Jamhuri Ya Kidemokrasia Ya Kongo (Kinshasa)
‘Sisi ni kama mbegu za mahindi ndani ya gunia. Mahali popote tuangushwapo, mmoja baada ya mwingine, hatimaye mvua hunyesha, na tunakuwa wengi.’ Maneno hayo yalisemwa zaidi ya miaka 50 iliyopita na Shahidi mmoja mwaminifu wa Yehova, ambaye aliteswa sana na wenye mamlaka katika nchi iliyoitwa Kongo ya Ubelgiji. Katika masimulizi yafuatayo, utaona jinsi ambavyo baraka za Yehova, kama mvua inayoburudisha, zimeleta ongezeko kubwa la watangazaji wa Ufalme kotekote nchini Kongo.
Nchi hiyo ambayo sasa inajulikana kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, au Kongo (Kinshasa), iko katikati ya bara la Afrika.a Ikweta inapita katika nchi hiyo iliyojaa misitu mingi mikubwa. Wanyama wa pori wa aina mbalimbali huishi kwenye nyanda pana na katika misitu mikubwa iliyo nchini humo. Kwa muda mrefu nchi hiyo imevutia mataifa mengine, imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, na hata imevamiwa kwa sababu ya rasilimali zake nyingi.
Nchi Huru ya Kongo ilianzishwa mnamo mwaka wa 1885. Mfalme Leopold wa Pili wa Ubelgiji akawa mtawala na mmiliki pekee wa nchi hiyo. Hata hivyo, Wakongomani hawakuwa huru hata kidogo. Wasimamizi waliowekwa na Leopold waliwatumikisha Wakongomani kwa ukatili sana ili kupora pembe za tembo na mpira. Leopold alilazimika kuondoka mamlakani baada ya nchi jirani za Ubelgiji kulalamika vikali. Katika mwaka wa 1908, Nchi Huru ya Kongo ilifutiliwa mbali na ikawa Kongo ya Ubelgiji, koloni iliyotawaliwa na bunge la Ubelgiji. Kongo ilipata uhuru mwaka wa 1960.
Wakongomani wanapenda dini sana. Kuna makanisa, seminari, na vyuo vingi vya kidini nchini humo. Ni jambo la kawaida kukutana na watu wanaoweza kunukuu maandiko mengi ya Biblia. Hata hivyo, sawa na nchi nyingine, haikuwa rahisi kuanzisha Ukristo wa kweli Kongo. Lakini jambo lililofanya iwe vigumu hata zaidi ni kwamba kwa muda fulani, watu walifikiri kimakosa kuwa Mashahidi wa Yehova ni wafuasi wa kikundi cha kidini cha Kitawala.
Tatizo la Kuwatambua Mashahidi wa Kweli wa Yehova
Jina “Kitawala” linatokana na neno la Kiswahili “-tawala.” Hivyo, lengo la kikundi cha Kitawala lilikuwa hasa la kisiasa, yaani, kupata uhuru kutoka kwa Wabelgiji. Wengi waliona kwamba dini ilikuwa njia bora ya kutimiza lengo hilo. Inasikitisha kwamba vikundi vya Kitawala vilipata, kusoma, na kusambaza vichapo vya Mashahidi wa Yehova. Makanisa ya Kitawala yalikuwa na ishara zenye maneno “Watch Tower.” Muda mrefu kabla ya Mashahidi wa Yehova kutia mizizi, vikundi vya Watch Tower Movement vilikuwa vimeenea sana katika jimbo la Katanga, kusini-mashariki mwa Kongo. Kwa miaka mingi watu walidhani kwamba wafuasi wa Kitawala walikuwa Mashahidi wa Yehova. Lakini, haikuwa hivyo.
Wafuasi wa Kitawala walipotosha mafundisho ya Biblia ili yaunge mkono maoni yao ya kisiasa, desturi zao za kishirikina, na maisha yao mapotovu. Waliwapinga watawala wakoloni na kukataa kulipa kodi. Baadhi yao walitumia silaha kupigana na wenye mamlaka. Si ajabu kwamba walipigwa marufuku na serikali ya Ubelgiji.
Katika mwaka wa 1956, mkuu mmoja wa wilaya wa Kongo ya Ubelgiji aliandika makala ambayo ilieleza jinsi kikundi cha Kitawala kilivyoanza. Makala hiyo ilimhusu Tomo Nyirenda, mwenyeji wa Nyasaland (sasa ni Malawi), aliyeishi Rhodesia Kaskazini (sasa ni Zambia). Inaonekana kwamba Nyirenda alifundishwa mambo ya kidini na mtu fulani aliyeshirikiana na Wanafunzi wa Biblia (sasa wanajulikana kama Mashahidi wa Yehova) huko Cape Town, Afrika Kusini. Makala hiyo ilisema: “[Nyirenda] aliingia Katanga [Kongo] mwaka wa 1925, . . . akijiita Mwana Lesa, yaani, ‘Mwana wa Mungu.’ Alifaulu kuwadanganya wenyeji kwa sababu tangu zamani wamekuwa wakiogopa kulogwa. Aliahidi kwamba wale ambao wangemfuata hawangelogwa na wachawi, hawangelipa kodi yoyote, na pia wangekuwa huru na sheria zote, ziwe za serikali au za Kanisa. Wale ambao walikataa kufuata sheria yake waliitwa wachawi, walipigwa hadi kupoteza fahamu, kisha ‘wakabatizwa’ kwa nguvu kwa kutupwa mtoni, wakafa maji. (Maiti 55 zilipatikana katika mto mmoja.) Baada ya kushutumiwa hadharani na naibu wa chifu katika kijiji kimoja, Tomo alitoroka na kurudi Rhodesia. Serikali ya Rhodesia ilikuwa ikimsaka kwa sababu ya mauaji aliyofanya, kwa hiyo alikamatwa, akahukumiwa, na kunyongwa.”
Serikali ya Ubelgiji ilisema kwamba kikundi cha Kitawala kilianza nchini Kongo wakati ambapo yule aliyejiita Mwana Lesa alipoanza kuingia Katanga mwaka wa 1923 hadi 1925. Miaka mingi ilipita kabla ya Mashahidi wa Yehova kuruhusiwa kuingia na kukaa nchini humo.
Ili tuelewe ni kwa nini watu hawakuweza kutofautisha wafuasi wa Kitawala na Mashahidi wa Yehova, ni lazima tukumbuke kwamba kuna makanisa mengi sana barani Afrika. Watu fulani wanakadiria kwamba kuna maelfu ya makanisa barani humo. John S. Mbiti, mtaalamu wa dini za Kiafrika, aliandika hivi: “Tatizo [moja] kubwa linalokabili Ukristo barani Afrika ni idadi kubwa ya vikundi vya kidini na madhehebu. Vingi vya vikundi hivyo vilianzia nchi za ng’ambo. Wakristo Waafrika walianzisha vikundi vingine vingi kwa sababu mbalimbali. Kwanza, hawakutaka kuongozwa daima na mishonari wa kigeni, pili, walitaka vyeo, na tatu, walitaka kuubadili Ukristo kupatana na utamaduni wa Waafrika na matatizo yao, na kwa sababu nyinginezo nyingi.”
Kwa hiyo, kulikuwa na makanisa mengi madogo, na idadi kubwa ya makanisa hayo yalifuata mafundisho ya dini kuu au yalijitenga na dini hizo. Kikundi cha Kitawala kilianzishwa kwa njia hiyo. Hata hivyo, kuwepo kwa kikundi cha Kitawala kulizipatia dini zinazojiita za Kikristo nafasi nzuri ya kuwazuia Mashahidi wa Yehova wasiingie Kongo. Ingawa viongozi wa kidini walijua vizuri tofauti kati ya wafuasi wa Kitawala na Mashahidi, walieneza kimakusudi maoni ya uwongo ya kwamba Kitawala na Mashahidi wa Yehova ni kitu kimoja.
Makanisa yalikuwa na uwezo wa kueneza uwongo huo. Mwanzoni mwa karne ya 20, dini zinazojiita za Kikristo, hasa Kanisa Katoliki, zilikuwa na uvutano mkubwa sana huko Kongo ya Ubelgiji. Lakini, Mashahidi wa Yehova hawakutambuliwa kisheria nchini humo, na viongozi wa dini za Kikristo walitaka hali ibaki hivyo. Walifanya juu chini kuwalinda wafuasi wao na hawakutaka Mashahidi wa Yehova waingilie mambo.
Kikundi cha Kitawala, ambacho mara nyingi kiliitwa Watch Tower Movement, kililaumiwa kila mara kulipotokea fujo, maasi, na vita vya kikabila. Jina Watch Tower lilichukiwa sana na maafisa wa umma na wenye mamlaka. Kwa hiyo wale waliotaka kumtumikia Yehova nchini Kongo walipata magumu mengi.
Kwa miaka mingi kabla ya Kongo kupata uhuru, Mashahidi wa Yehova katika nchi nyingine walituma barua nyingi kwa wenye mamlaka nchini humo, wakieleza kwamba shirika la Watch Tower Bible and Tract Society halikuwa na uhusiano wowote na Watch Tower Movement. Hata hivyo, kwa miaka mingi, wenye mamlaka walikuwa wakihusianisha utendaji wa kikundi hicho cha kienyeji na kazi ya watu wa Yehova. Jitihada za kuwatuma Mashahidi wa Yehova nchini Kongo ziliambulia patupu.
Kwa sababu Mashahidi hawakuruhusiwa nchini humo, hatuna habari kamili kuwahusu Mashahidi wa kweli waliokuwa humo. Hata hivyo, ofisi za tawi za karibu zina habari zenye kusisimua sana kuhusu utendaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Kongo katika miaka hiyo ya mapema yenye magumu. Hebu tuchunguze madondoo fulani ya historia ya miaka 30 ya kazi ya Mashahidi huko Kongo. Tumeongeza maelezo ya ziada.
Historia ya Kongo—Madondoo ya Ripoti Kutoka Nchi Mbalimbali Kuanzia 1930-1960
1930: Barua ya kuomba vichapo yapokewa kwa njia ya posta kutoka . . . Kongo ya Ubelgiji.
1932: Tunatumaini kwamba Kongo ya Ubelgiji na sehemu nyingine za Afrika ya Kati ambazo bado hazijahubiriwa zitahubiriwa baadaye.
Kuanzia Mei 1932, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova ya Afrika Kusini ilituma maombi mengi kwa serikali ya Ubelgiji ili wahudumu wa wakati wote waruhusiwe kuingia Kongo. Maombi hayo yalikataliwa. Hata hivyo, kwa sababu ya watu kuhama kati ya Kongo na Rhodesia Kaskazini, ndugu fulani wa Rhodesia waliweza kuingia Kongo kwa vipindi vifupi.
1945: Ni mtu jasiri tu anayeweza kumwakilisha Mungu na Ufalme wake katika [Kongo ya Ubelgiji]. Licha ya kwamba kazi na vichapo vimepigwa marufuku kabisa, Wakongomani Waafrika wanaoshirikiana nasi wanaweza kuhamishwa hadi wilaya nyingine na nyakati nyingine wanaishi huko chini ya vizuizi kwa miaka kadhaa. Mara nyingi barua tunazotumiwa kutoka Kongo hazifiki hapa [Rhodesia Kaskazini], na inaonekana kwamba barua tunazotuma hazipelekwi; lakini . . . tunafanya kila tuwezalo kuwasaidia wafanyakazi wenzetu wa Ufalme katika nchi hiyo yenye makasisi chungu nzima.
1948: Kuna wahubiri wawili wa Ufalme wanaoishi katika eneo hilo sasa, na wamekuwa wakituma ripoti kwenye ofisi ya Brussels. Tunatumaini kwamba siku moja ujumbe wa Ufalme utaweza kuhubiriwa katika eneo hilo kubwa.
1949: Kwa miaka mingi kazi ya kuhubiri imekuwa ikifanywa kwa shida sana katika eneo hili lenye Wakatoliki wengi. Zamani, makasisi walimwadhibu mtu yeyote aliyekuwa Shahidi wa Yehova kwa kumlazimisha kula chumvi nyingi bila maji, lakini sasa wanatumia njia zilizotumiwa na mahakama ya Katoliki ili kukomesha uasi nchini Hispania, yaani, wanataka serikali iwafanyie kazi hiyo mbovu ya kuwatesa watu. Kwa miaka mingi, wahubiri Waafrika wamefungwa gerezani kwa muda usiojulikana kwa sababu ya kazi yao ya kuhubiri, na jambo baya hata zaidi ni kwamba wao hupelekwa kwenye kambi maalumu ya mateso huko Kasaji, kilometa [500] hivi kutoka Elisabethville [sasa ni Lubumbashi]. Wanafanya kazi ngumu kwenye mashamba madogo kambini, na wanatengwa peke yao au pamoja na familia zao. . . . Wengine wao hukaa huko hata kwa miaka kumi. Kwa kawaida, wanakaa peke yao kwa miaka mingi sana bila kutarajia kuwekwa huru au kutendewa haki. Wanaweza kuwekwa huru tu wakifanya uamuzi mbaya wa kukana imani yao.
Kwa sababu hiyo ndugu wamelazimika kuendelea na kazi yao kisiri; mikutano hufanywa kisiri mahali mbalimbali ili ndugu wasikamatwe. Walihubiri hasa kwa kuwatembelea watu wenye urafiki na marafiki wao, lakini bado mashahidi wengi wametumbukia taabani licha ya tahadhari hizo. Mashahidi hukamatwa na kupelekwa himahima kwenye kambi ya Kasaji.
Karibu wakati huo, Llewelyn Phillips, kutoka ofisi ya tawi ya Rhodesia Kaskazini, alienda Kongo ya Ubelgiji ili kuwatetea Mashahidi waliokuwa wakiteswa. Gavana mkuu na maofisa wengine wa serikali walimsikiliza alipokuwa akiwaeleza kuhusu kazi ya kuhubiri ujumbe wa Ufalme na tofauti iliyopo kati ya mafundisho ya Mashahidi na ya Kitawala. Gavana mkuu alimkatiza na kumwuliza hivi huku akiwaza sana: “Nikiwasaidia, itakuwaje kwangu?” Alijua kwamba Kanisa Katoliki lilikuwa na uvutano mkubwa katika nchi hiyo.
1950: Mwaka uliopita ulikuwa mgumu kuliko miaka mingine yote, na ndugu wanaoishi Kongo ya Ubelgiji waliteseka sana. Mwanzoni mwa mwaka wa utumishi, hawakupokea vitabu wala barua zote zilizotumwa, na karibu mawasiliano na makutaniko yakatizwe kabisa. Kisha, Januari 12, gavana mkuu alipiga marufuku Sosaiti na akatangaza kwamba mtu yeyote atakayehudhuria mkutano, kuunga mkono Sosaiti kwa njia yoyote, au kuwa mfuasi wake, atahukumiwa kifungo cha miezi miwili na kulipa faini ya faranga 2,000. Wachapishaji wa vitabu vya Wakatoliki waliusifu sana uamuzi huo. Ndugu wakaanza kukamatwa. Orodha zilizochukuliwa mwaka uliotangulia kutoka kwa ndugu ambaye awali alikuwa mwangalizi [wa kutaniko] huko Elisabethville, zilitumiwa kuwasaka mamia ya watu walioshirikiana na Sosaiti, nao walikamatwa pamoja na wake zao. Baada ya kukamilisha vifungo vyao, Waafrika wa Rhodesia Kaskazini walifukuzwa nchini, lakini mara nyingi ndugu Wakongomani walipelekwa kwenye kambi ya mateso ya Kasaji, kilometa [500 hivi] kutoka Elisabethville. Ndugu fulani wangali kambini humo. Baadhi ya ndugu waliofukuzwa nchini walipewa chakula kidogo sana, wakalazimishwa kutembea umbali wa kilometa 30 kutoka Sakania hadi kwenye mpaka wa Rhodesia Kaskazini.
Idadi ya askari wapelelezi imeongezeka karibuni, na mtu yeyote aliye na Biblia anaweza kushukiwa kuwa Shahidi wa Yehova.
Tumepokea habari kwamba dada wawili Wazungu kutoka wilaya ya Elisabethville wamehukumiwa kifungo cha nje cha siku 45 kwa sababu ya kupatikana na gazeti la Mnara wa Mlinzi na kuhubiri, na watachunguzwa kwa miaka mitatu kuhakikisha kwamba hawahubiri (bila shaka hiyo inamaanisha kwamba hawawezi kufanya kazi ya Bwana). Kila siku dada hao hukabili uwezekano wa kufukuzwa nchini.
1951: Makala nyingi zimechapishwa katika magazeti ya Ubelgiji zikidai kwamba Watch Tower Society na Mashahidi wa Yehova wana uhusiano na “Kitawala,” kikundi chenye siasa kali katika Kongo ya Ubelgiji. Sheria ya Ubelgiji inasema kwamba mtu akijibu makala iliyochapishwa kwenye gazeti, basi ni lazima gazeti hilo lichapishe jibu lake. Tumetumia ifaavyo haki hiyo ili kutetea kazi ya Ufalme kwa kukanusha makala hizo za uwongo, na majibu yetu yamechapishwa.
Tangu Januari [12], 1949, kazi ya Watch Tower Society imepigwa marufuku katika Kongo ya Ubelgiji na mashahidi wa kweli wa Yehova wameteswa kwa sababu ya ripoti hizo za uwongo. Barua za malalamiko zimeandikwa na kupelekwa kwa waziri wa koloni, na uthibitisho wa kutosha umetolewa kuonyesha kwamba Mashahidi wa Yehova na Watch Tower Society hawana uhusiano wowote na kikundi cha mapinduzi cha “Kitawala,” lakini malalamiko hayo hayajajibiwa.
Njia zifuatazo zimetumiwa ili kujaribu kukomesha kabisa kazi ya ‘kuhubiri Neno’ katika Kongo ya Ubelgiji: kueneza habari za uwongo, kuwatesa ndugu, kuwatoza faini, kuwapiga, kuwafunga gerezani, na kuwafukuza nchini.
1952: Kama huko Ulaya Mashariki, kuna “pazia la chuma” pia katika Afrika ya Kati! Kwa maoni ya mashahidi wa Yehova, pazia hilo limezingira Kongo ya Ubelgiji. Kazi ya kuhubiri ingali imepigwa marufuku katika nchi hiyo yenye Wakatoliki wengi.
Ripoti zinazopokewa mara kwa mara zinaeleza kwamba wahubiri Waafrika wanafukuzwa nchini, wanafungwa gerezani, wanapigwa, na wanakosa mahitaji ya lazima. Inaonekana kwamba ukatili dhidi ya mashahidi umeongezeka katika sehemu nyingi. Wenyeji wa nchi wanaopatikana wakihubiri au wakiwa na kichapo cha Watchtower wanapelekwa kwenye kambi za kazi ngumu. Mtu yeyote mwenye Biblia anaonwa kuwa Shahidi wa Yehova.
Nyumba za [akina] ndugu zinachunguzwa daima na kupekuliwa mara kwa mara. Ndugu aliyetoa ripoti alisema hivi: “[Polisi wa Kongo ya Ubelgiji] hawalali kwa sababu yetu, bali wanazunguka-zunguka wakiwatafuta Mashahidi wa Yehova. Hali ni mbaya sasa kuliko zamani.”
Ripoti moja ya mwezi wa Agosti ilifika ofisini hapa kutoka kwa wahubiri 30, na andiko la 1 Wathesalonike 5:25, NW, lilikuwa limeandikwa kwenye sehemu ya chini: “Akina ndugu, endeleeni kusali kwa ajili yetu.”
Kama tulivyotaja awali, Mashahidi Waafrika kutoka Rhodesia Kaskazini waliingia Kongo. Lakini walipokamatwa, walifungwa gerezani na baadaye kufukuzwa nchini. Ingawa wengi wao walifungwa kwa muda mfupi, ndugu wengine walipelekwa kwenye kambi za kazi ngumu kwa miaka kadhaa. Ndugu mmoja alifungwa kwa miaka mitano hivi katika magereza mbalimbali nchini Kongo. Watu waliomkamata walimpiga tena na tena. Pia walimwambia kwamba wangemwachilia iwapo tu angeacha kuhubiri.
Ni mwaka huo wa 1952 ndipo ndugu yule mwaminifu aliposema maneno haya: ‘Sisi ni kama mbegu za mahindi ndani ya gunia. Mahali popote tuangushwapo, mmoja baada ya mwingine, hatimaye mvua hunyesha, na tunakuwa wengi.’ Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova ya Rhodesia Kaskazini iliandika hivi kuhusu jambo hilo: “Bila shaka ‘gunia la mahindi’ linatawanywa nchini Kongo licha ya, au kwa sababu ya, kuteswa kwa akina ndugu. Pindi moja ofisi ya tawi ya Lusaka ilipokea ripoti kutoka kwa mamia ya watu walioshirikiana na mashahidi katika sehemu ya Kolwezi. Hata hivyo, sasa inasemekana kwamba wengi wanapelekwa hadi sehemu nyingine za Kongo.” Kutawanyika kwa akina ndugu kulieneza kazi ya kufanya wanafunzi.
Ndugu walipokuwa wakijitahidi kuhubiri kusini-mashariki mwa nchi, wengine walikuwa wakifundisha kweli katika jiji la Léopoldville (sasa ni Kinshasa). Ndugu wa Brazzaville walikuwa wamefanya maendeleo makubwa ya kiroho na waliwafundisha wengine kweli kwa bidii. Baadhi yao walianza kuvuka Mto Kongo kwa feri na kuhubiri Léopoldville. Mwaka wa 1952, Victor Kubakani na mke wake walikuwa Mashahidi wa kwanza kubatizwa jijini Kinshasa. Baada ya muda kutaniko lilianzishwa.
1953: Tumepokea ripoti zinazoonyesha kwamba karibu ndugu 250 wanahubiri katika sehemu mbalimbali nchini, lakini huenda kuna wengine wengi. Ndugu wanafanya tu [ziara za kurudia] na kuongoza mafunzo ya Biblia wakiwa na vichapo vichache, au bila kichapo chochote, kwa sababu wanajua kwamba nyumba zao zinaweza kupekuliwa wakati wowote. Ndugu mmoja aliripotiwa kuwa na vijitabu viwili na mmoja wa wale waliodai kuwa “rafiki” zake, naye akafungwa miezi miwili katika gereza Kuu huko Elisabethville.
1954: Sosaiti na kazi ya mashahidi wa Yehova ingali imepigwa marufuku kabisa katika Kongo ya Ubelgiji . . . Mashahidi waaminifu wameendelea kuwahubiria wafungwa wengine gerezani. Wafungwa hao wanaandika Maandiko kwenye vikaratasi vidogo kwa vipande vya kalamu ili wayachunguze baadaye katika Biblia wanazopewa gerezani. Hapana shaka kwamba mashahidi wa Yehova hawaruhusiwi kuchangamana na wafungwa wengine katika baadhi ya magereza kwa sababu ya utendaji wao.
Utendaji wa Mashahidi wa Yehova na wa Kitawala ulipigwa marufuku. Maofisa walichukua vichapo vya Biblia vilivyoletwa nchini. Nyakati nyingine vichapo ambavyo havikuchukuliwa na maofisa viliibiwa na wafuasi wa Kitawala ambao walivitumia kueneza mafundisho yao. Mashahidi wa Yehova na wafuasi wa Kitawala walikamatwa, walipigwa, na kupelekwa kwenye kambi za mateso. Hata hivyo, Yesu alisema: “Kwa matunda yao mtawatambua.” (Mt. 7:16) Wakoloni wenye mamlaka waliona mwenendo mzuri wa akina ndugu, wakaanza kutambua kwamba kuna tofauti kati yao na Kitawala.
1955: Bado kazi imepigwa marufuku nchini na haielekei kwamba marufuku itaondolewa karibuni, lakini bidii ya wale wanaompenda na kumtumikia Yehova haijapungua. Bidii ya akina ndugu haijapungua licha ya kwamba wengi walifungwa gerezani na kufukuzwa nchini mwaka uliopita.
Ndugu wanafanya [ziara za kurudia] na kuongoza mafunzo ya Biblia kwa sababu hali haziwaruhusu kuhubiri nyumba kwa nyumba. Kutaniko moja linaandika kwamba wahubiri wangependa kutangaza habari njema waziwazi pia, ingawa “hatujui ikiwa Yehova ataturuhusu tuhubiri habari njema nyumba kwa nyumba katika nchi hii kabla ya vita vya Har-Magedoni.”
1957: Hapana shaka kwamba kazi yetu ilikaziwa fikira sana mwaka uliopita kuliko wakati mwingine wowote, hasa na maofisa wa serikali na vyombo vya habari. Mwezi wa Novemba, Ndugu [Milton G.] Henschel alifika Leopoldville, akakutana moja kwa moja na maofisa wa serikali ya Kongo ya Ubelgiji, akatoa ombi ili marufuku iliyowekewa Sosaiti na Mashahidi wa Yehova ifutiliwe mbali. Alirudi tena Leopoldville na baadaye wawakilishi kutoka New York na Brussels wakaja. Baadaye mtaalamu wa masuala ya Afrika kutoka Ubelgiji alitembelea ofisi ya tawi ya Rhodesia Kaskazini, na ndugu walitumia nafasi hiyo kumweleza kinaganaga kuhusu kazi yetu na ujumbe wetu.
Bado kazi imepigwa marufuku, na akina ndugu katika Kongo ya Ubelgiji wanafanya kazi chini ya hali ngumu sana. Watu 216 walihudhuria sherehe ya Ukumbusho, ingawa walikutana wakiwa vikundi vidogo.
1958: Mwaka uliopita, ujumbe wa Ufalme ulihubiriwa kotekote licha ya kwamba kazi ya kuhubiri habari njema ingali imepigwa marufuku, na ndugu wanafungwa gerezani.
1959: Kwa mara ya kwanza wakuu wa serikali waliwaruhusu akina ndugu wafanye mikutano ya kutaniko, ingawa bado kazi imepigwa marufuku. Kabla ya wakati huo, hawakuweza kufanya mkutano wowote wa kutaniko, na walikutana tu katika vikundi vidogo nyumbani ili kujifunza Biblia. Basi ndugu walipanga sherehe ya Ukumbusho kuwa mkutano wao wa kwanza hadharani, na watu 1,019 walihudhuria katika [makutaniko] matano huko Leopoldville. Watu wengi walishangaa kuwaona ndugu wakifanya mikutano, na pia walistaajabu kuona shangwe ya akina ndugu walipokutana na Wakristo wenzao. Baadhi ya watu waliokuwepo walitambua mara moja kwamba ndugu walikuwa tofauti na dini nyingine kwa sababu ‘wana upendo kati yao wenyewe.’
Ingawa haikuwezekana bado kuwatuma mishonari nchini Kongo, sheria iliyoidhinisha uhuru wa ibada wa kadiri fulani, ambayo ilitiwa sahihi Juni 10, 1958, iliwaruhusu Mashahidi wa Yehova “kukutana katika nyumba.” Ndugu walifurahi kwa sababu waliweza kufanya mikutano kwa uhuru. Nyakati nyingine maofisa wa usalama walihudhuria mikutano hiyo na kuwasifu ndugu kwa sababu ya utaratibu na mwenendo wao mzuri.
Kulikuwa na mabadiliko mengine muhimu. Shule zote zilidhaminiwa na dini hadi mwaka wa 1956, wakati waziri mpya mkoloni asiye na msimamo mkali alipoanzisha shule za serikali na kuwahimiza watu wasichukie vikundi vidogo. Maoni ya kwamba Mashahidi wa Yehova ni wafuasi wa Kitawala yalianza kutoweka pole kwa pole maofisa walipoanza kuona tofauti kati ya vikundi hivyo viwili. Ni kana kwamba mvua yenye kuburudisha ilikuwa imezinyeshea mbegu zilizotawanyika. Kila mahali watu walikuwa wakiwaunga mkono Mashahidi wa Yehova.
Wakati huo, chifu mmoja aliwakamata Mashahidi kadhaa na kuwapeleka mbele ya msimamizi wa jimbo ili wahukumiwe. Msimamizi huyo aliuliza kosa walilofanya. Chifu hakujua kosa lao. Msimamizi alimkemea chifu huyo kwa hasira na kuwaachilia ndugu hao, akaamuru wasafirishwe hadi nyumbani kwao.
1960: Kazi katika Kongo ya Ubelgiji iliendelea vizuri sana mwaka uliopita. Ndugu wamekuwa wakikutana kwa ukawaida kwenye Majumba ya Ufalme, licha ya kwamba kuna magumu nchini na kazi haijaandikishwa kisheria.
Kulikuwa na tukio la pekee katika majira ya Ukumbusho katika jiji kuu, Leopoldville. [Makutaniko] sita jijini humo yalipanga kukutana pamoja kwa ajili ya hotuba ya watu wote siku ya Jumapili na walifurahi sana kuwa na hudhurio la watu 1,417. [Mwangalizi] mmoja aliandika hivi wakati huo: “Tulifurahi sana, kwa sababu ilikuwa mara ya kwanza kujaribu kufanya hivyo; malaika wa Yehova walipiga kambi pande zote kutuzunguka.”
Historia hiyo ya miaka 30 inaeleza kwa ufupi utendaji nchini Kongo kama ilivyoripotiwa na ofisi za tawi jirani. Hebu tuone jinsi hali ilivyoendelea.
Taifa Lakaribia Kupata Uhuru
Mwishoni mwa miaka ya 1950, kazi ya kuhubiri ujumbe wa Ufalme nchini Kongo, chini ya uangalizi wa ofisi ya tawi ya Rhodesia Kaskazini, iliruhusiwa kuendelea ingawa haikuandikishwa kisheria. Hata hivyo, wasiwasi na matatizo mapya yalianza kutokea. Roho ya uzalendo ilikuwa imepamba moto na ndivyo na upinzani dhidi ya serikali ya ukoloni. Mnamo Januari 1959, wafanya fujo walipora na kuteketeza maduka jijini Léopoldville. Walipora pia makanisa na kutupa sanamu barabarani. Kwa hiyo maofisa wa Ubelgiji walifanya mkutano na wawakilishi wa vyama vya kisiasa nchini. Waliteua Juni 30, 1960, kuwa siku ya taifa hilo kupata uhuru. Bila shaka, hakuna Shahidi yeyote wa Yehova aliyeshiriki katika fujo hizo.
Vyama vya kisiasa vilianza kuibuka kotekote nchini. Kwa kawaida wanachama waliungana kwa sababu ya ukabila badala ya masuala ya kisiasa. Walijaribu kuwalazimisha akina ndugu kununua kadi za vyama vya kisiasa. Pierre Mafwa, ambaye alikuwa amebatizwa mwaka uliotangulia, alisema hivi: “Ilikuwa siku ya Jumamosi mnamo Juni mwaka wa 1960. Nilikuwa nikirudi nyumbani kutoka kazini wakati wa mchana. Nilipokuwa nikipita uwanja wa zamani wa ndege wa Léopoldville, mtu fulani mwenye upanga alinijia. ‘Kadi yako ya chama iko wapi?’ akaniuliza kwa nguvu. Sikumjibu. Kwa ghafula, alinipiga usoni kwa upanga na kuikata pua yangu. Aliendelea kunipiga kwa upanga huo. Nilijaribu kukimbia lakini nikaanguka chini. Nilisali kwa Yehova, na kumwomba anikumbuke wakati wa ufufuo ili niweze kumwona tena mke wangu na watoto wangu sita. Baada ya kutoa sala hiyo fupi, nilisikia risasi zikifyatuliwa. Askari walimpiga risasi kwenye magoti, na kumwangusha mtu huyo ambaye alitaka kuniua. Polisi mmoja alinipeleka hospitalini, ambako nilitibiwa. Maandiko ya Biblia yalinitia moyo sana.”
Mishonari wa Kwanza Wawasili na Kufungua Ofisi ya Tawi
Kama tulivyoona, jitihada nyingi za kuwatuma wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova nchini Kongo hazikufaulu. Hata hivyo, hali ya kisiasa ilikuwa ikibadilika, hivyo Ernest Heuse, Jr. aliruhusiwa nchini.
Ndugu Heuse alikuwa Mbelgiji mrefu, mwenye nguvu, na mwenye nywele nyeusi. Ingawa hakuwa mwoga, alijua kwamba yeye pamoja na mkewe Hélène, na binti yake Danielle, mwenye umri wa miaka 11, hawangekuwa na maisha rahisi nchini Kongo. Maisha ya awali ya Ernest yalimtayarisha ifaavyo kukabiliana na hali yoyote baadaye. Alianza utumishi wa Betheli huko Brussels mwaka wa 1947. Mwaka uliofuata alioa, naye pamoja na mkewe wakaanza utumishi wa painia. Baadaye, Ernest alipewa mgawo wa kuwatembelea mawakili na maofisa wa serikali na kuwaonyesha broshua ya pekee iliyozungumzia tofauti kati ya Mashahidi wa Yehova na Kitawala. Hatimaye akawa mwangalizi wa mzunguko.
Ernest alijaribu mara kadhaa kupata hati za kuingia Kongo, hata aliandika ombi lake na kulituma moja kwa moja kwa mfalme wa Ubelgiji. Ombi lake lilikataliwa. Badala yake, jina la Ernest liliandikwa kwenye orodha ya wale “wasiotakikana” nchini Kongo.
Ernest hakuchoka. Alikuja Afrika na kujaribu kuingia Kongo kupitia nchi jirani. Lakini alishindwa kabisa. Mwishowe, alipata viza ya kwenda Brazzaville, jiji kuu la Jamhuri ya Kongo. Kisha, alivuka mto kwa feri na kuingia Léopoldville. Alipowasili, maofisa walioshika zamu walianza kuzungumza kwa msisimuko. Baadhi yao walisema kwamba hapaswi kupewa viza kwa sababu jina lake liko kwenye orodha ya wasiotakikana. Hatimaye, ofisa mmoja, Cyrille Adoula, ambaye baadaye alikuja kuwa waziri mkuu, alisema kwamba alijua Ernest alikuwa amejaribu sana kuingia Kongo. Alisema kwamba ikiwa wakoloni hawakumpenda Heuse, basi yeye ni rafiki ya Wakongomani. Ernest alipewa viza ya muda na baadaye viza ya kuishi nchini. Kwa hiyo, mnamo Mei 1961, Mashahidi wa Yehova walikuwa na mwakilishi wa kusimamia kazi ya kufanya wanafunzi nchini Kongo.
Ernest alifanya mpango ili Hélène na Danielle wahamie Kongo, na mwezi wa Septemba, Danielle alijiunga na shule moja jijini Léopoldville. Ofisi ya kwanza ya tawi ilifunguliwa katika jiji kuu Juni 8, 1962. Ofisi na makao yalikuwa kwenye orofa ya tatu ya jengo moja kwenye barabara ya Avenue van Eetvelde (sasa ni Avenue du Marché). Hakukuwa na nafasi ya kutosha, kwa hiyo vichapo viliwekwa kwenye depo sehemu nyingine. Hali hiyo haikuwa nzuri, lakini hakukuwa na la kufanya kwa sababu ya ukosefu mkubwa wa nyumba.
Ndugu Heuse alianza kufanya kazi mara moja. Ofisi ya tawi ya Brazzaville ilimwazima projekta na sinema. Halafu alionyesha sinema yenye kichwa Furaha ya Jamii ya Ulimwengu Mpya (The Happiness of the New World Society) kwenye makutaniko ya Léopoldville, na aliwaonyesha pia maofisa fulani wa serikali sinema hiyo. Iliwasaidia sana akina ndugu na watu wanaopendezwa kutambua kwamba Mashahidi wana undugu wa kimataifa na wote wanaishi kwa amani na furaha. Walishangaa sana kumwona ndugu Mwafrika akiwabatiza Wazungu. Meya wa Léopoldville aliifurahia sana sinema hiyo hata akasema: “Kazi hii [ya Mashahidi wa Yehova] inapaswa kuendelezwa kadiri iwezekanavyo.” Watu wapatao 1,294 walihudhuria maonyesho manne ya kwanza.
Ndugu walifurahi sana kumpata mtu wa kuwasaidia baada ya kungoja kwa miaka mingi. Hawakuwa wamekutana na ndugu yeyote Mzungu, walisikia tu kwamba kuna ndugu Wazungu. Baadhi yao walikuwa na shaka kama kweli kuna ndugu Wazungu, kwa sababu wenye mamlaka Wabelgiji walidai kwamba hakuna Mashahidi wa Yehova nchini Ubelgiji. Ndugu walifurahi sana kuwa na Ndugu Heuse miongoni mwao.
Haikuwa Rahisi Kufuata Kweli
Kulikuwa na kazi kubwa ya kuwasaidia akina ndugu kuishi kupatana na kweli. Kwa mfano, kulikuwa na chuki ya kikabila, na baadhi ya waangalizi wa makutaniko hawakuzungumza kamwe na waangalizi wengine. Mtu aliyetengwa na ushirika kutoka kutaniko lenye ndugu wengi wa kabila fulani, alikubaliwa na wazee wa kutaniko lingine lenye ndugu wengi wa kabila lake. Maamuzi ya kutaniko moja yalipuuzwa na kutaniko lingine. Desturi za kikabila zilifuatwa sana, na ukabila uliathiri sana makutaniko.
Desturi za kikabila zilisababisha matatizo mengine. Katika makabila fulani, uhusiano kati ya mume na mke ulitegemea desturi za kabila lao. Kwa ujumla, mume na mke hawakuwa na uhusiano wa karibu. Mara nyingi ndoa ilionwa kuwa mpango wa kabila. Ikiwa watu wa kabila hawakukubali ndoa, wangeweza kumlazimisha mume amfukuze mke wake na kumchukua mwingine waliyemchagua.
Mume alipokufa hali ilikuwa mbaya sana. Kwa kawaida familia ya mume ilichukua kila kitu nyumbani, na kumwacha mke na watoto wakiwa maskini hohehahe. Katika makabila mengine, mume alionwa kuwa na hatia kama mke wake angekufa, na familia ya mke ilimtoza faini.
Kulikuwa na matatizo mengine pia. Hadi leo, watu wengi nchini Kongo wanaamini kwamba hakuna mtu anayekufa kwa sababu ya hali za kawaida. Kwa hiyo, kuna sherehe zinazofanywa wakati wa mazishi ili kumtambua yule aliyemuua mtu huyo. Nywele za mtu anayeonwa kuwa muuaji hunyolewa, na mila nyingine nyingi hufuatwa. Katika makabila fulani, mume anapokufa, inasemekana kwamba mke hutakaswa kwa kufanya ngono na mwanamume mwingine wa kabila la mume. Wakati wa mazishi, kwa kawaida wasemaji humhutubia mtu aliyekufa, kwa sababu wanaamini kwamba nafsi au roho huendelea kuishi baada ya mwili kufa. Kwa sababu ya desturi hizo zilizotia mizizi, wazia matatizo yaliyowakabili wale waliotaka kufuata ibada safi. Baadhi ya watu waliodai kuwa Wakristo wa kweli hawakuacha kabisa desturi hizo na hata walijaribu kuziingiza katika kutaniko la Kikristo.
Waangalizi jasiri na wanyofu walihitajiwa ili kunyoosha mambo. Wale waliompenda Yehova walikuwa tayari kufundishwa na waangalizi hao na kufanya mabadiliko yaliyohitajiwa. Haikuwa rahisi kubadili maoni thabiti ya wale walioamini kimakosa kwamba tayari walijua kweli. Lakini tatizo kubwa lilikuwa kwamba watu walidhani Mashahidi wa Yehova ni wafuasi wa Kitawala.
Habari za kufunguliwa kwa ofisi ya tawi zilipoenea kotekote nchini, vikundi vingi vya akina ndugu viliandika barua na kuomba vitambuliwe kuwa makutaniko. Vikundi vya Kitawala vilifanya vivyo hivyo. Ripoti moja inasema hivi: “Kuna watu fulani waliosafiri umbali wa kilometa 2,300 wakiwa na orodha ndefu za majina ya wale waliotaka kuwa Mashahidi wa Yehova. Nyakati nyingine orodha hizo ziliandikwa kwenye karatasi zenye upana wa sentimeta 70 na urefu wa sentimeta 90 na nyakati nyingine zilikuwa na majina ya wakazi wote wa vijiji viwili au vitatu.”
Kabla ya kumkubali mtu yeyote au kikundi chochote kuwa Mashahidi wa Yehova, ilikuwa muhimu kujua ni nani waliokuwa Wakristo wa kweli na ni nani waliokuwa wafuasi wa Kitawala. Ndugu Heuse aliwatuma ndugu wakomavu wakafanye uchunguzi. Walifanya uchunguzi huo kwa miaka mingi. Hebu tuone baadhi ya mambo ambayo ndugu hao waaminifu walipata.
Kupambana na Kitawala
Mnamo mwaka wa 1960, Pontien Mukanga, ndugu mwembamba mpole, aliwekwa kuwa mwangalizi wa kwanza wa mzunguko nchini Kongo. Baada ya kuzoezwa nchini Kongo (Brazzaville), alitembelea makutaniko ya Léopoldville na vikundi kadhaa vya karibu. Hata hivyo, kazi ngumu zaidi ilimngojea, yaani, kupambana na Kitawala.
Mojawapo ya safari za kwanza za Ndugu Mukanga ilikuwa kwenda Kisangani (zamani iliitwa Stanleyville), umbali wa zaidi ya kilometa 1,600 kutoka jiji kuu. Kwa nini alienda huko? Alipokuwa katika utumishi wa shambani, Ndugu Heuse alikutana na Mzungu mmoja ambaye alimwonyesha picha iliyopigwa huko Stanleyville baada tu ya uhuru. Picha hiyo ilikuwa na ishara kubwa mbele ya kituo cha magari-moshi, Biblia iliyofunguliwa, na maneno yafuatayo: “Watch Tower Bible and Tract Society—International Bible Students Association—Dini ya Kitawala ya Kongo—Patrice E. Lumumba Aishi Milele—Antoine Gizenga Aishi Milele—Serikali ya M.N.C. Idumu Milele.” Bila shaka, dini ya Kitawala huko Kisangani ilikuwa ikitumia vibaya majina ya mashirika ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova.
