Je, Unaweza Kufa kwa Mvunjiko wa Moyo?
KWA KUSIKITISHA, kifo kisababishwacho na mvunjiko wa moyo ni cha kawaida: Mtu mzee-mzee aliyeonekana kuwa na afya aliyempoteza mwenzi wa ndoa katika kifo azimia tu na kufa mnamo siku au majuma kadhaa baadaye. Kisababishi cha kifo ni nini? “Mvunjiko wa moyo,” wakasema marafiki.
Huu huenda ukawa zaidi ya usemi wa kitamathali. Watafiti wamejua kwa muda mrefu kwamba mkazo ikiwa hujaondolewa humimina kemikali katika moyo ambazo zaweza kusababisha moyo upige isivyo kawaida na hata mipigo ya kasi mno. Lakini utaratibu huu jinsi unavyoanza katika ubongo imebaki kuwa fumbo.
Stephen M. Oppenheimer, tabibu wa ubongo katika shule ya kitiba kwenye Chuo Kikuu cha Johns Hopkins katika Baltimore, Maryland, Marekani, aamini ametambulisha sehemu ya ubongo inayounganisha moyo na hisia-moyo. Koteksi-unganishi ni sehemu ndogo ya ubongo mahali ambapo mfumo wa neva zinazojiendesha, ambao huelekeza utendaji kama vile kupumua na mpigo wa moyo, hukutana na mfumo wa hisi, ambao hushughulikia hisia-moyo, kama vile hasira, hofu, na furaha. Dakt. Oppenheimer alipata kwamba utendeshaji wa koteksi-unganishi katika panya ulitokeza madhara ya misuli ya moyo sawa na yale yatokeayo kwa wanadamu wenye mpigo wa ghafula wa moyo. Kutendesha koteksi-unganishi katika wanadamu pia kumeonyesha kutokeza mabadiliko katika kiwango cha mpigo wa moyo na msongo wa damu. Uchunguzi huu wadokeza kwamba kwa hakika yawezekana kufa kutokana na mvunjiko wa moyo.
Wengine husema kwamba mvunjiko wa moyo ulikuwa kisababishi katika kifo cha Yesu Kristo, ambaye kuhusu yeye ilitabiriwa: “Laumu imenivunja moyo, nami ninaugua sana.” (Zaburi 69:20) Je, maneno haya yaeleweke kihalisi? Yamkini ndio, kwani saa zilizotangulia kifo cha Yesu zilikuwa zenye maumivu makali—si kimwili tu bali pia kihisia-moyo. (Mathayo 27:46; Luka 22:44; Waebrania 5:7) Zaidi ya hilo, moyo wenye kuvunjika waweza kuelewesha sababu ya mtiririko wa “damu na maji” kutoka mchomo wa fumo uliomfika Yesu mara tu baada ya kifo chake. Kupasuka kwa moyo au mshipa mkuu wa damu kungeweza kuachilia damu ama katika tundu la kifua ama katika ngozimoyo—kiwambo chenye umajimaji ambacho huwemo moyo. Katika mahali popote pale mpasuko unaweza kusababisha mtiririko wa kile ambacho kingeonekana kuwa “damu na maji.”—Yohana 19:34.
Bila shaka, visababishi vingine vilihusika katika kifo cha Yesu ambacho kwa kulinganishwa kilikuwa cha haraka mno, vilitia ndani jinsi alivyotundikwa na kutendwa vibaya alikovumilia kabla ya kifo. Tunashukuru kama nini kwamba chini ya hali hizi gumu mno, Yesu alidumisha uaminifu-mshikamanifu wake! Likiwa tokeo alikwezwa sana na Baba yake, Yehova. (Wafilipi 2:8-11) Zaidi ya hilo, alifanya iwezekane kwetu sisi kuishi milele katika dunia iliyo paradiso.—Yohana 17:3; Ufunuo 21:3, 4.