Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • wp21 Na. 3 kur. 6-8
  • Je, Elimu ya Juu na Pesa Zitakuhakikishia Maisha Bora ya Wakati Ujao?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Elimu ya Juu na Pesa Zitakuhakikishia Maisha Bora ya Wakati Ujao?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2021
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • UAMUZI AMBAO WATU WENGI WANAFANYA
  • MATOKEO NI NINI?
  • Mashahidi wa Yehova Wana Maoni Gani Kuhusu Elimu?
    Maswali Yanayoulizwa Mara Nyingi Kuhusu Mashahidi wa Yehova
  • Elimu—Gharama Yake? Faida Yake
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1982
  • Wazazi, Mnataka Watoto Wenu Wawe na Maisha ya Aina Gani Wakati Ujao?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
  • Kutafuta Maisha Yenye Usalama
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2021
wp21 Na. 3 kur. 6-8
Wasichana wawili wa chuo kikuu wakitembea kuelekea darasani.

Je, Elimu ya Juu na Pesa Zitakuhakikishia Maisha Bora ya Wakati Ujao?

Watu wengi wanafikiri kwamba wale wenye elimu ya juu na matajiri watakuwa na maisha bora wakati ujao. Wanaamini kwamba elimu ya chuo kikuu inaweza kumsaidia mtu awe mfanyakazi mzuri, anufaishe familia yake, na awe raia mwema. Pia, wanahisi kwamba kupata elimu ya juu kutamsaidia mtu kupata kazi yenye mshahara mkubwa, na kwamba mtu mwenye pesa nyingi atakuwa na furaha.

UAMUZI AMBAO WATU WENGI WANAFANYA

Fikiria jambo ambalo Zhang Chen, kutoka China alisema. Anasema, “Niliamini kwamba nilihitaji shahada ya chuo kikuu ili niondokane na umaskini, na kwamba kupata kazi yenye mshahara mkubwa kungenihakikishia maisha yenye kuridhisha na yenye furaha.”

Ili kupata maisha bora, watu wengi wanataka kusoma katika vyuo vikuu maarufu, ambavyo huenda vipo katika nchi nyingine. Watu wengi zaidi wamekuwa wakifanya hivyo mpaka vizuizi vya kusafiri kwenda nchi nyingine vilipowekwa kwa sababu ya janga la corona. Ripoti ya mwaka 2012 ya shirika moja la kimataifa (Organisation for Economic Co-operation and Development) inasema: “Asilimia 52 ya wanafunzi wote wanaosoma nchi nyingine wanatoka Asia.”

Mara nyingi wazazi wanajitahidi sana ili watoto wao waweze kusoma katika vyuo vikuu vya nchi nyingine. Qixiang, kutoka Taiwan, anasema: “Wazazi wangu hawakuwa matajiri, lakini walihakikisha sisi sote wanne tunapata elimu ya chuo nchini Marekani.” Kama familia nyingine nyingi, familia hiyo ilikopa pesa na kuwa na madeni mengi ili kulipia gharama ya elimu.

MATOKEO NI NINI?

Msichana mmoja ameketi mbele ya kompyuta usiku akiwa amechoka na ana mkazo.

Watu wengi waliofuatilia elimu ya juu na utajiri wamevunjika moyo

Elimu ya juu inaweza kuboresha maisha katika njia fulani, lakini si kila wakati inawasaidia wanafunzi kupata mambo waliyotarajia. Kwa mfano, baada ya miaka mingi ya kusoma kwa bidii na kukopa pesa nyingi, wengi hawapati kazi ambazo walitamani. Ripoti ya Rachel Mui katika gazeti la Business Times la Singapore inasema: “Idadi ya watu wanaohitimu vyuo vikuu na kukosa ajira inazidi kuongezeka.” Jianjie, msomi mwenye shahada kadhaa za chuo kikuu anayeishi Taiwan, anasema, “Watu wengi wanalazimika kufanya kazi ambazo hawajasomea.”

Hata wale ambao wamepata kazi zinazohusiana na taaluma waliyosomea wamegundua kwamba maisha yao hayajawa bora kama walivyotarajia. Niran alipohitimu chuo kikuu nchini Uingereza, alirudi Thailand na kupata kazi aliyosomea. Anasema: “Kama nilivyotarajia, elimu yangu iliniwezesha kupata kazi yenye mshahara mkubwa. Hata hivyo, nilihitaji kufanya kazi nyingi sana na kwa saa nyingi sana ili nipate mshahara huo mkubwa. Mwishowe, mimi na wafanyakazi wengine wengi wa kampuni hiyo tulifukuzwa kazi. Nilitambua kwamba hakuna kazi yoyote inayoweza kutegemeka.”