Je, kulikuwa na Mashahidi wa kweli wa Yehova Kisangani? Ndugu Mukanga alitumwa ili kuchunguza. Ofisi ya tawi ilikuwa imepata habari juu ya mtu fulani aliyeitwa Samuel Tshikaka, ambaye alijifunza kweli huko Bumba na kurudi Kisangani mwaka wa 1957. Samuel hakushirikiana na kikundi chochote cha Kitawala na alitaka sana kumsaidia Ndugu Mukanga, ambaye aliandika hivi baadaye: “Nilienda pamoja na Samuel kuchunguza watu waliokuwa wakitumia jina Watch Tower. Tulimtembelea kasisi wao, na akatueleza kuhusu kikundi chake. Tuligundua kwamba ingawa baadhi yao walitumia Biblia, wote waliamini kwamba nafsi haifi. Walikuwa wakifundisha upendo kwa kubadilishana wake zao.
“Muda mfupi baada ya mimi kuwasili, polisi walijaribu kuwakamata wafuasi wa Kitawala jijini. Wafuasi hao walianza kupigana nao. Polisi waliwaomba wanajeshi waje kuwasaidia. Wafuasi wengi wa Kitawala waliuawa. Siku iliyofuata, mashua moja yenye maiti na waliojeruhiwa ilipita mahali tulipokuwa. Mwandishi wa kasisi aliandamana nao na aliponiona alikumbuka kwamba nilikuwa nimemtembelea kiongozi wao siku mbili zilizopita. Alinisingizia kwamba niliwasaliti kwa wenye mamlaka na akasema kwamba mimi ndiye niliyesababisha vifo vya watu waliouawa katika mapigano. Aliwaambia rafiki zake wa Kitawala wahakikishe kwamba sitoroki, lakini nilifaulu kutoroka kabla hawajaniua.”
Magazeti ya Ubelgiji yaliyoripoti kisa hicho yalitumia kichwa, “Vita Kati ya Mashahidi wa Yehova na Polisi.” Hata hivyo, wenye mamlaka nchini Kongo ambao walijua tofauti kati ya Kitawala na Mashahidi wa Yehova walitoa ripoti sahihi. Hakuna gazeti hata moja nchini Kongo lililodai kwamba Mashahidi walihusika katika kisa hicho!
Samuel Tshikaka alienda wapi? Bado yuko katika kweli na anatumikia akiwa mzee katika Kutaniko la Kisangani Tshopo-Est. Hivi sasa, kuna makutaniko 22 yenye wahubiri 1,536 jijini Kisangani. Lotomo, mwana wa Samuel, anatumikia akiwa mwangalizi wa mzunguko kama Pontien Mukanga alivyofanya miaka 40 iliyopita.
Mwangalizi wa Mzunguko Aliyenyoosha Mambo
Mwangalizi mwingine wa mzunguko ambaye pia alijitahidi kuonyesha kwamba kuna tofauti kati ya Mashahidi na Kitawala ni François Danda. Anaeleza hivi: “Huo ulikuwa wakati mgumu, na kulikuwa na mvurugo mkubwa. Sikuzote wafuasi wa Kitawala waliweka ishara zenye jina la Kiingereza, ‘Watch Tower’ katika sehemu zao za ibada. Vichapo vyetu vyote, katika lugha yoyote ile, vilikuwa na jina ‘Watch Tower’ kwenye ukurasa wenye habari za wachapishaji. Sasa wazia mtu fulani ambaye alisoma vichapo vyetu alikuwa akiwatafuta watu wa Mungu. Huenda akaona jengo lenye ishara ‘Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova’ katika lugha ya kienyeji, na kisha jengo lingine lenye maneno ya Kiingereza ‘Watch Tower.’ Inaelekea angeingia katika jengo gani? Waweza kuona jinsi watu walivyovurugwa.
“Ndugu wengi hawakuwa na ujuzi sahihi, na walikuwa na vichapo vichache tu. Mara nyingi makutaniko yalichanganya kweli na mafundisho ya Kitawala, hasa kuhusu utakatifu wa ndoa. Katika jiji moja nililotembelea, ilidhaniwa kwamba andiko la 1 Petro 2:17 linalosema, ‘tuupende ushirika mzima wa akina ndugu,’ lilimaanisha kwamba akina ndugu waliruhusiwa kufanya ngono na dada yeyote kutanikoni. Ikiwa dada alipata mimba ya ndugu ambaye si mume wake, basi mume alimkubali mtoto huyo kuwa mtoto wake. Kama ilivyokuwa katika karne ya kwanza, ‘wale wasiofundishwa na wasio imara’ walikuwa wakiyapotosha Maandiko.—2 Pet. 3:16.
“Nilitoa hotuba za Kimaandiko zilizoonyesha wazi kanuni za Yehova, hata zile zinazohusu ndoa. Niliwaambia kwamba kuna mambo fulani ambayo tulihitaji kunyoosha polepole, kwa subira, lakini kubadilishana wake ni jambo ambalo linapaswa kukomeshwa mara moja. Inafurahisha kwamba akina ndugu walielewa na kukubali maoni sahihi ya Kimaandiko. Hata wafuasi fulani wa Kitawala walioishi jijini humo walikubali kweli.”
Jitihada za Ndugu Mukanga na Ndugu Danda, na wengine wengi, ziliwasaidia watu kuona waziwazi kwamba Mashahidi wa Yehova ni tofauti na Kitawala. Leo, hakuna mtu anayedhani kwamba kuna uhusiano kati ya “Kitawala” na “Watch Tower.” Bado dini ya Kitawala ipo, ingawa haina uvutano au uwezo mkubwa kama zamani. Hata haijulikani katika sehemu nyingi.
Mipango Mizuri Yaleta Ongezeko
Mwishoni mwa mwaka wa utumishi wa 1962, zaidi ya wahubiri 2,000 walikuwa wakimtumikia Yehova kwa bidii kotekote nchini Kongo. Hata hivyo, ni ndugu wachache tu waliostahili Kimaandiko kuwa waangalizi. Tatizo moja lilikuwa kutojua kusoma na kuandika hasa miongoni mwa watu wenye umri mkubwa. Tatizo lingine lilikuwa kwamba wengi walishikilia desturi za kikabila na hivyo hawakubadilika haraka kupatana na kanuni za Mungu za uadilifu. Isitoshe, mtu yeyote ambaye alishirikiana na Kitawala hapo awali alihitaji kungoja kwa miaka mingi kabla ya kupewa mapendeleo yoyote ya utumishi.
Hata hivyo, pole kwa pole mafundisho ya kweli ya Kimaandiko na roho ya Yehova iliwasaidia wanaume kustahili kuwa waangalizi wa makutaniko. Waangalizi wa mzunguko na mapainia wenye ujasiri walijitahidi sana kuwaimarisha na kuwazoeza akina ndugu nchini kote. Wakati huo, waangalizi wa mzunguko na mapainia wa pekee waliozoezwa nchini Zambia waliingia pia Katanga na kusini mwa Kasai, majimbo ambayo yalikuwa yamekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Dini Zaruhusiwa Baada ya Uhuru
Kumbuka kwamba mnamo mwaka wa 1958 serikali ilitoa sheria iliyoruhusu uhuru wa ibada, na hivyo akina ndugu wakapata uhuru wa kuabudu kwa kadiri fulani. Mapema miaka ya 1960, ndugu waliendelea kuomba waandikishwe kisheria. Hawakutaka msaada wa kifedha kutoka kwa serikali, walitaka tu waandikishwe kisheria. Kuandikishwa kisheria kungewawezesha kuhubiri habari njema bila kusumbuliwa. Huo ulikuwa uhitaji wa haraka kwa sababu katika sehemu nyingi, wenye mamlaka walifanya mipango ya kuwashambulia akina ndugu. Majumba yao yaliteketezwa, ndugu walipigwa, wakakamatwa, na kufungwa gerezani. Kila mara ndugu walipopeleka malalamiko yao kwa Wizara ya Sheria, waliambiwa hivi: ‘Poleni sana, hatuwezi kuwasaidia kwa sababu hamjaandikishwa kisheria.’
Hali ilikuwa ngumu hata zaidi katika sehemu za mashambani kwa sababu mambo yalifanywa kiholela-holela. Serikali haikutambuliwa katika sehemu fulani nchini. Katika maeneo mengine, barua kutoka ofisi ya tawi ilitosha kufanya akina ndugu waachiliwe kutoka gerezani. Hata hivyo, katika maeneo yenye upinzani mkali, hakukuwa na njia ya kuwalinda akina ndugu wasiteswe na kufungwa gerezani.
Ndugu wa Kinshasa hawakupata upinzani mkali sana. Hapo awali walikusanyika kwa wingi jijini kwa ajili tu ya sherehe za harusi na mazishi. Lakini mwaka wa 1964, ofisi ya tawi ilipanga makusanyiko mawili ya mzunguko katika jiji kuu. Hilo lingekuwa jambo jipya kwa ndugu wengi. Mikutano ya pekee ilifanywa ili kuwazoeza ndugu kutoa hotuba na kupanga idara za kusanyiko.
Ndugu walisisimuka sana hivi kwamba walizungumza waziwazi kuhusu kusanyiko hilo, na habari zikamfikia gavana wa jimbo lililoitwa Léopoldville. Gavana huyo hakuwapenda Mashahidi wa Yehova, kwa hiyo aliandika barua kwa stensili ili isambazwe kwa watu wote wenye mamlaka katika eneo hilo. Barua hiyo iliagiza kwamba Shahidi yeyote anayepatikana akihubiri au akihudhuria mkutano wa ibada akamatwe. Lakini bila kutarajia, ndugu mmoja alipewa kazi ya kutoa nakala za barua hiyo. Ndugu huyo alikuwa na karatasi chache sana za kutoa nakala, naye alijua kwamba hakukuwa na karatasi huko Léopoldville. Basi msimamizi alipomwomba nakala za barua hiyo, ndugu alimwonyesha rafu tupu ambazo hazikuwa na karatasi!
Wakati huo, ndugu walikuwa wakisali kwa bidii sana kwa Yehova kuhusu jambo hilo. Ikawaje? Kwa ghafula, serikali iliamua kuanzisha majimbo mapya, na jimbo la yule gavana mpinzani likavunjwa! Kwa miaka mingi, watu mbalimbali walijaribu kuwanyanyasa au kuwaangamiza watu wa Mungu. Hata hivyo, jitihada zao ziliambulia patupu.—Isa. 54:17.
Mishonari Wengine Wawasili
Katika miaka ya 1960, hali iliporuhusu, tengenezo liliwatuma mishonari nchini Kongo. Makao madogo ya mishonari yalifunguliwa jijini Kinshasa. Mnamo Machi 1964, mishonari Julian na Madeleine Kissel, waliwasili kutoka Kanada. Miaka 40 imepita na bado wanatumikia kwa uaminifu wakiwa Wanabetheli huko Kinshasa.
Baadhi ya mishonari waliokuja mwishoni mwa miaka ya 1960 walihamia nchi nyingine. Mwaka wa 1965, Stanley na Bertha Boggus walitumwa Kongo baada ya kutumikia nchini Haiti. Ndugu Boggus, ambaye alikuwa mwangalizi anayesafiri, alirudi Marekani mwaka wa 1971 kwa sababu ya matatizo ya kiafya. Mwishoni mwa mwaka wa 1965, Michael na Barbara Pottage walijiunga na mishonari wengine nchini Kongo. Hivi sasa wanatumikia katika Betheli ya Uingereza. William na Ann Smith walitumwa Kongo mwaka wa 1966; walitumikia hasa huko Katanga. Walitumwa Kenya mwaka wa 1986 kwa sababu ya marufuku. Manfred Tonak kutoka Ujerumani, mhitimu wa darasa la 44 la Gileadi, alikuwa mwangalizi anayesafiri nchini Kongo. Kazi ilipopigwa marufuku, alitumwa nchini Kenya. Hivi sasa yeye ni mratibu wa Halmashauri ya Tawi nchini Ethiopia. Dayrell na Susanne Sharp walikuja Kongo mwaka wa 1969 baada ya kuhitimu darasa la 47 la Gileadi. Baada ya kufukuzwa Kongo, walitumwa Zambia na wamekuwa katika Betheli ya Lusaka tangu wakati huo. Mishonari wengine waliokuwa Kongo walitumwa nchi nyingine za Afrika Magharibi. Baadhi yao ni Reinhardt na Heidi Sperlich, waliokufa katika msiba wa ndege. Msiba huo uliwahuzunisha sana watu wote waliowajua.
Makao ya kwanza ya mishonari nje ya Kinshasa yalifunguliwa mwaka wa 1966 huko Lubumbashi, kusini-mashariki mwa nchi. Baadaye, makao mengine yalifunguliwa huko Kolwezi, upande wa kaskazini-magharibi wa Lubumbashi, na huko Kananga (wakati huo iliitwa Luluabourg), Kasai. Mishonari waliwasaidia sana ndugu kuwa imara na kuishi kupatana na kweli. Kwa mfano, huko Kasai, bado ndugu walikuwa na chuki ya kikabila. Kwa kuwa mishonari hawakutoka kwenye makabila hayo, waliweza kuwapatanisha ndugu waliokosana na kushughulikia kesi za hukumu bila kumpendelea yeyote.
Kuanzia mwaka wa 1968 hadi 1986, zaidi ya mishonari 60 walitumikia katika sehemu mbalimbali za nchi. Baadhi yao walihudhuria Shule ya Biblia ya Gileadi huko Marekani, na wengine, Shule ya Gileadi huko Ujerumani. Isitoshe, mapainia walioongea Kifaransa walikuja moja kwa moja nchini Kongo wakiwa mishonari. Wengi wao walijifunza lugha za wenyeji, na wote walijitahidi sana kuwafariji watu kwa habari njema za Ufalme.
Majumba ya Ufalme Katika Miaka ya 1960
Kwa kawaida, katika majiji makubwa ndugu walikutana katika majengo yasiyo na kuta. Majengo hayo yalifaa maeneo yenye unyevu na joto kali sana, na mikutano mingi ilifanywa wakati wa jioni au mapema asubuhi kukiwa na baridi kidogo. Majengo hayo yalifaa wakati wa majira ya kiangazi. Hata hivyo, katika majira ya mvua, mara nyingi mikutano iliahirishwa na kufanywa siku nyingine.
Jumba la Ufalme la kwanza liliwekwa wakfu mwaka wa 1962. Lilikuwa huko Kimbanseke, Kinshasa, na lilitumiwa na kutaniko moja kati ya makutaniko sita yaliyokuwa katika mji huo. Tangu wakati huo, makutaniko nchini Kongo yamejitolea sana katika ujenzi wa Majumba ya Ufalme. Hata hivyo, matatizo ya kisheria yalizuka mara kwa mara. Nyakati nyingine ndugu aliruhusu kutaniko kujenga jumba kwenye kiwanja chake ambacho hakikuwa na hati za kisheria. Ndugu huyo alipokufa, familia yake ilikuja na kuchukua jumba na kila kitu kilichomo. Ilikuwa vigumu sana kuwazuia wasifanye hivyo. Baadaye, wakati wa marufuku, majumba mengi yalichukuliwa na wenye mamlaka na kutumiwa kwa makusudi yao. Matatizo hayo yalizuia ujenzi wa Majumba mengi ya Ufalme.
Hata hivyo, Majumba ya Ufalme yalijengwa kote nchini. Ingawa majumba mengi yalikuwa sahili, yote yalithibitisha imani ya wajenzi. Hebu soma maelezo haya ya mishonari mmoja kuhusu majumba ya mikutano mwishoni mwa miaka ya 1960.
“Ili kufika kwenye Jumba la Ufalme huko Léopoldville, lazima tutumie kijia kinachopita katikati ya nyumba zilizojengwa kwa saruji isiyo laini. Umati wa watoto unatufuata. Tunaingia kwenye eneo lililozingirwa na ukuta wa saruji. Jumba la Ufalme lisilo na kuta liko nyuma ya nyumba wanamoishi ndugu wawili. Ndugu wanajizoeza kuimba nyimbo za Ufalme. Sauti zao zinavutia wee! Wanaimba kwa moyo wao wote. Tunafurahi kwamba miti inafunika jumba na kutukinga na jua. Jumba hilo linaweza kutoshea watu 200 hivi. Jukwaa ni la saruji na paa ni la mabati. Ikiwa msemaji ni mrefu, atalazimika kuinama kidogo. Kuna ubao wa matangazo wenye migawo ya kutaniko na barua kutoka kwenye ofisi ya tawi. Kuna meza ya vichapo. Ndugu wameweka mimea kandokando ya jukwaa. Ndugu wanaweza kufanya mikutano yao jioni kwa sababu wana taa za mafuta. Tunapoondoka, twawakuta watoto wakitungoja nje ili watufuate hadi barabarani.
“Sasa twasafiri hadi eneo la mashambani kabisa nchini Kongo. Tunaingia kwenye kijiji chenye nyumba za nyasi na mara moja tunaliona Jumba la Ufalme. Ni jengo lenye milingoti tisa na limeezekwa kwa majani mengi. Kuna mitaro midogo ambayo imechimbwa kutoka upande mmoja wa jumba hadi mwingine. Tunashangaa kwamba tunapoketi chini na kuweka miguu kwenye mitaro hiyo tunastarehe. Ishara ‘Jumba la Ufalme’ iliyoandikwa kwa mkono katika lugha ya wenyeji inaning’inia karibu na kichwa cha ndugu anayeongoza mikutano. Kuna watu 30 hivi mkutanoni. Huenda ni nusu yao tu ndio walio wahubiri. Wanajua nyimbo chache za Ufalme. Ijapokuwa hawajui nyimbo hizo vizuri, wanaimba kwa shauku sana, nasi tunaimba kwa moyo wetu wote.
“Sasa tunaelekea upande wa kaskazini wa nchi. Tunasimamisha gari letu aina ya Land Rover na kutazama kijiji. Tunaona nyumba nyingi za nyasi, na nyuma yake kuna jengo moja ambalo ni tofauti sana. Jengo hilo limejengwa kwa nguzo kubwa za mianzi zilizofungwa pamoja vizuri. Mlango na madirisha yametobolewa kwenye ukuta wa mianzi. Paa limeezekwa kwa nyasi. Kuna kijia chembamba na uwanja maridadi mbele ya jengo hilo. Ishara ndogo yenye maneno, ‘Mashahidi wa Yehova,’ imewekwa uwanjani. Twatembea kwenye kijia hicho na kufika kwenye Jumba la Ufalme na tunakaribishwa kwa uchangamfu na ndugu zetu. Tunapoingia, tunaona benchi zilizotengenezwa kwa mianzi. Ni vizuri kwamba maji hayawezi kupenya paa la Jumba la Ufalme! Kwa sababu yakipenya, kutakuwa na matatizo: Maji yakiangukia fito za mianzi, zitatia mizizi na kumea haraka sana. Na badala ya benchi ya mianzi unayokalia kuwa na kimo cha sentimeta 30 kutoka ardhini, itakuwa ndefu zaidi. Ratiba za mikutano na barua kutoka ofisi ya tawi zimebandikwa kwenye ubao wa matangazo. Akina ndugu wanachukua vichapo kwenye meza iliyotengenezwa kwa mianzi iliyopasuliwa na kuunganishwa kwa matete.
“Tunasafiri kusini na kufika Katanga jua linapotua. Kuna baridi huko, kwa hiyo tunavalia mavazi yenye joto. Tunafika kwenye kijiji kimoja, na tunapokaribia Jumba la Ufalme, tunawasikia akina ndugu wakiimba. Ndugu wengi vijijini hawana saa za mkononi, kwa hiyo wao hukisia tu saa za mikutano kwa kutazama jua. Kwa kawaida wale wanaofika kwanza kwenye jumba huanza kuimba hadi watu wanapokuwa wengi halafu mikutano huanza. Tunasongamana kwenye kiti kilichotengenezwa kwa gogo la mti lililopasuliwa mara mbili na kulazwa juu ya viegemeo viwili. Vichapo vinawekwa ndani ya kabati zee, lakini haviwezi kuhifadhiwa humo kwa muda mrefu kwa sababu vitavamiwa na kuharibiwa na mende na mchwa. Mkutano unapomalizika, ndugu wanatukaribisha tulitazame jumba lao. Kuta zimetengenezwa kwa matawi madogo yaliyounganishwa kwa matete na kufunikwa na udongo. Paa limeezekwa kwa nyasi zilizofumwa na hivyo maji hayawezi kupenya.”
Yehova Awalinda Watumishi Wake
Katika miaka ya 1960, vita vya wenyewe kwa wenyewe na jeuri ilikuwa imeenea sana. Watu wengi waliuawa, kutia ndani baadhi ya watu wa Yehova. Ndugu walihitaji imani na ujasiri ili kufanya mikutano kwa sababu nyakati nyingine mikutano ilidhaniwa kimakosa kuwa ya kisiasa. Katika Jimbo la Équateur, wanajeshi wenye silaha walifika kwenye Jumba la Ufalme na kuwakuta ndugu wakiwa mkutanoni. Wanajeshi hao walitambua mara moja kwamba ndugu walikutana ili kumwabudu Mungu wala si kuzungumzia siasa, kwa hiyo waliondoka huku wakisema kwamba hawampingi Mungu wala dini.
Siku moja, huko Kisangani, Bernard Mayunga na wahubiri wengine kadhaa walikamatwa na waasi ambao walikuwa wakiwatafuta machifu wa eneo hilo ili wawaue. Bernard alipoulizwa kabila lake, alijibu hivi: “Mimi ni Shahidi wa Yehova.” Kiongozi wa waasi alishangazwa na jibu hilo, akataka kujua anachomaanisha. Bernard alitoa ushahidi kwa kutumia Maandiko, na baadaye kiongozi huyo wa waasi akasema: “Ikiwa kila mtu angekuwa kama ninyi, hakungekuwa na vita.” Bernard pamoja na Mashahidi wengine waliokuwa wamekamatwa waliachiliwa huru.
Hatimaye Kazi Yaandikishwa Kisheria!
Kufikia mwaka wa 1965, nyumba moja ya ghorofa katikati ya jiji la Kinshasa bado ilikuwa ikitumiwa kama Betheli ya Kongo. Ilikuwa ndogo na haikuwa na nafasi ya kutosha. Idadi ya wahubiri wa Ufalme ilikuwa ikikaribia 4,000, na nyumba kubwa ilihitajiwa. Baada ya kutafuta kwa bidii, akina ndugu walipata nyumba iliyojengwa miaka sita iliyopita, kwenye barabara ya Avenue des Elephants namba 764, huko Limete, Kinshasa. Nyumba hiyo ilikuwa na orofa mbili na vyumba vinne vya kulala. Mara moja ndugu walianza kazi ya kubadili chumba kikubwa cha kupumzikia na cha kulia chakula vilivyokuwa kwenye orofa ya kwanza ili vitumiwe kama ofisi. Kazi ya kupakia vichapo na kupiga chapa ilifanyiwa katika gereji. Nyumba hiyo ilipanuliwa mwaka wa 1972.
Mnamo Novemba 1965, Joseph-Désiré Mobutu alipindua serikali na kuwa rais. Kwa mara nyingine tena, ofisi ya tawi iliomba kazi iandikishwe kisheria, na Juni 9, 1966, Rais Mobutu alitia sahihi sheria ya kuandikisha kazi yetu. Sasa watu wa Yehova walikuwa na haki na mapendeleo sawa na dini nyingine zilizoandikishwa kisheria nchini Kongo. Hatimaye sala za akina ndugu zilijibiwa na wakapata kile walichokuwa wamejitahidi kupata tangu mwaka wa 1932. Walikuwa huru kuhubiri hadharani, kufanya makusanyiko makubwa, na kumiliki mali. Hata hivyo, uhuru huo ulidumu kwa miaka sita tu.
Makusanyiko Yatoa Ushahidi Mkubwa
Ndugu walifurahi sana kupanga makusanyiko ya mzunguko huku wakilindwa na sheria! Jumla ya watu 11,214 walihudhuria makusanyiko ya kwanza 11 na 465 wakabatizwa.
Makanisa yalikerwa mno na makusanyiko hayo. Makasisi walifanya juu chini kuwazuia Mashahidi wa Yehova wasiandikishwe kisheria katika eneo hilo lenye watu wengi wanaopendezwa, ambalo waliliona kuwa eneo lao. Huko Gandajika katika Jimbo la Kasai, viongozi wa kidini walipeleka malalamiko kwa meya. Walipoona meya haogopi vitisho vyao, walituma vijana kuvuruga kusanyiko. Hata hivyo, sinema ya Biblia ilikuwa ikionyeshwa kwenye kusanyiko wakati huo, na umati mkubwa ulikuwa umekuja kuitazama. Vijana hao wenye fujo walipofika hapo, walitulia na kuanza kuitazama pia. Sinema hiyo iliwavutia sana. Kila mara ukanda wa sinema ulipobadilishwa, umati wa maelfu ya watu ulipaaza sauti hivi: “Mashahidi wa Yehova na waishi milele!”
Sasa Mashahidi wa Yehova walikuwa na idhini ya kufanya makusanyiko makubwa, lakini walihitaji kufanya matayarisho mengi. Walihitaji kupanga drama za Biblia na kutafuta mavazi ya waigizaji. Ndugu walihitaji kuweka vifaa vya sauti. Walifaulu kwa sababu walijitolea kwa hiari na walikuwa tayari kujifunza.
Kusafiri ili Kutumikia Kwenye Makusanyiko ya Mzunguko
Katika mwaka wa 1964, kulikuwa na mizunguko ya kutosha kuunda wilaya mbili nchini Kongo. Wilaya ya tatu ilianzishwa mwaka wa 1969 huko Kasai, na kufikia mwaka wa 1970, kulikuwa na wilaya nne. Kwa sababu ya barabara mbovu, mara nyingi ilikuwa vigumu kwa waangalizi wa wilaya na wengine kufika kwenye makusanyiko. Hebu tuandamane na mwangalizi wa wilaya, William Smith anapoenda kwenye kusanyiko la mzunguko.
“Mito ilifurika baada ya mvua kubwa sana kunyesha sehemu za mashambani. Tulikuwa tukienda Kamina kuhudhuria kusanyiko la mzunguko. Tulisafiri zaidi ya kilometa 320 ili kufika huko. Mvua hiyo kubwa iligeuza barabara fulani kuwa madimbwi ya matope, na katika sehemu nyingine maji yalifurika kabisa barabarani. Bonde moja liligeuka kuwa ziwa. Magari ya watu na ya serikali, na malori yalisimama kila mahali huku watu wakingoja maji yapungue. Wengi walitarajia safari yao kuchelewa kwa majuma mawili.
“Nilijua kwamba ndugu walikuwa wakingoja kwa hamu kusanyiko la mzunguko. Baadhi yao walitembea kwa siku kadhaa ili kuhudhuria. Niliuliza kama kuna barabara nyingine ya kuvuka bonde hilo. Nilishangaa watu waliponiambia kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa wametengeneza barabara ndogo, lakini kwa sababu udongo ulikuwa umelowa chepechepe, hawangemruhusu mtu yeyote kuitumia hadi mwangalizi wa wilaya apite kwanza na kwenda Kamina.
“Ndugu kutoka vijiji viwili walifanya kazi siku nzima, usiku kucha, na siku iliyofuata ili kutengeneza barabara mpya kuzunguka sehemu isiyopitika. Muda si muda nilifika mahali hapo na nikajitayarisha kuendesha gari langu aina ya jeep kwenye barabara waliyotengeneza. Umati mkubwa ulikuwa umekusanyika ili kuona kama gari langu lingepita. Baada ya gari hilo kwenda kwa umbali wa meta chache tu kwenye barabara hiyo mpya, tulivunjika moyo sana kuona likizama kwenye udongo uliolowa maji!
“Ndugu walilisukuma, lakini halikusogea hata kidogo. Walikuwa wamejikakamua sana, na nyuso zao zilionyesha kwamba wamekata tamaa. Hata hivyo, bado waliazimia kufanya yote wawezayo ili mwangalizi wa wilaya afike kwenye kusanyiko. Watazamaji walirudi kwenye magari yao, wakidhani kwamba barabara hiyo mpya ilikuwa balaa tupu. Ndugu waliamua kujaribu tena. Sasa walitoa kila kitu kwenye gari hilo ambalo lilikuwa limebeba vichapo, vifaa vya sauti, jenereta, na vitu vingine. Walichimba barabara na kulisukuma gari, na likaanza kusogea polepole huku magurudumu yakizunguka kwa kasi.
“Baada ya muda wa saa moja, kulikuwa na shangwe na vigelegele na nyimbo za Ufalme tulipofaulu kupita kwenye matope hayo. Ndugu walitimiza kile ambacho watu walioketi kwenye magari walidhani hakiwezekani. Kusanyiko lilifanikiwa kwa sababu ya jitihada za akina ndugu. Yehova alikuwa pamoja na watu wake na aliwasaidia kufanya mapenzi yake.”
Serikali Mpya Yaleta Mabadiliko
Haikuwa rahisi kuwafikia watu waliotapakaa kwenye nyanda tambarare na msitu wa mvua ulioenea kwa maelfu ya kilometa za mraba. Mishonari walihubiri kwenye miji mikubwa, na ndugu na dada wenyeji ambao ni mapainia wa pekee walihubiri katika maeneo ya mashambani. Watu wengi vijijini hawakujua kusoma na kuandika, kwa hiyo ilikuwa vigumu kuwa na makutaniko yaliyo imara. Isitoshe, mabadiliko ya kisiasa nchini yangeathiri maisha ya akina ndugu.
Mfumo wa chama kimoja cha kisiasa ulianza mwaka wa 1970. Chama hicho kiliitwa Chama cha Raia cha Mapinduzi (Mouvement Populaire de la Révolution katika Kifaransa), au MPR. Chama hicho kilikusudia kurudisha mambo ya kale, kutia ndani kubadili majina ya miji na majiji. Stanleyville liliitwa Kisangani, na Elisabethville likaitwa Lubumbashi. Mnamo mwaka wa 1971, serikali ilibadili jina la nchi na mto wake mkuu kuwa Zaire badala ya Kongo. Pesa zilibadilishwa kuwa zaires badala ya faranga. Serikali ilitaka watu wabadili majina yao pia: Walipaswa kuacha majina ya Kikristo na kutafuta majina ya Kiafrika. Tai zilipigwa marufuku kwa sababu zilionwa kuwa za Wazungu. Akina ndugu walitii kwa heshima mambo hayo yote.—Mt. 22:21.
Wanasiasa waliamini kwamba kila mtu aliyezaliwa Kongo alikuwa mwanachama mtendaji wa MPR. Watu walilazimishwa kuwa na kadi ya kisiasa ili kuajiriwa, kwenda shuleni, au kufanya biashara sokoni. Isitoshe, kila mtu alipaswa kuvaa alama ya chama hasa alipoingia kwenye ofisi ya serikali. Huo ulikuwa wakati mgumu kwa watu wa Yehova. Ndugu walifutwa kazi na watoto walifukuzwa shuleni.
Hata hivyo, maofisa fulani wa serikali walielewa msimamo wa Mashahidi wa Yehova. Waziri wa mambo ya ndani alimuuliza ndugu mmoja aliyekuwa akimfanyia kazi ni kwa nini havai alama ya chama. Ndugu huyo alimweleza sababu zake za Kimaandiko. Waziri huyo akasema: “Sisi tunakujua, na hatutakusumbua; lakini chama cha vijana kitakusumbua sana.”
Iliripotiwa kwamba Rais Mobutu mwenyewe, baada ya kupokea malalamiko mengi kuwahusu Mashahidi wa Yehova, aliwaambia hivi wanachama wake kwenye mkutano mmoja: ‘Ikiwa nitapata matatizo yoyote, hayataletwa na Mashahidi wa Yehova. Kumbukeni ni nani aliyemsaliti Yesu. Ni Yuda, mmoja wa wanafunzi Wake. Mtu atakayenisaliti ni yule ninayekula naye.’
Betheli Yapanuliwa kwa Sababu ya Ongezeko
Nathan H. Knorr, kutoka makao makuu huko Brooklyn, alitembelea Kongo mnamo Januari 1971. Jambo moja lililozungumziwa wakati wa ziara yake ni upanuzi wa Makao ya Betheli na ofisi. Mwaka wa 1970 kulikuwa na wahubiri 14,000 hivi katika makutaniko 194 na zaidi ya vikundi 200. Kwa sababu ya uhitaji uliokuwa ukiongezeka wa vichapo nchini Kongo, hakukuwa na nafasi ya kutosha ya kuhifadhi vichapo Betheli. Ilikuwa furaha iliyoje wakati Ndugu Knorr alipotangaza kwamba jengo hilo litapanuliwa! Mchora-ramani alichora ramani ya jengo jipya la kisasa lenye orofa mbili, na ukubwa wake ulikuwa maradufu ya ukubwa wa Betheli. Lingekuwa na ofisi kubwa, sehemu kubwa ya kuweka vichapo, na vyumba vingine vya kulala.
Ramani hizo ziliidhinishwa mnamo Juni 1971, na ujenzi ukaanza. Don Ward alitumwa kutoka Dahomey (sasa ni Benin) ili kusimamia ujenzi. Ndugu wengi waliojitolea kutoka makutaniko 39 ya Kinshasa walikuja kusaidia, wakamaliza ujenzi huo. Kama tutakavyoona, dini zinazodai kuwa za Kikristo zilizidi kukerwa na ongezeko kubwa la Mashahidi na upanuzi wa Betheli.
Ujasiri na Tahadhari Zahitajika Miaka ya 1970
Mnamo Desemba 1971, serikali ilitunga sheria ya kudhibiti dini na madhehebu mengi mapya ambayo yalikuwa yakichipuka nchini kote. Kulingana na sheria hiyo mpya, ni dini tatu tu zilizokuwa halali: Kanisa Katoliki, makanisa ya Kiprotestanti, na kanisa la kienyeji la Kimbangu. Dini nyingine tatu ziliandikishwa mwaka wa 1972: Uislamu, Kanisa Othodoksi, na dini ya Kiyahudi. Dini nyingi ndogo ziliandikishwa chini ya Uprotestanti.
Kwa hiyo, kuanzia mwaka wa 1971 hadi 1980, kulikuwa na marufuku ya kadiri ambayo ilizuia kwa njia fulani utendaji wa watu wa Mungu. Ingawa Mashahidi wa Yehova hawakuandikishwa kisheria, mishonari hawakufukuzwa, na kazi iliendelea Betheli bila shida. Makao ya mishonari huko Kananga yalifungwa, lakini makao ya mishonari huko Bukavu, Kisangani, Kolwezi, na Lubumbashi hayakufungwa. Ndugu hawakuweza tena kupanga makusanyiko makubwa ya wilaya. Lakini katika sehemu nyingi, ndugu walikutana katika Majumba yao ya Ufalme. Walifanya makusanyiko madogo ya mzunguko katika majumba makubwa. Mipango hiyo ilitegemea mtazamo wa wenye mamlaka katika sehemu mbalimbali. Katika sehemu zenye upinzani mkali, ndugu walijua kwamba wangeteswa na kukamatwa. Mamia ya ndugu walifungwa gerezani. Katika maeneo ambayo wenye mamlaka hawakupinga, ndugu waliendelea na utendaji wao wa kidini kwa uhuru.
Mashahidi waliendelea kuhubiri kwa ujasiri licha ya vizuizi hivyo. Ndugu watatu na dada mmoja walienda sokoni kuhubiri. Wanaume wawili waliwakaribia na kumkamata ndugu mmoja alipokuwa akimwachia kitabu mtu fulani mwenye kupendezwa. Walimpeleka kwenye makao makuu ya chama cha kisiasa na kumtia ndani ya chumba fulani ili amngoje mwenyekiti wa chama. Mwenyekiti wa chama aliingia na kumkuta ndugu huyo akimwonyesha mtu mwingine kitabu Je, Mwanadamu Alitokana na Mageuzi au Aliumbwa? (Did Man Get Here by Evolution or by Creation?)
“Je, unaeneza uwongo wako hapa?” mwenyekiti akamuuliza kwa ukali.
Ndugu akajibu: “Ikiwa mtu fulani angekuuliza, ‘Je, mwanadamu alitokana na mageuzi au aliumbwa?’ ungemjibuje?”
Mwenyekiti hakumjibu. Aliwatazama watu waliomkamata ndugu huyo na kusema: “Mwacheni aende. Havunji sheria yoyote.”
Ndugu huyo alirudi sokoni na kuendelea kuhubiri. Baadaye, mwenyekiti alipitia sokoni, akamwona. Aliwaambia wenzake hivi huku akimwelekezea ndugu huyo kidole: “Yule ni mwanamume jasiri, sivyo?”
Mwaka wa 1974, mwangalizi wa ofisi ya tawi, Ernest Heuse alilazimika kurudi Ubelgiji baada ya kushauriana na madaktari wake. Ernest aliugua ugonjwa wa kuvimba mapafu kwa kipindi fulani na afya yake ilizorota zaidi kwa sababu ya kushikwa na malaria mara nyingi. Ndugu waliipenda familia ya Heuse ambayo ilikuwa imechangia sana kazi ya Ufalme. Waliendelea kumtumikia Yehova kwa bidii nchini Ubelgiji. Ernest alikufa mwaka wa 1986; mkewe, Hélène, alikufa miaka minane baadaye. Timothy A. Holmes, ambaye alikuwa mishonari tangu mwaka wa 1966 alikabidhiwa daraka la kuwa msimamizi wa ofisi ya tawi ya Kinshasa.
Kazi Yaandikishwa Tena Kisheria Mwaka wa 1980
Mnamo Aprili 30, 1980, rais wa jamhuri alitia sahihi amri iliyoruhusu Shirika la Mashahidi wa Yehova liandikishwe kisheria. Watu wengi walipendezwa na kweli kuliko wakati mwingine wowote, watu 90,226 walihudhuria Ukumbusho na watu wenye kupendezwa wapatao 35,000 walikuwa wakijifunza Biblia. Kulikuwa na vilele vipya vya idadi ya wahubiri na mapainia. Majengo bora yalihitajiwa ili kutosheleza mahitaji ya eneo hilo. Kwa hiyo, akina ndugu walifurahi wakati Baraza Linaloongoza lilipoidhinisha ununuzi wa kiwanja chenye ukubwa unaozidi kwa mara mbili na nusu ukubwa wa kiwanja cha ofisi ya tawi ya Kongo. Hata hivyo, matatizo yalizuka kama tutakavyoona.
Kwa miaka mingi akina ndugu hawakuweza kupanga makusanyiko makubwa ya wilaya. Sasa walikuwa huru kufanya hivyo. Mnamo mwaka wa 1980, Makusanyiko matano ya Wilaya ya “Upendo wa Kimungu” yalifanywa nchini kote. Baadhi ya ndugu walisafiri mbali sana. Familia nyingi zilitembea umbali wa zaidi ya kilometa 400 ili kuhudhuria. Mapainia wawili wa pekee kutoka eneo la mbali sana walisafiri kwa majuma mawili zaidi ya kilometa 700 kwa baiskeli zao, kupitia kwenye mchanga mwingi na msitu mkubwa wa mvua. Ndugu fulani hata walitoka Kongo (Brazzaville), Burundi, na Rwanda.
Katika miaka iliyofuata, kulikuwa na uhitaji wa kupanga makusanyiko ya wilaya katika sehemu nyingi zaidi. Ni kweli kwamba ndugu walikuwa na uhuru wa kuabudu, lakini matatizo ya kiuchumi yalizidi kuongezeka. Wengi walishindwa kupata hata mahitaji ya lazima. Bei zilipanda, lakini mishahara haikuongezwa. Nauli ya magari ilikuwa juu sana hivi kwamba ndugu wengi hawakuweza kusafiri mbali. Kwa hiyo, ofisi ya tawi ilionyesha upendo kwa kufanya makusanyiko karibu na maeneo ambayo ndugu wengi waliishi.
Kwa kweli si rahisi kusafiri kwenye barabara za Kongo. Ni kawaida kupata miti iliyoanguka barabarani, madaraja yaliyoharibika, mchanga mwingi, na mashimo yenye matope. Wawakilishi wa ofisi ya tawi na wake zao hujidhabihu sana wanapotumikia kwenye makusanyiko. Lakini, ndugu na dada waaminifu ambao ni wenyeji hujidhabihu hata zaidi kwa sababu mara nyingi wao hulazimika kutembea kwa siku nyingi na kulala vichakani. Bado ndugu wengi hutembea umbali wa kati ya kilometa 50 na 150 ili kuhudhuria makusanyiko ya wilaya.
Makao Mapya ya Mishonari Yafunguliwa
Baada ya Mashahidi kuandikishwa kisheria mwaka wa 1980, mishonari wapya walikuja nchini. Makao mapya ya mishonari yalifunguliwa mwaka wa 1981 huko Goma (Jimbo la Kivu). Katika miaka miwili iliyofuata, makao mengine yalifunguliwa huko Likasi (Katanga), Mbuji-Mayi (Kasai), Kikwit (Bandundu), na jiji lenye bandari la Matadi (Kongo Kusini). Makao yaliyokuwa yamefungwa yalifunguliwa tena. Hatimaye, makao mengine ya mishonari yalifunguliwa mwaka wa 1986 huko Isiro (Jimbo la Orientale), kukawa na jumla ya makao 11 ya mishonari nchini. Makao hayo yalitumiwa pia kama depo za vichapo. Ofisi ya tawi ilipokea habari kuhusu eneo kutoka kwa mishonari. Ndugu na dada wenyeji walithamini kitia-moyo na mazoezi waliyopokea. Kulikuwa na kilele kipya cha wahubiri 25,753 mwishoni mwa mwaka wa utumishi wa 1981. Kulikuwa na mataraja makubwa sana ya ongezeko.
Hawamwogopi Kimbilikiti
Kimbilikiti ni jina la roho wa kabila fulani. Roho huyo huabudiwa na watu wa kabila la Rega, ambao wanaishi katika msitu mkubwa ulio upande wa mashariki ya kati wa Kongo. Maisha ya watu hao, ambao hasa ni wawindaji, wakulima, na wavuvi huongozwa na imani ya kidini inayohusiana na Kimbilikiti. Madhehebu hayo hufanya mambo kisiri, na makasisi wake wana uvutano mkubwa juu ya wale wanaomwogopa roho huyo.
Mashahidi wa Yehova katika eneo hilo hawamwogopi Kimbilikiti kwa sababu wanajua kwamba Yehova ndiye Mungu wa pekee wa kweli. Ni wao tu wasiofuata maagizo ya makasisi wa Kimbilikiti, kama vile kutoa dhabihu za mbuzi na kuku ili ziliwe na makasisi hao.
Kuanzia mwaka wa 1978, wafuasi wa madhehebu hayo walianza kuwatesa Mashahidi wa Yehova waziwazi. Waliteketeza Majumba kadhaa ya Ufalme, waliwafukuza ndugu fulani kutoka nyumbani kwao na kupora mali zao. Madhehebu hayo yalitumia pia uchawi na ulozi kujaribu kuwadhuru akina ndugu, lakini jitihada zao ziliambulia patupu. Kisha mnamo Agosti, 1983, wafuasi wa madhehebu hayo walitekeleza njama ya kikatili sana—waliwaua kinyama ndugu wanane karibu na kijiji cha Pangi.
Kisa hicho chenye kutisha kiliwashtua wote kutanikoni, hasa wale waliowapoteza waume au baba wapendwa. Ofisi ya tawi na ndugu wengine walipanga haraka kuandaa msaada wa kiroho na wa kimwili kwa familia zilizoathiriwa.
Wakati huo, wauaji walijificha msituni. Hata hivyo, hatimaye wale waliohusika walikamatwa. Kesi ilisikilizwa kwenye mahakama ya wilaya huko Kindu. Washtakiwa walidai kwamba roho wa Kimbilikiti ndiye aliyewachochea kuua. Lakini mwendesha-mashtaka wa serikali alitaja wazi wale waliopaswa kulaumiwa. Alisema: “[Watu fulani wa kabila la Rega] ambao wakati uliopita walishiriki katika desturi za Kimbilikiti na wanajua siri zinazohusika sasa wanashirikiana na Mashahidi wa Yehova. Wamefunua siri, hasa zile ambazo zinahusu kutokuwako kwa yule roho anayeitwa Kimbilikiti. Kwa hiyo, wao wamefunua uwongo wa matoleo yanayodaiwa na anayesemwa kuwa roho ambaye, kulingana na Mashahidi wa Yehova, ni udanganyifu mkubwa sana uliopangwa na wanaume wazee ambao wanaelekeza sherehe hizo.”
Kwa hiyo, washtakiwa hao walipatikana na hatia wala si Kimbilikiti. Walipokata rufani, mahakama kuu ya Bukavu iliunga mkono hukumu ya kifo waliyohukumiwa. Waendesha-mashtaka wa serikali walionya kwamba waabudu wa Kimbilikiti wataadhibiwa wakiwashambulia Mashahidi wa Yehova wakati ujao.b
Tangu wakati huo, kumekuwa na visa vingine, lakini wafuasi wa madhehebu hayo sasa wametambua kwamba hawawezi kujificha msituni wala Kimbilikiti hawezi kuwalinda kwa sababu roho huyo hayuko. Mashahidi wa Yehova wanaendelea kwa uaminifu kuwasaidia wengine watoke katika madhehebu hayo. Kwa upendo, Yehova amebariki jitihada hizo. Hivi sasa kuna zaidi ya wahubiri 300 wenye bidii katika makutaniko ya eneo hilo. Wanampenda Yehova; hawamwogopi Kimbilikiti.
Kazi Yapigwa Marufuku
Mwaka wa 1985, kazi ya Ufalme ilikuwa ikisitawi nchini Kongo. Betheli mpya ilikuwa imeanza kujengwa kwenye kiwanja kilichonunuliwa mwaka wa 1980. Wafanyakazi 60 hivi wa kujitolea kutoka nchi nyingine walikuja kusaidia. Mwishoni mwa mwaka wa utumishi, kulikuwa na wahubiri wapatao 35,000 na kilele kipya cha mapainia. Mishonari 60 walikuwa wakihubiri kwa bidii nchini kote. Waangalizi wanaosafiri walikuwa wakiwazoeza wazee wa makutaniko na mapainia. Kulikuwa na taraja la kupata ongezeko kubwa zaidi.
Hata hivyo, si kila mtu aliyefurahia ufanisi wa kiroho na wa kimwili wa watu wa Mungu. Makasisi waliwatumia wanasiasa kuvuruga utendaji wa akina ndugu. Machi 12, 1986, Rais Mobutu alitia sahihi sheria ya kupiga marufuku kazi ya Mashahidi wa Yehova. Siku iliyofuata, redio ya taifa ilitangaza marufuku hiyo. Mtangazaji mmoja alisema: “Huu ndio mwisho wa Mashahidi wa Yehova nchini [Kongo].” Alikuwa amekosea sana!
Ofisi ya tawi iliwarudisha ofisini mishonari wanne waliokuwa waangalizi wa wilaya na ikawatuma ndugu wenyeji waendelee na kazi hiyo. Mishonari walihisi kana kwamba wamefungiwa nyumbani kwa sababu hawangeweza kuhubiri hadharani. Ndugu wenyeji walihubiri kwa tahadhari sana. (Mt. 10:16) Kwa kusikitisha, watu wengi waliopendezwa waliacha kujifunza kwa sababu ya woga. Majumba fulani ya Ufalme yalifungwa au hata kuharibiwa. Mengine yalichukuliwa na chama cha kisiasa. Ndugu walilazimika kukutana katika vikundi vidogo. Walikamatwa usiku wakiwa nyumbani mwao, na mali zao kuporwa.
Katika Jimbo la Équateur, ndugu wengi walipigwa na kutupwa gerezani. Painia mmoja wa pekee alipigwa vibaya sana na kutiwa gerezani kwa miezi mitatu. Lile tangazo la redio ndilo lililosababisha mambo hayo yote. Kufikia wakati huo, hakukuwa na sheria rasmi ya kutekeleza marufuku hiyo. Punde tu baada ya marufuku kutangazwa, ndugu walikata rufani lakini hawakupata jibu lolote. Kisha mnamo Juni 1986, rais wa nchi alitoa hotuba ya hadharani akiwalaani Mashahidi eti wao si wazalendo na hawaheshimu mamlaka.
Mambo yalikuwa yamebadilika ghafula! Kikundi kilichoheshimiwa awali, kwa ghafula hakikuheshimiwa tena. Kazi ya ujenzi wa ofisi mpya ya tawi ilisimama, kukawa na kimya kwenye uwanja ambao awali ulikuwa na shangwe na utendaji mwingi. Iliwabidi wafanyakazi wote wa kujitolea kutoka nchi nyingine waondoke nchini, na vifaa vya ujenzi viliuzwa. Ndugu wenyeji 20 hivi walibaki ili kulinda mahali hapo.
Kisha, kwa ghafula, afisa mkuu wa usalama alituma barua iliyoandikwa Juni 26, 1986, ambayo ilisema kwamba mishonari wote wanapaswa kuondoka nchini. Marufuku hiyo ilikuwa tofauti sana na marufuku ya mwaka wa 1972, ambayo iliwaruhusu mishonari kubaki nchini. Ilihuzunisha sana kuiona Idara ya Upakizi na Usafirishaji ikiwa imejaa mizigo ya mishonari walipokuwa wakijitayarisha kuondoka! Mnamo Julai, mishonari 23 walifunga safari kwenda nchi nyingine. Mishonari waliokuwa likizoni hawakurudi nchini. Huo ulikuwa mwanzo wa kipindi kingine cha marekebisho nchini Kongo.
Mipango Mipya ya Utendaji wa Kisiri
Ikiwa wapinzani walidhani kwamba wangewavunja moyo au kuwaangamiza watu wa Yehova, walikuwa wamekosea sana. Hawakujua nguvu za roho takatifu ya Yehova na azimio la watu wa Mungu. Mishonari wachache wenye uzoefu walibaki nchini ili kuongoza kazi. Wasimamizi wa ofisi ya tawi walisimamia kazi ya kuhubiri Ufalme wakiwa kwenye nyumba kadhaa za kibinafsi. Shule ya Utumishi wa Painia iliongozwa katika nyumba za ndugu kotekote nchini.
Kulikuwa na chakula tele cha kiroho. Ndugu waliendelea kuchapa na kugawa vichapo vya Biblia. Ofisi ya tawi ilituma mihtasari ya makusanyiko ya wilaya na ya mzunguko kwenye makutaniko, ambako ilitolewa kama hotuba. Waangalizi wa mzunguko walipotembelea makutaniko, walicheza kanda za drama za makusanyiko ya wilaya katika lugha za kienyeji. Walifanya hivyo kila mwaka kuanzia mwaka wa 1986 hadi marufuku ilipoondolewa. Ingawa hiyo ilikuwa kazi nyingi, akina ndugu walifaidika sana.
Wakati huohuo, wazee waliwasiliana na wakuu wa serikali ili kueleza msimamo wetu wa kutounga mkono siasa na walijaribu kueleza waziwazi kwamba hiyo haimaanishi sisi tunaipinga serikali. Kupitia jitihada hizo, jina la Yehova na kusudi lake lilijulikana kwa watu wote, hata kwa watu wenye mamlaka ya juu nchini. Watumishi wa Yehova walikuwa tofauti sana—hawakuunga mkono upande wowote bali walikuwa wenye amani na hawakuipinga serikali.
Wahubiri wa Ufalme Wapungua Kisha Waongezeka
Ripoti ya utumishi ya mwaka wa 1987 ilionyesha kwamba idadi ya wahubiri ilipungua kwa asilimia 6. Baadhi ya wahubiri waliogopa na hawakutaka kuhusianishwa na tengenezo lililopigwa marufuku. Mateso makali yalizuka katika sehemu kadhaa.
Hata hivyo, nyakati nyingine wapinzani hawakufaulu. Kwa mfano, chifu mmoja alifanya mkutano wa pekee ili kuwashutumu Mashahidi wa Yehova. Chifu huyo aliinua Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia na kuwaambia watu wamkamate yeyote anayegawa kitabu hicho. Watu wakamwambia kwamba wangependa kukichunguza kitabu hicho ili waweze kukitambua. Alikubali, na watu walipendezwa na kitabu hicho. Baadhi yao waliomba nakala za kitabu hicho kutoka kwa painia wa pekee aliyeishi katika kijiji kingine. Painia huyo anasema hivi: “Nilianzisha mafunzo kumi ya Biblia. Sikuwahi kuhubiri katika kijiji cha chifu huyo. Kama hangetushutumu, huenda watu hao hawangepata nafasi ya kujifunza kweli!”
Akina ndugu walizoea hali hizo mpya. Ingawa kulikuwa na vizuizi vingi, ‘hawakubanwa kupita kiasi cha kuweza kusonga.’ (2 Kor. 4:8) Kufikia mwisho wa mwaka wa utumishi wa 1988, idadi ya wahubiri ilikuwa imeongezeka kwa asilimia 7. Mafunzo ya Biblia yapatayo 60,000 yalikuwa yakiongozwa. Ndugu wa Idara ya Utumishi huko Betheli walitembelea majiji makubwa ili kuwatia akina ndugu moyo na kukutana na wazee na waangalizi wanaosafiri. Ofisi ya tawi iliendelea kusimamia kazi katika nchi ya Burundi, na nchi jirani ya Kongo (Brazzaville), ambako kazi ilikuwa imepigwa marufuku pia.
Ndugu mmoja, mwalimu mkuu wa shule huko Kolwezi, alikataa kula kiapo cha kisiasa. Alipigwa vibaya sana kwa sababu ya kukataa, halafu akapelekwa Lubumbashi, ambako wapinzani wake walidhani angeuawa. Kwa utulivu, ndugu huyo aliwaeleza msimamo wake wa kutounga mkono siasa. Aliachiliwa na kurudishwa Kolwezi. Wale waliompiga waliamriwa wamwombe msamaha! Aliendelea na kazi yake ya ualimu na akateuliwa kuwa mkaguzi wa shule!
Mnamo Oktoba 1988, machifu fulani walichukua kiwanja cha Betheli huko Kinshasa na vichapo vingi sana vya Biblia. Kwa kawaida wanajeshi waliiba vitabu na Biblia nyingi na kuziuza sokoni. Watu walizinunua, hivyo akina ndugu walipata nafasi bora sana ya kuanzisha mafunzo ya Biblia.c
Licha ya marufuku, idadi ya wahubiri wa Ufalme ilifikia 40,707 mwaka wa 1989. Maadui wa kidini wa Mashahidi wa Yehova walikasirika sana. Yule aliyekuwa waziri wa sheria, na pia rafiki mkubwa wa Kanisa Katoliki, alituma barua kwa waendesha-mashtaka wote wa serikali nchini Kongo, akieleza kwamba anashangaa kuwaona watu wa Yehova wakiendelea na utendaji wao. Aliwaamuru wawashtaki Mashahidi wa Yehova na kufunga Majumba ya Ufalme. Baadaye, alipokuwa akiwahutubia viongozi wa kidini, alisema kwamba watu wa Yehova ni “mashetani halisi.” Kwa hiyo ndugu walianza kuteswa katika jimbo la Bandundu ambako waziri huyo anatoka.
Watoto Wafungwa Gerezani
Wakati huo, baadhi ya watoto wa Mashahidi wa Yehova walikamatwa shuleni kwa sababu ya kukataa kushiriki katika sherehe fulani za kisiasa. Baba mmoja mwenye wavulana wawili alikamatwa pia na kutiwa gerezani pamoja na wavulana wake wadogo. Walinzi wa gereza waliagizwa wasiwape chakula chochote. Mlinzi mmoja aliuliza hivi kwa mshangao: “Katika gereza hili tuna wauaji na wezi, na tunawapa chakula. Mbona tumnyime chakula mtu huyu pamoja na watoto wake wawili?” Mlinzi huyo alipokosa kupata jibu lenye kuridhisha, yeye mwenyewe aliwapa chakula. Wavulana hao walikaa gerezani kwa siku 11, na baba yao ambaye ni painia wa pekee alikaa humo kwa siku 7. Jaribu hilo halikuwavunja moyo hata kidogo.
Huko Kikwit, mtu mmoja ambaye hakuwa Shahidi wa Yehova alikamatwa baada ya mke wake ambaye ni Shahidi, kufungwa gerezani pamoja na binti zake wawili. Maofisa walipogundua kwamba mtu huyo si Shahidi, walimwamuru aondoke gerezani. Alikataa kwenda, huku akisema kwamba hatamwacha mke wake na watoto. Alipoachiliwa hatimaye pamoja na familia yake, alijifunza Biblia, akabatizwa. Hivi sasa yeye ni mzee wa kutaniko.
Msukosuko Nchini
Mapinduzi ya kijeshi yalipotokea Kinshasa mnamo Septemba 1991, watu walipora sana. Hilo lilisababisha upungufu mkubwa wa chakula na mafuta, na vilevile ukosefu mkubwa wa kazi, huku bei za bidhaa zikipanda sana. Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova ya Afrika Kusini na Ufaransa zilituma msaada.
Mbali na kushughulikia matatizo nchini humo, ofisi ya tawi ya Kongo iliwatunza pia Mashahidi wakimbizi kutoka nchi jirani ya Angola na Sudan. Huko kaskazini-mashariki mwa Kongo, Zekaria Belemo, ambaye alikuwa mwangalizi anayesafiri wakati huo, alitembelea kikundi cha ndugu wakimbizi kutoka Sudan. Alitoa hotuba katika Kiingereza ingawa hakukijua vizuri, na ikatafsiriwa katika Kiarabu. Zekaria hakuwa na hakika iwapo ndugu walielewa hotuba hiyo. Baada ya miaka mitano hivi, vijana wawili waliotembelea Betheli walimjia na kumuuliza: “Je, unatukumbuka? Tulikuwa miongoni mwa watu waliosikiliza hotuba yako katika kambi ya wakimbizi. Tulikumbuka kitia moyo chako, tukaanza kujifunza Biblia.” Baadaye, vijana hao waliweka maisha yao wakfu kwa Yehova.
Migogoro ya kikabila ilikuwa pia tatizo kubwa nchini kote. Wakazi wengi wa Kasai walikuwa wamehamia upande wa kusini huko Katanga. Mwaka wa 1992 na 1993, wakazi wa Katanga waliwafukuza kutoka jimbo hilo. Wengi wao walipoteza kazi, mali, na nyumba zao. Walikimbilia kambi, au sehemu nyingine, ili waokoe uhai wao na kuishi pamoja ili wawe salama. Zaidi ya watu 100,000 walirudi nyumbani kwao huko Kasai. Kulikuwa na Mashahidi wa Yehova 4,000 miongoni mwao. Ndugu walioishi karibu walijitahidi sana kuwasaidia ingawa wao pia walikuwa maskini na chakula kilikuwa haba. Kutaniko moja kwenye barabara kuu inayoelekea kaskazini kutoka Katanga, liliwatuma akina ndugu wawatafute Mashahidi katika kila lori lililowasili. Mara tu baada ya kutambuliwa, ndugu hao walitunzwa.
Ofisi ya tawi ya Afrika Kusini ilituma malori kadhaa yaliyojaa chakula na dawa kwa ajili ya akina ndugu wakimbizi waliokuwa kambini. Misaada hiyo iliokoa uhai wao. Baraza Linaloongoza pia liliwaagiza ndugu wa Kinshasa wanunue chakula, dawa, majembe, na vijiko vya kuchimbia, ili familia hizo ziweze kurudi Kasai na kulima mashamba yao.
Dalili Nyingine za Mabadiliko
Hotuba ya rais na mkutano aliofanya na waandishi wa habari Aprili 24, 1990, ulionyesha kwamba maoni ya serikali kuwahusu Mashahidi wa Yehova yalikuwa yamebadilika sana. Rais aliwahakikishia waandishi wa habari nchini na wa kigeni kwamba serikali inatetea uhuru wa msingi, kutia ndani uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kidini. Hivyo ndugu walitumia nafasi hiyo kuhubiri na kukutana waziwazi zaidi. Wale waliokuwa gerezani waliachiliwa.
Je, unamkumbuka yule mtangazaji wa redio ambaye mwaka wa 1986 alitangaza kwa uhakika kwamba huo ulikuwa mwisho wa Mashahidi wa Yehova nchini Kongo? Utabiri wake ulithibitika kuwa wa uwongo. Mashahidi walipopigwa marufuku mwaka wa 1986, kulikuwa na wahubiri 34,207 nchini Kongo. Kufikia mwisho wa mwaka wa utumishi wa 1990, kulikuwa na wahubiri 50,677 nchini Kongo, na watu 156,590 walihudhuria Ukumbusho. Mahindi yaliyokuwa katika gunia letu yalikuwa yameongezeka licha ya upinzani, uchongezi, mateso, na hasira ya viongozi wa kidini na wa kisiasa. Mnamo mwaka wa 1997, wakati serikali ya Rais Mobutu ilipopinduliwa, ni mtangazaji huyo ndiye aliyelazimika kutoroka nchini, wala si Mashahidi wa Yehova.
Uhuru Tena
Amri ya rais ya mwaka wa 1986 ilipiga marufuku utendaji wote wa Mashahidi wa Yehova, na ikavunja shirika lao la kisheria nchini humo. Hata hivyo, Januari 8, 1993, Mahakama Kuu ya Sheria ya Zaire (Kongo) ilitoa uamuzi wa Kesi Kati ya Mashahidi wa Yehova na Jamhuri ya Zaire. Mahakama hiyo iliamua kwamba agizo la rais halikuwa la haki, na hivyo likafutiliwa mbali. Ndugu walikuwa na furaha iliyoje!
Uamuzi wa Mahakama Kuu ulizusha ubishi mkali kwa sababu mahakama hiyo ilifuata katiba mpya ya mabadiliko, ambayo haikukubaliwa na rais na wale waliomuunga mkono. Baadhi ya watu waliona uamuzi huo kuwa kielelezo cha kutumiwa wakati ujao na mahakama. Mashahidi hawakushiriki ubishi huo, lakini ushahidi mkubwa sana ulitolewa kwa utukufu wa jina la Yehova! Magazeti mengi yalizungumzia kesi hiyo muhimu. Kisha Idara ya Sheria iliwajulisha magavana wa majimbo mbalimbali kwamba Mashahidi wa Yehova waliruhusiwa kisheria kuendelea na utendaji wao wa kidini. Ulikuwa ushindi ulioje kwa watu wa Yehova na kwa ibada ya kweli!
Matatizo ya Kusafirisha Vichapo Nchini Kongo
Kongo ni nchi kubwa sana. Hata hivyo, nchi hiyo imezungukwa na nchi nyingine na ina sehemu ndogo tu ya pwani huko Bas-Kongo. Shehena kubwa huingia katika bandari ya Matadi. Kuna reli moja tu na barabara moja ya lami kati ya Matadi na jiji kuu, umbali wa kilometa 300 hivi.
Ofisi za tawi huko Ulaya ziliitumia ofisi ya tawi ya Kongo malori kadhaa ambayo yametumiwa kusafirisha vichapo na katika ujenzi. Tangu mwaka wa 1999, kumekuwa na depo ya Betheli huko Matadi. Depo hiyo imesaidia sana kwa sababu vichapo hutolewa moja kwa moja kutoka kwenye meli na kuhifadhiwa kwenye depo hiyo hadi lori linapokuja kutoka ofisi ya tawi na kuvisafirisha hadi Kinshasa.
Katika miaka ya 1980, vichapo vilikuwa vikisafirishwa moja kwa moja kutoka Kinshasa hadi Lubumbashi. Ndugu waliosafirisha vichapo walipitia kwenye makao ya mishonari yaliyotumiwa kama depo huko Kananga na Mbuji-Mayi. Ndege ilisafiri kutoka Kinshasa hadi Lubumbashi kwa muda wa saa mbili hivi, lakini lori lililojaa mizigo lilitumia majuma mawili! Hata hivyo, barabara zilizidi kuharibika kadiri miaka ilivyopita hivi kwamba mwishowe hazikupitika. Ingawa kuna mito mingi sana inayoweza kutumiwa kwa usafiri, mashua zinazoenda mbali kutoka Kinshasa hazitegemeki. Mbali na magumu hayo, magari ya Betheli hayawezi kusafiri mbali sana kutoka Kinshasa kwa sababu bado kuna migogoro ya kisiasa katika maeneo fulani. Njia bora ya kusafirisha vichapo kutoka ofisi ya tawi hadi maeneo ya mbali ni kwa ndege.
Ofisi nyingine zimesaidia kuwapelekea akina ndugu vichapo. Ofisi ya Kamerun husafirisha vichapo kwa lori kupitia Jamhuri ya Afrika ya Kati hadi kaskazini mwa Kongo. Ofisi ya Rwanda na ya Kenya hupeleka vichapo upande wa mashariki wa nchi hiyo. Makutaniko katika sehemu fulani za kusini hupokea vichapo kutoka Afrika Kusini na Zambia.
Shule ya Mazoezi ya Kihuduma Yaboresha Utumishi
Darasa la kwanza la Shule ya Mazoezi ya Kihuduma lilifanywa Kinshasa mwaka wa 1995. Kufikia Aprili 2003, zaidi ya ndugu 400 walikuwa wamezoezwa katika madarasa 16. Wanafunzi 5 wa shule hiyo ni waangalizi wa wilaya, na zaidi ya 60 ni waangalizi wa mzunguko. Wanafunzi wengine 50 wamewekwa kuwa mapainia wa pekee. Ndugu hao wamewatia wengi moyo kushiriki kwa bidii katika kazi ya kuhubiri.
Haikuwa rahisi kwa baadhi yao kuhudhuria shule hiyo. Georges Mutombo alipopokea barua ya kumwalika kwenye shule hiyo, alikuwa akiishi katika eneo lililo chini ya majeshi yanayoipinga serikali. Alilazimika kusafiri umbali wa kilometa 400 kwa baiskeli hadi Kamina, ili apande ndege ya kwenda Kinshasa, ambako shule ingefanywa. Akiwa safarini, alinyeshewa kwa siku tatu na alipita vituo 16 vya ukaguzi vya wanajeshi. Alipitia pia eneo lenye wahalifu chungu nzima. Pindi moja, alifukuzwa na genge la wezi waliokuwa wakiendesha baiskeli. Mbio hizo zilifika mwisho wakati gurudumu la baiskeli ya kiongozi wa genge hilo lilipopasuka. Bila shaka wezi hao walitambua kwamba Georges alikuwa Shahidi kwa sababu ya mavazi yake. Walimwambia kwa sauti kwamba hawangemfukuza tena kwa kuwa waliona kwamba Yehova, Mungu wake alikuwa pamoja naye.
Majengo kwa Ajili ya Ongezeko la Kitheokrasi
Tangu mwaka wa 1965, ofisi ya tawi ilikuwa kwenye barabara ya Avenue des Elephants namba 764, Limete, Kinshasa. Mnamo mwaka wa 1991, uwanja ulinunuliwa katika eneo la viwanda jijini. Uwanja huo ulikuwa na majengo matatu makubwa ambayo hapo awali yalitumiwa na kampuni ya kufuma vitambaa, na baadaye yakatumiwa kama karakana. Ndugu walirekebisha majengo hayo ili shughuli zote za ofisi ya tawi ziwe mahali pamoja. Mradi huo ulikawia kwa sababu ya misukosuko ya kisiasa na ukosefu wa usalama, lakini ujenzi wa ofisi mpya ya tawi ulianza baada ya watumishi wa kimataifa kuwasili mnamo mwaka wa 1993. Mnamo Aprili 1996, wafanyakazi wa ofisi ya tawi walihamia majengo hayo mapya. Baada ya kuhama, mzee mmoja wa Betheli alisema hivi: “Kuiona familia yetu yote ikiwa pamoja tena, kunatukumbusha miaka kumi iliyopita wakati kazi yetu ilipopigwa marufuku. Tunamshukuru sana Yehova Mungu na tengenezo lake linaloonekana kwa sababu ya majengo haya maridadi sana.” Mnamo Oktoba 1996, kulikuwa na kilele kipya cha wahubiri 100,000. Mataraja ya ongezeko kubwa zaidi yaliwasisimua akina ndugu.
Mishonari Waja Kusaidia
Katika miaka ya 1990, mishonari wengine walitumwa nchini Kongo ili wajiunge na wale mishonari saba waliobaki nchini wakati wa marufuku. Katika Julai 1995, Sébastien Johnson na mkewe, Gisela, walitumwa nchini Kongo kutoka Senegal. Mishonari wengine walikuja baadaye. Baadhi yao walikuwa wahitimu wa shule ya Gileadi huko Marekani, hali wengine walitoka Ubelgiji, Ufaransa, na Uingereza. Christian na Juliette Belotti waliwasili kutoka Guiana ya Ufaransa mwezi wa Machi 1998. Mnamo Januari 1999, Peter Wilhjelm na mkewe, Anna-Lise, walitumwa Kongo kutoka Senegal. Baadaye, mishonari wengine waliwasili Kongo kutoka Kamerun, Mali, na Senegal.
Mnamo Desemba 1999, makao mapya ya mishonari yalifunguliwa jijini Kinshasa. Mishonari 12 wanaishi katika makao hayo. Jiji la Lubumbashi limekuwa na makao ya mishonari tangu 1965. Makao mengine yalifunguliwa jijini humo mwaka wa 2003. Hivi sasa, wenzi wanne wa ndoa wanaishi kwenye makao hayo. Mnamo Mei 2002, makao mapya ya mishonari yalifunguliwa huko Goma, upande wa mashariki wa nchi. Mishonari wanne walitumwa huko. Mishonari hao wanaendelea kusaidia sana katika shamba hili kubwa lenye ongezeko.
Msimamo wa Kikristo wa Kutounga Mkono Vita
Mishonari wengi waliwasili wakati wa mapinduzi na fujo nchini humo. Vita vilizuka upande wa mashariki mnamo Oktoba 1996, na kuenea haraka hadi sehemu nyingine. Wanajeshi walipigana ili kumpindua Rais Mobutu. Majeshi ya Laurent-Désiré Kabila yaliingia Kinshasa Mei 17, 1997, naye akawa rais.
Watu ulimwenguni pote walipokuwa wakitazama kwenye televisheni picha zenye kuogofya za wakimbizi waliokonda kwa sababu ya njaa na magonjwa, watu wa Yehova waliendelea kutangaza ujumbe wa Biblia wa tumaini na faraja. Inasikitisha kwamba maelfu ya watu, kutia ndani Mashahidi 50 hivi, waliangamia wakati wa vita. Baada ya vita, watu wengi walikufa kutokana na kipindupindu na magonjwa mengine.
Watu wengi walipoteza vitambulisho vyao wakati wa vita, kwa hiyo, ndugu wanaoenda kuhubiri maeneo ya mbali hukabili matatizo. Kuna vituo vingi vya ukaguzi vya wanajeshi barabarani. Wahubiri wa kutaniko moja hawakuwa na vitambulisho, kwa hiyo, mzee mmoja alidokeza kwamba akina ndugu waonyeshe kadi zao za Mwelekezo wa Mapema Kuhusu Tiba/Ondoleo la Hatia, nao wakafanya hivyo. Katika kituo kimoja cha ukaguzi, wanajeshi waliwaambia: “Hatutaki kadi hizo. Tunataka kitambulisho cha raia!”
Ndugu waliwajibu hivi: “Hii ndiyo kadi inayotutambulisha kuwa Mashahidi wa Yehova.” Wanajeshi wakawaruhusu kupita.
Huko Kisangani, askari wa kukodiwa waliokuwa wakisaidia majeshi ya serikali walitia gerezani ndugu wanne vijana. Ilisemekana kwamba ndugu hao walikuwa wanawapasha habari maadui. Kila asubuhi, askari wa kukodiwa waliwachagua wafungwa kumi, kisha waliwapeleka msituni na kuwaua. Asubuhi moja, waliwachagua ndugu wawili pamoja na wafungwa wengine wanane, wakaanza safari kuelekea msituni. Lori lilisimama njiani kwa sababu kulikuwa na maiti barabarani. Askari hao waliwaamuru wale ndugu wawili wamzike maiti huyo. Baada ya kumzika, ndugu hao walingoja lori lirudi, kwa sababu liliwaacha hapo na kuendelea na safari. Ingawa walikuwa na nafasi ya kutoroka, hawakutoroka kwa sababu hawakutaka kuhatarisha uhai wa ndugu zao wawili waliobaki gerezani. Lori lilirudi bila wale wafungwa wanane, kwani walipigwa risasi. Kila mtu gerezani alipigwa na bumbuazi kuwaona ndugu hao wawili wakirudi wakiwa hai. Baada ya muda mfupi, majeshi ya upinzani yaliuteka mji huo na kulipua mlango wa gereza. Askari wa kukodiwa walitoroka, na ndugu wakaachiliwa huru.
Ofisi za Tawi za Ulaya Zasaidia Nyakati za Shida
Maeneo mengi ya Kongo yamekumbwa na vita tangu mwaka wa 1996, na watu wengi wamekuwa wakimbizi. Maelfu ya akina ndugu kutoka Kongo walikimbilia kambi za wakimbizi nchini Tanzania na Zambia. Majeshi ya waasi yalipozidi kuteka maeneo mengi ya Kongo, ikawa vigumu zaidi kwa ofisi ya tawi kuwatunza na kuwasiliana na ndugu wanaoishi kwenye maeneo ya waasi. Halmashauri za kutoa misaada ziliundwa katika majiji makubwa ili kugawa misaada. Familia ya Betheli ilionyesha roho ya kujitoa na kujidhabihu kwa kufanya kazi hadi usiku wa manane ili kusaidia kugawa misaada. Mashahidi wa Yehova nchini Ubelgiji, Ufaransa, na Uswisi walisafirisha kwa ndege tani nyingi za chakula, mavazi, dawa, majozi 18,500 ya viatu, na mablangeti 1,000. Kazi ya kutoa misaada ingali inaendelea na inapunguza matatizo. Mashahidi wa Yehova na watu wengine wanafaidika.
Mnamo Oktoba 1998, makala moja katika gazeti fulani la Kinshasa ilisema hivi: “Makutaniko ya Kikristo ya Mashahidi wa Yehova katika nchi mbalimbali za Ulaya yamekusanya zaidi ya tani 400 za bidhaa za misaada na kuzituma Kongo-Kinshasa na Kongo-Brazzaville. Watu ambao wamejitolea kutoka Uingereza, Ufaransa, na Uswisi, tayari wamepeleka jijini Kinshasa tani 37 za mchele, maziwa ya unga, maharagwe, na biskuti zenye vitamini. Zilisafirishwa kwa ndege kutoka Ostend, Ubelgiji, zikafika kwenye ofisi kuu ya Mashahidi wa Yehova huko Kinshasa. Ndege nyingine . . . itafika . . . ikiwa na tani 38 za chakula.
“Inapendeza kwamba Mashahidi wa Yehova wamewasaidia wakimbizi katika Afrika Mashariki tangu yale mauaji makubwa yaliyotukia nchini Rwanda. . . . Msemaji wa Mashahidi wa Yehova alitangaza kwamba misaada hiyo ya hiari yenye uzito wa zaidi ya tani 200, kutia ndani chakula na dawa, ilisaidia kupambana na ugonjwa wa kipindupindu. Wakati huo, Mashahidi wa Yehova kutoka Ufaransa na Ubelgiji waliunda vikundi kadhaa vya kuwasaidia wakimbizi kambini. Alitaja pia misaada ambayo Mashahidi wa Yehova wamewapa maskini huko Ulaya Mashariki na Bosnia.”
Vita Havizuii Maendeleo ya Kiroho
Mnamo Septemba 1998, waasi waliushambulia mtaa wa Ndjili karibu na Kinshasa. Wakati wa msukosuko huo, ndugu kadhaa walienda kujificha katika nyumba ambamo mwangalizi wa mzunguko alikuwa akiishi. Mwangalizi wa mzunguko alisali kwa ajili yao, halafu akawasomea andiko la Isaya 28:16. Mstari huo wasema: “Yeyote anayeonyesha imani hataingiwa na wasiwasi.” Aliwatia moyo wote wawe watulivu na wamtegemee Yehova ili awaongoze.
Baadhi yao walipendekeza wavuke daraja na kukimbia Ndjili, hali wengine walidokeza wafuate reli. Mwishowe, ndugu hao waliamua kubaki walipokuwa. Siku tatu baadaye, majeshi ya serikali yaliteka tena eneo hilo. Ndugu walipata habari kwamba kama wangalifuata mojawapo ya njia walizopendekeza, wangalinaswa katika vita.
Ndugu mmoja wa Kutaniko la Museka Kipuzi huko Katanga alikuwa akiwauzia wanajeshi kadhaa samaki. Baada ya mazungumzo, mwanajeshi mmoja alimshtaki kuwa mpelelezi wa chama cha upinzani. Alifungwa, akapigwa vibaya, kisha akapelekwa kwenye makao makuu ya kijeshi ya jimbo hilo. Walifika huko usiku. Wanajeshi walimwamuru ndugu huyo awachezee dansi. Ndugu huyo aliwauliza hivi: “Mtafurahiaje dansi yangu gizani?”
Wakamwambia: “Waweza kuimba badala ya kucheza dansi.” Ndugu huyo aliimba kwa moyo wake wote wimbo, “Mtupie Yehova Mzigo Wako.” Wanajeshi hao waliguswa moyo na maneno ya wimbo huo, wakamwomba aurudie. Aliimba wimbo huo mara ya pili. Mwanajeshi mmoja alimwomba aimbe wimbo mwingine. Sasa aliimba wimbo “Asante, Yehova,” katika lugha yake ya Kikiluba. Alipomaliza kuimba, wanajeshi hao walimfungua. Asubuhi iliyofuata walimpeleka mjini na kuwahoji majirani wake ili kuhakikisha kwamba hakuwa mpelelezi. Kabla ya kuondoka, wanajeshi walimwambia hivi: “Tulitaka kukuua, lakini sasa hatutakuua. Dini yako imeokoa uhai wako! Tulivutiwa sana na maneno ya nyimbo mbili ulizoimba. Usichoke kumtumikia Mungu wako!”
Ujenzi wa Majumba ya Ufalme Wamletea Yehova Sifa
Katika miaka ya karibuni, Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova limefanya jitihada ya pekee ya kusaidia kujenga Majumba ya Ufalme katika nchi maskini. Ndugu Wakongomani walifurahia sana mpango huo kwa sababu kulikuwa na uhitaji mkubwa sana wa Majumba ya Ufalme. Kwa mfano, jiji la Kinshasa lilikuwa na makutaniko 298, lakini idadi ya majumba yanayofaa haikuzidi 20. Mamia ya majumba yalihitajiwa nchini kote. Katika Aprili 1999, mpango wa ujenzi wa Majumba ya Ufalme ulianza huko Kinshasa. Baadaye, ujenzi ulianza kwenye majimbo mengine ya Kongo. Kufikia mwanzoni mwa mwaka wa 2003, Majumba ya Ufalme yapatayo 175 yalikuwa yamejengwa katika nchi mbili za Kongo.
Mtu mmoja aliyefahamu kweli tangu miaka ya 1950 alifurahi sana kuona Jumba la Ufalme likijengwa mbele ya nyumba yake. Alisema: “Sikupendezwa na kazi ya Mashahidi. Sasa naona matokeo ya jitihada zao. Walijenga Jumba la Ufalme karibu na nyumba ya kaka yangu, na sasa kuna Jumba la Ufalme mbele ya nyumba yangu. Ni kana kwamba Mashahidi wananifuata popote niendapo!” Mtu huyo alikubali mwaliko wa kuhudhuria Ukumbusho wa kifo cha Kristo na kuwekwa wakfu kwa Jumba hilo jipya la Ufalme. Sasa anahudhuria mikutano kwa ukawaida.
Makutaniko matatu huko Matete yalifanya mikutano kwenye jengo lililochakaa, ambalo walinunua mwaka wa 1994. Akina ndugu hawakuwa na pesa za kurekebisha jengo hilo, basi lilibaki hivyo kwa miaka sita. Kulikuwa na kanisa kubwa ng’ambo ya barabara. Kanisa hilo lilipojengwa, kasisi alisema kwamba Mashahidi wa Yehova watahama karibuni. Majirani waliwadhihaki akina ndugu kwa sababu hawakuwa na mahali pazuri pa mikutano. Hata kutaniko lilipoanza kutengeneza matofali ya Jumba jipya la Ufalme, majirani fulani waliendelea kuwadhihaki. Walishangaa sana walipoona matokeo! Sasa wanasema kwamba jengo la Mashahidi wa Yehova ndilo maridadi zaidi katika eneo hilo. Jirani mmoja ambaye hakutaka kamwe kuongea na Mashahidi hapo awali alivutiwa na kazi iliyofanywa na akina ndugu. Alikuja mahali pa ujenzi akaahidi kwamba atawasikiliza Mashahidi watakapomtembelea.
Katika sehemu moja ambapo ujenzi ulikuwa ukiendelea, mwanamke fulani alimfikia dada aliyekuwa akiwapikia wafanyakazi. Mwanamke huyo akamuuliza: “Je, mnajenga kanisa?”
“Tunajenga Jumba letu la Ufalme,” dada akamjibu.
Mwanamke huyo akasema: “Jengo hili litakuwa kama ninyi mlivyo. Ninyi huwa safi na nadhifu sikuzote. Kanisa lenu litakuwa kama ninyi!”
Mabadiliko Katika Usimamizi wa Ofisi ya Tawi
Ili kushughulikia mahitaji ya eneo, mabadiliko yalihitaji kufanywa katika Halmashauri ya Tawi. Baraza Linaloongoza lilifanya mabadiliko hayo Mei 1996. Sébastien Johnson aliteuliwa kuwa mratibu wa Halmashauri ya Tawi Mei 20, 1996. Halmashauri ya Tawi ambayo ilisimamia kazi ilikuwa na ndugu wawili tu, Sébastien Johnson na Peter Ludwig, ambaye alikuwa ameteuliwa miezi miwili awali. Miaka iliyofuata, wengine waliteuliwa: David Nawej, Christian Belotti, Benjamin Bandiwila, Peter Wilhjelm, Robert Elongo, Delphin Kavusa, na Uno Nilsson. Kwa sababu ya matatizo ya kiafya, Peter Ludwig na mkewe, Petra, walilazimika kurudi Ujerumani ambako sasa wanafanya kazi kwenye ofisi ya tawi.
Ndugu wa Halmashauri ya Tawi wanajitahidi sana kutoa mwelekezo wa kitheokrasi katika eneo lote. Kwa kuongezea, watumishi wa Yehova kutoka Amerika Kaskazini, Ulaya, na Japani, wametumwa nchini Kongo wakiwa watumishi wa kimataifa, Wanabetheli wanaotumikia katika nchi nyingine, na mishonari. Katika mwaka wa utumishi wa 2003, familia ya Betheli ya Kinshasa ilikuwa na zaidi ya Wanabetheli 250. Kwa wastani, wana umri wa miaka 34.
Bado Kuna Kazi Nyingi
Nabii mmoja wa kale aliandika hivi: “Amebarikiwa yule mtu hodari anayemtegemea Yehova, na ambaye Yehova amekuwa uhakika wake.” (Yer. 17:7) Ndugu wanaendelea kuwatangazia wengine habari njema ya Ufalme kujapokuwa na vita katika maeneo kadhaa nchini Kongo. Ingawa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinazuia jitihada za ofisi ya tawi za kutoa msaada wa kiroho katika nchi yote, inatia moyo kuona idadi ya wahubiri ikifikia kilele kipya kabisa cha 122,857.
Katika habari hii, tumesimulia mambo yaliyowapata watumishi waaminifu nchini Kongo. Haiwezekani kutaja majina ya ndugu na dada wote ambao wametetea na kuithibitisha kisheria habari njema nchini Kongo. Hata hivyo, wote wanaweza kuwa na hakika kwamba Yehova anawathamini na atawapa thawabu. Mtume Paulo aliwaandikia hivi Wakristo wenzake: “Mungu hakosi kuwa mwadilifu hivi kwamba asahau kazi yenu na upendo mlioonyesha kwa ajili ya jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu nanyi mnaendelea kuhudumu.”—Ebr. 6:10.
Bado kuna kazi nyingi sana inayohitaji kufanywa. Kuna maeneo mapya yanayohitaji kuhubiriwa. Majumba ya Ufalme yanahitaji kujengwa. Ofisi ya tawi inahitaji kupanuliwa. Hata hivyo, baada ya kuchunguza utendaji wa kitheokrasi wa zaidi ya miaka 50 nchini Kongo, tunakubaliana na ndugu aliyesema hivi katika mwaka wa 1952: ‘Sisi ni kama mbegu za mahindi ndani ya gunia. Mahali popote tuangushwapo, mmoja baada ya mwingine, hatimaye mvua hunyesha na tunakuwa wengi.’ Tunangoja kwa hamu kuona jinsi Baba yetu wa mbinguni, Yehova Mungu, atakavyokuza mbegu ya Ufalme.—1 Kor. 3:6.
