Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Unapaswa Kumwamini Nani?
    Amkeni!—2006 | Septemba
    • Unapaswa Kumwamini Nani?

      “Bila shaka, kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini yeye aliyevijenga vitu vyote ni Mungu.”—WAEBRANIA 3:4.

      JE, UNAKUBALIANA na maneno hayo yanayopatana na akili ya mwandikaji wa Biblia? Mwanadamu amefanya maendeleo makubwa ya kisayansi katika muda wa miaka 2,000 hivi tangu maneno hayo yalipoandikwa. Je, bado kuna watu wanaofikiri kwamba ubuni unaoonekana katika vitu vya asili unapaswa kumchochea mtu kuamini kwamba kuna Mbuni, kuna Muumba, kuna Mungu?

      Hata katika nchi zilizoendelea watu wengi wangesema ndiyo. Kwa mfano, huko Marekani, uchunguzi uliofanywa na Newsweek mnamo 2005 ulionyesha kwamba asilimia 80 ya watu “wanaamini kwamba Mungu aliumba ulimwengu.” Je, wana maoni hayo kwa kuwa hawana elimu? Kwa mfano, je, kuna wanasayansi wowote wanaoamini kwamba kuna Mungu? Katika mwaka wa 1997 jarida la kisayansi Nature liliripoti kwamba asilimia 40 kati ya wataalamu wa biolojia, fizikia, na hisabati walioombwa maoni, hawaamini tu kwamba kuna Mungu, bali pia Yeye husikiliza na kujibu sala.

      Hata hivyo, wanasayansi wengine wanapinga kabisa imani hiyo. Hivi karibuni Dakt. Herbert A. Hauptman, mshindi wa Tuzo la Nobeli alisema katika warsha ya kisayansi kwamba kuamini nguvu zinazozidi zile za asili, hasa kuamini kuna Mungu hakupatani na mambo hakika ya kisayansi. Alisema kwamba “imani kama hiyo inaweza kuwadhuru wanadamu.” Hata wanasayansi wanaoamini kuna Mungu husita kufundisha kwamba ubuni unaoonekana katika mimea na wanyama ulitokezwa na Mbuni fulani. Kwa nini? Akitaja sababu moja, Douglas H. Erwin, mtaalamu wa biolojia ya mabaki ya kale ya wanyama na mimea katika Taasisi ya Smithsonia, alisema: “Kanuni moja ni kwamba sayansi haikubali eti miujiza hutokea.”

      Je, ungependa kuwaacha wengine wakuambie kile utakachofikiri na kuamini? Au ungependa kujichunguzia baadhi ya uthibitisho na kukata kauli yako mwenyewe? Unaposoma habari kuhusu ugunduzi wa karibuni wa kisayansi katika kurasa zinazofuata, jiulize hivi, ‘Je, ni jambo linalopatana na akili kuamini kwamba kuna Muumba?’

      [Blabu katika ukurasa wa 3]

      Jichunguzie uthibitisho

      [Sanduku katika ukurasa wa 3]

      Je, Mashahidi wa Yehova Ni Wanauumbaji?

      Mashahidi wa Yehova wanaamini masimulizi ya uumbaji katika kitabu cha Mwanzo cha Biblia. Hata hivyo, imani ya Mashahidi wa Yehova kuhusu uumbaji inatofautiana na ya wale wanaoitwa eti wanauumbaji. Kwa nini? Wanauumbaji huamini kwamba vitu vyote viliumbwa katika kipindi cha siku sita zenye urefu wa saa 24 kila moja, miaka 10,000 hivi iliyopita. Hata hivyo, Biblia haifundishi hivyo.a Watu hao pia huamini mafundisho mengi yasiyoungwa mkono na Biblia. Mafundisho ya Mashahidi wa Yehova hutegemea tu Neno la Mungu.

      Isitoshe, katika maeneo fulani, neno “wanauumbaji” huhusianishwa na vikundi ambavyo hushikilia pia imani nyingine kali za kidini na kujihusisha sana katika siasa. Vikundi hivyo hujaribu kuwashinikiza wanasiasa, mahakimu, na walimu wafuate sheria na mafundisho yanayopatana na imani yao kuhusu uumbaji.

      Mashahidi wa Yehova hawajihusishi katika siasa. Wao hutambua kwamba serikali zina haki ya kutunga na kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa. (Waroma 13:1-7) Hata hivyo, wao huchukua kwa uzito maneno ya Yesu kwamba wao “si sehemu ya ulimwengu.” (Yohana 17:14-16) Wanapohubiri, wao huwatolea watu nafasi ya kujifunza manufaa ya kuishi kulingana na viwango vya Mungu. Lakini hawavunji msimamo wao wa Kikristo wa kutokuwamo kwa kuunga mkono jitihada za watu wenye imani kali za kidini ambao hujaribu kutunga sheria za kijamii za kuwalazimisha watu wafuate viwango vya Biblia.—Yohana 18:36.

      [Maelezo ya Chini]

      a Tafadhali ona makala “Maoni ya Biblia: Je, Sayansi Inapingana na Masimulizi ya Mwanzo?” iliyo kwenye ukurasa wa 18 wa gazeti hili.

  • Vitu vya Asili Vinatufundisha Nini?
    Amkeni!—2006 | Septemba
    • Vitu vya Asili Vinatufundisha Nini?

      “Tafadhali uliza wanyama wa kufugwa, nao watakufundisha; pia viumbe vya mbinguni vyenye mabawa, navyo vitakuambia. Au onyesha kupendezwa kwako na dunia, nayo itakufundisha; na samaki wa baharini watakutangazia.”—AYUBU 12:7, 8.

      KATIKA miaka ya karibuni, wanasayansi na mainjinia wamekubali mimea na wanyama iwafundishe. Wao huiga uumbaji wanapobuni mashine mpya na kuboresha mashine za zamani. Unapofikiria mifano ifuatayo, jiulize hivi, ‘Ni nani kwa kweli anayestahili kusifiwa kwa ubuni huo?’

      Kujifunza Kutokana na Mapezi ya Nyangumi

      Wabuni wa ndege za abiria wanaweza kujifunza nini kutokana na nyangumi mwenye nundu? Inaonekana wanaweza kujifunza mengi. Nyangumi mwenye nundu aliyekomaa huwa na uzito wa tani 30, uzito sawa na wa lori lililojazwa, na ana mwili mgumu na mapezi makubwa yanayofanana na mabawa. Mnyama huyo mwenye urefu wa meta 12 anaweza kusonga kasi majini. Kwa mfano, anapokula, nyangumi mwenye nundu anaweza kuogelea akielekea juu kwa mzunguko chini ya krasteshia au samaki, huku akitokeza mawimbi ya mapovu. Mawimbi hayo yaliyo kama wavu yana kipenyo cha meta 1.5, nayo hukusanya viumbe hao juu ya maji. Kisha nyangumi huyo anawanyafua kwa ghafula.

      Jambo ambalo liliwashangaza watafiti ni jinsi kiumbe huyo aliye na mwili mgumu anavyoweza kuogelea kwa kuzunguka katika eneo dogo jinsi hiyo. Waligundua kwamba mapezi yake ndiyo humwezesha kuzunguka hivyo. Ncha ya mbele ya mapezi yao si laini kama bawa la ndege ya abiria, lakini imechongoka na ina sehemu zinazotokeza.

      Nyangumi anapoogelea kwa kasi, sehemu hizo humsaidia kusonga juu. Kwa njia gani? Jarida Natural History linasema kwamba sehemu hizo hufanya maji yapite kasi na kuyazunguka mapezi kwa utaratibu, hata nyangumi anapoogelea kwenda juu akiwa wima kwa kadiri fulani. Ikiwa mapezi ya nyangumi huyo yangekuwa na ncha laini, hangeweza kuogelea kwenda juu kwa kuzunguka katika eneo dogo jinsi hiyo kwani maji yangekuwa yakizunguka chini ya mapezi na kuzuia asiinuke.

      Ugunduzi huo unaweza kutumiwaje? Mabawa ya ndege za abiria yaliyoundwa kwa kuiga ubuni huo yatahitaji sehemu chache za mabawa zinazokunjwa au vifaa vingine vya kusaidia ndege kupaa. Mabawa kama hayo yangekuwa salama zaidi na rahisi kudumisha. John Long mtaalamu wa kuunda vitu kwa kuiga uumbaji anaamini kuwa hivi karibuni “kuna uwezekano mkubwa kwamba ndege zote za usafiri zitakuwa na mabawa yaliyo kama mapezi ya nyangumi mwenye nundu.”

      Kuiga Mabawa ya Korongo

      Bila shaka, mabawa ya ndege za abiria yanafanana na mabawa ya ndege wa angani. Hata hivyo, hivi karibuni mainjinia wamefanya maendeleo katika kuiga mabawa hayo. Gazeti New Scientist linaripoti hivi: “Watafiti katika Chuo Kikuu cha Florida wameunda ndege ndogo isiyoendeshwa na rubani iliyo na uwezo kama wa korongo wa kuelea, kuruka, na kupaa kwa kasi.”

      Korongo hufaulu kuruka kwa njia hiyo kwa kukunja na kunyoosha mabawa yao kwenye viwiko na mabega. Gazeti New Scientist linasema kwamba kwa kuiga ubuni huo, “ndege hiyo ndogo ya sentimeta 60 isiyoendeshwa na rubani hutumia mtambo fulani na vyuma kadhaa kukunja na kupanua mabawa yake.” Mabawa hayo yaliyoundwa kwa ustadi yatawezesha ndege hiyo ndogo kuelea na kuruka katikati ya majengo marefu. Jeshi la Angani la Marekani linajitahidi sana kuunda ndege kama hiyo inayoweza kuendeshwa kwa urahisi ili kuitumia kutafuta silaha za kemikali na za kibiolojia katika majiji makubwa.

      Kuiga Miguu ya Mjusi

      Hata wanyama wa nchi kavu hutufunza mengi. Kwa mfano, mjusi ana uwezo wa kupanda kuta na kujishikilia akiwa chini juu kwenye dari. Hata katika nyakati za Biblia kiumbe huyo alijulikana kwa sababu ya uwezo huo wa ajabu. (Methali 30:28) Ni nini kinachomfanya asianguke?

      Uwezo wa mjusi wa kujishikilia hata kwenye sehemu zilizo laini kama kioo unatokana na nywele ndogo zinazoitwa setae ambazo hufunika miguu yake. Miguu ya mjusi haitoi gundi. Badala yake, hiyo hutumia nguvu fulani ndogo za molekuli. Molekuli zilizo kwenye miguu yake na kwenye dari hushikamana kwa sababu ya nguvu ndogo zinazoitwa nguvu za van der Waals. Kwa kawaida nguvu za uvutano huzidi nguvu hizo, na ndiyo sababu wewe huwezi kupanda ukuta kwa kuwekelea mikono yako sambamba ukutani. Hata hivyo, nywele ndogo zilizo kwenye miguu ya mjusi humwezesha kushikilia eneo kubwa zaidi ukutani. Nguvu za van der Waals zinazotokezwa na maelfu ya nywele hizo ndogo hutokeza nguvu za kutosha kumshikilia mjusi ambaye hana uzito mkubwa.

      Ugunduzi huo unaweza kutumiwaje? Vitu fulani vinavyotengenezwa viwandani kwa kuiga miguu ya mjusi vinaweza kutumiwa badala ya velcro, ambayo pia iliundwa kwa kuiga uumbaji.a Jarida The Economist linamnukuu mtafiti mmoja aliyesema kwamba kishikizo kinachotengenezwa kwa kuiga ubuni wa nywele ndogo kwenye miguu ya mjusi kinaweza kufaa sana katika “matibabu ambapo vishikizo vyenye kemikali haviwezi kutumiwa.”

      Ni Nani Anayestahili Kusifiwa?

      Wakati huu, shirika la NASA linatengeneza roboti yenye miguu mingi inayotembea kama nge, na mainjinia huko Finland tayari wametengeneza trekta yenye miguu sita ambayo inaweza kupanda kwenye vizuizi kama mdudu mkubwa anavyoweza kufanya. Watafiti wengine wamebuni kitambaa chenye pindo kwa kuiga ubuni wa kifuko cha mbegu za msindano ambacho hujifungua na kujifunga. Watengenezaji wa magari wanaunda gari kwa kuiga ubuni wa samaki anayeitwa boxfish ambaye anasonga kwa wepesi sana. Na watafiti wengine wanachunguza uwezo wa kuhimili mshtuko wa gamba la aina fulani ya konokono, ili kutengeneza mavazi ya kujikinga yaliyo mepesi zaidi.

      Miundo mbalimbali imebuniwa kwa kuiga uumbaji hivi kwamba watafiti wameorodhesha maelfu ya mifumo ya kibiolojia. Wanasayansi wanaweza kufanya utafiti kwa kutumia orodha hiyo ili kupata “masuluhisho kutoka kwa vitu vya asili wanapokabili ugumu wa kubuni vitu fulani,” linasema jarida The Economist. Mifumo ya kiasili iliyo katika orodha hiyo husemwa kuwa “haki-miliki ya kibiolojia.” Kwa kawaida, mwenye haki-miliki ni mtu au kampuni iliyo ya kwanza kuandikisha kisheria wazo au mashine mpya. Likizungumza kuhusu orodha hiyo ya haki-miliki ya kibiolojia, jarida The Economist linasema hivi: “Kwa kurejelea vitu vilivyoigwa ambavyo vimebuniwa kwa ustadi kuwa ‘haki-miliki ya kibiolojia’, watafiti wanakazia tu kwamba kwa kweli vitu vya asili ndivyo vilivyo na haki-miliki.”