Hata matajiri au wale wanaoonekana kuwa na maisha mazuri wanaweza kukabili matatizo ya familia, matatizo ya afya, na kuwa na wasiwasi kuhusu pesa. Katsutoshi, kutoka Japani, anasema, “Nilifurahia kuwa na pesa nyingi na vitu vingi vizuri, lakini nilikuwa na mkazo kwa sababu ya mashindano, wivu, na kutendewa kwa njia mbaya wa wengine.” Lam, mwanamke anayeishi Vietnam, anasema, “Watu wengi wanahangaika kupata kazi nzuri ili wawe na pesa nyingi, wakifikiri kwamba zitawapatia maisha bora. Hata hivyo, hilo linawafanya wawe na wasiwasi zaidi, wawe na matatizo ya afya, wapate mkazo, na kushuka moyo.”

KWA NINI ELIMU NA PESA PEKEE HAZIWEZI KUTUHAKIKISHIA MAISHA BORA?

Ni kweli kwamba watu wanahitaji elimu ya msingi na pesa ili kuandaa mahitaji yao na ya familia zao. Hata hivyo, mambo hayo hayatuhakikishii kwamba tutakuwa na maisha bora ya wakati ujao. Kwa nini? Fikiria mambo yanayosemwa kwenye Maandiko Matakatifu.

ELIMU YA JUU HAILETI MAFANIKIO SIKUZOTE.

“Sikuzote si wenye mbio wanaoshinda mbio, . . . wala werevu hawawi na utajiri sikuzote, wala wenye ujuzi hawafanikiwi sikuzote, kwa sababu wakati na matukio yasiyotarajiwa huwapata wote.”​—MHUBIRI 9:11.

Mara nyingi, wale ambao wanaonekana watafanikiwa hawafanikiwi kwa sababu ya mambo yaliyo nje ya uwezo wao. Matatizo ya kiuchumi, ya kisiasa, na ubaguzi unaweza kufanya hata watu walio na elimu bora wasifanikiwe.

UTAJIRI UNAWEZA KUPOTEA.

“Usijichoshe kupata utajiri. Acha, na uonyeshe uelewaji. Ukiutupia jicho, haupo, kwa maana hakika utaota mabawa kama ya tai na kuruka mbali angani.”​—METHALI 23:4, 5.

Usalama wowote ambao unapata kutokana na pesa ni wa muda tu. Mabadiliko ya uchumi ulimwenguni yanaweza kufanya mtu apoteze pesa zake zote alizotunza kwa muda mrefu. Majanga ya asili kama vile matetemeko ya ardhi, moto wa msituni, na vimbunga, yanaweza kufanya mtu afilisike na kupoteza makao.

MARA NYINGI PESA HULETA MATATIZO.

“Wingi alionao tajiri haumruhusu kulala usingizi.”​—MHUBIRI 5:12.

Franklin, anayeishi Hong Kong, alijionea ukweli wa maneno hayo yenye hekima. Alikuwa na elimu ya juu na kazi yenye mshahara mkubwa. Kisha akapandishwa cheo. Anasema: “Mkazo ulianza kuathiri afya yangu. Nilikuwa na wasiwasi sana kiasi kwamba sikuweza kulala.” Hatimaye, hakuweza kuendelea na maisha hayo tena. Anakumbuka: “Nilianza kujiuliza kwa nini ninafanya mambo haya yote, na hilo lilifanya nifikirie zaidi kuhusu kusudi la maisha.”

“Usijichoshe kupata utajiri.”​—METHALI 23:4

Kama Franklin, watu wengi wametambua kwamba kuna mambo mengine muhimu zaidi maishani kuliko kufuatilia elimu ya juu na utajiri. Badala ya kuhangaika kutafuta pesa, wengine wanatafuta maisha bora kwa kuwa watu wema na kuwafanyia wengine mambo mazuri. Je, kufanya hivyo kutamhakikishia mtu maisha bora ya wakati ujao? Makala inayofuata itajibu swali hilo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki