nimeota moto, nimeona moto; na kwa sehemu iliyobakia hufanya mungu, yaani, sanamu yake ya kuchonga; husujudu mbele yake akaiabudu, akaiomba, akasema, Uniokoe; maana wewe u mungu wangu. Hawajui wala hawafikiri; maana umewafumba macho, wasione, na mioyo yao, wasiweze kufahamu. Wala hapana atiaye moyoni, wala hapana maarifa, wala fahamu kusema, Nimeteketeza sehemu motoni, naam, pia nimeoka mkate juu ya makaa yake; nimeoka nyama nikaila; nami, je! Kilichobaki nikifanye kuwa chukizo? Je! nisujudie shina la mti?”
Eze. 14:6, UV: “Bwana Mungu asema hivi; Rudini ninyi, mkageuke na kuviacha vinyago vyenu [“sanamu zenu za mavi,” NW]; mkageuze nyuso zenu zisielekee machukizo yenu yote.”
Eze. 7:20, UV: “Uzuri wa pambo lake, yeye aliuweka katika enzi, lakini wao walifanya sanamu za machukizo yao, na vitu vyao vichukizavyo, ndani yake; ndiyo maana nimeifanya kuwa kama kitu cha unajisi kwao [“kitu kichafu,” ZSB; “vitu vya kuwachukiza,” VB] kwao.”
Tunapaswa kuzionaje sanamu ambazo huenda tumekuwa tukiziabudu?
Kum. 7:25, 26, UV: “Sanamu za kuchonga za miungu yao mtaziteketeza kwa moto; usitamani fedha wala dhahabu iliyo juu yao, wala usiitwae iwe yako usije ukanaswa nayo; kwa maana ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako; na machukizo usitie ndani ya nyumba yako, usije wewe kuwa kitu cha haramu mfano wake; ukichukie kabisa, na kukikataa kabisa [“kinai kitu hicho na kukichukia kabisa,” NW].” (Ingawa watu wa Yehova leo hawajaamriwa waharibu sanamu za watu wengine, amri hii ambayo Waisraeli walipewa inaonyesha jinsi wanavyopaswa kuziona sanamu zozote walizo nazo ambazo huenda wamekuwa wakiabudu. Linganisha na Matendo 19:19.)
1 Yoh. 5:21, UV: “Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu [“sanamu za miungu,” BHN, VB].”
Eze. 37:23, UV: “Wala hawatajitia uchafu tena kwa vinyago [“sanamu,” VB, ZSB; “sanamu za miungu,” BHN] vyao . . . Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.”
Kutumia sanamu katika ibada kunaweza kuathiri jinsi gani wakati wetu ujao?
Kum. 4:25, 26, UV: “Mkajiharibu, na kufanya sanamu ya kuchonga kwa umbo la kitu cho chote, mkafanya ambayo ni maovu machoni pa BWANA, Mungu wako, na kumtia hasira; nawashuhudizia mbingu na nchi hivi leo, . . . mtaangamizwa kabisa.” (Maoni ya Mungu hayajabadilika. Ona Malaki 3:5, 6.)
1 Kor. 10:14, 20, UV: “Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu. . . . Vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani.”
Ufu. 21:8, UV: “Waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”
Zab. 115:4-8, UV: “Sanamu zao ni fedha na dhahabu, kazi ya mikono ya wanadamu. Zina vinywa lakini hazisemi, zina macho lakini hazioni, zina masikio lakini hazisikii, zina pua lakini hazisikii harufu, mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, wala hazitoi sauti kwa koo zake. Wazifanyazo watafanana nazo, kila mmoja anayezitumainia.”