      Ubuni huo wa ajabu katika vitu vya asili ulitokeaje? Watafiti wengi wanaweza kudai kwamba ubuni wote huo ulio katika vitu vya asili ulijitokeza wenyewe kupitia mageuzi ambayo yametukia kwa mamilioni ya miaka. Hata hivyo, watafiti wengine wamekata kauli tofauti. Mnamo 2005 mtaalamu wa biolojia Michael Behe aliandika hivi katika gazeti The New York Times: “Ubuni uliopo [katika vitu vya asili] huandaa hoja rahisi yenye kusadikisha: ikiwa anafanana, anatembea, na kulia kama bata, na ikiwa hakuna hoja zilizo kinyume, basi lazima tukate kauli kwamba ni bata.” Alifikia mkataa gani? “Ubuni wa kitu haupaswi kupuuzwa eti kwa sababu tu uthibitisho unapatikana kwa urahisi.”

      Bila shaka, injinia anayebuni bawa la ndege ya abiria lililo salama na linalofanya kazi vizuri zaidi anastahili kusifiwa. Hali kadhalika, mbuni anayevumbua bendeji yenye matumizi mbalimbali, kitambaa laini zaidi, au gari bora zaidi, anastahili kusifiwa kwa sababu ya ubuni wake. Kwa kweli, mtengenezaji wa bidhaa anayeiga ubuni wa mvumbuzi fulani lakini anakataa kumpa sifa mvumbuzi huyo, anaweza kuonwa kuwa mhalifu.

      Hivyo, je, unaona kwamba inapatana na akili kwa watafiti walio na elimu ya hali ya juu kuiga mifumo ya asili kutatua matatizo magumu ya kiinjinia na kusema kwamba ubuni huo wa hali ya juu ulitokana na mageuzi bila akili yoyote? Ikiwa lazima kuwe na mbuni mwenye akili ili kutokeza nakala, vipi kuvumbua kitu chenyewe? Kwa kweli, ni nani anayestahili kusifiwa zaidi, msanii mkuu au mwanafunzi anayeiga ubuni wa msanii?

      Mkataa Unaopatana na Akili

      Baada ya kuchunguza uthibitisho uliopo kwamba vitu vya asili vilibuniwa, watu wengi wamekata kauli inayopatana na ile ya mtunga-zaburi aliyeandika hivi: “Jinsi kazi zako zilivyo nyingi, Ee Yehova! Zote umezifanya kwa hekima. Dunia imejaa vitu ulivyotokeza.” (Zaburi 104:24) Paulo ambaye pia aliandika Biblia alikata kauli kama hiyo. Alisema: “Kwa maana sifa [za Mungu] ambazo hazionekani, zinaonekana waziwazi tangu kuumbwa kwa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zinaeleweka kwa vitu vilivyofanywa, yaani, nguvu zake za milele na Uungu.”—Waroma 1:19, 20.

      Hata hivyo, watu wengi wanyoofu ambao wanaiheshimu Biblia na wanaamini kwamba kuna Mungu wanaweza kusema kwamba huenda Mungu aliumba vitu vyote vya asili kupitia mageuzi. Lakini, Biblia inafundisha nini?

      [Maelezo ya Chini]

      a Velcro ni aina ya kishikizo cha kubandika na kubandua kinachoundwa kwa kuiga ubuni wa mbegu za mmea unaoitwa burdock.

      [Blabu katika ukurasa wa 5]

      Ubuni wa ajabu katika vitu vya asili ulitokeaje?

      [Blabu katika ukurasa wa 6]

      Ni nani aliye na hati-miliki ya vitu vya asili?

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      Ikiwa lazima kuwe na mbuni mwenye akili ili kutokeza nakala, vipi kuvumbua kitu chenyewe?

      Ndege inayoweza kuendeshwa kwa urahisi imebuniwa kwa kuiga bawa la korongo

      Miguu ya mjusi haiwezi kuchafuka wala kuacha alama, nayo hujishikilia kwenye sehemu yoyote isipokuwa “Teflon” na inaweza kushikilia na kuacha kitu bila tatizo. Watafiti wanajaribu kuiga miguu hiyo

      Ubuni wa samaki anayeitwa “boxfish” anayesonga kwa wepesi sana ulichochea kubuniwa kwa gari fulani

      [Hisani]

      Airplane: Kristen Bartlett/ University of Florida; gecko foot: Breck P. Kent; box fish and car: Mercedes-Benz USA

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

      WASAFIRI WENYE HEKIMA YA KISILIKA

      Viumbe wengi hutumia “hekima ya kisilika” kusafiri huku na huku duniani. (Methali 30:24, 25) Fikiria mifano miwili.

      ◼ Chungu Hujiongozaje Barabarani? Chungu wanaotoka kutafuta chakula hujuaje njia ya kurudi kwenye makao yao? Watafiti huko Uingereza waligundua kwamba mbali na kuacha harufu kwenye njia, chungu fulani hutumia hesabu za maumbo kuweka alama zinazowasaidia kurudi kwenye makao yao. Kwa mfano, gazeti New Scientist linasema kwamba chungu wanaoitwa pharaoh “wanapotoka katika makao yao wao huacha mistari inayongaa ambayo inaachana kwa pembe ya digrii 50 au 60.” Ni nini kinachostaajabisha kuhusu tabia hiyo? Chungu anapokuwa njiani kurudi nyumbani na afike kwenye njia panda, kisilika yeye hutumia njia ambayo haitampoteza sana lakini mwishowe itamfikisha nyumbani. Makala hiyo inasema: “Jambo hilo huwasaidia chungu wasipotee njia na hivyo wasitumie nguvu nyingi wanapotafuta njia ya kurudi nyumbani.”

      ◼ Dira ya Ndege Ndege wengi wanaweza kutambua wanakoelekea kwa usahihi wa hali ya juu wanapofunga safari ndefu haidhuru hali ya hewa. Jinsi gani? Ndege wanaweza kuhisi nguvu ya sumaku ya dunia. Hata hivyo, jarida Science linasema “mistari ya nguvu ya sumaku [ya dunia] hutofautiana kutoka mahali pamoja kwenda pengine na nyakati nyingine haielekezi kaskazini kabisa.” Ni nini huwasaidia ndege wanaosafiri wasipotee njia? Kila jioni ndege hurekebisha dira yao ya kiasili kulingana na jua linavyotua. Kwa kuwa jua hutua sehemu mbalimbali ikitegemea mabadiliko ya latitudo na majira, watafiti wanafikiri kwamba ni lazima ndege hao wawe na uwezo wa kufanya mabadiliko kwa kutumia “saa ya kiasili ambayo huwawezesha kujua wakati hususa wa mwaka,” linasema jarida Science.

      Chungu walipataje uwezo wa kufanya hesabu za maumbo? Ndege walipataje dira, saa ya kiasili, na ubongo unaoweza kuchanganua habari hiyo? Je, ni kutokana na mageuzi? Au ni kutoka kwa Muumba mwenye akili?

      [Hisani]

      © E.J.H. Robinson 2004

  • Je, Mungu Alitumia Mageuzi Kuumba Uhai?
    Amkeni!—2006 | Septemba
    • Je, Mungu Alitumia Mageuzi Kuumba Uhai?

      “Unastahili, Ee Yehova, naam, Mungu wetu, kupokea utukufu na heshima na nguvu, kwa sababu uliumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako navyo vikaumbwa.”—UFUNUO 4:11.

      MUDA mfupi baada ya Charles Darwin kufanya nadharia ya mageuzi iwapendeze watu wengi, madhehebu mengi yanayodai kuwa ya Kikristo yalianza kutafuta njia ya kupatanisha imani kwamba kuna Mungu na nadharia ya mageuzi.

      Leo, inaonekana vikundi vingi maarufu vya kidini vinavyodai kuwa vya Kikristo vinakubali kuwa Mungu alitumia mageuzi kwa njia fulani kuumba uhai. Wengine hufundisha kwamba Mungu aliutayarisha ulimwengu kwa njia ambayo uhai ungetokana na kemikali zisizo na uhai ambazo zingebadilika hatua kwa hatua na hatimaye kutokeza wanadamu. Wale wanaounga mkono fundisho hilo, hawahisi kwamba Mungu aliingilia kati baada ya mageuzi hayo kuanza. Wengine hufikiri kwamba kwa ujumla Mungu aliacha mageuzi yatokeze jamii nyingi za mimea na wanyama lakini mara kwa mara akaingilia mambo ili kuendeleza mageuzi hayo.

      Je, Mafundisho Hayo Yanaweza Kupatanishwa?

      Je, nadharia ya mageuzi inapatana na mafundisho ya Biblia? Ikiwa nadharia ya mageuzi ingekuwa kweli, basi simulizi la Biblia kuhusu uumbaji wa mtu wa kwanza, Adamu, lingekuwa tu hadithi iliyokusudiwa kufunza mambo fulani mazuri lakini haipaswi kuchukuliwa kihalisi. (Mwanzo 1:26, 27; 2:18-24) Je, Yesu aliona simulizi hilo la Biblia kuwa hadithi tu? “Je, hamkusoma,” Yesu akasema, “kwamba yeye aliyewaumba hao kutoka mwanzo aliwafanya mwanamume na mwanamke na kusema, ‘Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye atashikamana na mke wake, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’? Hivi kwamba wao si wawili tena, bali mwili mmoja. Kwa hiyo, kile ambacho Mungu ameunganisha mtu yeyote asikitenganishe.”—Mathayo 19:4-6.

      Yesu alikuwa akinukuu simulizi la uumbaji lililorekodiwa katika Mwanzo sura ya 2. Ikiwa Yesu aliamini kwamba ndoa hiyo ya kwanza ilikuwa hadithi ya kuwaziwa tu, je, angeirejelea ili kuthibitisha fundisho lake kuhusu utakatifu wa ndoa? Hapana. Yesu alitaja simulizi hilo la Mwanzo kwa sababu alijua lilikuwa ni jambo hakika.—Yohana 17:17.

      Vilevile, wanafunzi wa Yesu waliamini kwamba simulizi la Mwanzo kuhusu uumbaji lilikuwa la kweli. Kwa mfano, injili ya Luka ina orodha ya ukoo wa Yesu inayorudi nyuma hadi kwa Adamu. (Luka 3:23-38) Ikiwa Adamu alikuwa mtu wa kuwaziwa tu, ni majina mangapi katika orodha hiyo yangekuwa ya watu halisi na mangapi ya watu wa kuwaziwa tu? Ikiwa mtu wa kwanza katika orodha hiyo ya ukoo angekuwa wa kuwaziwa tu, dai la Yesu kwamba alikuwa Mesiya aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi lingekuwa thabiti kadiri gani? (Mathayo 1:1) Luka, mwandikaji wa Injili alisema kwamba alikuwa ‘amefuata kwa uangalifu mambo yote tangu mwanzo kwa usahihi.’ Kwa wazi yeye aliamini simulizi la uumbaji katika kitabu cha Mwanzo.—Luka 1:3.

      Imani ya mtume Paulo katika Yesu ilihusiana na imani yake katika simulizi la Mwanzo. Aliandika hivi: “Kwa kuwa kifo ni kupitia mwanadamu, ufufuo wa wafu pia ni kupitia mwanadamu. Kwa maana kama vile katika Adamu wote wanakufa, vivyo hivyo pia katika Kristo wote watafanywa kuwa hai.” (1 Wakorintho 15:21, 22) Ikiwa kwa kweli Adamu hakuwa babu ya wanadamu wote, yule ambaye kupitia kwake “dhambi iliingia katika ulimwengu na kifo kupitia dhambi,” kwa nini Yesu alilazimika kufa kutangua matokeo ya dhambi iliyorithiwa?—Waroma 5:12; 6:23.

      Kudhoofisha imani katika simulizi la uumbaji katika kitabu cha Mwanzo ni kudhoofisha misingi ya imani ya Kikristo. Nadharia ya mageuzi na mafundisho ya Kristo hayapatani. Kujaribu kupatanisha mafundisho hayo mawili kunaweza tu kutokeza imani dhaifu ambayo inaweza ‘kurushwa huku na huku kama kwa mawimbi na kuchukuliwa huku na huku na kila upepo wa fundisho.’—Waefeso 4:14.

      Imani Juu ya Msingi Imara

      Kwa karne nyingi, Biblia imechambuliwa na kushambuliwa. Lakini, tena na tena maandishi ya Biblia yamethibitishwa kuwa ya kweli. Inapozungumzia mambo ya historia, afya, na sayansi, masimulizi yake yamethibitika kuwa yenye kutegemeka. Mashauri yake kuhusu mahusiano ya watu ni yenye kutumainika na yanayoweza kutumika wakati wowote ule. Falsafa na nadharia za wanadamu ni kama majani mengi mabichi ambayo hukua na kukauka, lakini Neno la Mungu “litadumu mpaka wakati usio na kipimo.”—Isaya 40:8.

      Nadharia ya mageuzi si fundisho la wanasayansi tu. Ni falsafa ya wanadamu ambayo ilianza na kusitawi kwa makumi ya miaka. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni mafundisho ya awali ya Darwin yamebadilika hatua kwa hatua kadiri ambavyo watu wamejaribu kupatanisha nadharia hiyo na uthibitisho unaozidi kuongezeka wa kwamba vitu vya asili vimebuniwa. Tunakutia moyo uichunguze habari hiyo zaidi. Unaweza kufanya hivyo kwa kusoma makala nyingine zilizo katika gazeti hili. Isitoshe, unaweza kusoma vichapo vilivyoonyeshwa kwenye ukurasa huu na ukurasa wa 32.

      Baada ya kuchunguza habari hiyo, inaelekea kwamba imani yako katika yale ambayo Biblia inasema kuhusu wakati uliopita itaimarishwa. La muhimu zaidi, imani yako katika ahadi za Biblia kuhusu wakati ujao itaimarishwa. (Waebrania 11:1) Huenda pia ukachochewa kumsifu Yehova, ‘Mtengenezaji wa mbingu na dunia.’—Zaburi 146:6.

      UNAWEZA KUSOMA HABARI ZAIDI KATIKA

      Kitabu kwa Ajili ya Watu Wote Mifano hususa inayothibitisha usahihi wa maandishi ya Biblia inapatikana katika broshua hii

      Je, Kuna Muumba Anayekujali? Chunguza uthibitisho zaidi wa kisayansi, na upate kujua sababu inayomfanya Mungu anayejali aruhusu watu wateseke sana

      Biblia Inafundisha Nini Hasa? Jibu la swali “Mungu ana kusudi gani kwa dunia?” linapatikana katika sura ya 3 ya kitabu hiki

      [Blabu katika ukurasa wa 10]

      Yesu aliamini masimulizi ya uumbaji yaliyo katika kitabu cha Mwanzo. Je, alikosea?

      [Sanduku katika ukurasa wa 9]

      MAGEUZI NI NINI?

      Maana moja ya neno “mageuzi” ni: “Mabadiliko ya hatua kwa hatua.” Hata hivyo, neno hilo hutumiwa katika njia kadhaa. Kwa mfano, hutumiwa kurejelea mabadiliko makubwa ya vitu visivyo na uhai, yaani, jinsi ulimwengu ulivyotokea. Pia, hutumiwa kufafanua mabadiliko madogo ya vitu vilivyo hai, yaani, jinsi mimea na wanyama wanavyobadilika ili wapatane na mazingira yao. Hata hivyo, mara nyingi neno hilo hutumiwa kufafanua nadharia ya kwamba uhai ulitokana na kemikali zisizo na uhai ambazo zilijifanyiza kuwa chembe zinazogawanyika na kutokeza chembe mpya. Kisha chembe hizo zikasitawi polepole na kuwa vitu tata vyenye uhai, mwanadamu akiwa kitu tata zaidi kilichotokezwa na mageuzi hayo. Ufafanuzi huo wa tatu ndio unaowakilishwa na neno “mageuzi” katika makala hii.

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]

      Space photo: J. Hester and P. Scowen (AZ State Univ.), NASA

  • Kumhoji Mtaalamu wa Biokemia
    Amkeni!—2006 | Septemba
    • Kumhoji Mtaalamu wa Biokemia

      MNAMO 1996, Michael J. Behe, ambaye sasa ni profesa wa biokemia katika Chuo Kikuu cha Lehigh, Pennsylvania, Marekani alitoa kitabu chake kiitwacho Darwin’s Black Box—The Biochemical Challenge to Evolution. Toleo la Amkeni! la Mei 8, 1997, lilikuwa na makala ya mfululizo yenye kichwa “Tulikujaje Kuwapo?—Kwa Aksidenti au kwa Ubuni?” ambayo ilirejelea kitabu cha Behe. Katika kipindi cha miaka kumi hivi tangu kitabu Darwin’s Black Box kichapishwe, wanasayansi wanaotetea mageuzi wamejitahidi kupinga hoja za Behe. Wachambuzi wamemlaumu Behe, ambaye ni Mkatoliki, wakidai kwamba ameruhusu imani yake ya kidini iathiri maoni yake ya kisayansi. Wengine wanadai kwamba maoni yake hayapatani na sayansi. Mwandishi wa Amkeni! alimhoji Profesa Behe ili kujua kwa nini maoni yake yamezua ubishi.

      MWANDISHI WA AMKENI!: KWA NINI UNAFIKIRI VITU VILIVYO HAI VINATHIBITISHA KWAMBA VILIBUNIWA NA MTU MWENYE AKILI?

      PROFESA BEHE: Tunapoona sehemu za mashine zilizopangwa kwa utaratibu ili kufanya kazi fulani tunakata kauli kwamba ilibuniwa. Kwa mfano, fikiria mashine tunazotumia kila siku kama vile mashine ya kukata nyasi, gari, au zile ambazo si tata. Mimi hupenda kutoa mfano wa mtego wa panya. Unakata kauli kwamba mtego wa panya ulibuniwa kwa kuwa una sehemu zilizopangwa kwa utaratibu ili kumnasa panya.

      Wanasayansi wamefanya maendeleo hivi kwamba wamegundua jinsi ambavyo sehemu ndogo zaidi za vitu hai hufanya kazi ili kuendeleza uhai wa vitu hivyo. Inashangaza kwamba wanasayansi wamegundua kuna mashine tata zinazofanya kazi katika sehemu hizo za vitu hai. Kwa mfano, katika chembe kuna “malori” madogo yanayosafirisha vitu muhimu katika chembe. Kuna “ishara ndogo za barabarani” zinazoelekeza “malori” hayo kulia au kushoto. Chembe fulani zina “mota” ndogo ambazo huzisukuma kwenye umajimaji. Watu wakiona mashine nyingine yoyote tata inayofanya kazi, watakata kauli kwamba ilibuniwa. Licha ya madai ya nadharia ya Darwin kuhusu mageuzi, hakuna kauli nyingine tunayoweza kukata. Kwa kuwa ni kawaida kukubali kwamba mashine yenye sehemu zilizopangwa kwa utaratibu ilibuniwa, tuna sababu nzuri ya kukata kauli kwamba mifumo ya sehemu hizo ndogo zaidi za vitu hai ilibuniwa na mtu mwenye akili.

      MWANDISHI WA AMKENI!: UNAFIKIRI NI KWA NINI WENGI WA WANASAYANSI WENZAKO HAWAKUBALIANI NA MAONI YAKO KWAMBA VITU VILIBUNIWA NA MTU MWENYE AKILI?

      PROFESA BEHE: Wanasayansi wengi hawakubaliani na maoni yangu kwamba kuna mbuni mwenye akili kwa kuwa wazo hilo linapita ufafanuzi wa kisayansi, kwani linaonyesha waziwazi kwamba kuna chanzo kikuu kuliko ulimwengu wa asili. Watu wengi hawafurahishwi na kauli hiyo. Hata hivyo, inakubalika kwamba sayansi inapaswa kukubaliana na uthibitisho uliopo bila kuegemea upande wowote. Kwa maoni yangu, kukataa jambo ambalo limethibitishwa kabisa kwa sababu tu ya kuogopa matokeo ya kufanya hivyo si tendo la ujasiri.

      MWANDISHI WA AMKENI!: UNA MAONI GANI KUHUSU WACHAMBUZI WANAODAI KWAMBA WATU WASIO NA UJUZI NDIO WANAOAMINI KWAMBA KUNA MBUNI MWENYE AKILI?

      PROFESA BEHE: Hatuamini kwamba kuna mbuni kwa sababu hatuna ujuzi. Imani hiyo haitegemei yale tusiyojua; inategemea yale tunayojua. Darwin alipochapisha kitabu chake The Origin of Species miaka 150 iliyopita, uhai ulionekana kuwa kitu rahisi sana. Wanasayansi walifikiri kwamba chembe haikuwa tata sana na hivyo ingeweza kujitokeza kutokana na matope ya bahari. Lakini tangu hapo, wanasayansi wamegundua kwamba chembe ni tata sana kuliko mashine yoyote ya karne hii ya 21. Chembe hizo tata zinazofanya kazi zinathibitisha kwamba kuna mbuni mwenye kusudi.

      MWANDISHI WA AMKENI!: JE, SAYANSI IMETOA UTHIBITISHO WOWOTE KWAMBA MAGEUZI, KUPITIA UTEUZI WA KIASILI, YAMETOKEZA MASHINE HIZO TATA ZA SEHEMU NDOGO ZAIDI ZA VITU HAI AMBAZO UNAZUNGUMZIA?

      PROFESA BEHE: Ukichunguza vitabu vya sayansi, utagundua kwamba hakuna mwanasayansi ambaye amejaribu sana, iwe kwa kufanya majaribio au kwa kuunda vigezo vya kisayansi, kuthibitisha jinsi mashine hizo ndogo zilivyojitokeza kwa mageuzi. Wameshindwa kufanya hivyo licha ya kwamba katika kipindi cha miaka kumi tangu kitabu changu kilipochapishwa, mashirika mengi ya kisayansi kama vile Shirika la Kitaifa la Sayansi la Marekani na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kisayansi, yamewahimiza washiriki wake wajitahidi wawezavyo kupinga wazo la kwamba vitu hai vinathibitisha kuwa kuna mbuni mwenye akili.

      MWANDISHI WA AMKENI!: UNA MAONI GANI KUHUSU WALE WANAOSEMA KWAMBA BAADHI YA VIUNGO AU SEHEMU ZA MIMEA NA WANYAMA ZILIBUNIWA VIBAYA?

      PROFESA BEHE: Kutojua kazi ya viungo au sehemu fulani za mimea na wanyama hakumaanishi kwamba havina kazi muhimu. Kwa mfano, ilifikiriwa kwamba viungo fulani ambavyo husemwa kuwa havina kazi, vinathibitisha kuwa mwili wa binadamu na vitu vingine vilibuniwa vibaya. Viungo kama vile kidole cha tumbo na mafindo vilionwa kuwa havina kazi na mara nyingi viliondolewa. Lakini baadaye ikagunduliwa kwamba vina kazi muhimu katika mfumo wa kinga na havikuonwa tena kuwa havina kazi.

      Jambo lingine tunalopaswa kukumbuka ni kwamba katika biolojia vitu fulani hutukia kana kwamba kwa aksidenti. Gari langu likibonyea au gurudumu lake likitoboka, hilo halimaanishi kwamba gari hilo au gurudumu lake halikubuniwa. Hali kadhalika, uhakika wa kwamba vitu fulani vilitokea kwa aksidenti katika biolojia haumaanishi kwamba mashine ndogo zilizo tata sana za vitu hai zilijitokeza. Hoja kama hiyo haipatani na akili hata kidogo.

      [Blabu katika ukurasa wa 12]

      “Kwa maoni yangu, kukataa jambo ambalo limethibitishwa kabisa kwa sababu tu ya kuogopa matokeo ya kufanya hivyo si tendo la ujasiri”

  • Je, Mageuzi Ni Jambo Hakika?
    Amkeni!—2006 | Septemba
    • Je, Mageuzi Ni Jambo Hakika?

      “MAGEUZI ni jambo hakika kama tu joto la jua lilivyo hakika,” anadai Profesa Richard Dawkins, mwanasayansi maarufu wa mageuzi. Bila shaka, majaribio na mambo hakika yanayotukia yanathibitisha kwamba jua lina joto. Lakini je, majaribio na mambo hakika yanayotukia yanatoa uthibitisho kama huo usioweza kupingwa kwamba mageuzi yalitukia?

      Kabla ya kujibu swali hilo tunahitaji kufafanua jambo moja. Wanasayansi wengi wameona kwamba baada ya muda, wazao wa vitu vilivyo hai hubadilika kidogo. Charles Darwin aliita hatua hiyo “mnyumbuliko unaotokeza mabadiliko.” Mabadiliko hayo yameonekana, yakafanyiwa majaribio, na kutumiwa kwa mafanikio na wazalishaji wa wanyama na mimea.a Mabadiliko hayo yanaweza kuonwa kuwa mambo hakika. Hata hivyo, wanasayansi huita mabadiliko hayo madogo “mageuzi madogo.” Taarifa hiyo inaonyesha dhana ya wanasayansi wengi kwamba mabadiliko hayo madogo yanathibitisha jambo tofauti kabisa, jambo ambalo halijaonekana na yeyote, jambo ambalo wao huliita mageuzi makubwa.

      Darwin alidai mengi zaidi kuliko mabadiliko yanayoweza kuonekana. Aliandika hivi katika kitabu chake maarufu The Origin of Species: “Sivioni vitu vyote kuwa viumbe vya pekee, bali naviona kuwa vitu vilivyotokana na vitu vichache vyenye uhai.” Darwin alisema kwamba katika kipindi kirefu cha wakati, vitu hivyo “vichache vilivyo hai” au vitu visivyo tata vyenye uhai, viligeuka polepole, kupitia “mabadiliko madogo sana,” na kutokeza mamilioni ya vitu vyenye uhai duniani. Wanamageuzi wanafundisha kwamba mabadiliko mengi madogo yalitokeza mabadiliko makubwa yaliyohitajika ili kugeuza samaki kuwa amfibia na sokwe kuwa watu. Mabadiliko hayo makubwa yanayodaiwa kuwa yalitukia ndiyo yanayorejelewa kuwa mageuzi makubwa. Wengi hufikiri kwamba dai hilo la pili linapatana na akili. Wao hujiuliza, ‘Ikiwa mabadiliko madogo yanaweza kutukia katika spishi, je, mageuzi hayawezi kutokeza mabadiliko makubwa katika kipindi kirefu cha wakati?’b

      Fundisho kuhusu mageuzi makubwa linategemea dhana tatu kuu:

      1. Mabadiliko ya chembe za urithi yanaandaa vitu vinavyohitajika kutokeza jamii mpya.c

      2. Uteuzi wa kiasili hutokeza jamii mpya.

      3. Mabaki ya kale ya wanyama na mimea huonyesha kwamba mageuzi makubwa yalitukia katika mimea na wanyama.

      Je, uthibitisho wa mageuzi makubwa ni wenye nguvu sana hivi kwamba inapaswa kuonwa kwamba yalitukia?

      Je, Mabadiliko ya Chembe za Urithi Yanaweza Kutokeza Jamii Mpya?

      Habari nyingi kuhusu mimea na wanyama zinategemea maagizo yaliyo katika chembe za urithi, yaani, maagizo yaliyo katika kiini cha kila chembe.d Watafiti wamegundua kwamba mabadiliko ya chembe za urithi, au mabadiliko yasiyo na mpango ya maagizo katika chembe za urithi yanaweza kutokeza mabadiliko katika vizazi vya wanyama na mimea. Mnamo 1946, Hermann J. Muller, mshindi wa Tuzo la Nobeli na mwanzilishi wa uchunguzi wa mabadiliko ya chembe za urithi, alidai hivi: “Mabadiliko mengi madogo ambayo hayatokei mara nyingi si njia ya msingi ya mwanadamu kuboresha wanyama na mimea tu, bali ndiyo njia hasa ambayo mageuzi yakiongozwa na uteuzi wa kiasili yametukia.”

      Kwa kweli, fundisho la mageuzi makubwa linategemea dai la kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayatokezi tu spishi mpya, yaani, aina za mimea na wanyama, bali pia jamii mpya kabisa. Je, kuna njia yoyote ya kuthibitisha dai hilo la kishupavu? Hebu fikiria kile ambacho kimefunuliwa katika miaka 100 hivi ya uchunguzi wa chembe za urithi.

      Katika miaka ya 1930, wanasayansi walisisimkia wazo la kwamba ikiwa uteuzi wa kiasili, yaani, kusalimika kwa viumbe bora na kufa kwa visivyo bora, kungeweza kutokeza spishi mpya za mimea kutokana na mabadiliko yanayotukia bila mpango, basi mabadiliko hayo yakiongozwa na mwanadamu yanapaswa kuwa na matokeo makubwa zaidi. Wolf-Ekkehard Lönnig, mwanasayansi katika Taasisi ya Max Planck ya Utafiti wa Kuzalisha Mimea nchini Ujerumani, alimwambia mwandishi wa Amkeni! hivi: “Msisimko huo hasa ulienea miongoni wa wanabiolojia, na hasa miongoni mwa wataalamu wa chembe za urithi na wazalishaji wa mimea na wanyama.” Kwa nini kulikuwa na msisimko huo? Lönnig, ambaye amechunguza mabadiliko ya chembe za urithi kwa miaka 28 hivi, anasema: “Watafiti hao walidhani wakati wa kubadili njia za msingi za kuzalisha mimea na wanyama ulikuwa umewadia. Walifikiri kwamba kwa kuchochea mabadiliko ya chembe za urithi na kuchagua chembe bora, wangeweza kutokeza mimea na wanyama wapya walio bora.”e

      Wanasayansi nchini Marekani, Asia, na Ulaya walianzisha miradi ya utafiti iliyodhaminiwa kwa pesa nyingi, nao walitumia njia walizotarajia kwamba zingeharakisha hatua za mageuzi. Kumekuwa na matokeo gani baada ya utafiti mkubwa ambao umechukua miaka 40? “Licha ya gharama kubwa,” asema mtafiti Peter von Sengbusch, “majaribio ya kutokeza mabadiliko ya chembe za urithi kupitia njia fulani ya kisayansi, yaliambulia patupu.” Lönnig alisema: “Kufikia miaka ya 1980, matumaini na msisimko uliokuwapo miongoni mwa wanasayansi yaligonga mwamba ulimwenguni pote. Miradi ya uchunguzi wa kuzalisha mimea na wanyama kwa kubadili chembe za urithi ilitupiliwa mbali katika nchi za Magharibi. Karibu mimea na wanyama wote waliotokezwa kwa kubadili chembe za urithi walikuwa na ‘dosari,’ nao walikufa au wakawa dhaifu kuliko wale ambao chembe zao zilibadilika kiasili.”f

      Hata hivyo, habari ambayo imekusanywa kwa miaka 100 ya utafiti wa mabadiliko ya chembe za urithi na hasa miaka 70 ya utafiti wa kuzalisha mimea na wanyama kwa kubadili chembe hizo, imewawezesha wanasayansi kukata kauli mbalimbali kuhusu uwezo wa kutokeza jamii mpya kwa kubadili chembe hizo. Baada ya kuchunguza uthibitisho uliokuwa umetolewa Lönnig alisema: “Mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadili spishi za awali [za wanyama na mimea] na kutokeza spishi mpya kabisa. Kauli hiyo inapatana na majaribio na matokeo ya utafiti ambao umefanywa katika karne ya 20 na pia inapatana na sheria za uwezekano. Hivyo, sheria ya mabadiliko yanayojirudia-rudia huonyesha kwamba spishi ambazo zinatofautiana na spishi nyingine kwa kutegemea chembe za urithi huwa na mipaka hususa isiyoweza kuvunjwa au kuvukwa wakati mabadiliko ya chembe hizo yanapotokea kiaksidenti.”

      Fikiria uzito wa kauli hiyo. Ikiwa wanasayansi stadi hawawezi kutokeza aina mpya za mimea na wanyama kwa kuchochea mabadiliko ya chembe za urithi na kuchagua chembe bora, je, mageuzi yasiyoongozwa na mtu mwenye akili yanaweza kuwa na matokeo bora? Ikiwa utafiti umethibitisha kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadilisha spishi za awali na kutokeza mpya, mageuzi makubwa yangewezaje kutokea?

      Je, Uteuzi wa Kiasili Unaweza Kutokeza Spishi Mpya?

      Darwin aliamini kwamba ule aliourejelea kuwa uteuzi wa kiasili ungechagua viumbe ambavyo vingefaana na mazingira huku viumbe visivyofaana na mazingira vikifa na kutoweka. Wanamageuzi wa kisasa wanafundisha kwamba kadiri spishi zilivyoenea na kutengana, ndivyo uteuzi wa kiasili ulivyochagua viumbe ambavyo mabadiliko ya chembe zao za urithi yalivifanya vipatane zaidi na mazingira mapya. Wanamageuzi wanadai kwamba spishi hizo zilizojitenga hatimaye zilitokeza spishi mpya kabisa.

      Kama ilivyosemwa mwanzoni, uchunguzi umethibitisha kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kamwe kutokeza aina mpya kabisa za mimea na wanyama. Hata hivyo, wanamageuzi wana uthibitisho gani wa kuunga mkono dai lao kwamba uteuzi wa kiasili unachagua chembe bora za urithi zilizobadilishwa ili kutokeza spishi mpya? Kijitabu kilichochapishwa mnamo 1999 na Shirika la Kitaifa la Sayansi (NAS) nchini Marekani kilisema hivi: “Mfano mmoja wenye kusadikisha wa mageuzi ya spishi mpya ulihusisha spishi 13 za shorewanda waliochunguzwa na Darwin katika Visiwa vya Galápagos. Ndege hao sasa wanaitwa shorewanda wa Darwin.”

      Katika miaka ya 1970, watafiti kadhaa wakiongozwa na Peter na Rosemary Grant, walianza kuwachunguza shorewanda hao na wakagundua kwamba baada ya mwaka mzima wa ukame, idadi ya shorewanda wenye midomo mirefu waliosalimika ilizidi ile ya wale wenye midomo mifupi. Kwa kuwa ukubwa na umbo la midomo yao ndiyo njia moja kuu ya kutambulisha spishi hizo 13 za shorewanda, huo ulidhaniwa kuwa ugunduzi muhimu. Kijitabu hicho cha NAS kinasema, “Peter na Rosemary Grant wamekadiria kwamba ikiwa visiwa hivyo vitakumbwa na ukame mwaka moja katika kila kipindi cha miaka 10, spishi mpya ya shorewanda itatokezwa baada ya miaka 200 hivi.”

      Hata hivyo, kile kijitabu cha NAS hakizungumzii baadhi ya mambo hakika yenye kuaibisha. Katika miaka iliyofuata mwaka huo wa ukame, shorewanda wenye midomo mifupi walikuwa wengi tena kuliko wale wenye midomo mirefu. Hivyo mnamo 1987, Peter Grant na mhitimu wa chuo kikuu, Lisle Gibbs, waliandika katika jarida la sayansi Nature kwamba walishuhudia “uteuzi ukichukua mkondo ulio kinyume.” Katika 1991, Grant aliandika kwamba “idadi ya ndege, ikiongozwa na uteuzi wa kiasili, ilikuwa ikiongezeka na kupungua,” kila mara hali ya hewa ilipobadilika. Watafiti hao waligundua pia kwamba ndege wa “spishi” kadhaa tofauti walizalisha pamoja na kutokeza ndege waliostahimili kuliko wazazi wao. Peter na Rosemary Grant walikata kauli kwamba ikiwa ndege hao wangeendelea kuzalisha pamoja, baada ya kipindi cha miaka 200 hivi, “spishi” hizo mbili zingeungana na kuwa spishi moja.

      Katika 1966, mwanabiolojia wa mageuzi George Christopher Williams aliandika hivi: “Nasikitika kwamba mwanzoni nadharia ya uteuzi wa kiasili ilianzishwa ili kufafanua jinsi mageuzi yalivyotokea. Nadharia hiyo inafaa zaidi kutumiwa kuelezea jinsi ambavyo viumbe hubadilika kulingana na mazingira yao.” Mnamo 1999, mtungaji wa nadharia za mageuzi Jeffrey Schwartz, aliandika kwamba ikiwa kauli ya Williams ni sahihi, uteuzi wa kiasili unaweza kusaidia wanyama na mimea kubadilika kulingana na hali zilizopo, lakini “hautokezi spishi mpya.”

      Kwa kweli, shorewanda wa Darwin hawabadiliki na “kuwa ndege wapya.” Bado wao ni shorewanda. Na uhakika wa kwamba wanazalisha pamoja unatilia shaka mbinu za wanasayansi fulani za kuainisha spishi. Isitoshe, hilo limefichua kwamba hata taasisi mashuhuri za sayansi huripoti matokeo ya utafiti mbalimbali huku zikiegemea maoni yao.

      Je, Mabaki ya Kale ya Wanyama Yanathibitisha Kwamba Mageuzi Makubwa Yalitokea?

      Kijitabu cha NAS kilichonukuliwa mapema kinafanya msomaji afikiri kuwa mabaki ya kale ya wanyama ambayo wanasayansi wamepata yanathibitisha kabisa kwamba mageuzi makubwa yalitokea. Kinasema hivi waziwazi: “Aina nyingi za viumbe zimepatikana kati ya samaki na amfibia, reptilia na mamalia, na pia katika vizazi vya sokwe hivi kwamba imekuwa vigumu kutambua hasa wakati spishi moja inapobadilika na kuwa nyingine.”

      Taarifa hiyo ya kishupavu inashangaza sana. Kwa nini? Mnamo 2004, jarida National Geographic lilisema kwamba rekodi ya mabaki ya kale ya wanyama ni kama “sinema ya mageuzi ambayo picha zake za matukio ya miaka 999 katika kila kipindi cha miaka 1,000, huondolewa katika chumba cha kutayarishia sinema.” Je, “picha” za matukio ya mwaka mmoja tu zinaweza kutoa habari ya kutosha kuhusu jinsi mageuzi makubwa yalivyotokea? Mabaki ya kale ya wanyama yanaonyesha nini hasa? Niles Eldredge, ambaye ni mwanamageuzi mshupavu anakubali kwamba uchunguzi wa mabaki ya kale ya wanyama umeonyesha kwamba katika vipindi virefu vya wakati “ni mageuzi madogo sana yaliyotukia katika spishi nyingi.”

      Kufikia leo, wanasayansi ulimwenguni pote wamechimbua na kuorodhesha visehemu milioni 200 vikubwa na mabilioni ya visehemu vidogo vya mabaki ya kale ya wanyama. Watafiti wengi wanakubali kwamba mabaki hayo mengi yanaonyesha jamii zote kuu za wanyama zilitokea wakati mmoja na hazijabadilika sana, na spishi nyingi zilitoweka ghafula kama zilivyotokea. Baada ya kuchunguza uthibitisho unaotegemea mabaki hayo, mwanabiolojia Jonathan Wells aliandika: “Wazo la kwamba wanyama wamechimbuka kutoka katika chanzo kimoja huku wakibadilika ikitegemea mazingira si jambo hakika ambalo limethibitishwa kisayansi. Uchunguzi wa mabaki ya kale na wa mifumo midogo iliyo tata ya vitu hai unaonyesha kwamba hiyo si nadharia iliyothibitishwa kabisa.”

      Mageuzi—Ni Jambo Hakika au Ni Hadithi?

      Kwa nini wanamageuzi wengi mashuhuri wanasisitiza kuwa mageuzi makubwa ni hadithi? Baada ya kuchambua baadhi ya sababu alizotoa Richard Dawkins, Richard Lewontin, ambaye ni mwanamageuzi mwenye ushawishi mkubwa aliandika kwamba wanasayansi wengi wako tayari kukubali madai ya kisayansi ambayo hayapatani na akili “kwa sababu tayari tumeazimia kushikamana na nadharia fulani, nadharia ya kwamba vitu halisi ndivyo vitu pekee vya hakika na vitu vyote ulimwenguni, kutia ndani vitu hai vilitokea bila ya msaada wa nguvu fulani zinazozidi zile za asili.” Wanasayansi wengi hukataa hata uwezekano wa kuwa kuna Mbuni mwenye akili. Lewontin anasema, “sisi hatuwezi kamwe kukubali uwezekano wa kwamba kuna Mungu.”

      Kuhusiana na hilo, jarida Scientific American lilimnukuu mwanasosholojia Rodney Stark aliyesema hivi: “Kwa zaidi ya miaka 200 kumekuwa na wazo la kwamba ikiwa unataka kuonekana kuwa mwanasayansi basi hupaswi kuruhusu dini ikupumbaze akili.” Aliongezea kusema kwamba katika vyuo vikuu vya utafiti, “wanadini hufyata midomo yao,” huku “wale ambao si wanadini wakiwabagua.” Kulingana na Stark, “mtu hupata thawabu kwa kutokuwa mwanadini miongoni mwa watu mashuhuri [yaani, wanasayansi].”

      Ikiwa utakubali fundisho la mageuzi makubwa kuwa kweli, utalazimika kuamini kwamba wanasayansi, wanaoamini ya Mungu hayawezi kujulikana na wanaoamini hakuna Mungu, hawataruhusu maoni yao yaathiri kauli zao wanapofanya utafiti. Utalazimika kuamini mabadiliko ya chembe za urithi na uteuzi wa asili ulitokeza vitu vyote tata vyenye uhai, licha ya kwamba utafiti wa karne moja wa kuchunguza mabilioni ya vitu ambavyo chembe zake za urithi zimebadilika, umeonyesha hakuna hata spishi moja ambayo imegeuzwa na kutokeza kitu kipya. Lazima uamini kuwa viumbe vyote viligeuka polepole kutoka kwa kiumbe kimoja, licha ya kwamba mabaki ya kale ya wanyama na mimea inaonyesha aina kuu za mimea na wanyama zilitokea ghafula na hazikubadilika na kuwa aina nyingine, hata baada ya muda mrefu sana kupita. Je, unafikiri imani kama hiyo inategemea mambo hakika? Au, ni hadithi tu?

      [Maelezo ya Chini]

      a Wazalishaji wa mbwa wanaweza kuchagua mbwa watakaozalisha ili wazao wa mbwa hao wawe na miguu mifupi au manyoya marefu kuliko wazazi wao. Hata hivyo, mabadiliko katika mbwa wanaozaliwa mara nyingi hutokana na kasoro katika utendaji wa chembe. Kwa mfano, mbwa anayeitwa dachshund ana umbo dogo kwa sababu tishu zake hazisitawi kwa njia ya kawaida, na hilo humfanya awe mfupi mno.

      b Ijapokuwa neno “spishi” limetumiwa mara nyingi katika makala hii, neno hilo halimo katika Biblia, kwani Biblia inatumia neno “aina” ambalo lina maana pana. Kwa kawaida, kile ambacho wanasayansi hurejelea kuwa badiliko katika spishi ni tofauti zilizopo katika “aina” fulani ya viumbe katika Biblia.

      c Ona sanduku “Kuainishwa kwa Viumbe.”

      d Utafiti unaonyesha kwamba sitoplazimu, tando, na maumbo ya chembe hutimiza fungu muhimu katika sura na utendaji wa kiumbe.

      e Maelezo ya Lönnig katika makala hii ni yake binafsi wala si ya Taasisi ya Max Planck ya Utafiti wa Kuzalisha Mimea.

      f Katika majaribio mengi ya kubadili chembe za urithi, idadi ya viumbe wapya ilizidi kupungua huku aina zilezile za mimea na wanyama zikitokezwa. Hilo lilimfanya Lönnig aanzishe “sheria ya mabadiliko yanayojirudia-rudia.” Isitoshe, chini ya asilimia 1 ya mimea iliyotokezwa kwa kubadili chembe za urithi ilitumiwa katika uchunguzi zaidi, na chini ya asilimia 1 ya mimea hiyo ndiyo ilifaa kwa matumizi ya kibiashara. Matokeo ya utafiti uliohusisha wanyama yalikuwa mabaya sana kuliko yale ya mimea hivi kwamba majaribio hayo yakasimamishwa.

      [Blabu katika ukurasa wa 15]

      “Mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadili spishi za awali [za wanyama na mimea] na kutokeza spishi mpya kabisa”

      [Blabu katika ukurasa wa 16]

      Kauli bora tunayoweza kukata ni kwamba shorewanda wa Darwin wanaonyesha kuwa spishi fulani inaweza kubadilikana kulingana na hali ya hewa

      [Blabu katika ukurasa wa 17]

      Kulingana na mabaki ya kale ya wanyama, jamii zote kuu zilitokea wakati mmoja na hazijabadilika sana

      [Chati katika ukurasa wa 14]

      (Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

      KUAINISHWA KWA VIUMBE

      Viumbe vimeainishwa katika vikundi mbalimbali kuanzia spishi, ambacho ndicho kikundi kidogo zaidi, hadi kikundi kikubwa zaidi kinachoitwa himaya.g Kwa mfano, ona jinsi wanadamu na nzi-tunda wanavyoainishwa hapa chini.

      WANADAMU NZI-TUNDA

      Spishi sapiens melanogaster

      Jenasi Homo Drosofila

      Jamii Hominidi Drosophilids

      Oda Sokwe Diptera

      Tabaka Mamalia Wadudu

      Faila Kodata Arithropoda

      Himaya Wanyama Wanyama

      [Maelezo ya Chini]

      g Taarifa: Mwanzo sura ya 1 inasema mimea na wanyama waliumbwa “kulingana na aina yake.” (Mwanzo 1:12, 21, 24, 25) Hata hivyo, neno “aina” katika Biblia halitumiwi kwa njia hususa na halipaswi kueleweka kuwa na maana sawa na neno “spishi” linalotumiwa katika sayansi.

      [Hisani]

      Chati hii imetolewa kwenye kitabu Icons of Evolution—Science or Myth? Why Much of What We Teach About Evolution Is Wrong, cha Jonathan Wells.

      [Picha katika ukurasa wa 15]

      Nzi-tunda ambaye chembe zake za urithi zilibadilika (juu), bado ni nzi-tunda, ingawa ana kasoro

      [Hisani]

      © Dr. Jeremy Burgess/Photo Researchers, Inc.

      [Picha katika ukurasa wa 15]

      Majaribio ya kubadili chembe za urithi za mimea yalionyesha tena na tena kwamba idadi ya mimea mipya ilipungua sana, huku aina ileile ya mimea iliyobadilika ikitokezwa (Mmea ambao chembe zake za urithi zimebadilishwa una maua makubwa zaidi)

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

      From a Photograph by Mrs. J. M. Cameron/ U.S. National Archives photo

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

      Finch heads: © Dr. Jeremy Burgess/ Photo Researchers, Inc.

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

      Dinosaur: © Pat Canova/Index Stock Imagery; fossils: GOH CHAI HIN/AFP/Getty Images

  • Kwa Nini Tunaamini Kuna Muumba?
    Amkeni!—2006 | Septemba
    • Kwa Nini Tunaamini Kuna Muumba?

      Wataalamu wengi katika nyanja mbalimbali za sayansi wanatambua vitu vilibuniwa kwa akili. Wanaona si jambo linalopatana na akili kuamini kwamba uhai ulio tata sana ulijitokeza wenyewe tu. Hivyo, wanasayansi na watafiti kadhaa wanaamini kuna Muumba.

      Baadhi yao wamekuwa Mashahidi wa Yehova. Wanasadiki kuwa Mungu wa Biblia ndiye Mbuni na Mjenzi wa ulimwengu. Kwa nini wamekata kauli hiyo? Mwandishi wa Amkeni! aliwahoji baadhi yao. Huenda ukapendezwa na majibu waliyotoa.a

      “Utata Usio na Kifani wa Uhai”

      ◼ WOLF-EKKEHARD LÖNNIG

      MAELEZO YAKE: Kwa miaka 28 iliyopita, nimefanya kazi ya sayansi inayohusu mabadiliko ya chembe za urithi za mimea. Nimeajiriwa na Taasisi ya Utafiti wa Kuzalisha Mimea ya Max Planck huko Cologne, Ujerumani, kwa miaka 21 kati ya miaka hiyo 28. Nimekuwa mzee wa kutaniko la Kikristo la Mashahidi wa Yehova kwa miaka 30 hivi.

      Utafiti wangu unaotegemea majaribio na uchunguzi wa chembe za urithi na uchunguzi wangu wa mambo kama vile utendaji na maumbo ya vitu hai, umeniwezesha kutambua utata usio na kifani wa uhai. Kujifunza mambo hayo kumeimarisha usadikisho wangu kwamba uhai umetokana na chanzo chenye akili.

      Wanasayansi wanafahamu vizuri utata wa uhai. Lakini mambo ya hakika kuhusu uhai hufafanuliwa kwa njia inayounga mkono mageuzi. Hata hivyo, kwa maoni yangu, sababu zinazotolewa ili kupinga masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji huvunjwa-vunjwa zinapochunguzwa kisayansi. Nimechunguza sababu hizo kwa makumi ya miaka. Nimechunguza kwa makini vitu vilivyo hai na pia jinsi sheria za asili zinavyoendesha ulimwengu wote, nami sina budi kuamini kuna Muumba.

      “Kila Jambo Ambalo Nimechunguza Lina Kisababishi”

      ◼ BYRON LEON MEADOWS

      MAELEZO YAKE: Ninaishi Marekani na ninafanya kazi katika idara ya fizikia ya miale ya leza ya shirika la NASA. Kwa sasa ninahusika katika mradi wa kiteknolojia wa kuboresha uwezo wa kuchunguza hali ya hewa ya dunia na matukio katika sayari mbalimbali. Mimi ni mzee wa kutaniko la Mashahidi wa Yehova mjini Kilmarnock, Virginia.

      Mara nyingi kazi yangu inahusu sheria za fizikia. Mimi hutafuta visababishi vya mambo fulani na jinsi yanavyotukia. Ninapofanya uchunguzi, ninapata uthibitisho ulio wazi kwamba kila jambo lina kisababishi. Ninaamini kwamba ni jambo linalopatana na sayansi kuamini kuwa Mungu ndiye aliyetokeza vitu vyote. Sheria za asili ni imara sana hivi kwamba sina budi kuamini kuwa ziliwekwa na Msimamizi, yaani, Muumba.

      Ikiwa ni rahisi kukata kauli hiyo, mbona wanasayansi wengi wanaamini mageuzi? Je, huenda ni kwa sababu wanamageuzi hufanya uchunguzi wao huku wakishikilia kauli zao? Hilo si jambo geni miongoni mwa wanasayansi. Lakini si lazima uchunguzi wowote, hata uwe wenye kusadikisha jinsi gani, utokeze matokeo sahihi. Kwa mfano, mtu anayefanya utafiti wa fizikia ya leza anaweza kusisitiza kwamba nuru ni mawimbi, kama vile sauti ilivyo mawimbi, kwa kuwa kwa kawaida nuru hutenda kama mawimbi. Lakini, kauli yake si sahihi kwani uthibitisho pia unaonyesha nuru hutenda kama kikundi cha chembe zinazoitwa fotoni. Hali kadhalika, wale wanaosisitiza kwamba mageuzi ni jambo hakika hawakati kauli kwa msingi wa uthibitisho wote uliopo, na maoni yao kuhusu uthibitisho unaotolewa hutegemea kauli wanazoshikilia.

      Nashindwa kuelewa jinsi mtu anavyoweza kuamini kwamba nadharia ya mageuzi ni jambo hakika ilhali “wataalamu” wa mageuzi hawaafikiani kuhusu jinsi yalivyotokea. Kwa mfano, je, ungeamini hesabu kuwa jambo hakika iwapo mtaalamu fulani angekuambia kwamba 2 ukiongeza 2 ni 4, huku wataalamu wengine wakisema kwamba jumla yake inaaminika kuwa 3 au hata 6? Ikiwa wanasayansi wanapaswa kuamini mambo yanayoweza kuthibitishwa, kuchunguzwa, na kurudiwa, basi nadharia ya kwamba vitu vyote hai vilitokea kwa njia ya mageuzi kutokana na chanzo kimoja si jambo hakika la kisayansi.

