JINSI MICHANGO YAKO INAVYOTUMIWA
Kituo cha Satelaiti cha JW Kinachofika Maeneo Ambapo Intaneti Haifiki
APRILI 1, 2021
Kila mwezi tunatazamia kwa hamu programu za kiroho na video zinazotolewa katika JW Broadcasting. Hata hivyo, ndugu zetu wengi barani Afrika hawawezi kupata programu hizo kupitia Intaneti. Kwa nini?
Sehemu kubwa ya bara la Afrika haina huduma ya Intaneti. Na katika maeneo ambayo Intaneti inapatikana, mara nyingi haishiki vizuri au ni ghali sana. Kwa mfano, pindi moja mwangalizi wa mzunguko nchini Madagaska alipakua programu ya JW Broadcasting katika duka linalotoa huduma za Intaneti. Alilipia dola 16, pesa ambazo zinazidi mshahara wa watu fulani wa juma zima nchini humo!a
Licha ya changamoto hizo, mamilioni ya watu barani Afrika sasa wanaweza kufurahia kutazama JW Broadcasting bila kutumia Intaneti. Jinsi gani?
Tangu mwaka wa 2017, JW Broadcasting imeanza kupatikana kwa watu wanaoishi Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia kituo cha satelaiti. Kituo hicho hutoa matangazo yake bila malipo, saa 24 kila siku katika lugha 16.
Ndugu nchini Msumbiji wakirekebisha kifaa kinachotumika kupokea matangazo ya kituo cha satelaiti cha JW kwenye Jumba la Ufalme, 2018
Ili kutimiza hilo, Mashahidi wa Yehova waliandikisha mkataba na kituo cha televisheni ili kupeperusha matangazo yake kupitia satelaiti. Satelaiti hiyo inapeperusha matangazo katika nchi zaidi ya 35 zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Mkataba huo unagharimu zaidi ya dola 12,000 kwa mwezi. Mara kwa mara, gharama za ziada hulipwa ili kupeperusha matukio ya moja kwa moja katika kituo tofauti. Kufanya hivyo huwezesha maelfu ya watu kufurahia makusanyiko au programu za pekee zinazotia ndani ziara za wawakilishi wa makao makuu.
Washiriki wa kikundi cha Usanifu-Majengo na Ujenzi nchini Malawi wakitazama kituo cha satelaiti cha JW, 2018
Watu wengi, kutia ndani wale ambao si Mashahidi, hutazama kituo cha satelaiti cha JW kupitia televisheni zao nyumbani. Hata hivyo, baadhi ya ndugu zetu hawana uwezo wa kununua vifaa vinavyohitajika ili kutazama kituo hicho cha satelaiti. Ili kuwasaidia, vifaa hivyo viliwekwa katika Majumba 3,670 ya Ufalme ili ndugu na dada waweze kutazama JW Broadcasting. Kifaa hicho, pamoja na usafirishaji hugharimu dola 70 hivi ikiwa Jumba la Ufalme tayari lina televisheni au projekta. Vinginevyo, vifaa vyote vinaweza kugharimu zaidi ya dola 530.
Ndugu na dada zetu wanathamini sana kituo hicho. Mzee mmoja nchini Kamerun anasema hivi: “Familia yetu inaona kituo hicho sawa na mana jangwani.” Ndugu nchini Nigeria anayeitwa Odebode anasema hivi: “Tukiwa familia sisi hutazama kituo hicho mara tatu kila juma. Watoto wangu hutazamia kwa hamu pindi hizo. Pindi nyingine hata wanaomba tubadili vituo vingine ili watazame kituo cha JW.” Rose, anayeishi pia Nigeria, anasema hivi: “Ninafurahi kusema kwamba kituo cha JW kimechukua nafasi ya vituo vya habari nilivyopenda sana kutazama. Nilipotazama habari, nilikasirishwa haraka na mambo niliyoona na shinikizo langu la damu lingepanda. Hata hivyo, kituo cha JW Broadcasting kinajenga na kumfanya mtu atulie! Ni kituo ninachokipenda sana. Ni baraka kubwa kutoka kwa Yehova.”
Familia nchini Malawi ikitazama video za watoto kupitia kituo chetu cha satelaiti
Mwangalizi wa mzunguko nchini Msumbiji anasema kwamba katika mzunguko wake, vifaa vinavyopokea matangazo ya kituo cha satelaiti vimewekwa katika Majumba ya Ufalme. Ndugu katika makutaniko hayo hufika saa moja au zaidi kabla ya mkutano ili kutazama JW Broadcasting kupitia satelaiti.
Kutaniko hili nchini Ethiopia lilifurahia kutazama programu ya kila mwezi ya JW Broadcasting bila kutumia Intaneti, 2018
Wakati wa kusanyiko la kimataifa la 2019 katika jiji la Johannesburg, Afrika Kusini, kituo hicho kilitumiwa kupeperusha hotuba mbalimbali katika maeneo mengine tisa, kutia ndani zile zilizotolewa na mshiriki wa Baraza Linaloongoza. Sphumelele, anayetumikia katika Idara ya Utangazaji ya ofisi ya tawi nchini Afrika Kusini anasema hivi: “Zamani tungepeperusha hotuba hizo kupitia Intaneti. Hivyo tulihitaji kuwa na mtandao mzuri wa Intaneti na kulipia gharama za mtandao. Kituo cha satelaiti cha JW kina gharama nafuu zaidi na kinategemeka.”
Kupitia michango yenu ya ukarimu kuelekea kazi ya ulimwenguni pote, ndugu na dada zetu wengi barani Afrika wanaweza kutazama JW Broadcasting kupitia satelaiti. Tunathamini sana michango yenu mliyotoa kupitia njia mbalimbali zinazotajwa kwenye donate.jw.org.
a Dola zinazotajwa katika makala hii ni za Marekani.