[Maelezo ya Chini]
a Katika vipindi mbalimbali, nchi hiyo iliitwa Nchi Huru ya Kongo, Kongo ya Ubelgiji, Kongo, Zaire, na tangu mwaka wa 1997 imekuwa ikiitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa kawaida huitwa Kongo (Kinshasa) ili kuitofautisha na nchi jirani ya Kongo (Brazzaville). Tutatumia jina Kongo katika masimulizi haya yote.
b Ona gazeti la Amkeni! la Januari 1986, ukurasa wa 12-19.
c Hatimaye, Mahakama Kuu iliamua kwamba akina ndugu warudishiwe kiwanja chao ambapo Betheli ilikuwa imeanza kujengwa mwanzoni mwa miaka ya 1980. Baadaye wanajeshi waliishi kwenye kiwanja hicho. Hata hivyo, wanajeshi walipoondoka hatimaye mwaka wa 2000, wakuu wa eneo hilo waligawanya kiwanja hicho visehemu-visehemu na kuwauzia maskwota kwa njia haramu. Sasa mamia ya maskwota wanaishi kwenye kiwanja hicho. Tatizo hilo bado halijasuluhishwa.
[Blabu katika ukurasa wa 229]
“Huu ndio mwisho wa Mashahidi wa Yehova nchini [Kongo]”
[Blabu katika ukurasa wa 249]
“Tulitaka kukuua, lakini sasa hatutakuua. Dini yako imeokoa uhai wako!”
[Sanduku katika ukurasa wa 168]
Maelezo Mafupi Kuhusu Kongo (Kinshasa)
Nchi: Ikweta inapita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ukubwa wa nchi hiyo ni zaidi ya mara sita ya ukubwa wa nchi jirani ya Kongo (Brazzaville). Sehemu kubwa ya eneo la kaskazini la Kongo ina misitu mikubwa ya mvua ambayo haipenywi na mwangaza wa jua. Kuna milima na volkeno zilizo hai mashariki mwa nchi hiyo. Magharibi mwa nchi hiyo kuna pwani yenye urefu wa kilometa 37 kwenye Bahari ya Atlantiki.
Watu: Kuna watu milioni 55 nchini Kongo kutoka makabila zaidi ya 200 ya Kiafrika. Asilimia 50 ni Wakatoliki; asilimia 20 ni Waprotestanti; asilimia 10 ni wafuasi wa Kimbangu; na asilimia 10 ni Waislamu.
Lugha: Kuna lugha nyingi nchini Kongo. Ingawa lugha rasmi ni Kifaransa, lugha za Kiafrika zinazotumiwa sana ni Kilingala, Kingwana, Kiswahili, Kikongo, na Kitshiluba.
Kazi: Kongo ina rasilimali nyingi kama vile, mafuta, almasi, dhahabu, fedha, na urani. Lakini mapigano ya karibuni yameathiri sana uuzaji wa bidhaa katika nchi za ng’ambo na kuongeza madeni ya nchi hiyo. Familia za mashambani wanapanda vyakula wanavyohitaji kama vile mihogo, mahindi, na mpunga.
Wanyama wa Pori: Kuna wanyama wengi wa pori nchini humo. Misitu imejaa nyani, sokwe-mtu, na tumbili. Paa, chui, simba, vifaru, na punda-milia wanaishi kwenye nyanda tambarare. Kuna mamba na viboko mitoni.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 173, 174]
Aliitafuta Kweli, Akaipata
Henry Kanama alikuwa mfuasi wa Kanisa la Kiinjilisti huko Luena lakini baadaye aligundua kwamba dini yake haikuwa ya kweli. Mara nyingi alienda milimani kusali na kutafakari. Huko milimani alikutana na kikundi kilichodai kwamba kinawasiliana na roho wasioonekana. Wafuasi wa kikundi hicho walimwambia Henry kwamba wanadhani Mungu yuko mbali sana, lakini hawakujua yuko wapi.
Henry alianza kumtafuta Mungu wa kweli. Baada ya muda, alikutana na mtu mmoja ambaye alimpa gazeti la Amkeni! la Kifaransa. Punde si punde, Henry aligundua kwamba amepata kweli ya Biblia ambayo alikuwa akitafuta. Aliwaandikia Mashahidi wa Yehova akitumia anwani iliyokuwa ndani ya gazeti hilo, na baada ya muda alikuwa akijifunza Biblia kupitia barua. Hatimaye, Henry pamoja na mkewe, Elisabeth, na baadhi ya rafiki zao waliandika barua na kuuliza jinsi wanavyoweza kubatizwa. Walipokea barua iliyowaomba wawasiliane na ofisi za tawi katika nchi jirani. Ofisi nyingi zilikuwa mbali sana.
Henry na Elisabeth pamoja na Hyppolite Banza na mkewe, Julienne, waliamua kwenda Rhodesia Kaskazini. Wote walijua kwamba walihitaji kujifunza lugha ya Cibemba ili kuongeza ujuzi wao wa kweli. Walihesabu gharama kisha wakahama. Baada ya kukaa huko kwa miezi sita, walibatizwa mwaka wa 1956.
Walirudi Kongo mwaka huohuo, na kuhubiri habari njema kwa bidii. Mnamo mwaka wa 1961, Henry na wenzake walikamatwa na kutiwa gerezani. Walishtakiwa kuwa wafuasi wa Kitawala ambao walimuua chifu ambaye alipanga njama ya kumuua chifu mwingine. Baadaye waliachiliwa huru kwa sababu hakukuwa na uthibitisho kwamba walifanya hivyo.
Henry na Elisabeth walianza utumishi wa painia. Hatimaye wakawa mapainia wa pekee na baadaye wakafanya kazi ya mzunguko. Henry alikufa mwaka wa 1991, lakini Elisabeth angali painia wa kawaida. Mwana wao anayeitwa Ilunga ni mwangalizi wa mzunguko.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 178]
Albert Luyinu—Shahidi Mwaminifu
Albert alihubiriwa kweli kwa mara ya kwanza mwaka wa 1951 na mfanyakazi mwenzake, Simon Mampouya, kutoka Kongo (Brazzaville). Albert alikuwa Mkongomani wa kwanza kuwa daktari wa meno, na haikuwa rahisi kwake kukubali kweli kwa sababu ya cheo chake kikubwa. Alibatizwa pamoja na mkewe mwaka wa 1954, baada ya mwadhimisho wa Ukumbusho. Walibatizwa usiku kwa sababu kazi ilikuwa imepigwa marufuku wakati huo.
Kuanzia mwaka wa 1958 hadi 1996, Albert alikuwa mwakilishi wa Shirika la Mashahidi wa Yehova ambalo lilikuwa limeandikishwa kisheria nchini Kongo. Anakumbuka kwamba siku moja alitafsiri hotuba ya ndoa iliyotolewa na Ndugu Heuse mbele ya umati wa watu 1,800. Kwanza hotuba hiyo ilifafanua majukumu ya mke Mkristo. Albert anakumbuka jinsi alivyojiona kuwa mtu wa maana alipomtazama mkewe na dada wengine waliokuwepo. Hata hivyo, anasema kwamba aliposikia majukumu ya mume Mkristo, alinyenyekea na kujiona duni. Hotuba ilipomalizika alijiona duni hata zaidi!
[Picha]
Albert na Emilie Luyinu
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 191-193]
Mahojiano na Pontien Mukanga
Alizaliwa: 1929
Alibatizwa: 1955
Maisha yake: Alikuwa mwangalizi wa kwanza wa mzunguko nchini Kongo.
Nilienda hospitalini kwa sababu ya maumivu ya jino mwaka wa 1955. Daktari wa meno anayeitwa Albert Luyinu alinitibu kisha akanionyesha andiko la Ufunuo 21:3, 4, linalozungumza kuhusu wakati ambapo maumivu hayatakuwapo tena. Nilimweleza mahali nilipoishi, na Albert akanitembelea jioni hiyo. Nilifanya maendeleo ya kiroho haraka na kubatizwa mwaka huohuo.
Niliwekwa kuwa mwangalizi wa mzunguko wa nchi nzima ya Kongo mnamo mwaka wa 1960. Kazi ya mzunguko haikuwa rahisi. Nilisafiri kwa siku nyingi, hata majuma mengi, juu ya malori yaliyojaa mizigo ambayo yalipitia barabara mbovu, huku kukiwa na jua kali sana. Mbu walinisumbua usiku. Mara nyingi, lori liliharibika, na ilinibidi kungoja hadi lirekebishwe. Nilitembea peke yangu kwenye vijia visivyo na ishara yoyote na nyakati nyingine nilipotea.
Siku moja, nilitembelea mji fulani kaskazini mwa Kongo. Nilikuwa na Leon Anzapa. Tulisafiri pamoja kwa baiskeli kuelekea mji mwingine uliokuwa umbali wa zaidi ya kilometa 120. Tulipotea njia na tukalazimika kulala katika nyumba ya kuku usiku mmoja. Wadudu wanaowavamia kuku walikuwa wakituuma, kwa hiyo, mwenye nyumba aliwasha moto sakafuni licha ya kwamba hakukuwa na dirisha lolote.
Usiku huo vita vilizuka kati ya mtoto wa mwenye nyumba na wanakijiji wengine. Punde si punde, mwenye nyumba alianza kupigana pia. Tulijua kwamba ikiwa angeshindwa, basi tungejikuta taabani. Hatukulala hata kidogo usiku huo kwa sababu ya wadudu, moshi, na vita.
Kabla ya mapambazuko, tulichukua baiskeli zetu na kutoroka kimya-kimya, lakini baada ya kilometa chache, tulipotea njia tena. Tulisafiri siku nzima kwenye barabara isiyo na watu. Wakati wa jioni, Leon alianguka kutoka kwenye baiskeli yake kwa sababu ya njaa na uchovu. Uso wake uligonga mwamba na mdomo wake wa juu ukapasuka. Alikuwa akivuja damu nyingi sana, lakini tuliendelea na safari hadi tulipofika kwenye kijiji kimoja. Wanakijiji walipomwona Leon, walitaka kujua ni nani aliyemjeruhi. Tuliwaeleza kwamba alianguka kutoka kwenye baiskeli yake. Hawakuamini na wakadai kwamba ni mimi niliyemjeruhi. Hatukulala usiku huo; Leon alihisi maumivu makali sana, na wanakijiji walipanga kuniumiza kama adhabu. Asubuhi iliyofuata tuliendelea na safari hadi tulipofika kwenye kijiji kimoja ambako tulipata dawa. Walitia dawa ya Mercurochrome kwenye mdomo wa Leon na kufunga kidonda kwa vibanio sita. Tulisafiri kilometa nyingine 80 hadi Gemena, ambako nilimwacha Leon kwenye hospitali ndogo ili apate matibabu. Nilisafiri peke yangu ili nijiunge na mke wangu. Baadaye tuliendelea kuhubiri kandokando ya mto hadi Kinshasa.
Kwa kawaida Marie, mke wa Pontien, aliandamana naye katika safari hizo. Alikufa mwaka wa 1963. Mwaka wa 1966, Pontien alioa tena, na akaendelea na kazi ya mzunguko hadi mwaka wa 1969. Angali katika utumishi wa wakati wote akiwa painia wa kawaida.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 195, 196]
Mahojiano na François Danda
Alizaliwa: 1935
Alibatizwa: 1959
Maisha yake: Alikuwa mwangalizi anayesafiri kuanzia mwaka wa 1963 hadi 1986. Alifanya kazi katika Betheli ya Kongo kuanzia mwaka wa 1986 hadi 1996. Sasa yeye ni mzee na painia wa pekee.
Mnamo mwaka wa 1974, nilipokuwa nikitembelea kutaniko moja huko Kenge, Jimbo la Bandundu, mimi pamoja na ndugu wengine sita tulikamatwa na wanamgambo wa chama kinachotawala. Walitushtaki kwamba tulikataa kushiriki katika sherehe za kisiasa za kumheshimu kiongozi wa taifa. Walitutia katika chumba kidogo cha gereza kisicho na madirisha chenye upana na urefu wa meta mbili. Hatukuweza kuketi wala kulala chini; tuliegemeana tu. Tulikaa ndani ya chumba hicho kwa siku 45, na tuliruhusiwa kutoka nje mara mbili tu kwa siku. Mke wangu, Henriette alipopata habari, alisafiri umbali wa kilometa 290 kutoka Kinshasa kuja kuniona. Hata hivyo, walimruhusu kuniona mara moja tu kwa juma.
Siku moja mwendesha-mashtaka wa serikali alitembelea gereza hilo. Sherehe ya kisiasa ilifanywa kwa heshima yake. Kila mtu, isipokuwa sisi, aliimba nyimbo za kisiasa na kukariri wito wa chama. Mwendesha-mashtaka alikasirika sana, akaniamuru niwaagize ndugu wenzangu sita waimbe. Nilimjibu kwamba sina mamlaka juu yao na wanapaswa kuamua wenyewe kuimba au kutoimba. Nilipigwa kwa sababu ya kusema hivyo.
Baadaye, tulibebwa nyuma ya gari. Askari wawili waliandamana nasi ili kutulinda, na mwendesha-mashtaka aliketi mbele pamoja na dereva. Tulikuwa tukienda Bandundu, jiji kuu la jimbo la Bandundu. Gari lilikuwa likienda kasi mno. Niliwaambia akina ndugu wajishikilie kwa nguvu, halafu nikaanza kusali. Nilipokuwa nikimaliza kusali, gari lilipiga kona kali sana, likapinduka. Ni ajabu kwamba hakuna yeyote aliyekufa wala kujeruhiwa. Tuliona kwamba Yehova alikuwa ametulinda. Baada ya kulirudisha gari barabarani, mwendesha-mashtaka aliwaamuru wale askari wawili waturudishe gerezani kwa miguu. Lakini gari liliendelea na safari hadi Bandundu.
Tulipofika gerezani, askari hao waliwaambia wakuu wa gereza kile kilichotukia na wakawasihi watuachilie. Msimamizi wa gereza alishangaa sana na kama sisi, aliamini kwamba Mungu alikuwa ametulinda. Kwa siku kadhaa tulikaa ndani ya chumba cha kawaida gerezani na tuliruhusiwa kuchangamana na wafungwa wengine uani. Baadaye tuliachiliwa huru.
François na Henriette waliitwa Betheli baada ya kufanya kazi ya mzunguko kwa miaka 24. Miaka kumi baadaye wakawa mapainia wa pekee. Henriette alikufa Agosti 16, 1998.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 200-202]
Mahojiano na Michael Pottage
Alizaliwa: 1939
Alibatizwa: 1956
Maisha yake: Michael na mkewe, Barbara, walitumikia nchini Kongo kwa miaka 29. Sasa wako katika Betheli ya Uingereza na Michael ni mzee katika kutaniko la Kilingala jijini London.
Tatizo kubwa tulilokabili ni kujifunza lugha. Kwanza tulihitaji kujua vizuri Kifaransa, lugha rasmi ya Kongo. Huo ulikuwa mwanzo tu. Huko Katanga, tulijifunza Kiswahili; huko Kananga, tulihitaji kuongea Kitshiluba; na tulipotumwa Kinshasa, tulijifunza Kilingala.
Jitihada hizo zilitufaidi sana. Kwanza, ndugu zetu walifurahi sana tulipojitahidi kuzungumza nao. Waliona jitihada zetu za kuongea lugha yao kuwa uthibitisho wa kwamba tunawapenda kikweli na tunawajali. Pili, tuliwagusa mioyo watu tuliowahubiria. Mwanzoni wenye nyumba walishangaa sana kusikia kwamba tunaongea lugha yao, kisha walifurahi na kusikiliza ujumbe wetu kwa heshima na kwa hamu.
Tulipokuwa tukifanya kazi ya wilaya, tuliokoka hatari nyingi kwa sababu ya kujua lugha za wenyeji. Wakati wa vita, wanajeshi na wafuasi wa vyama vya kisiasa waliweka vizuizi barabarani ili kuwatoza watu pesa kwa nguvu. Waliwalenga hasa wageni kwa sababu walidhani kwamba wana pesa nyingi na wanaweza kudanganywa kwa urahisi. Kila tuliposimamishwa kwenye kizuizi, tuliwasalimu askari kwa lugha ya kienyeji. Na hilo liliwashtua. Walituuliza sisi ni nani. Tulipowaeleza kuhusu kazi yetu tukitumia lugha yao, kwa kawaida walifurahi na kukubali vichapo vyetu, na hata walitutakia safari njema na baraka za Mungu.
Mara nyingi tuliguswa moyo sana na upendo wa kweli na roho ya kujidhabihu ya ndugu zetu Waafrika. Kwa miaka mingi, Kongo ilikuwa na serikali ya chama kimoja ambayo iliwapinga vikali na hata kuwatesa watu ambao hawakuunga mkono siasa, kama vile Mashahidi wa Yehova. Wakati huo mgumu, tulitumia gari aina ya jeep katika kazi ya wilaya tulipotembelea makusanyiko.
Nakumbuka vizuri kusanyiko moja. Kipindi cha jioni cha siku ya mwisho kilipokuwa kikiendelea, kiongozi wa chama cha kisiasa katika eneo hilo alikuja nyuma ya jukwaa. Alikuwa mlevi na aliropoka matusi, na kusisitiza tumruhusu apande jukwaani na kuwaambia wote kwamba ni lazima wanunue kadi za chama. Tulipokataa, alikasirika sana na kututukana kwa sauti akisema kwamba Mashahidi wa Yehova wanaipinga serikali na wanapaswa kufungwa gerezani. Ndugu walifaulu kumsihi aondoke. Aliondoka, akisema kwa sauti ya juu kwamba angewaambia wenye mamlaka, kisha angerudi na kuteketeza gari letu na nyumba ya nyasi tulimokuwa tukiishi. Tulijua kwamba huo haukuwa mzaha.
Ndugu walitusaidia sana. Badala ya kukimbia kwa woga, walituzunguka na kututia moyo tumtumaini Yehova na kuacha mambo mikononi mwake. Kisha walilinda kwa zamu nyumba yetu ya nyasi na gari letu usiku kucha. Tuliguswa moyo sana na jambo hilo. Mbali na kuwa tayari kufa ili kutulinda, ndugu walikuwa tayari kuvumilia ukatili wowote ambao huenda wangetendewa baada ya sisi kuondoka kwa sababu ya kukataa kuunga mkono chama hicho cha kisiasa. Hatujawahi kusahau jinsi ndugu walivyoonyesha upendo wa Kikristo wa kujidhabihu. Na hatujasahau mambo mengine mengi yenye kugusa moyo tuliyofanyiwa kwa upendo miaka yote tuliyoishi Kongo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 211-213]
Mahojiano na Terence Latham
Alizaliwa: 1945
Alibatizwa: 1964
Maisha yake: Alikuwa mishonari kwa miaka 12. Alijifunza Kifaransa, Kilingala, na Kiswahili. Hivi sasa anatumikia nchini Hispania pamoja na mke na watoto wake wawili.
Niliwasili Kisangani kwa ndege mwaka wa 1969, pamoja na Raymond Knowles. Wakati huo, jiji hilo lilikuwa na wakazi wapatao 230,000 na lilikuwa jiji kuu la jimbo la kaskazini-mashariki la Kongo.
Tulikaribishwa kwa uchangamfu sana na wahubiri wachache na watu wengi wenye kupendezwa katika eneo hilo! Walitupatia zawadi nyingi sana kama vile, mapapai, mananasi, ndizi pamoja na matunda mengine ambayo hatukuwa tumewahi kuyaona. Wengine walileta kuku na kobe walio hai. Samuel Tshikaka alitukaribisha kwa fadhili nyumbani kwake. Lakini baada ya muda tulikodi nyumba. Nicholas na Mary Fone na vilevile Paul na Marilyn Evans walijiunga nasi. Tulikuwa na furaha iliyoje! Tulisaidiana kurekebisha na kupaka rangi makao ya kwanza ya mishonari huko Kisangani. Nyumba hiyo ilifunikwa na mimea inayotambaa na nyasi ndefu, na tuliwaondoa fungo wawili darini tulipokuwa tukifanya usafi. Baadaye, Peter na Ann Barnes walijiunga nasi katika makao hayo, pamoja na Ann Harkness, ambaye nilikuwa nimemwoa.
Katika miaka minne ya kwanza tuliyohubiri Kisangani, tulijifunza Kilingala na Kiswahili na tukaja kuwapenda wakazi wakarimu na wenye urafiki wa jiji hilo. Tulikuwa na mafunzo mengi sana hivi kwamba tulianza kuhubiri mapema asubuhi hadi jioni sana ili kujifunza na wote. Miaka tuliyoishi Kisangani, tuliona kikundi cha wahubiri wasiozidi kumi kikiongezeka na kuwa makutaniko manane.
Siku moja tulipokuwa tukiendesha gari kwenye barabara ya Ituri, tuliona kijiji cha Mbilikimo. Tulikuwa na hamu ya kuwahubiria wanakijiji hao. Wasomi fulani wanasema kwamba Mbilikimo huuita msitu baba au mama yao kwa sababu ndimo wanamopata chakula, mavazi, na makao. Kwa hiyo, Mbilikimo huuona msitu kuwa mtakatifu na wanaamini kwamba wanaweza kuwasiliana nao kupitia sherehe inayoitwa molimo. Wakati wa sherehe hiyo, wao hucheza dansi na kuimba huku wakizunguka moto. Wakati wa dansi, tarumbeta ya molimo hupulizwa. Wanaume hupuliza tarumbeta hiyo, iliyotengenezwa kwa mti, na kutokeza muziki na milio ya wanyama.
Tulivutiwa sana na kambi maridadi ya watu hao wanaohama-hama ambao kwa kawaida huishi mahali fulani kwa mwezi mmoja hivi. Kambi hiyo ilikuwa na nyumba zenye umbo la mzinga zilizotengenezwa kwa miti michanga na majani mabichi. Nyumba hizo zilikuwa na mlango mmoja tu na zilijengwa kwa muda wa saa mbili au muda mfupi zaidi. Watu kadhaa wangeweza kujikunja na kulala ndani ya nyumba moja. Watoto walitukaribia na kugusa nywele na ngozi yetu; ilikuwa mara yao ya kwanza kuwaona wazungu. Tulikuwa na pendeleo kubwa sana la kukutana na kuwahubiria watu hao wenye urafiki wa msituni! Walituambia kwamba wamewahi kutembelewa na Mashahidi kutoka vijiji vilivyo karibu na kambi zao.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 215, 216]
Mahojiano na David Nawej
Alizaliwa: 1955
Alibatizwa: 1974
Maisha yake: Yeye ndiye Mkongomani ambaye ametumikia kwa muda mrefu zaidi katika Betheli ya Kongo. Yeye pia ni mshiriki wa Halmashauri ya Tawi.
Nilishangaa sana nilipopokea barua ya kunialika Betheli mnamo mwaka wa 1976. Katika barua hiyo, mstari ulitiwa chini ya neno “muhimu” na “haraka.” Niliishi Kolwezi, umbali wa kilometa 2,450 kutoka Kinshasa. Haikuwa rahisi kuondoka nyumbani, lakini nilitaka kumwiga Isaya aliyesema: “Mimi hapa! Nitume mimi.”—Isa. 6:8.
Nilipofika Betheli, akina ndugu walinionyesha taipureta na kuniuliza kama ninajua kuitumia. Niliwaambia kwamba mimi ni mshonaji wa nguo kwa hiyo ninajua kutumia cherehani wala si taipureta. Lakini nilijitahidi sana na nikajifunza kuitumia. Wakati huo nilikuwa nikifanya kazi katika Idara ya Kutafsiri na Idara ya Utumishi.
Baadaye nilifanya kazi katika ofisi ya Barua. Miongoni mwa kazi nilizokuwa nikifanya ilikuwa kushughulikia maombi ya vichapo ambayo watu walituma kwenye ofisi. Kwa kawaida waliomba vichapo vingine. Mara nyingi sikujua jinsi watu walivyoitikia baada ya kupokea vichapo hivyo. Lakini ninajua kisa cha vijana wawili ambao walifanya maendeleo ya haraka. Baadaye wakawa mapainia wa kawaida, kisha mapainia wa pekee. Walipoitwa Betheli, niliishi na mmoja wao.
Nyakati nyingine watu walituma barua za kuomba pesa Betheli. Barua maalumu iliandikwa kuwaeleza kwamba kazi yetu ni ya kujitolea na iliwahimiza wajifunze Biblia. Wakati mmoja, ndugu mmoja aliniambia kwamba alijifunza kweli baada ya kupokea barua kama hiyo. Alinionyesha barua hiyo. Miaka kadhaa mapema alituma barua Betheli akiomba pesa. Alifanya kama alivyohimizwa na sasa yuko katika kweli.
Baadaye nilishughulikia mambo ya kisheria. Siku moja niliwasaidia ndugu kadhaa ambao walishtakiwa kwa sababu ya kutovaa alama ya chama. Nilijipa ujasiri na nikawaambia wenye mamlaka hivi: “Alama hiyo inamaanisha nini? Tumemaliza tu vita vya wenyewe kwa wenyewe, na watu wote mliopigana nao walivaa alama hizo. Alama hiyo haina maana yoyote; haionyeshi maoni ya mtu. Jambo muhimu ni jinsi mtu alivyo moyoni. Mashahidi wa Yehova ni raia ambao hawawezi kamwe kuanzisha vita nchini. Kutii sheria ni muhimu zaidi kuliko kuvaa alama ya chama.” Ndugu hao waliachiliwa huru. Yehova alitusaidia daima katika hali kama hizo.
Nimekuwa nikitumikia Betheli kwa zaidi ya miaka 27. Ingawa nina matatizo ya kiafya na sina elimu nyingi ya kilimwengu, mimi huendelea kujitahidi ili Yehova aweze kunitumia. Bado Betheli ina kazi muhimu na ya haraka!
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 219, 220]
Mahojiano na Godfrey Bint
Alizaliwa: 1945
Alibatizwa: 1956
Maisha yake: Mhitimu wa darasa la 47 la Gileadi. Alitumikia nchini Kongo kwa miaka 17. Hivi sasa yeye ni mshiriki wa Halmashauri ya Tawi nchini Rwanda. Anajua Kifaransa, Kiingereza, Kilingala, Kiswahili, na Kitshiluba.
Mnamo mwaka wa 1973, nilikuwa nikihubiri na ndugu mmoja huko Kananga. Wenye mamlaka walitupata tukiongoza funzo la Biblia katika nyumba moja, wakatukamata. Tulikaa gerezani kwa majuma mawili. Wakati huo, mishonari mwenzangu, Mike Gates, alituletea chakula kwa sababu hakukuwa na chakula gerezani. Hatimaye tuliachiliwa. Miezi mitatu baadaye, siku ambayo mimi na Mike tulikuwa tumepanga kusafiri kwa ndege kwenda kuhudhuria kusanyiko la kimataifa nchini Uingereza, tulipata habari kwamba ndugu wote wa kutaniko la karibu walikuwa wamekamatwa. Tulitaka kuwatembelea na kuwapa chakula. Tuliuliza kama tunaweza kuwaona ndugu hao, lakini tulishangaa hakimu mmoja alipoamuru tukamatwe. Tulipokuwa tukingoja kupelekwa gerezani kwa basi la gereza, tulisikia ndege yetu ikipaa. Wazia jinsi tulivyohuzunika tuliposikia sauti ya ndege hiyo!
Tulipofika gerezani, niligundua kwamba wafungwa wengi niliokuwa nao miezi mitatu awali bado walikuwa gerezani. Mishonari mwenzangu ambaye alikuwa akiniletea chakula wakati huo, alikuwa gerezani pia, hivyo wafungwa waliuliza: “Ni nani atakayewaletea chakula?”
Tuliwaambia kwamba ndugu zetu watatuletea chakula, lakini wafungwa hao walitikisa vichwa vyao na hawakuamini. Walijua kwamba hakukuwa na Mashahidi wengine Wazungu katika sehemu hiyo. Walistaajabu sana siku iliyofuata ndugu zetu Wakongomani walipoleta chakula kingi sana hivi kwamba tuliwagawia wafungwa hao! Jambo hilo lilitoa ushahidi mzuri sana kuhusu undugu wetu wa kimataifa na upendo ambao unatuunganisha. Ndugu hao wapendwa walituletea chakula ijapokuwa walikabili hatari ya kutiwa gerezani kwa sababu ya kufanya hivyo. Baada ya siku tano, tuliachiliwa huru. Tulisafiri hadi Uingereza, tukafika kwa wakati kwa ajili ya kusanyiko.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 224-226]
Mahojiano na Nzey Katasi Pandi
Alizaliwa: 1945
Alibatizwa: 1971
Maisha yake: Alihubiri bila woga kwenye maeneo magumu akiwa mseja na baadaye aliandamana na mumewe katika kazi ya kusafiri kuanzia mwaka wa 1988 hadi 1996. Kwa sasa wako katika utumishi wa pekee wa wakati wote huko Kinshasa.
Mnamo mwaka wa 1970, nilikuwa nikisoma Biblia yangu niliposikia mlango wa nyumba yangu huko Kinshasa ukibishwa. Mwanamume mmoja alinitembelea akiwa na mvulana wake mdogo. Mvulana huyo alianza kuongea kuhusu Biblia, akaniomba nifungue andiko la Mathayo 24:14 katika Biblia yangu. Nilijiona kuwa mtu wa kidini sana, lakini nilishindwa kupata andiko hilo. Alinisaidia kulipata, kisha tukawa na mazungumzo mazuri sana.
Ndugu huyo aliona kwamba ninapendezwa, akanialika kwenye mkutano Jumapili iliyofuata. Mkutano huo ulifanyiwa nyuma ya nyumba ya ndugu mmoja kwa kuwa kazi ya Kuhubiri ilikuwa imepigwa marufuku. Nilifurahia hotuba na Funzo la Mnara wa Mlinzi. Jioni hiyo ndugu walikuja nyumbani kwangu na kuanza kujifunza nami.
Baada ya muda, nilibatizwa na kuanza utumishi wa wakati wote. Huduma Yetu ya Ufalme ilieleza kwamba sehemu nyingine za nchi zilikuwa na uhitaji mkubwa. Niliuliza kama ningeweza kwenda Kenge, katika Jimbo la Bandundu. Ndugu walikubali lakini walinionya kwamba baadhi ya ndugu katika sehemu hiyo walikuwa wamekamatwa. Nilijiambia, ‘Hawawezi kumkamata kila mtu.’ Kwa hiyo niliamua kwenda.
Niliwasili jioni na nilifurahi kusikia kwamba mwangalizi wa mzunguko, François Danda, alikuwa akitembelea kutaniko la huko. Asubuhi iliyofuata nilihudhuria mkutano wa utumishi wa shambani, lakini nilishangaa kusikia kwamba François na ndugu wengine kadhaa walikuwa wamekamatwa. Afisa mkuu wa usalama alitaka kuzungumza nami. Alisema hivi: “Tunajua kwamba wewe ni Shahidi wa Yehova. Unaweza kuishi Kenge ukitaka, lakini siku tutakayokuona ukitembea-tembea na mkoba wako, tutakukamata.”
Wakazi wa mjini walikasirishwa sana na afisa mkuu wa usalama na maafisa wenzake. Walijua kwamba Mashahidi wa Yehova hawakuwa wakimdhuru mtu yeyote. Wakazi hao walisema kwamba kulikuwa na wahalifu wengi sana, kwa hiyo maafisa wa usalama wanapaswa kupambana na uhalifu badala ya kupoteza wakati wao wakiwatafuta Mashahidi wa Yehova. Hatimaye, akina ndugu waliachiliwa.
Niliwekwa kuwa painia wa pekee mwaka wa 1975 na nilitembelea miji na vijiji vingi. Nilikaa katika kila mji au kijiji kwa majuma mawili au matatu. Muda si muda, vikundi sita vya watu wanaopendezwa vilianzishwa. Niliandikia ofisi ya tawi, nikiomba ndugu watumwe huko ili kuchunga na kutunza vikundi hivyo.
Nilikutana na Jean-Baptiste Pandi, ambaye alikuwa pia painia wa pekee. Zamani nilikuwa nimezungumza na mishonari kuhusu ndoa na utumishi wa wakati wote. Waliniambia kwamba ingekuwa rahisi kwangu kuendelea na utumishi wa wakati wote kwa muda mrefu bila watoto. Jean-Baptiste alikubali, na tukafunga ndoa. Watu huamini kwamba watoto watawatunza wanapozeeka. Lakini mambo yamebadilika, ninajua wazazi wengi ambao wamekata tamaa kabisa. Mimi na Jean-Baptiste hatujakata tamaa hata kidogo.
Katika miaka iliyopita, tumewaona watu wengi wakija kwenye kweli. Ninafurahishwa hasa na familia yetu. Niliwasaidia baba na mama na vilevile ndugu zangu wanne na dada mmoja kukubali kweli.
Zaburi 68:11 yasema: “Wanawake wanaotangaza habari njema ni jeshi kubwa.” Hiyo inamaanisha kwamba sisi dada tuna kazi kubwa sana na lazima tufanye yote tuwezayo. Ninamshukuru sana Yehova kwa sababu ameniruhusu kushiriki katika kazi hiyo.
[Sanduku katika ukurasa wa 240]
Kutafsiri Chakula cha Kiroho
Ingawa Kifaransa ndiyo lugha rasmi ya Kongo, Kilingala ndiyo lugha inayotumiwa sana Kinshasa na kwenye maeneo yaliyo karibu na Mto Kongo. Ingawa lugha ya Kilingala haina misamiati mikubwa, ina maneno fulani yenye maana sana. Kwa mfano, tafsiri ya neno “kutubu” ni kobongola motema, usemi huo unamaanisha kihalisi “kuupindua moyo.” Usemi mwingine unaohusiana na moyo na hisia ni kokitisa motema, ambao kihalisi unamaanisha “kuuweka moyo chini” au, kwa njia nyingine, “kutulia.”
Gazeti la Mnara wa Mlinzi limetafsiriwa katika Kilingala kwa miaka mingi. Hivi sasa vichapo vinatafsiriwa katika lugha zifuatazo zinazozungumzwa nchini Kongo: Kilingala, Kilingombe, Kilomongo, Kikiluba, Kimashi, Kimonokutuba, Kinande, Kingbaka, Kiotetela, Kipende, Kisonge, Kiswahili (cha Kongo), Kitshiluba, Kituba, na Kiuruundi.
[Sanduku katika ukurasa wa 247]
Mwenye Bidii Licha ya Ulemavu
Richard, mwenye umri wa miaka 20, amepooza na amekuwa kitandani kwa miaka 15. Anaweza tu kusogeza kichwa chake. Hata hivyo, mnamo Januari 1997 aliwekwa kuwa mhubiri asiyebatizwa. Kwa kawaida, Richard huwahubiria watu wanaokuja kumtembelea. Yeye huongea kwa usadikisho kabisa. Kwa wastani, yeye huhubiri saa kumi kila mwezi. Katika Aprili 12, 1998, alibebwa kwa machela yake na kubatizwa kwenye kijito kilicho karibu na nyumbani kwao. Sasa anaweza kuhudhuria mikutano kwa ukawaida. Anamfundisha kweli mtu mmoja wa ukoo ambaye anahudhuria mikutano ya Kikristo, na anafanya maendeleo mazuri. Ingawa ndugu huyu amedhoofika kimwili, ametiwa nguvu na roho ya Mungu.
[Sanduku katika ukurasa wa 248]
“Si Sehemu ya Ulimwengu”
Siku moja akiwa shuleni, Esther mwenye umri wa miaka 12, alishangaa wakati mwalimu alipomwambia kila mwanafunzi asimame mbele ya wanafunzi wengine na kuimba wimbo wa taifa. Zamu yake ilipofika, Esther alimwambia mwalimu kwa upole kwamba hangeweza kuimba. Esther anasimulia kilichotukia:
“Mwalimu alikasirika. Nilimuuliza kama angeniruhusu kuimba wimbo mwingine. Akakubali. Niliimba wimbo, ‘Si Sehemu ya Ulimwengu.’ Kisha mwalimu akawaambia wanafunzi wote wapige makofi, na wote wakafanya hivyo.
“Baada ya masomo, mwalimu aliniita kando na kuniambia kwamba aliupenda sana wimbo huo, hasa maneno yake. Akaongezea hivi: ‘Naona kwamba ninyi Mashahidi wa Yehova mmejitenga kabisa na ulimwengu. Mwenendo wako darasani unaonyesha hivyo pia.’
“Mmoja wa wanafunzi wenzangu alivutiwa pia. Alianza kuniuliza maswali, nami nikayajibu. Mwishoni mwa mwaka, tulilazimika kuachana, lakini nilimtia moyo awatafute Mashahidi wa Yehova katika eneo ambalo angehamia. Alifanya hivyo, na sasa yeye ni dada.”
[Sanduku katika ukurasa wa 251]
Unyofu Humletea Mungu Heshima
Ndugu mmoja alifanya kazi katika kiwanda kimoja. Siku moja mashine iliharibika kwa sababu ya kosa lililofanywa na wafanyakazi wa zamu ya kikundi cha ndugu huyo. Mkurugenzi aliamua kuwafukuza wafanyakazi wote. Aliwalipa mshahara na kuwafuta kazi. Ndugu huyo alipofika nyumbani, aligundua kwamba alikuwa amepewa faranga 500 zaidi (zaidi ya dola moja ya Marekani), kwa hiyo alirudi kiwandani ili kurudisha pesa hizo. Alitumia nafasi hiyo kutoa ushahidi, na mkurugenzi akavutiwa sana na unyofu wa ndugu huyo hivi kwamba alimwambia abaki na kuendelea na kazi yake.
[Chati/Grafu katika ukurasa wa 176, 177]
MFUATANO WA MATUKIO NCHINI KONGO (KINSHASA)
1932: Jitihada zafanywa ili kuwatuma Mashahidi wa Yehova nchini Kongo.
1940
1949: Sheria yatungwa kuthibitisha kwamba Mashahidi wa Yehova wamepigwa marufuku.
1960
1960: Kongo yapata uhuru, na uhuru wa ibada wa kadiri fulani waruhusiwa kwa muda.
1962: Ofisi ya tawi yafunguliwa huko Léopoldville (sasa ni Kinshasa). Mishonari wa kwanza wawasili.
1966: Mashahidi wa Yehova waandikishwa kisheria.
1971: Kuandikisha kisheria kwafutiliwa mbali.
1980
1980: Kazi yaandikishwa tena kisheria.
1986: Mashahidi wa Yehova wapigwa marufuku.
1990: Uhuru wa ibada waruhusiwa isivyo rasmi.
1993: Mahakama Kuu yafutilia mbali marufuku ya mwaka wa 1986. Ujenzi wa ofisi mpya ya tawi waanza.
2000
2003: Wahubiri watendaji wafikia 122,857 nchini Kongo (Kinshasa).
[Grafu]
(See publication)
Jumla ya Wahubiri
Jumla ya Mapainia
120,000
80,000
40,000
1940 1960 1980 2000
[Ramani katika ukurasa wa 169]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
SUDAN
JAMHURI YA AFRIKA YA KATI
JAMHURI YA KONGO
BRAZZAVILLE
JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO
Isiro
Bumba
Mto Kongo
Kisangani
Goma
Bukavu
Bandundu
KINSHASA
KASAI
Kenge
Kikwit
Matadi
Kananga
Mbuji-Mayi
KATANGA
Kamina
Luena
Kolwezi
Likasi
Lubumbashi
ANGOLA
ZAMBIA
[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 162]
[Picha katika ukurasa wa 185]
Hélène, Ernest, na Danielle Heuse jijini Kinshasa katika miaka ya 1960
[Picha katika ukurasa wa 186]
Wakongomani wengi walifurahi kuwaona watu wakibatizwa kwenye makusanyiko ya kimataifa yaliyoonyeshwa katika sinema “Furaha ya Jamii ya Ulimwengu Mpya”
[Picha katika ukurasa wa 199]
Madeleine na Julian Kissel
[Picha katika ukurasa wa 205]
Majumba sahili ya mikutano yalijengwa kotekote nchini
[Picha katika ukurasa wa 207]
Ofisi ya tawi ya Kinshasa, 1965
[Picha katika ukurasa wa 208]
Kusanyiko huko Kolwezi, 1967
[Picha katika ukurasa wa 209]
Haikuwa rahisi kusafiri kwa sababu ya barabara mbovu
[Picha katika ukurasa wa 221]
Kusanyiko la Wilaya la “Upendo wa Kimungu” huko Kinshasa, mwaka wa 1980, lilikuwa kusanyiko kubwa la kwanza kufanywa huko baada ya miaka minane
[Picha katika ukurasa wa 223]
Wengi hutembea kwa siku nyingi wakiwa wamebeba vyakula na mizigo mingine ili kuhudhuria makusanyiko
[Picha katika ukurasa wa 228]
Mnamo Desemba 1985, miezi mitatu tu kabla ya marufuku kali kutangazwa, Kusanyiko la “Washika-Ukamilifu” lafanywa Kinshasa
[Picha katika ukurasa wa 230]
Wakati wa marufuku, ndugu zetu walifungwa gerezani na kupigwa kikatili
[Picha katika ukurasa wa 235]
Zekaria Belemo atembelea kikundi cha ndugu wakimbizi kutoka Sudan akiwa mwangalizi anayesafiri
[Picha katika ukurasa wa 237]
Magari yenye nguvu hutumiwa kusafirisha vichapo kwenye barabara mbovu
[Picha katika ukurasa wa 238]
Darasa la kwanza la Shule ya Mazoezi ya Kihuduma nchini Kongo (Kinshasa), 1995
[Picha katika ukurasa wa 241]
Gisela na Sébastien Johnson
[Picha katika ukurasa wa 243]
Mishonari 12 wanaishi katika makao haya jijini Kinshasa
[Picha katika ukurasa wa 244, 245]
Misaada iliwasili kutoka Ulaya na kugawiwa wenye uhitaji mwaka wa 1998
[Picha katika ukurasa wa 246]
Waangalizi wanaosafiri, kama vile Ilunga Kanama (chini kushoto) na Mazela Mitelezi (picha ndogo, kushoto), hukabili magumu mengi katika maeneo yenye vita
[Picha katika ukurasa wa 252, 253]
(1) Majengo ya Betheli ya Kinshasa
(2-4) Majumba mapya ya Ufalme
(5) Ndugu asaidia katika ujenzi wa Jumba la Ufalme
[Picha katika ukurasa wa 254]
Halmashauri ya Tawi, kuanzia kushoto hadi kulia: Peter Wilhjelm, Benjamin Bandiwila, Christian Belotti, David Nawej, Delphin Kavusa, Robert Elongo, Sébastien Johnson, na Uno Nilsson