      “Kitu Hakiwezi Kutokea Pasipo Kitu Kingine”

      ◼ KENNETH LLOYD TANAKA

      MAELEZO YAKE: Mimi ni mtaalamu wa jiolojia. Kwa sasa nimeajiriwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Jiolojia ya Marekani, iliyoko jijini Flagstaff, Arizona. Kwa miaka 30 hivi, nimetumia wakati mwingi kufanya utafiti katika nyanja mbalimbali za jiolojia, kutia ndani jiolojia ya sayari mbalimbali. Makala zangu nyingi za utafiti na ramani za Mars za jiolojia zimechapishwa katika majarida ya kisayansi yanayoheshimiwa. Nikiwa Shahidi wa Yehova, mimi hutumia saa 70 hivi kila mwezi kuwafundisha watu Biblia.

      Nilifundishwa kuamini mageuzi, lakini singeweza kusadiki kwamba nguvu nyingi iliyohitajiwa ili kutokeza ulimwengu ilijitokeza yenyewe tu pasipo Muumba mwenye nguvu. Kitu hakiwezi kutokea pasipo kitu kingine. Isitoshe nimepata katika Biblia, uthibitisho mzuri kwamba kuna Muumba. Kitabu hicho kina mifano chungu nzima ya mambo hakika ya sayansi yanayohusiana na taaluma yangu. Mfano mmoja ni fundisho lake kwamba dunia ni duara nayo imetundikwa “pasipo na kitu.” (Ayubu 26:7; Isaya 40:22) Mambo hayo ya hakika yaliandikwa katika Biblia muda mrefu kabla wanadamu hawajafaulu kuyachunguza na kuyathibitisha.

      Fikiria jinsi tulivyoumbwa. Sisi tunaweza kujitambua, kuwaza, kuwasiliana, na tuna hisia mbalimbali. Isitoshe, tunaweza kuhisi tunapendwa, kufurahi kwa sababu tunapendwa, na kuwapenda wengine. Nadharia ya mageuzi haiwezi kueleza jinsi wanadamu walivyopata sifa hizo.

      Jiulize, ‘Vyanzo vya habari inayotumiwa kuunga mkono mageuzi ni sahihi na vyenye kutegemeka kadiri gani?’ Habari za kijiolojia si kamili, ni tata, na zenye kukanganya. Wanamageuzi wameshindwa kuthibitisha nadharia zao kuhusu mageuzi kwa kufanya majaribio wakitumia mbinu za kisayansi. Na ingawa wanasayansi hutumia mbinu nzuri kufanya utafiti, mara nyingi wao huongozwa na maoni yao ya ubinafsi wanapofafanua matokeo ya utafiti wao. Inajulikana kwamba wanasayansi hupigia debe maoni yao wakati matokeo ya utafiti yanapopingana au yanapokosa kutoa uthibitisho wa kutosha. Kazi na tamaa yao ya kuheshimiwa ndiyo huwachochea.

      Nikiwa mwanasayansi na mwanafunzi wa Biblia mimi hutafuta kweli kamili, inayopatana na mambo yote ya hakika yajulikanayo na inayopatana pia na matokeo ya utafiti, ili niweze kukata kauli iliyo sahihi zaidi. Ninasadiki kwamba ni jambo linalopatana kabisa na akili kuamini kuna Muumba.

      “Uthibitisho wa Kwamba Chembe Ilibuniwa”

      ◼ PAULA KINCHELOE

      MAELEZO YAKE: Kwa miaka kadhaa nimekuwa nikifanya utafiti wa chembe, biolojia ya molekuli, na mikrobiolojia. Kwa sasa nimeajiriwa na Chuo Kikuu cha Emory, Atlanta, Georgia, Marekani. Pia mimi hujitolea kufundisha Biblia katika eneo fulani la Warusi.

      Kwa miaka minne ya masomo yangu ya biolojia, nilifanya tu utafiti wa chembe na sehemu zake mbalimbali. Kadiri nilivyojifunza kuhusu DNA, RNA, protini, na njia za kuyeyusha chakula, ndivyo nilivyostaajabia utata, utaratibu, na usahihi katika chembe. Na ingawa nilivutiwa na yale ambayo mwanadamu amefaulu kujifunza kuhusu chembe, nilishangazwa hata zaidi kutambua bado kuna mengi sana tusiyoyajua. Ninaamini kuna Mungu kwa sababu kuna uthibitisho kwamba chembe ilibuniwa.

      Kwa kujifunza Biblia nimemfahamu Muumba huyo, yaani, Yehova Mungu. Nasadiki kwamba yeye si Mbuni mwenye akili tu, bali pia Baba mwenye upendo na anayenijali. Biblia inafafanua kusudi la uhai na kutoa taraja la maisha yenye furaha ya wakati ujao.

      Huenda vijana wanaofundishwa mageuzi shuleni wasijue wataamini nini. Wanaweza kuchanganyikiwa sana wakiwa shuleni. Iwapo wanaamini kuna Mungu, imani yao hujaribiwa wanapofundishwa mageuzi. Lakini wanaweza kushinda jaribu hilo kwa kuchunguza vitu vingi vya asili vinavyotuzunguka na kwa kuendelea kupata ujuzi juu ya Mungu na sifa zake. Mimi binafsi nimefanya hivyo na nimekata kauli kwamba masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji ni sahihi na hayapingani na mambo hakika ya sayansi.

      “Sheria Zenye Utaratibu Zilizo Rahisi Sana”

      ◼ ENRIQUE HERNÁNDEZ-LEMUS

      MAELEZO YAKE: Mimi ni mhubiri wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova. Pia mimi ni mtaalamu wa fizikia ya nadharia katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Mexico. Kwa sasa ninafanya utafiti kuhusu ufafanuzi unaofaa wa jinsi joto linavyohusika katika utendaji wa uvutano wa athari ya joto ambao husababisha kupanuka kwa nyota. Pia nimewahi kuchunguza utata wa mifuatano ya DNA.

      Uhai ni tata sana hivi kwamba haungeweza kujitokeza wenyewe. Kwa mfano, fikiria habari chungu nzima iliyo katika molekuli ya DNA. Uwezekano wa kromosomu moja tu kujitokeza ni mdogo kuliko 1 ikigawanywa mara trilioni 9. Uwezekano huo ni mdogo sana hivi kwamba jambo hilo halingewezekana. Nafikiri ni upuuzi kuamini kwamba nguvu fulani isiyo na utu ingeweza kuumba si kromosomu moja tu, bali pia vitu vyote hai vilivyo tata sana na vyenye kustaajabisha.

      Isitoshe, nichunguzapo utendaji wa vitu, kuanzia vitu vidogo visivyoonekana kwa macho hadi mawingu makubwa angani, ninavutiwa na sheria zenye utaratibu zilizo rahisi sana zinazoviongoza. Uhakika huo unanionyesha kwamba aliyeviumba si Mwanahisabati Stadi tu, bali pia ni Msanii Stadi.

      Mara nyingi watu hushangaa ninapowaambia kwamba mimi ni Shahidi wa Yehova. Nyakati nyingine wao huniuliza ninawezaje kuamini kuna Mungu. Ninaelewa kinachowafanya waulize hivyo, kwani dini nyingi haziwahimizi waumini wao watafute uthibitisho wa mambo wanayofundishwa au wafanye utafiti kuhusu imani zao. Hata hivyo, Biblia inatuhimiza tutumie “uwezo wa kufikiri.” (Methali 3:21) Uhakika kwamba vitu vya asili vimebuniwa kwa akili, kutia ndani uthibitisho unaotolewa na Biblia, umenisadikisha kwamba kuna Mungu anayesikiliza sala zetu.

      [Maelezo ya Chini]

      a Maoni ya wataalamu katika makala hii huenda yasipatane na maoni ya waajiri wao.

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]

      Mars in background: Courtesy USGS Astrogeology Research Program, http://astrogeology.usgs.gov

  • Maumbo Yanayovutia ya Mimea
    Amkeni!—2006 | Septemba
    • Maumbo Yanayovutia ya Mimea

      JE, UMEGUNDUA kwamba mimea mingi hukua kwa umbo la mzunguko? Kwa mfano, mananasi yanaweza kuwa na safu 8 za magamba zikielekea upande mmoja huku safu nyingine 5 au 13 zikielekea upande tofauti. (Ona picha ya 1.) Ukitazama mbegu za alizeti unaweza kuona safu 55, 89, au zaidi zinazokua kwa mzunguko. Huenda pia ukaona safu kama hizo kwenye koliflawa. Baada ya kugundua kwamba mimea ina safu hizo, huenda ukavutiwa zaidi na matunda na mboga unapoenda sokoni. Kwa nini mimea huwa na maumbo hayo? Je, idadi ya safu hizo ina umuhimu wowote?

      Mimea Inakuaje?

      Mimea mingi hufanyiza viungo vipya kama vile shina, majani, na maua kutoka kwenye meristemu, ambayo ni sehemu ya mmea iliyo na uwezo wa kujigawanya na kutokeza sehemu mpya. Kila sehemu mpya inayofanyizwa hutokea na kukua kuelekea upande tofauti ikifanyiza pembenukta.a (Ona picha ya 2.) Katika mimea mingi, sehemu mpya hufanyiza pembenukta na hivyo kutokeza safu. Pembenukta hiyo ina ukubwa gani?

      Fikiria tatizo hili: Wazia unabuni ua kwa njia ambayo sehemu zake mpya zitakazotokezwa karibu-karibu kuzunguka kiini cha ukuzi bila kuacha nafasi yoyote kati ya safu. Vipi ukitaka kutokeza sehemu mpya za mmea kwa mzunguko ulio pembenukta yenye ukubwa wa sehemu mbili juu ya tano. Utakabili tatizo kila mara sehemu mpya ya tano inapotokezwa mahali hapohapo na kukua kuelekea upande uleule. Sehemu hizo zingefanyiza safu huku kukiwa na nafasi kubwa kati ya safu hizo. (Ona picha ya 3.) Ukweli ni kwamba, tofauti yoyote ndogo katika ukubwa wa pembenukta ya kila mzunguko hutokeza safu huku kukiwa na nafasi kubwa kati ya safu. “Pembenukta bora” iliyo digrii 137.5 hivi ndiyo inayotokeza safu zinazokaribiana zaidi. (Ona picha ya 5.) Ni nini kinachofanya pembenukta hiyo iwe ya pekee sana?

      Pembenukta hiyo bora inafaa kwa sababu haiwezi kusababisha badiliko katika sehemu ndogo ya mzunguko. Pembenukta yenye ukubwa wa 5/8 wa mzunguko inaikaribia sana hiyo pembenukta bora, 8/13 inaikaribia hata zaidi, nayo 13/21 inaikaribia kwa ukaribu zaidi. Hata hivyo, hakuna pembenukta nyingine inayoweza kutokeza mzunguko wa safu unaofaa kabisa. Hivyo, sehemu mpya ya mmea inapotokezwa ikiwa kwenye pembenukta ya digrii 137.5 hivi kutoka kwa sehemu iliyoitangulia, hakuna sehemu mbili za mmea zitakazokua kuelekea upande uleule mmoja. (Ona picha ya 4.) Hivyo, badala ya kutokeza umbo lililo sawa na miale ya nuru kutoka chanzo kimoja, sehemu hizo mpya za mmea hufanyiza safu zinazozungukana.

      Kwa kushangaza, picha za kompyuta za sehemu za mimea zinazokua kutoka katika kiini kimoja, zinaweza kuonyesha safu hizo za mzunguko ikiwa tu ukubwa wa pembenukta kati ya kila sehemu mpya ni sahihi kabisa. Ukubwa wa pembenukta ukitofautiana hata kwa asilimia kumi na pembenukta bora, safu hazitapangika ifaavyo.—Ona picha ya 5.

      Ua Lina Petali Ngapi?

      Inapendeza kwamba kwa kawaida idadi ya safu zinazotokana na pembenukta yenye ukubwa wa digrii 137.5 ni idadi inayopatana na mfumo wa nambari unaoitwa Fibonacci. Mfumo huo ulifafanuliwa kwanza katika karne ya 13 na mwanahisabati Mwitaliano aliyeitwa Leonardo Fibonacci. Katika mfumo huo, baada ya nambari 1 kila nambari inayofuata inalingana na jumla ya nambari mbili zinazoitangulia.—1, 1, 2, 3, 5, 8, 13, 21, 34, 55, na kuendelea.

      Maua ya mimea mingi inayofanyiza safu huwa na idadi ya petali inayopatana na mfumo wa nambari wa Fibonacci. Kulingana na wataalamu fulani, kombetindi huwa na petali 5, bloodroots petali 8, fireweeds petali 13, asta petali 21, aina fulani ya daisy petali 34, na Michaelmas daisy petali 55 au 89. (Ona picha ya 6.) Mara nyingi, matunda na mboga huwa na umbo linalopatana na mfumo wa nambari wa Fibonacci. Kwa mfano, ndizi huwa na sehemu-mkato yenye pande tano.

      “Amefanya Kila Kitu Kiwe Chenye Kupendeza”

      Kwa muda mrefu wasanii wamejua kwamba kiwango bora ndicho kinachotuvutia zaidi. Ni nini kinachofanya sehemu mpya ya mimea ikue kwa usahihi katika pembenukta bora? Watu wengi wanakata kauli kwamba huo ni uthibitisho mwingine kwamba vitu hai vilibuniwa na mtu mwenye akili.

      Kutafakari jinsi ambavyo vitu hai vilibuniwa na jinsi vinavyofurahisha watu, kumewafanya wengi waamini kwamba kuna Muumba anayetaka tufurahie maisha. Biblia inasema hivi kumhusu Muumba wetu: “Amefanya kila kitu kiwe chenye kupendeza kwa wakati wake.”—Mhubiri 3:11.

      [Maelezo ya Chini]

      a Inashangaza kwamba, alizeti ni mmea ulio tofauti kwani maua yake madogo ambayo hubadilika na kuwa mbegu, huanza kufanyiza safu kuanzia sehemu ya nje ya ua la alizeti badala ya sehemu yake ya katikati.

      [Picha katika ukurasa wa 24, 25]

      Picha ya 1

      (See publication)

      Picha ya 2

      (See publication)

      Picha ya 3

      (See publication)

      Picha ya 4

      (See publication)

      Picha ya 5

      (See publication)

      Picha ya 6

      (See publication)

      [Picha katika ukurasa wa 24]

      Picha ya meristemu

      [Hisani]

      R. Rutishauser, University of Zurich, Switzerland

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

      White flower: Thomas G. Barnes @ USDA-NRCS PLANTS Database

  • Je, Unayoamini Ni Muhimu?
    Amkeni!—2006 | Septemba
    • Je, Unayoamini Ni Muhimu?

      JE, UNAFIKIRI uhai una kusudi? Ikiwa fundisho la mageuzi lingekuwa la kweli basi taarifa hii iliyonukuliwa katika jarida Scientific American ingekuwa sahihi: “Ufahamu wetu wa sasa kuhusu mageuzi unadokeza . . . kwamba uhai hauna kusudi halisi.”

      Maneno hayo yanamaanisha nini? Ikiwa uhai hauna kusudi halisi, basi hauna kusudi lingine maishani ila tu kujaribu kutenda mema na, labda, kupitisha chembe zako za urithi kwa kizazi kinachofuata. Ukifa utakoma kuwako. Ubongo wako, pamoja na uwezo wake wa kuwaza, kufikiri, na kutafakari kuhusu kusudi la uhai ungekuwa tu umetokea bila mpango.

      Lakini si hayo tu. Wengi wanaoamini mageuzi hudai kwamba hakuna Mungu au kwamba hataingilia mambo ya wanadamu. Vyovyote vile, wakati wetu ujao ungekuwa mikononi mwa wanasiasa, wasomi, na viongozi wa kidini. Matukio ya wakati uliopita yanaonyesha kwamba michafuko, mizozo, na ufisadi ambao umekithiri katika jamii ungeendelea. Ikiwa fundisho la mageuzi lingekuwa la kweli, yaelekea ingefaa kuishi kupatana na kauli hii ya watu wasiokuwa na tumaini: “Na tule na tunywe, kwa maana kesho tutakufa.”—1 Wakorintho 15:32.

      Uwe na uhakika huu. Mashahidi wa Yehova hawakubaliani na maoni hayo yote. Wala hawakubaliani na fundisho la mageuzi ambalo ndilo msingi wa maoni hayo. Kinyume na hilo, Mashahidi wanaamini kwamba Biblia ni ya kweli. (Yohana 17:17) Kwa hiyo wanaamini kile ambacho Biblia inasema kuhusu wanadamu walivyotokea: “Kwako wewe iko chemchemi ya uzima.” (Zaburi 36:9) Maneno hayo yana maana kubwa.

      Uhai una kusudi. Muumba wetu ana kusudi lenye upendo kuwaelekea watu wote wanaochagua kufanya mapenzi yake. (Mhubiri 12:13) Kusudi hilo linatia ndani ahadi ya kuishi katika ulimwengu usiokuwa na michafuko, mizozo, ufisadi, na hata kifo. (Isaya 2:4; 25:6-8) Mamilioni ya Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanaweza kuthibitisha kwamba kujifunza kumhusu Mungu na kufanya mapenzi yake humpa mtu kusudi maishani, kusudi ambalo hawezi kupata mahali pengine popote!—Yohana 17:3.

      Kile unachoamini ni muhimu kwani kinaweza kuathiri furaha yako ya sasa na maisha yako ya wakati ujao. Chaguo ni lako. Je, utaamini nadharia ambayo imeshindwa kutupa sababu thabiti ya kupuuza uthibitisho mwingi uliopo kwamba ulimwengu ulibuniwa? Au utakubaliana na yale ambayo Biblia husema, yaani, ulimwengu na uhai ulitokezwa na Mbuni mwenye kustaajabisha, Yehova, Mungu ‘aliyeumba vitu vyote’?—Ufunuo 4:11.

  • Je, Sayansi Inapingana na Masimulizi ya Mwanzo?
    Amkeni!—2006 | Septemba
    • Maoni ya Biblia

      Je, Sayansi Inapingana na Masimulizi ya Mwanzo?

      WATU wengi hudai kwamba sayansi inapinga masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji. Lakini, sayansi haipingani na Biblia bali inapingana na maoni ya Wakristo wenye imani kali. Baadhi ya Wakristo hao husisitiza kwa uwongo kwamba, kulingana na Biblia, vitu vyote vinavyoonekana viliumbwa katika kipindi cha siku sita zenye urefu wa saa 24 kila moja, yapata miaka 10,000 hivi iliyopita.

      Hata hivyo, Biblia haiungi mkono fundisho hilo. Iwapo ingefanya hivyo, uvumbuzi mwingi wa kisayansi, ambao umefanywa katika muda wa miaka mia moja iliyopita, ungefanya Biblia itiliwe shaka. Kuchunguza Biblia kwa makini kumethibitisha kwamba mambo hakika ya sayansi hayapingani na Biblia. Kwa sababu hiyo, Mashahidi wa Yehova hawakubaliani na “Wakristo” wenye imani kali wala wanauumbaji, yaani, watu wanaodai kwamba vitu vyote vinavyoonekana viliumbwa katika kipindi cha siku sita zenye urefu wa saa 24 kila moja, yapata miaka 10,000 hivi iliyopita. Habari ifuatayo inaonyesha kile ambacho Biblia inafundisha hasa.

      “Mwanzo” Ulikuwa Lini?

      Masimulizi ya Mwanzo yanaanza kwa taarifa hii fupi yenye nguvu: “Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.” (Mwanzo 1:1) Wasomi wa Biblia wanakubali kwamba taarifa hiyo inafafanua jambo tofauti na matukio yaliyotendeka katika zile siku sita za uumbaji. Matukio hayo yanasimuliwa kuanzia mstari wa 3 na kuendelea. Hilo ni jambo muhimu sana. Kulingana na taarifa ya ufunguzi ya Biblia, ulimwengu wote, kutia ndani Dunia, ulikuwapo kwa kipindi kisichojulikana kabla ya zile siku sita za uumbaji.

      Wanajiolojia wanakadiria kwamba dunia imekuwapo kwa miaka bilioni 4, nao wanaanga wanasema huenda ulimwengu umekuwapo kwa miaka bilioni 15. Je, kauli hizo, au marekebisho yoyote ya ufahamu wetu kuhusu muda ambao ulimwengu, kutia ndani dunia, umekuwapo, zinapingana na Mwanzo 1:1? La. Biblia haisemi chochote kuhusu muda ambao “mbingu na dunia” zimekuwapo. Sayansi haipingi masimulizi ya Biblia.

      Siku za Uumbaji Zilikuwa na Urefu Gani?

      Vipi zile siku za uumbaji? Je, zilikuwa siku halisi zenye urefu wa saa 24 kila moja? Watu fulani hudai kwamba kwa kuwa Musa—aliyeandika kitabu cha Mwanzo—alirejelea siku iliyofuata siku sita za uumbaji kuwa mfano wa Sabato ya kila juma, lazima kila mojawapo ya siku hizo za uumbaji iwe ilikuwa na urefu wa saa 24. (Kutoka 20:11) Je, maneno ya Mwanzo yanaunga mkono kauli hiyo?

      La hasha. Ukweli ni kwamba, neno la Kiebrania linalotafsiriwa “siku” halimaanishi tu kipindi cha saa 24, bali pia linamaanisha vipindi vya wakati vyenye urefu tofauti. Kwa mfano, akieleza kwa ufupi kazi ya Mungu ya uumbaji, Musa anarejelea kipindi hicho cha siku sita kuwa siku moja tu. (Mwanzo 2:4) Bila shaka, hatuna msingi wowote wa Kimaandiko wa kukata kauli kwamba kila mojawapo ya siku za uumbaji ilikuwa na urefu wa saa 24.

      Hivyo basi, siku hizo zilikuwa na urefu gani? Maneno ya Mwanzo sura ya 1 na ya 2 yanaonyesha zilikuwa vipindi virefu sana vya wakati.

      Viumbe Vyatokea Hatua kwa Hatua

      Musa aliandika masimulizi yake katika Kiebrania, naye alisimulia mambo kama mtu ambaye yuko duniani. Mambo hayo mawili, kutia ndani uhakika wa kwamba ulimwengu wote ulikuwapo kabla ya zile “siku” za uumbaji, hujibu maswali mengi ambayo yamezushwa kuhusu masimulizi ya uumbaji. Jinsi gani?

      Uchunguzi makini wa masimulizi ya Mwanzo unaonyesha kwamba matukio yanayoanza katika “siku” fulani yanaendelea kutukia siku moja au siku kadhaa zinazofuata. Kwa mfano, kabla ya “siku” ya kwanza, nuru ya jua, ambalo tayari lilikuwapo, ilizuiwa kwa njia fulani isiupige uso wa dunia. Labda ilikuwa ikizuiwa na mawingu mazito. (Ayubu 38:9) Kizuizi hicho kilianza kuondoka katika “siku” ya kwanza, na hivyo kuruhusu nuru ipenye kwenye anga la dunia.a

      Katika “siku” ya pili, anga lilizidi kuwa wazi, na hivyo kukawa na nafasi kati ya mawingu mazito yaliyokuwa juu na bahari iliyokuwa chini. Katika “siku” ya nne, anga lilikuwa wazi kabisa hatua kwa hatua hivi kwamba jua na mwezi zilionekana “katika anga la mbingu.” (Mwanzo 1:14-16) Kwa maneno mengine, mtu aliye duniani angeweza kuona jua na mwezi. Yote hayo yalitukia hatua kwa hatua.

      Masimulizi ya Mwanzo yanataja pia kwamba anga lilizidi kuwa wazi, kisha viumbe wanaoruka—kutia ndani wadudu na viumbe wengine wenye mabawa—wakaanza kutokea katika “siku” ya tano. Hata hivyo, Biblia inaonyesha kwamba katika “siku” ya sita, bado Mungu alikuwa “akifanya kutoka katika udongo kila mnyama wa mwituni na kila kiumbe kinachoruka cha mbinguni.”—Mwanzo 2:19.

      Kwa wazi, maneno ya Biblia, yanaonyesha kwamba kuna uwezekano matukio fulani muhimu ya kila “siku” au kipindi cha uumbaji hayakutendeka mara moja bali yalitendeka hatua kwa hatua. Baadhi ya matukio hayo huenda hata yaliendelea hadi “siku” ya uumbaji iliyofuata.

      Kulingana na Aina Yake

      Je, uhakika wa kwamba mimea na wanyama walitokezwa hatua kwa hatua unamaanisha Mungu alitumia mageuzi kutokeza aina mbalimbali za vitu hai? La. Masimulizi hayo yanataja waziwazi kwamba Mungu aliumba “aina” zote za msingi za mimea na wanyama. (Mwanzo 1:11, 12, 20-25) Je, “aina” hizo za awali zilipewa uwezo wa kiasili wa kubadilika kulingana na mazingira? Kila “aina” ina mipaka gani ya kiasili? Biblia haisemi chochote kuhusu jambo hilo pia. Hata hivyo, inasema viumbe hai ‘walijaa kulingana na aina zake.’ (Mwanzo 1:21) Taarifa hiyo inamaanisha kwamba kulikuwa na mipaka ya kiasili iliyodhibiti tofauti za viumbe katika kila “aina.” Uchunguzi wa mabaki ya kale ya mimea na wanyama na pia utafiti wa karibuni, unaunga mkono kauli ya kwamba aina za msingi za mimea na wanyama zimebadilika kidogo katika kipindi kirefu sana cha wakati.

      Kinyume na madai ya watu fulani, kitabu cha Mwanzo hakifundishi kwamba ulimwengu, kutia ndani dunia na viumbe hai vilivyomo, viliumbwa katika kipindi kifupi cha wakati, muda usio mrefu sana uliopita. Badala yake, masimulizi ya Mwanzo kuhusu kuumbwa kwa ulimwengu na vitu hai duniani yanapatana na uvumbuzi wa karibuni wa kisayansi.

      Imani za kifalsafa za wanasayansi wengi huwafanya wapinge fundisho la Biblia kwamba Mungu aliumba vitu vyote. Hata hivyo, inapendeza kwamba, katika kitabu cha Biblia cha Mwanzo kilichoandikwa zamani, Musa aliandika kuwa ulimwengu ulikuwa na mwanzo na uhai ulitokea hatua kwa hatua, katika vipindi vya wakati. Musa angewezaje kupata habari hizo zilizo sahihi kisayansi yapata miaka 3,500 hivi iliyopita? Kuna jibu moja tu linalopatana na akili. Yule aliye na nguvu na hekima ya kuumba mbingu na dunia angeweza kwa hakika kumpa Musa habari hizo zilizo sahihi kisayansi. Jibu hilo linaunga mkono dai la Biblia kwamba ‘imeongozwa na roho ya Mungu.’—2 Timotheo 3:16.

      JE, UMEJIULIZA HIVI?

      ◼ Mungu aliumba ulimwengu kitambo gani?—Mwanzo 1:1.

      ◼ Dunia iliumbwa katika kipindi cha siku sita zenye urefu wa saa 24 kila moja?—Mwanzo 2:4.

      ◼ Masimulizi ya Musa kuhusu mwanzo wa dunia yanawezaje kuwa sahihi kisayansi?—2 Timotheo 3:16.

      [Maelezo ya Chini]

      a Katika masimulizi ya matukio ya “siku” ya kwanza, neno la Kiebrania linalotafsiriwa nuru ni ʼohr, lakini kuhusu “siku” ya nne, neno linalotumiwa ni ma·ʼohrʹ, linalomaanisha vyanzo vya nuru.

      [Blabu katika ukurasa wa 19]

      Kitabu cha Mwanzo hakifundishi kwamba ulimwengu uliumbwa katika kipindi kifupi cha wakati miaka kadhaa iliyopita

      [Blabu katika ukurasa wa 20]

      “Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.”—Mwanzo 1:1

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

      Universe: IAC/RGO/David Malin Images

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]

      NASA photo

  • Ninaweza Kuiteteaje Imani Yangu Katika Uumbaji?
    Amkeni!—2006 | Septemba
    • Vijana Huuliza . . .

      Ninaweza Kuiteteaje Imani Yangu Katika Uumbaji?

      “Suala la mageuzi lilipoanza kujadiliwa darasani lilikuwa tofauti na kila kitu nilichokuwa nimefundishwa. Lilifundishwa kama jambo hakika na hilo liliniogopesha.” —Ryan, 18.

      “Nilikuwa na miaka 12 hivi, na mwalimu wangu alishikilia sana fundisho la mageuzi. Hata aliweka alama ya Darwin kwenye gari lake! Hilo lilinifanya nisite kuzungumza kwa uhuru kuhusu imani yangu katika uumbaji.”—Tyler, 19.

      “Mwalimu wangu wa somo la elimu ya jamii aliposema kwamba tutazungumzia mageuzi katika somo ambalo lingefuata niliogopa sana. Nilijua kwamba itanibidi kuwaelezea wanafunzi wenzangu kuhusu msimamo wangu juu ya suala hilo lenye kubishaniwa.”—Raquel, 14.

      LABDA kama vile Ryan, Tyler, na Raquel, wewe huingiwa na wasiwasi somo la mageuzi linapofundishwa darasani. Unaamini kwamba Mungu “aliumba vitu vyote.” (Ufunuo 4:11) Unaona uthibitisho wa kwamba vitu vyote viliumbwa na mbuni mwenye akili. Lakini vitabu vya mafunzo na vilevile walimu husema kwamba tulitokea kwa mageuzi. Wewe ni nani hata ushindane na “wataalamu”? Na wanafunzi wenzako watatendaje ukianza kuzungumza juu ya . . . Mungu?

      Tulia, maswali kama hayo yasikubabaishe! Si wewe tu unayeamini uumbaji. Ukweli ni kwamba hata idadi kubwa ya wanasayansi hawakubaliani na nadharia ya mageuzi. Pia walimu wengi hawaiamini. Haidhuru vitabu vya mafunzo vinasema nini, wanafunzi 4 kati ya 5 huko Marekani wanaamini kwamba kuna Muumba!

      Hata hivyo, huenda ukajiuliza, ‘Ninaweza kusema nini ili kutetea imani yangu katika uumbaji?’ Uwe na hakika kwamba ujapokuwa na woga, bado unaweza kueleza msimamo wako kwa uthabiti. Hata hivyo, utahitaji kujitayarisha.

      Chunguza Yale Unayoamini!

      Ikiwa umelelewa na wazazi Wakristo, huenda unaamini uumbaji kwa sababu tu umefundishwa hivyo. Lakini sasa una umri mkubwa na unataka kumwabudu Mungu kwa kutumia ‘nguvu zako za kufikiri,’ ukiwa na msingi thabiti wa yale unayoamini. (Waroma 12:1) Paulo aliwatia moyo Wakristo wa karne ya kwanza ‘wahakikishe mambo yote.’ (1 Wathesalonike 5:21) Unaweza kuthibitishaje imani yako katika uumbaji?

      Kwanza ona kile ambacho Paulo aliandika kuhusu Mungu: “Sifa zake ambazo hazionekani, zinaonekana waziwazi tangu kuumbwa kwa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zinaeleweka kwa vitu vilivyofanywa.” (Waroma 1:20) Ukiwa na wazo hilo fikiria mwili wa binadamu, dunia, anga, na kina cha bahari. Chunguza ulimwengu wa ajabu wa wadudu, mimea, na wanyama au jambo lolote linalokuvutia. Halafu kwa kutumia “nguvu zako za kufikiri,” tafakari swali hili, ‘Ni nini kinachonithibitishia kwamba kuna Muumba?’

      Ili kujibu swali hilo, Sam mwenye umri wa miaka 14 anatoa mfano wa mwili wa binadamu. Anasema kwamba mwili wa binadamu “umeumbwa vizuri na ni tata sana, sehemu zake zote zinafanya kazi pamoja vizuri. Mwili wa binadamu haungeweza kujitokeza kwa mageuzi!” Holly mwenye miaka 16, anakubaliana na hilo. Anasema, “tangu ilipogunduliwa kwamba nina kisukari, nimejifunza mengi kuhusu jinsi mwili unavyofanya kazi. Kwa mfano, inashangaza jinsi kongosho ambacho ni kiungo kidogo kinachopatikana sehemu ya nyuma ya tumbo kinavyofanya kazi kubwa ya kusaidia damu na viungo vingine kufanya kazi.”

      Vijana wengine wana maoni tofauti kuhusu suala hilo. Jared mwenye miaka 19 anasema hivi, “kwangu uthibitisho wenye nguvu unahusiana na ukweli wa kwamba tuna hamu ya mambo ya kiroho, tunapendezwa na mambo yenye kuvutia na tuna tamaa ya kujifunza. Hatuhitaji sifa hizo ili tuendelee kuwa hai, kama wanamageuzi wanavyotaka tuamini. Ufafanuzi pekee ambao ninahisi unapatana na akili ni huu, kwamba tumewekwa hapa na mtu ambaye alitaka tufurahie uhai.” Tyler, aliyetajwa mwanzoni amekata kauli kama hiyo. “Ninapofikiria jinsi mimea inavyotegemeza uhai na pia jinsi ilivyoundwa kwa njia tata yenye kustaajabisha, ninasadikishwa kwamba kuna Muumba.”

      Ni rahisi kutetea uumbaji ikiwa umetafakari fundisho hilo vizuri na kusadikishwa. Kwa hiyo, kama vile Sam, Holly, Jared, na Tyler, tumia wakati kufikiria vitu ambavyo Mungu ameumba. Kisha “sikiliza” yale ambayo vitu hivyo “vinakuambia.” Bila shaka utakata kauli ileile ambayo mtume Paulo aliikata, kwamba vitu hivyo vinathibitisha kuna Mungu na pia vinafunua sifa zake ambazo “zinaeleweka kwa vitu vilivyofanywa.”a

      Fahamu Kile Ambacho Biblia Inafundisha Hasa

      Ili utetee fundisho la uumbaji unapaswa kuchunguza vitu ambavyo Mungu ameumba na pia kufahamu kile ambacho Biblia inafundisha hasa kuhusiana na suala hilo. Hakuna sababu nzuri ya kubishana kuhusu mambo ambayo Biblia haitaji moja kwa moja. Fikiria mifano kadhaa.

      ◼ Kitabu changu cha sayansi kinasema kwamba dunia na mfumo wa jua vimekuwapo kwa mabilioni ya miaka. Biblia haisemi chochote kuhusu muda ambao dunia au mfumo wa jua umekuwapo. Kwa hakika, kulingana na masimulizi ya Biblia huenda ulimwengu ulikuwapo mabilioni ya miaka kabla ya “siku” ya kwanza ya uumbaji kuanza.—Mwanzo 1:1, 2.

      ◼ Mwalimu wangu anasema kwamba dunia haingeweza kuumbwa kwa siku sita tu. Biblia haisemi kwamba kila mojawapo ya “siku” sita za uumbaji ilikuwa na urefu wa saa 24. Kwa habari zaidi ona ukurasa wa 18-20 wa gazeti hili.

      ◼ Darasani tulizungumzia mifano kadhaa kuhusu jinsi wanyama na wanadamu wamebadilika kadiri ambavyo muda umepita. Biblia inasema kwamba Mungu aliumba kila kitu “kulingana na aina yake.” (Mwanzo 1:20, 21) Biblia haiungi mkono wazo la kwamba vitu hai vilitokana na vitu visivyo na uhai au kwamba Mungu alianzisha hatua za mageuzi kwa kuumba chembe moja tu. Hata hivyo, kila “aina” ina uwezo mkubwa wa kutokeza viumbe wenye sifa tofauti-tofauti. Hivyo masimulizi ya Biblia yanapatana na wazo la kwamba mabadiliko yanaweza kutokea katika kila “aina.”

      Shikilia Imani Yako kwa Uhakika!

      Huna sababu ya kuaibika kwa sababu unaamini uumbaji. Kwa kutegemea uthibitisho uliopo, ni jambo linalopatana kabisa na akili, naam la kisayansi, kusadiki kwamba tuliumbwa na mbuni mwenye akili. Kwa ujumla fundisho la mageuzi, wala si la uumbaji, ndilo linalomtaka mtu awe na imani kubwa isiyo na msingi na linalohitaji mtu aamini kwamba miujiza hutukia bila mfanya-miujiza. Bila shaka, baada ya kusoma makala mbalimbali za toleo hili la Amkeni! hapana shaka utasadikishwa kwamba uthibitisho unaunga mkono uumbaji. Na baada ya kufikiria jambo hilo kwa uzito ukitumia nguvu zako za kufikiri, utaweza kutetea imani yako kwa uhakika zaidi darasani.

      Hilo ndilo jambo ambalo Raquel aliyetajwa mwanzoni aligundua. Anasema hivi: “Ilinichukua siku kadhaa kutambua kwamba ninapaswa kuwaeleza wengine mambo ninayoamini. Nilimpa mwalimu wangu kitabu Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation? ambacho nilikuwa nimekiweka alama katika sehemu nilizotaka asome. Baadaye, aliniambia kwamba kitabu hicho kilimpa maoni mapya kabisa kuhusu mageuzi na kwamba wakati ujao atazingatia habari hiyo anapofundisha somo la mageuzi!”

      [Maelezo ya Chini]

      a Vijana wengi wamenufaika kwa kusoma habari iliyo katika vitabu kama vile Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation? na Je, Kuna Muumba Anayekujali? Vitabu hivyo viwili vimechapishwa na Mashahidi wa Yehova.

      MAMBO YA KUFIKIRIA

      ◼ Ni zipi baadhi ya njia rahisi unazoweza kueleza imani yako katika uumbaji unapokuwa shuleni?

      ◼ Unaweza kuonyeshaje uthamini wako kwa ajili ya Yule aliyeuumba vitu vyote?—Matendo 17:26, 27.

      [Sanduku katika ukurasa wa 27]

      “KUNA UTHIBITISHO MWINGI SANA”

      “Ungemwambia nini kijana aliyefundishwa tangu utotoni kwamba kuna Muumba lakini sasa anafundishwa mageuzi shuleni?” Mtaalamu wa mikrobiolojia ambaye ni Shahidi wa Yehova aliulizwa swali hilo. Alijibuje? “Unapaswa kuiona kuwa nafasi ya kujithibitishia kuwa kuna Mungu, si kwa sababu tu ulifundishwa hivyo na wazazi wako, bali kwa sababu umejichunguzia uthibitisho na kukata kauli yako mwenyewe. Nyakati nyingine walimu wanapoombwa ‘wathibitishe’ fundisho la mageuzi, wao hushindwa kufanya hivyo, nao hutambua kwamba wanaamini fundisho hilo kwa sababu tu wamefundishwa hivyo. Tunaweza kunaswa na mtego huohuo kuhusiana na imani ya kwamba kuna Muumba. Hiyo ndiyo sababu ni jambo muhimu sana ujithibitishie kwamba kweli kuna Mungu. Kuna uthibitisho mwingi sana. Si vigumu kuupata.”

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 28]

      NI NINI KINACHOKUSADIKISHA?

      Andika hapa chini mambo matatu yanayokusadikishia kwamba kuna Muumba:

      1. ․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․

      2. ․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․

      3. ․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki