Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • yb05 kur. 66-133
  • Tahiti

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tahiti
  • 2005 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Vichwa vidogo
  • Wazungu Wafika
  • Ujumbe wa Ufalme Wafika
  • Habari Njema Zahubiriwa Tahiti
  • Dada Mtahiti Arudi Nchi ya Kwao
  • Wakati wa Kuimarisha
  • Jumba la Ufalme la Kwanza
  • Mambo ya Kisheria Yashughulikiwa
  • Biblia ya Kitahiti Ni Baraka
  • Wachina Wapata Kumjua Yehova
  • Maisha Yaliyobadilika Baharini
  • Familia Zatumikia Mahali Penye Uhitaji Mkubwa
  • Watoto wa Kiroho Wapata Majaribu
  • Habari Njema Yahubiriwa na Kukubaliwa Kisiwani Huahine
  • Familia Kutoka Ufaransa Zaja Kusaidia
  • Ofisi ya Tawi Yafunguliwa
  • Kuhubiri Kwenye Visiwa vya Tuamotu na vya Gambier
  • Wamishonari Wafika Visiwani
  • ‘Ilitubidi Kujua Maandiko Tulipohubiri’
  • “Yehova Atakuzoeza”
  • Wamishonari Waseja Watumwa Kwenye Maeneo Magumu
  • Wamishonari wa Mwisho Wafika
  • Kweli ya Biblia Yahubiriwa Gerezani
  • Makusanyiko ya Kimataifa Huko Tahiti
  • Kutafsiri Katika Kitahiti
  • Mradi wa Ujenzi Waanzishwa
  • Mabadiliko Kwenye Ofisi ya Tawi na Mazoezi Zaidi
  • Magumu ya Jamii Inayobadilika Haraka
2005 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
yb05 kur. 66-133

Tahiti

Ukiwa juu angani, visiwa vya Polinesia ya Ufaransa, kama vile Tahiti, Mooréa, na Bora Bora, huonekana kama vito vya thamani katika Bahari kubwa ya Pasifiki yenye rangi ya bluu. Vidimbwi vyenye kung’aa, vilivyopambwa kwa matumbawe na kujaa samaki maridadi, vinapakana na fuo zenye rangi ya dhahabu au nyeusi. Minazi iliyojaa nazi hupepea katika upepo. Maeneo ya katikati ya nchi kavu yana milima iliyojaa mimea na vilele vyake kufunikwa na mawingu. Mazingira hayo ni yenye kuvutia sana.

Wasanii na waandishi walikuwa na sababu nzuri ya kuvifafanua visiwa hivyo kama paradiso duniani. Na bila shaka vilionekana kama paradiso kwa mabaharia wa kale ambao walikuwa wa kwanza kuviona na kuhamia huko, labda miaka elfu moja au zaidi iliyopita. Watu hao hodari, ambao huenda walitoka Asia ya Kusini-Mashariki, ni baadhi ya mababu wa Wapolinesia. Kwa karne nyingi walisambaa kutoka kwenye visiwa walikokaa na kusafiri kwa mashua hadi visiwa vya mbali katika Bahari ya Pasifiki na kuvimiliki visiwa vingi humo.

Eneo ambalo leo linaitwa Polinesia, jina linalomaanisha “Visiwa Vingi,” ni kubwa sana. Kisiwa cha Hawaii kiko upande wa kaskazini kabisa, Kisiwa cha Easter upande wa kusini-mashariki, na New Zealand upande wa kusini-magharibi. Masimulizi haya yanahusu sehemu moja ya Polinesia, yaani, Polinesia ya Ufaransa. Tahiti ndicho kisiwa kikuu katika sehemu hiyo.a Katika eneo la Polinesia ya Ufaransa kuna makundi matano ya visiwa, yaani, Visiwa vya Tubuaï (Austral), Visiwa vya Gambier, Visiwa vya Marquesas, Visiwa vya Society na Visiwa vya Tuamotu. Wavumbuzi kutoka Ulaya waligundua visiwa hivyo vya Pasifiki bila kutarajia katika miaka ya 1500.

Wazungu Wafika

Mhispania anayeitwa Álvaro de Mendaña de Neira aligundua baadhi ya Visiwa vya Marquesas mwaka wa 1595. Pedro Fernandes de Queirós, aliyekuwa msaidizi wa Mendaña de Neira, aligundua visiwa kadhaa vya Visiwa vya Tuamotu mwaka wa 1606. Mvumbuzi Mholanzi anayeitwa Jacob Roggeveen aligundua kisiwa cha Bora Bora, Makatéa, na Maupiti mwaka wa 1722. Nahodha Samuel Wallis, aliyesafiri kwa meli ya vita ya Uingereza inayoitwa Dolphin, alifika Tahiti mwaka wa 1767. Tahiti ndicho kisiwa kikubwa zaidi cha Polinesia ya Ufaransa. Mwaka uliofuata nahodha Mfaransa Louis-Antoine de Bougainville pia alifika Tahiti.

Kitabu kimoja kuwahusu wavumbuzi wawili (Cook & Omai—The Cult of the South Seas) kinasema kwamba Bougainville alivutiwa na uzuri wa kisiwa cha Tahiti na kushangazwa sana na wenyeji waliopenda mahaba, hivi kwamba alikiita “Nouvelle Cythère. Jina hilo lilitokana na jina la Kisiwa cha Kithira huko Peloponnesia, ambako inasemekana Afrodito [mungu wa kike wa mapenzi na urembo] alitokea baharini.” Mvumbuzi Mwingereza James Cook alitembelea Tahiti mara nne, kati ya mwaka wa 1769 na 1777. Aliviita visiwa vinavyotia ndani Tahiti, Visiwa vya Society.

Wamishonari walifika kwenye visiwa hivyo baada ya wavumbuzi hao. Wale waliotumwa na Shirika la Umishonari la London linalotegemezwa na Waprotestanti ndio waliokuwa na matokeo mazuri zaidi. Wamishonari wawili waliotumwa na shirika hilo, Henry Nott na John Davies, walitimiza kazi kubwa ya kuitia lugha ya Kitahiti katika maandishi, kisha wakatafsiri Biblia nzima katika lugha hiyo. Biblia hiyo ya Kitahiti bado inatumiwa sana katika Visiwa vya Polinesia ya Ufaransa, hasa katika visiwa ambako Kanisa la Kiprotestanti lina wafuasi wengi. Wamishonari wa Kanisa la Wasabato, Kanisa Katoliki, na Kanisa la Wamormoni pia walifanikiwa kwa kadiri fulani. Kwa mfano, Kanisa Katoliki lina wafuasi wengi kwenye Visiwa vya Marquesas, Gambier, na Tuamotu mashariki.

Ufaransa ilipataje kuvitawala visiwa hivyo? Kuanzia mwaka wa 1880, Ufaransa ilivitwaa visiwa hivyo hatua kwa hatua na kuanzisha koloni jipya. Mji wa Papeete, kisiwani Tahiti, ulichaguliwa kuwa mji mkuu, na watu wa eneo hilo wakawa raia wa Ufaransa. Katika mwaka wa 1946 visiwa hivyo vikawa eneo la ng’ambo la Ufaransa na mwaka wa 1957 vikapewa jina Polinesia ya Ufaransa.

Ujumbe wa Ufalme Wafika

Sydney Shepherd ndiye Shahidi wa kwanza kwenda kuhubiri Tahiti, naye alifika mwaka wa 1931. Kwa muda wa miaka miwili, Sydney alikuwa akisafiri kwa mashua hadi visiwa kadhaa vya Pasifiki ili kuwahubiria watu. Frank Dewar kutoka New Zealand alikuja baada yake. Ijapokuwa ndugu hao hawakuweza kukaa kwa muda mrefu, waliwaachia watu vitabu vingi. Miaka 20 hivi baadaye, mwangalizi wa mzunguko, Mwaustralia Leonard (Len) Helberg, alisema hivi: “Nilikuwa nikisafiri kwenye eneo la Papeete pamoja na msimamizi wa kutaniko, halafu akasimamisha gari lake ili ambebe mzee fulani Mmarekani aliyemfahamu. Mzee huyo alipoambiwa kwamba mimi ni Shahidi, alisema hivi: ‘Ehee, nakumbuka kwamba mmoja wenu alipitia hapa miaka mingi iliyopita na kunipa rundo la vitabu vya Hakimu Rutherford.’ Jambo hilo ni uthibitisho mmoja wa kazi iliyofanywa na mapainia waliotutangulia. Yule painia aliyemwachia mzee huyo vitabu ni Sydney Shepherd au Frank Dewar.”

Kati ya wahubiri wa kwanza wa Ufalme kutoa ushahidi kikamili huko Polinesia ya Ufaransa ni Jean-Marie na Jeanne Félix, mume na mke waliojifunza kweli huko Algeria, ambayo wakati huo ilikuwa koloni la Ufaransa. Walibatizwa mwaka wa 1953. Mwaka wa 1955, wahubiri wa Ufalme walitiwa moyo wahamie maeneo yaliyokuwa na uhitaji mkubwa wa wahubiri. Polinesia ya Ufaransa ilikuwa mojawapo ya maeneo hayo. Ndugu na Dada Félix na mwana wao mchanga, Jean-Marc, waliitikia mwito huo, nao wakahamia Tahiti mwaka wa 1956. Lakini, Jean-Marie, aliyekuwa injinia, hakuweza kupata kazi kisiwani Tahiti. Hivyo, wakahamia Makatéa, kimojawapo cha Visiwa vya Tuamotu vilivyo umbali wa kilometa 230 upande wa kaskazini-mashariki wa Tahiti, ambako Jean-Marie alipata kazi katika kampuni ya fosfati.

Mara moja, Ndugu na Dada Félix walianza kuwahubiria majirani na watu waliofanya kazi pamoja na Jean-Marie. Jeanne anaandika hivi: “Wenyeji wa kisiwa hicho waliiheshimu sana Biblia, wakasikiliza ujumbe wa Ufalme kwa makini, na kujifunza Biblia kwa bidii. Jambo hilo lilitutia moyo. Hata hivyo, makasisi wa eneo hilo walitupinga sana. Hata waliwaonya wafuasi wao wajihadhari na ‘manabii wa uwongo’ walio katikati yao, na wasiongee nasi au hata kupita karibu na nyumba yetu!”

Lakini baada ya muda, watu walio wengi walibadili maoni yao kuwahusu Wakristo hao. Wakaaji wengi wa visiwa hivyo hata walipata kuwaheshimu sana Jean-Marie na Jeanne kwa sababu hawakuwadharau Wapolinesia, kama Wazungu wengine kwenye kisiwa cha Makatéa.

Hata hivyo, walihitaji ujasiri ili waendelee na kazi ya kuhubiri, kwa sababu mkurugenzi wa ile kampuni ya fosfati alikuwa na uwezo wa kumfuta kazi mfanyakazi yeyote wakati wowote. Isitoshe, nyakati nyingine wale polisi wawili wa kisiwa hicho waliwatembelea Jean-Marie na Jeanne, na kuwahoji kuhusu kazi yao ya kuhubiri. Pole kwa pole, polisi hao Wafaransa walitambua kwamba Jean-Marie na Jeanne hawakuwa watu hatari. Hata wakawa wenye urafiki.

Mpolinesia Maui Piirai, aliyefanya kazi na Jean-Marie, ndiye mwanafunzi wa kwanza wa Biblia kufanya maendeleo ya kiroho. Kweli ilipoingia moyoni mwake, Maui alifanya mabadiliko makubwa maishani mwake. Kwa mfano, aliacha ulevi na kuvuta sigara, naye akamwoa mwanamke aliyekuwa ameishi naye kwa miaka 15. Maui aliyebatizwa Oktoba 1958, ndiye Mpolinesia wa kwanza katika eneo hilo kujiweka wakfu kwa Yehova. Yeye pia alianza kuhubiri habari njema, jambo ambalo liliwakasirisha makasisi. Kasisi mmoja hata alipanga njama ili Maui afutwe kazi. Lakini njama hiyo ilishindwa kwa sababu Maui alikuwa mfanyakazi mwenye bidii na mwenye sifa nzuri.

Mwanamke aitwaye Germaine Amaru ndiye mtu wa pili kisiwani Makatéa kukubali Neno la Mungu. Germaine alikuwa mkuu wa shule na alihubiriwa kwa mara ya kwanza na mmoja wa wanafunzi wake, Jean-Marc, mwana wa Ndugu na Dada Félix. Ingawa Jean-Marc alikuwa na umri wa miaka saba tu, mwalimu wake alivutiwa sana na ujuzi wake wa Biblia hivi kwamba aliwapigia wazazi wake simu. Wazazi hao wakaanza kumfundisha mwalimu huyo Biblia. Lakini mambo hayakuishia hapo kwa kuwa Germaine naye alimsaidia mwalimu mwenzake anayeitwa Monique Sage, na mumewe Roger, kumjua Yehova.

Ndugu na Dada Félix na Maui Piirai walianza pia kujifunza na Manuari Tefaatau, aliyekuwa shemasi kijana katika kanisa la Kiprotestanti la Makatéa, na vilevile pamoja na rafiki yake, anayeitwa Arai Terii. Mwanzoni, watu hao wawili waliendelea kwenda katika kanisa lao na kuwahubiria waamini wenzao kweli za Maandiko kuhusu Utatu, moto wa mateso, kutoweza kufa kwa nafsi, na mafundisho mengineyo. Jambo hilo lilisababisha mgogoro miongoni mwa wafuasi wa kanisa la Kiprotestanti. Hata hivyo, kama watu wa mji wa Beroya wa kale, wengi wenye mioyo minyoofu walichunguza Biblia zao ili kuona kama mambo waliyokuwa wakiyasikia yalikuwa ya kweli.—Mdo. 17:10-12.

Bila shaka kasisi wa kanisa hilo alikasirika. Hata alitisha kumfukuza kanisani mtu yeyote aliyeendelea kuwasikiliza Mashahidi. Baadhi yao waliacha kusikiliza kwa sababu ya woga, lakini wengine wakafanya maendeleo ya kiroho na kuliacha kanisa. Miongoni mwa wale walioacha kanisa ni Manuari na Arai, Moea, mke wa Maui Piirai, na Taina Rataro, anayetajwa baadaye katika masimulizi haya.

Mwanzoni, wahubiri na wanafunzi wa Biblia, ambao waliendelea kuongezeka, walifanya mikutano nyumbani kwa Ndugu na Dada Félix, ambako Jean-Marie alitoa hotuba katika Kifaransa na Maui akafasiri katika Kitahiti. Familia ya Félix ilipohama Makatéa mwaka wa 1959, mikutano ilifanywa nyumbani kwa Maui, ambaye wakati huo alikuwa amebatizwa. Jean-Marie na Jeanne walionaje utumishi wao katika visiwa hivyo? Jeanne, ambaye sasa ni mjane anayeishi nchini Italia, anatoa maoni yake mwenyewe na ya mumewe aliyekufa anaposema: “Hatukujuta hata kidogo. Huduma yetu katika kisiwa cha Makatéa ndilo jambo bora zaidi katika maisha yetu.”

Habari Njema Zahubiriwa Tahiti

Mwaka wa 1955, muda mfupi tu kabla ya Ndugu na Dada Félix kuhamia Makatéa, ofisi ya tawi ya Australia ilimweka Len Helberg kuwa mwangalizi wa mzunguko katika eneo la Pasifiki Kusini. Eneo la mzunguko wake lilikuwa lenye ukubwa wa mamilioni ya kilometa za mraba, kuanzia New Caledonia hadi Polinesia ya Ufaransa. Hata hivyo, eneo hilo kubwa lilikuwa na wahubiri wasiozidi 90, na hakukuwa na mhubiri yeyote kisiwani Tahiti. Len alikuwa na miradi mitatu hasa, yaani, kutembelea makutaniko yote na vikundi vyote kila baada ya miezi sita; kumtembelea kila mhubiri na yeyote mwenye kupendezwa aliyeishi mbali na kutaniko; na kuanzisha kazi ya kuhubiri kwenye maeneo mapya kwa kutumia ile sinema kuhusu jamii ya ulimwengu mpya (The New World Society in Action) ilipowezekana.

Len alifika Tahiti kwa mara ya kwanza mnamo Desemba 1956, naye akakaa kwa muda wa miezi miwili. Alikuwa amejifunza Kifaransa shuleni lakini alikuwa amekisahau. Kwa hiyo alianza kuhubiri katika eneo la biashara akitumaini kuwapata watu waliojua Kiingereza. Katika eneo hilo, alikutana na mmoja wa watu matajiri zaidi kisiwani Tahiti. Mtu huyo alisikiliza kwa makini sana na akamwalika Len arudi tena. Jumamosi iliyofuata, baada ya kula chakula cha mchana pamoja na Len, mtu huyo alimkaribisha nyumbani kwake, na akampeleka huko kwa gari lake. Len anaandika: “Halafu, wakati wa alasiri, nilishangaa kumwona mtu huyo akichukua gamba la konokono na kulipuliza. Niligundua kwamba hiyo ni ishara kwa waheshimiwa wote kijijini kukusanyika kwenye jumba la mkutano lililopakana na nyumba ya mtu huyo.

“Watu 12 hivi walifika, akiwemo meya, mkuu wa polisi, na mashemasi kadhaa wa kanisa la Kiprotestanti. Baada ya kunitambulisha kuwa mwakilishi wa Mashahidi wa Yehova, ‘dini mpya visiwani,’ yule mtu aliyenikaribisha alitangaza, ‘Sasa Bwana Helberg atajibu maswali yoyote ya Biblia mliyo nayo.’ Nilijibu maswali yote waliyouliza.” Walifanya vivyo hivyo kila Jumamosi kwa miezi miwili iliyofuata. Ingawa mtu huyo tajiri hakukubali kweli, alifanya mpango ili Len aonyeshe ile sinema kuhusu jamii ya ulimwengu mpya katika hospitali ya watu wenye ukoma. Zaidi ya watu 120 walihudhuria.

Je, kuna yeyote aliyekubali ujumbe wa Ufalme? Ndugu Helberg anasema hivi: “Nilipokuwa nikihubiri nyumba kwa nyumba katika wilaya ya Arue siku ya Krismasi mwaka wa 1956, nilitembelea familia ya Micheli, nao wakakubali ujumbe kwa furaha.” Familia ya Micheli ilifahamu gazeti la Mnara wa Mlinzi na la Amkeni! kwa sababu mtu wao wa ukoo aliyeishi Marekani alikuwa amepanga ili wapokee magazeti hayo kwa njia ya posta. Baadaye Irene binti ya Micheli pamoja na mumewe walikubali kweli. Len alifaulu pia kuanzisha funzo la Biblia pamoja na Bwana Garnier, jambo lililofanya watu wengine katika familia yake waikubali kweli. Kutaniko la Papeete lilipoanzishwa mwaka wa 1959, watu wa familia ya Micheli na ya Garnier walikuwa miongoni mwa ndugu wa kwanza wa kutaniko hilo.

Ndugu Helberg alipoenda Shule ya Gileadi mwaka wa 1957, mwangalizi wa mzunguko Paul Evans na mkewe, Frances, waliombwa na ofisi ya tawi ya Australia waende wakahubiri kisiwani Tahiti. Walikaa kisiwani humo kwa muda mfupi tu lakini waliwaachia watu Biblia na vitabu zaidi ya 70, na wengi wakaagiza gazeti la Mnara wa Mlinzi na la Amkeni! kwa njia ya posta. Ndugu Evans aliandika: “Sasa kuna watu kadhaa kisiwani Tahiti walio na ujuzi wa kutosha wa Biblia, nao wanapendezwa sana hivi kwamba wana hamu ya kuanza kuhubiri chini ya mwelekezo wa tengenezo.” Je, watu hao waliopendezwa wangepata msaada na mwongozo waliohitaji?

Dada Mtahiti Arudi Nchi ya Kwao

Agnès, mwanamke kijana kutoka Tahiti alihamia Marekani mwaka wa 1936 ili aolewe na Mmarekani Earl Schenck. Agnès na Earl walitembelewa na Mashahidi wa Yehova, wakakubali kweli, na kubatizwa huko San Diego, California, mwaka wa 1954. Mwaka wa 1957, wao na marafiki wao, Clyde na Ann Neill, waliketi pamoja kwenye kusanyiko la wilaya huko Los Angeles wakati Nathan Knorr kutoka makao makuu ya ulimwengu alipotaja maeneo kadhaa ambako kulikuwa na uhitaji mkubwa wa wahubiri. Tahiti ilikuwa mojawapo ya maeneo hayo.

Ndugu Neill anasema: “Mara moja Agnès aliinuka kwa msisimko na kulia. . . . Ndipo nikamwambia yeye na Earl kwamba nitafanya yote niwezayo kuwasaidia wao na mwanao mwenye umri wa miaka 11, kwenda Tahiti. Earl naye, ambaye aliyekuwa mlemavu, akaanza kulia. Alikuwa ameishi Pasifiki Kusini kwa miaka 17, akifanya kazi ya usanii na uandishi, na alikuwa na hamu ya kurudi. Isitoshe, mkewe Agnès bado alikuwa raia wa Ufaransa.”

Clyde anaongeza: “Baada ya kusali sana, mimi na Ann tuliamua kwenda Tahiti pamoja na wana wetu watatu, waliokuwa na umri wa miaka 12, 8, na 3. Marafiki wetu David na Lynne Carano na mwana wao, David, Jr., waliamua kujiunga nasi. Hivyo, baada ya kuhudhuria kusanyiko la kimataifa la mwaka wa 1958 huko New York City, tulisafiri kwa meli kwenda Tahiti.

“Ofisi ya tawi ya Marekani ilikuwa imetupatia majina ya watu fulani waliopendezwa, kwa hiyo mara tulipofika, tulianza kuwatembelea watu hao. Agnès, ambaye alikuwa amefika mbele yetu, tayari alikuwa akihubiri kwa bidii. Ilipowezekana, mimi na Ann tuliandamana na Agnès katika kazi ya kuhubiri kwa kuwa hatukujua Kifaransa wala Kitahiti. Tulipohubiri peke yetu, tulikuwa tukibeba nakala ya Kiingereza na ya Kifaransa ya kitabu, ‘Mungu na Awe wa Kweli,’ ambacho tulikitumia kuongoza mafunzo siku hizo.”

Kwa sababu ya jitihada hizo, pamoja na msingi uliokuwa umewekwa na Ndugu Helberg na Ndugu na Dada Evans, watu 17 walianza kujifunza Neno la Mungu baada ya majuma machache tu. Clyde anasema hivi: “Mwanafunzi mmoja ninayemkumbuka sana ni Teratua Vaitape, aliyekuwa kasisi wa kanisa la Kiprotestanti hapo awali. Alifutwa kazi kwa sababu aliuliza maswali mengi kuhusu mafundisho ya kanisa. Teratua aliishi pamoja na familia yake katika nyumba ndogo, ambayo haikuwa na maji wala umeme. Aliniambia kwamba amejifunza mambo mengi kuhusu Biblia katika majuma machache tu tuliyokuwa tumejifunza, kuliko yale aliyojifunza kwa miaka minne alipokuwa kwenye chuo cha dini na kwa miaka saba alipokuwa kasisi.”

Clyde anaongeza: “Baada ya kukaa kisiwani humo kwa majuma kadhaa, habari kutuhusu zilienea haraka. Hilo lilikuwa jambo zuri kwa sababu Watahiti ni wenye urafiki na wanaipenda Biblia.”

Mwanzoni, wahubiri hao wachache walifanya mikutano nyumbani kwa Schenck. Ni watu wawili tu wenye kupendezwa waliohudhuria. Ndugu Neill anasema: “Lakini muda si muda, watu 15 hivi wakajiunga nasi kwa ukawaida. Mwanamke mmoja tuliyemfundisha alikuwa amemsaidia Len Helberg wakati baiskeli yake ilipoharibikia karibu na nyumba ya mwanamke huyo miaka miwili au mitatu mapema. Len alikuwa amemwachia vitabu, na alifurahi sana kusikia kwamba tulikuwa wa dini hiyohiyo. Aliishi mbali nasi, kwa hiyo kila tulipomtembelea alitukaribisha kwa chakula cha mchana ambacho kwa kawaida kilikuwa samaki mtamu aliyechomwa kwenye pipa.”

Kabla ya familia ya Neill na ya Carano kuondoka mwezi wa Desemba 1958, Clyde alitoa hotuba ya ubatizo. Hiyo ilikuwa hotuba ya pili ya ubatizo kutolewa katika eneo la Polinesia ya Ufaransa, ile ya kwanza ilitolewa mwezi wa Oktoba kwenye kisiwa cha Makatéa, wakati Maui Piirai alipobatizwa. Watu 60 walihudhuria, na 8 wakabatizwa. Steven, mwana wa Ndugu na Dada Neill, na Auguste Temanaha, Mtahiti ambaye baadaye alisaidia kuanzisha kutaniko kisiwani Huahine, walikuwa miongoni mwa wale waliobatizwa.

Wakati wa Kuimarisha

John Hubler na mkewe Ellen kutoka Australia walihamia Tahiti mwaka wa 1959 baada ya ofisi ya tawi ya Fiji kuwaomba waende huko ili wasaidie Kutaniko jipya la Papeete. John alikuwa mtumishi wa kutaniko kwa ule muda wa miezi saba ambao yeye na Ellen walikaa Tahiti. John alijua Kifaransa vizuri kwa sababu alizaliwa nchini Uswisi. Ellen pia alijua lugha hiyo, kwa kuwa alikuwa ametumikia pamoja na mumewe kwa miaka kadhaa huko New Caledonia. Ndugu na Dada Hubler waliwazoeza wale wahubiri wapya kuhubiri nyumba kwa nyumba, kwa kuwa wengi wao hawakuwa wameanza kufanya hivyo.

John na Ellen walianza kazi ya mzunguko mwaka wa 1960. Mzunguko wao ulikuwa Polinesia ya Ufaransa, kwa hiyo waliendelea kuwasaidia wahubiri katika eneo hilo. John anasema hivi: “Katika mwaka wa 1961, nilialikwa kuhudhuria Shule ya Gileadi. Baada ya kuhitimu, niliwekwa kuwa mwangalizi wa mzunguko wa visiwa vyote vya Bahari ya Pasifiki ambako Kifaransa hutumiwa.”

Jumba la Ufalme la Kwanza

Ndugu Hubler anasema hivi: “Katika ziara yetu ya pili huko Tahiti, nilifurahia kuanzisha funzo la Biblia pamoja na Marcelle Anahoa, aliyekuwa mwalimu wa shule hapo zamani. Wakati huo, tulikuwa tukitafuta kiwanja kwa bidii ili tujenge Jumba la Ufalme. Lakini kulikuwa na vizuizi viwili. Kwanza, hakuna mtu aliyekuwa na kiwanja aliyetaka kuuza; pili, kutaniko halikuwa na pesa za kutosha. Hata hivyo, tuliendelea kutafuta, tukitumaini kwamba Yehova atatuongoza.

“Nilipokuwa nikijifunza pamoja na Marcelle, nilimtajia jambo hilo, naye akasema: ‘Ninataka kukuonyesha kitu fulani.’ Alinipeleka nje, kisha akanyoosha mkono na kusema: ‘Unaona kiwanja hiki? Ni changu. Nilikuwa na mpango wa kujenga nyumba za kukodisha, lakini kwa kuwa sasa ninajifunza kweli, nimeamua kuacha mradi huo. Nitachanga nusu ya kiwanja hiki kwa ajili ya Jumba la Ufalme.’ Niliposikia jambo hilo, mara moja nilisali kimoyo-moyo na kumshukuru Yehova.”

Mara baada ya mambo ya kisheria kushughulikiwa, ndugu katika Kutaniko la Papeete walianza kujenga Jumba lao la kwanza la Ufalme, nao wakalimaliza mwaka wa 1962. Jumba la Ufalme lilijengwa kama nyumba ya kawaida visiwani, yaani, bila kuta, nalo lilikuwa na paa lililoezekwa kwa makuti. Hata hivyo, kuku wa majirani walianza kutaga mayai na kuangulia kwenye viti na kulala kwenye boriti za paa. Basi ikawa kwamba ndugu walipofika mikutanoni, walikuta mayai na mavi ya kuku kwenye sakafu na juu ya viti. Lakini jumba hilo lilifaa hadi walipojenga jumba kubwa lenye kudumu.

Mambo ya Kisheria Yashughulikiwa

Katika siku za kwanzakwanza, Mashahidi wa Yehova hawakuwa na uhakika kuhusu hali yao ya kisheria kwenye visiwa vya Polinesia ya Ufaransa. Gazeti la Mnara wa Mlinzi lilikuwa limepigwa marufuku nchini Ufaransa tangu mwaka wa 1952, lakini kazi ya kuhubiri haikuwa imepigwa marufuku. Je, marufuku hiyo ilihusu pia visiwa hivyo vilivyotawaliwa na Ufaransa? Idadi ya wahubiri iliendelea kuongezeka, na Mashahidi wa Yehova wakajulikana zaidi. Hata wakati mmoja, mwishoni mwa mwaka wa 1959, polisi waliingia katika Jumba la Ufalme wakati wa mkutano ili wajionee yale yaliyokuwa yakiendelea.

Kwa hiyo, ndugu walishauriwa waanzishe shirika la kisheria. Kuandikishwa kisheria kungeondoa mashaka. Ndugu walifurahi sana walipojulishwa mnamo Aprili 2, 1960 kwamba Shirika la Mashahidi wa Yehova lilikuwa limeandikishwa kisheria!

Hata hivyo, gazeti la Mnara wa Mlinzi bado lilikuwa limepigwa marufuku nchini Ufaransa. Kwa sababu ndugu walifikiri kwamba marufuku hiyo ilihusu pia Polinesia ya Ufaransa, walipata makala za Mnara wa Mlinzi katika gazeti liitwalo Mlinzi (La Sentinelle) lililotumwa kutoka Uswisi. Siku moja polisi walimweleza Michel Gelas, aliyekuwa msimamizi wa shirika la kisheria la Mashahidi kwamba walijua kuwa gazeti hilo lilitumiwa badala ya Mnara wa Mlinzi. Hata hivyo, polisi hawakuzuia gazeti hilo lisiingizwe kisiwani. Baadaye, wakati marufuku ya Mnara wa Mlinzi ilipoondolewa mwaka wa 1975, ndugu walielewa sababu gazeti Mlinzi halikuzuiwa.

Marufuku hiyo ilipoondolewa nchini Ufaransa, ndugu wa Tahiti waliomba ruhusa kuingiza Mnara wa Mlinzi kisiwani humo. Ndipo ilipojulikana kwamba marufuku hiyo haikuwa imetangazwa kamwe katika gazeti rasmi la serikali ya Polinesia ya Ufaransa. Kwa hiyo, gazeti la Mnara wa Mlinzi halikuwa limepigwa marufuku kamwe huko Polinesia ya Ufaransa. Wengi walishangaa kujua jambo hilo.

Kwa upande mwingine, serikali iliweka sheria kali kuhusu kuwapa wageni ruhusa ya kukaa Tahiti au kuwaongezea muda wa kukaa humo. Kwa hiyo, watu ambao hawakuwa raia wa Ufaransa, kama vile Clyde na Ann Neill, waliotajwa mapema, waliweza kukaa humo kwa miezi michache tu. John na Ellen Hubler pia hawakuwa raia wa Ufaransa. Lakini haikuwa vigumu sana kwao kupata ruhusa ya kukaa Tahiti kwa sababu John alikuwa mwanachama wa shirika la kisheria la Mashahidi, na sheria ya Ufaransa iliruhusu mtu mmoja kutoka nchi ya kigeni kuwa kwenye halmashauri ya wakurugenzi.

Jambo hilo lilimwezesha John kufanya kazi ya mzunguko. Siku moja, mkuu wa polisi alimwita John aje ofisini mwake, kwa sababu alitaka kujua kwa nini John alitembelea visiwa mbalimbali mara nyingi. John alieleza kwamba alikuwa mwanachama wa halmashauri ya wakurugenzi, kwa hiyo, ilimbidi kuhudhuria mikutano ya halmashauri hiyo. Ingawa mkuu huyo aliridhika na maelezo hayo alimwita John ofisini mwake tena na tena.

Kuanzia mwaka wa 1963, Wapolinesia wengi, na angalau kasisi mmoja mashuhuri, walikasirishwa na majaribio ya silaha za nyukilia katika Bahari ya Pasifiki. Mwasi-imani mmoja alitumia nafasi hiyo kupeleka malalamiko kwa polisi, na kumshtaki Ndugu Hubler kwa uwongo kuwa mmoja wa wale waliopinga majaribio hayo. Kwa hiyo, John akaitwa tena na mkuu huyo. Badala ya kumshutumu mshitaki wake, John alieleza kwa upole msimamo wetu unaotegemea Biblia, wa kutounga mkono upande wowote katika masuala kama hayo na wa kuwaheshimu wenye mamlaka. (Rom. 13:1) Pia alimpa mkuu huyo vitabu. Ofisa huyo alielewa kwamba mtu fulani alikuwa akijaribu kuwaletea Mashahidi matatizo.

Hata hivyo, hatimaye Ndugu na Dada Hubler walinyimwa ruhusa ya kukaa Tahiti. Kwa hiyo, walirudi Australia, ambako ndugu aliendelea kufanya kazi ya mwangalizi anayesafiri hadi mwaka wa 1993, walipolazimika kuacha utumishi huo kwa sababu ya matatizo ya afya.

Walipokuwa visiwani humo, Ndugu na Dada Hubler waliona mabadiliko makubwa ambayo watu kadhaa walifanya maishani mwao ili wampendeze Yehova. Mmoja kati ya wale waliofanya mabadiliko makubwa ni mwanamke aliyekuwa na umri wa miaka 74 mwenye watoto 14 waliozaliwa nje ya ndoa. John anasema hivi: “Tulimwita Mama Roro. Wakati Mama Roro alipojifunza kweli, alifunga ndoa na yule mtu aliyekuwa akiishi naye, kisha akawaandikisha watoto wake wote, hata ingawa walikuwa na baba tofauti-tofauti. Ili kuandika majina ya watoto hao wote, meya alilazimika kuunganisha karatasi mbili. Mama Roro alisisitiza kwamba mambo yote yafanywe kulingana na sheria ya Yehova.” Baada ya kubatizwa, dada huyo mwaminifu akawa painia naye alikuwa stadi katika kuwaachia watu magazeti. Hata alijiunga na wahubiri wengine walipoenda kuhubiri kwenye visiwa vya mbali.

Biblia ya Kitahiti Ni Baraka

Katika miaka ya 1960 lilikuwa jambo la kawaida kuwapata watu waliosema Kitahiti tu. Kwa sababu ya bidii ya watafsiri Nott na Davies, Biblia imepatikana katika lugha hiyo tangu mwaka wa 1835.b Jambo moja lenye kuvutia ni kwamba jina la Mungu (Iehova katika Kitahiti) linapatikana kotekote katika Biblia hiyo, na hata katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo.

Biblia ya Kitahiti, ambayo imesambazwa kotekote visiwani humo, imewasaidia watu wengi kupata ujuzi sahihi wa ile kweli. Mmoja wa watu hao ni Taina Rataro. Taina, aliyezaliwa mwaka wa 1927, ni mmoja wa wale wanafunzi wa kwanza wa Biblia kisiwani Makatéa. Hata hivyo, hapo mwanzoni hakuweza kusoma wala kuandika Kitahiti, lugha yake ya asili. Lakini alijitahidi sana na kufanya maendeleo. Hata alijiandikisha katika Shule ya Huduma ya Kitheokrasi na baadaye akawekwa kuwa mtumishi wa huduma.

Elisabeth Avae mwenye umri wa miaka 78, alizaliwa kwenye kisiwa cha mbali cha Rimatara, kimojawapo cha Visiwa vya Tubuaï, umbali wa kilometa 600 hivi kutoka Tahiti. Katika miaka ya 1960, hakuelewa hata neno moja la Kifaransa, lakini alijua kusoma na kuandika Kitahiti. Baada ya kuolewa, yeye na mumewe walihamia Papeete. Alipokuwa huko, binti yake mkubwa, Marguerite, ambaye alikuwa ameanza kuhudhuria mikutano ya Kikristo, alimweleza kuhusu kweli ya Biblia. Elisabeth pia alianza kuhudhuria mikutano pamoja na watoto wake wengine tisa, licha ya upinzani mkali kutoka kwa mume wake aliyekuwa akitupa nje nguo zake zote alipokuwa mkutanoni.

Wakati huo, mikutano iliongozwa katika Kifaransa, na mara nyingine sehemu fulani zilitafsiriwa katika Kitahiti. Elisabeth alilishwa kiroho mikutanoni kwa kusoma katika Biblia yake ya Kitahiti maandiko yaliyotajwa. Dada aliyejifunza naye alitumia kijitabu “Habari Njema Hizi za Ufalme,” na kumtafsiria kutoka Kifaransa hadi Kitahiti, huku Elisabeth akisoma maandiko katika Biblia yake. Alifanya maendeleo na akabatizwa mwaka wa 1965. Yeye naye aliwafundisha wengine waliojua Kitahiti peke yake. Pia aliwafundisha watoto wake na sita kati yao wakajiweka wakfu kwa Yehova. Vilevile aliwafundisha baadhi ya wajukuu wake, ambao wengine wao aliwalea mwenyewe.

Mjukuu wake mmoja, Diana Tautu, amefanya kazi ya kutafsiri katika ofisi ya tawi ya Tahiti kwa miaka 12. Diana anasema hivi: “Ninamshukuru Nyanya kwa kunisaidia kukijua Kitahiti vizuri. Sasa ninafurahia kuwasaidia wengine kupata chakula cha kiroho chenye kuokoa uhai katika lugha yao.”

Wachina Wapata Kumjua Yehova

Katika miaka ya 1960, karibu asilimia 10 ya watu wa Tahiti walikuwa Wachina. Mchina wa kwanza kukubali kweli ya Biblia ni Clarisse Lygan, aliyekuwa kijana wakati huo. Familia ya Clarisse ilikuwa maskini. Ili kusaidia familia yake kifedha, msichana huyo alifanya kazi kila Jumatano, siku ambayo watoto hawakwenda shuleni. Alikuwa ameajiriwa kazi na familia ya Mashahidi. Walimhubiria Clarisse, na ingawa wazazi wake walimpinga sana, alibatizwa mwaka wa 1962, alipokuwa na umri wa miaka 18.

Alexandre na Arlette Ly Kwai na Ky Sing Lygan pia walikuwa kati ya Wachina wa kwanza kuwa watumishi wa Yehova kisiwani Tahiti. Siku moja Alexandre, aliyekuwa dereva wa teksi, alikutana na Jim na Charmian Walker, Mashahidi kutoka New Zealand ambao walikuwa wamefika mwaka wa 1961 ili kusaidia katika kazi ya kuhubiri. Alexandre alitaja kwamba alitaka kujifunza Kiingereza. Charmian anasema hivi: “Wakati huo nilikuwa painia. Kwa hiyo Jim akamwambia Alexandre kwamba mimi ningeweza kumfundisha Kiingereza, naye akakubali. Funzo hilo lilikuwa na sehemu mbili; somo la Kiingereza la dakika 30 na funzo la Biblia la dakika 30 katika kitabu Kutoka Paradiso Iliyopotea Mpaka Paradiso Iliyopatikana.”

Wakati huohuo, Ky Sing, ndugu ya Alexandre, pia alianza kujifunza kweli. Hata hivyo, wanaume hao wawili walikuwa wamejiunga na Kanisa Katoliki hivi karibuni na walikuwa wakijifunza kuhusu dini hiyo. Kwa hiyo, walianza kuona tofauti kati ya mafundisho ya Biblia na yale ya kanisa hilo. Kisha, mwishoni mwa masomo hayo, kasisi aliwauliza wale wanadarasa wapatao 100 iwapo walikuwa na maswali yoyote. Alexandre aliinua mkono na kumwomba kasisi huyo atumie Maandiko kuthibitisha kwamba nafsi haiwezi kufa. Kasisi huyo akajibu hivi kwa ukali: “Ninajua kwa nini unauliza swali hilo. Wewe huongea na Mashahidi wa Yehova, sivyo?” Halafu akamdhihaki kijana huyo mbele ya wanadarasa wenzake.

Jambo hilo lilimsadikisha Alexandre na Ky Sing kwamba Kanisa Katoliki halifundishi kweli. Hatimaye wao pamoja na wake zao walijiweka wakfu kwa Yehova, na baadaye ndugu hao wawili wakawekwa kuwa wazee wa kutaniko. Alexandre hata alifanya kazi kwenye Halmashauri ya Ofisi ya Tawi ya Tahiti kwa muda fulani. Baada ya hapo, yeye na mkewe walihamia Raïatéa, kimojawapo cha Visiwa vya Society, ili kusaidia kuhubiri ujumbe wa Ufalme, kisha wakaenda Bora Bora, ambako Alexandre alitumikia kwa uaminifu hadi alipokufa.

Maisha Yaliyobadilika Baharini

Antonio Lanza alikuwa fundi katika kiwanda cha televisheni huko Milan, Italia. Mnamo mwaka wa 1966, kampuni hiyo ilihitaji mtu wa kujitolea kwenda Tahiti ili kusimamia huduma ya kurekebisha bidhaa ambazo zimekwisha uzwa. Antonio alikubali kazi hiyo, ambayo angeifanya kwa miaka mitatu. Hata hivyo, alikusudia kumwacha mkewe Anna, na wana wao wawili wachanga. Anna alilia kwa majuma kadhaa, akijaribu kumshawishi mume wake asiende, lakini wapi.

Ilichukua siku 30 kusafiri kwa meli kutoka Marseilles, Ufaransa, hadi Papeete. Antonio ni mtu mwenye urafiki anayependa kuongea na watu, lakini karibu kila mtu melini alisema Kifaransa tu, lugha ambayo hakuielewa. Hata hivyo, katika siku ya pili alikutana na watawa wawili wa Kanisa Katoliki kutoka Italia. Lakini walishughulikia sana desturi zao za kila siku, kwa hiyo hawakuwa na muda mwingi wa kuongea. Hata hivyo, walimwambia Antonio kwamba kulikuwa na mwanamke fulani Mfaransa melini anayejua Kiitaliano. Mwanamke huyo alikuwa Lilian Selam, mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Lilian aliyekuwa na watoto wake, alikuwa safarini kwenda Tahiti kujiunga na mumewe, aliyekuwa amepata kazi huko.

Antonio alimpata Lilian na akafurahia kuzungumza naye. Lilian naye alimpa kitabu fulani kuhusu Biblia katika Kiitaliano. Baadaye, walizungumzia mambo ya kiroho mara nyingi. Wakati mmoja, Lilian alimkumbusha Antonio kwamba alikuwa akijihatarisha kiadili kwa kumwacha mke na watoto wake kwa ule muda wa miaka mitatu ambao angefanya kazi Tahiti. Pia alimwonyesha maoni ya Mungu kuhusu utakatifu wa ndoa na kumsomea maandiko ya Biblia kama vile Waefeso 5:28, 29 na Marko 10:7-9.

Baada ya kutafakari mambo hayo, Antonio alianza kujutia uamuzi wake. Kwa hiyo, alipokuwa Panama, alimwandikia mke wake barua, na kumwambia kwamba mara akipata pesa atatuma nauli ya ndege ili yeye na watoto wao wawili wajiunge naye Tahiti. Baadaye akaandika tena, na kumwambia Anna amwombe kasisi Biblia na kuileta. Kasisi alionaje jambo hilo? Alimwambia Anna kwamba iwapo mume wake anataka kusoma kitabu hicho kigumu, bila shaka amerukwa na akili.

Miezi sita baada ya Antonio kufika Tahiti, mkewe na watoto wake walijunga naye. Siku moja baada ya kufika, Anna, ambaye alikuwa mtu wa dini, alimwomba Antonio awapeleke kanisani ili wakamshukuru Mungu kwa kuwa pamoja tena. Antonio akasema: “Sawa, tutakwenda kanisani.” Lakini badala ya kuwapeleka kwenye Kanisa Katoliki, aliwapeleka kwenye Jumba la Ufalme! Anna alishangaa sana. Hata hivyo, alifurahia mkutano na hata akakubali kujifunza Biblia. Ni nani aliyemfundisha? Si mwingine ila Lilian Selam, yule dada aliyemhubiria Antonio melini.

Badala ya kukaa peke yake kwa miaka mitatu huko Tahiti, Antonio sasa amekaa huko kwa miaka 35 pamoja na familia nzima. Isitoshe, Antonio, Anna, na wana wao wanne, wanamwabudu Yehova pamoja, na Antonio ni mzee wa kutaniko.

Familia Zatumikia Mahali Penye Uhitaji Mkubwa

Katika miaka iliyopita, ndugu na dada wengi wamehamia visiwa vya mbali vilivyo na uhitaji mkubwa wa wahubiri wa Ufalme. Baadhi ya familia hizo ni ile ya Mara, Haamarurai, Terii, na ya Ato Lacour, ambaye mke wake na watoto wake hawakuwa katika kweli. Familia ya Mara, yaani, Vaieretiai, Marie-Medeleine, na watoto watano, walihamia Raïatéa kutoka Tahiti. Mume na mke waliokuwa mapainia wa pekee ambao walikuwa wakitumikia huko, walitumwa eneo lingine. Dada wawili tu pamoja na wahubiri wachache wasiobatizwa ndio waliobaki kisiwani humo.

Ndugu Vaieretiai alikuwa mchongaji wa sanaa za mbao, na baadaye akawa mchongaji wa sanaa za matumbawe. Kazi hiyo ilimwezesha kuhama bila kubadili kazi yake. Huko Raïatéa hakukuwa na mzee mwingine ila yeye, na alikisaidia kikundi kidogo kisiwani humo kwa miaka mitano hadi ndugu mwingine alipokuja. Halafu familia ya Mara ikahamia kisiwa cha Tahaa, ambako ilikaa kwa miaka minne.

Haikuwa rahisi kwa familia ya Mara kupata riziki kwenye visiwa hivyo. Vaieretiai anasema: “Ilinibidi kwenda Tahiti ili kuuza sanaa zangu. Nyakati nyingine sikuwa na nauli ya ndege. Pindi hizo, nilimwomba msimamizi wa ndege anipe tiketi kwa mkopo, na kumwahidi kwamba ningelipa nauli kamili niliporudi. Naam, nyakati nyingine hatukuwa na pesa nyingi, lakini hatukukosa kamwe mahitaji ya maisha.” Jeanne, binti ya Vaieretiai na Marie-Medeleine, alichochewa na mfano mzuri wa kujidhabihu wa wazazi wake, naye amekuwa katika utumishi wa wakati wote kwa miaka 26. Sasa yeye ni Mwanabetheli huko Tahiti.

Mnamo mwaka wa 1969, Ato Lacour pamoja na familia yake walihamia Rurutu, kimojawapo cha Visiwa vya Tubuaï. Tayari alikuwa ameomba ahamishiwe huko kikazi. Alikuwa amebatizwa kwa miaka mitatu tu na hakuna mtu mwingine katika familia yake aliyekuwa Shahidi. Hakukuwa na wahubiri wengine kwenye visiwa hivyo. Siku moja baada ya kufika, alianza kuhubiri. Aliandika hivi katika kitabu chake cha kumbukumbu: “Nimeanza kuhubiri, mimi peke yangu. Si rahisi. Babiloni Mkubwa ametia mizizi kabisa hapa.”

Hata hivyo, baada ya muda mfupi watu waliopendezwa walianza kukubali habari njema, na kikundi kikaanzishwa. Mwanzoni, walifanya mikutano katika nyumba ya Lacour. Ato anasema hivi: “Kwa kuwa dini yetu ilikuwa mpya kwenye kisiwa hicho, kikundi chetu kilibandikwa jina ‘dini ya Lacour.’ Lakini Yehova ‘aliendelea kukikuza’ kikundi chetu, nacho kikawa kutaniko mwaka wa 1976.” (1 Kor. 3:6) Kabla ya Ndugu Lacour kufa mwaka wa 2000, watu kadhaa wa familia yake, na hata mkewe, Perena, walijiunga naye katika ibada ya kweli.

Rudolphe na Narcisse Haamarurai walihamia Bora Bora. Rudolphe, aliyekuwa msimamizi wa kampuni ya umeme katika eneo fulani la Tahiti, aliacha kazi hiyo na akapata kazi ya kuchuma na kukausha nazi huko Bora Bora. Hakupata kazi nyingine kwa miaka miwili. Lakini Yehova alimbariki sana yeye na mkewe, kwa kuwa hatimaye kutaniko lilianzishwa kwenye kisiwa hicho! Kutaniko hilo lilifanya mikutano nyumbani kwa Ndugu Haamarurai kwa zaidi ya miaka 25. Kisha, katika mwaka wa 2000, wakaanza kutumia Jumba lao jipya la Ufalme lililo karibu na kidimbwi maridadi cha Bora Bora.

Taaroa na Catherine Terii walio na watoto 15, walihamia kisiwa kidogo cha Maupiti, pamoja na watoto 7 ambao bado waliishi nyumbani. Kisiwa hicho pia ni kimojawapo cha Visiwa vya Society. Familia ya Terii ilipofika huko mwaka wa 1977, hakukuwa na wahubiri wengine kisiwani Maupiti. Waliishi kwenye motu, yaani, kisiwa kidogo chenye mimea inayositawi kilicho ukingoni mwa kidimbwi. Chakula chao hasa kilikuwa samaki na nazi zilizokunwa. Pia, walikusanya na kuwauza samaki-gamba wenye kuliwa. Walipoenda kuhubiri, walivuka kidimbwi kwa miguu hadi kwenye kisiwa kikuu, huku wakijihadhari wasije wakamkanyaga samaki yeyote mwenye sumu.

Katika mwaka wa 1980, Taaroa na Catherine waliwekwa kuwa mapainia wa pekee na kutumwa Bora Bora. Baada ya kuwa mapainia wa pekee kwa miaka 5, walikuwa mapainia wa kawaida kwa miaka 15. Kama tutakavyoona, miongoni mwa wanafunzi wao wa kwanza wa Biblia ni mume na mke waliovumilia upinzani mwingi kwa ajili ya habari njema.

Watoto wa Kiroho Wapata Majaribu

Edmond (Apo) na Vahinerii Rai ndio wanafunzi wa kwanza wa Biblia wa Ndugu na Dada Terii kukubali kweli kwenye kisiwa cha Bora Bora, nao waliishi katika nyumba ya mama ya Edmond. Baada ya Apo na Vahinerii kujifunza kwa miezi sita hivi, mama ya Edmond alichochewa na kasisi kuwafukuza nyumbani. Edmond, Vahinerii, na mwanao mwenye umri wa miaka miwili, walilazimika kuishi katika kibanda kichakani. Kasisi huyo pia alimshawishi mwajiri wa Edmond amfute kazi, hata aliwaambia waajiri wengine wasimwajiri Edmond kazi! Kwa miezi minane, walijipatia riziki hasa kwa kuvua samaki.

Siku moja mwanamke fulani aliyetaka kujenga nyumba alimwendea mwajiri wa zamani wa Edmond. Mwanamke huyo alivutiwa sana na ustadi wa Edmond naye alitaka Edmond ajenge nyumba hiyo. Aliposikia kwamba Edmond alifutwa kazi kwa sababu alishirikiana na Mashahidi wa Yehova, mwanamke huyo alimwambia mwajiri huyo kwamba angempa kazi hiyo ikiwa tu angemrudisha Edmond kazini. Hivyo, Edmond akarudishwa kazini. Wakati huohuo, mama yake alikuwa amebadili mtazamo wake, naye akamkaribisha yeye na Vahinerii nyumbani tena. Leo, Edmond ni mzee katika Kutaniko la Bora Bora.

Habari Njema Yahubiriwa na Kukubaliwa Kisiwani Huahine

Auguste Temanaha ni mmojawapo wa wanafunzi wa kwanza wa Biblia waliobatizwa mwaka wa 1958 huko Tahiti. Baada ya kubatizwa, Auguste alihamia Marekani, na akarudi Tahiti mwishoni mwa miaka ya 1960 pamoja na mkewe Stella, na watoto wao watatu. Alikuwa na biashara nzuri kisiwani Tahiti. Mwaka wa 1971, baada ya kutiwa moyo na mwangalizi mmoja wa mzunguko, na kwa sababu ya mfano mzuri wa familia ya Mara iliyotajwa mapema, familia ya Temanaha iliuza biashara yao na kuhamia kisiwani Huahine, kilometa 160 hivi kutoka Tahiti.

Wakati huo, kulikuwa na dada mmoja na watu wachache waliopendezwa kwenye kisiwa hicho. Hawakuweza kuwasiliana na tengenezo la Yehova ila tu wakati mapainia na waangalizi wa mzunguko walipowatembelea mara chache. Kwa hiyo walifurahi sana familia ya Temanaha ilipokuja. Mara moja Auguste alipanga mikutano, ambayo ilifanywa jikoni, nyumbani kwake. Watu 20 hivi walikuwa wakihudhuria.

Mwanzoni, Auguste hakufaulu kupata kazi. Hata hivyo, yeye na familia yake waliendelea kuhubiri kwa bidii, wakitumaini kwamba Yehova angewasaidia kupata riziki. Na hawakukosea. Kwa mfano, wakati familia ya Temanaha ilipoenda kuhubiri, kwa kawaida Auguste aliacha gari katika eneo walilohubiri. Mara nyingi waliporudi kwenye gari walipata likiwa limejaa chakula. Hawakujua ni nani aliyekiweka humo. Walifikiri ni watu wenye fadhili katika eneo walilohubiri ambao walijua tatizo lao. Jambo hilo liliendelea kwa majuma kadhaa, mpaka hali ya uchumi ya familia hiyo ikawa nzuri.

Tukifikiria uvumilivu na bidii ya familia ya Temanaha na wengine kama wao, na vilevile urafiki wa wenyeji wa kisiwa hicho, haishangazi kwamba leo kuna kutaniko lenye ongezeko huko Huahine. Sasa kuna mhubiri 1 kati ya watu 53 kwenye kisiwa hicho. Na katika miaka ya majuzi, mtu 1 kati ya watu 12 wamehudhuria Ukumbusho!

Familia nyingine nyingi za Mashahidi zimeonyesha roho iyo hiyo ya kujidhabihu. Kwa mfano, kuanzia mwaka wa 1988, Jean-Paul na Christiane Lassalle walitumikia kwenye Visiwa vya Marquesas kwa miaka miwili. Jean-Paul alikuwa mwanachama wa baraza la wasimamizi wa idara ya huduma za jamii kisiwani Tahiti, lakini aliacha kazi hiyo yenye umashuhuri ili afanye zaidi katika huduma. Mwaka wa 1994, Ndugu na Dada Lassalle walihamia Rangiroa, kimojawapo cha Visiwa vya Tuamotu, na walikaa huko kwa muda wa miaka mitatu. Leo Jean-Paul anatumikia kwa uaminifu nchini Ufaransa.

Hivi majuzi, Colson Deane aliyekuwa msaidizi wa msimamizi wa gereza huko Tahiti alistaafu, naye pamoja na mkewe Lina wakahamia kisiwa cha Tubuaï, kimojawapo cha Visiwa vya Tubuaï. Wote wawili ni mapainia na wanasaidia sana kutaniko dogo kwenye kisiwa hicho, ambacho kiko katika eneo lenye uhitaji mkubwa wa wazee.

Familia Kutoka Ufaransa Zaja Kusaidia

Familia kadhaa zilifunga safari ndefu kutoka Ufaransa hadi Tahiti ili kusaidia katika kazi ya kuhubiri. Kwa mfano, fikiria familia ya Sicari, Francis, Jeannette, na binti zao wawili wenye umri wa miaka sita na tisa. Francis anasema: “Tulitaka kufanya mengi zaidi katika huduma. Kisha tukasoma katika Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova cha 1971 kwamba kulikuwa na uhitaji wa wahubiri huko Pasifiki Kusini.” Ijapokuwa baadhi ya marafiki na watu wa ukoo walijaribu kuwavunja moyo wasihame, familia ya Sicari ilikubali mwito huo nayo ilifika Papeete mnamo Aprili 1972.

Kwa kuwa Francis alikuwa mzee, kutaniko la pili kisiwani Tahiti liliweza kuanzishwa katika mji wa Punaauia alipofika. Francis na Jean-Pierre Francine (Jean-Pierre alikuwa mwangalizi-msimamizi katika kutaniko lile lingine), walikuwa na pendeleo la kufanya kazi katika Halmashauri ya Ofisi ya Tawi ya Tahiti, ilipofunguliwa mwaka wa 1976. Francis alikuwa na pendeleo hilo kwa miaka 12.

Je, marafiki na watu wa ukoo wa familia ya Sicari walikuwa na sababu nzuri ya kuwa na wasiwasi? Francis anasema hivi: “Tofauti na vile wengine walivyosema, binti zetu wamenufaika kwa kuishi Pasifiki Kusini. Pamoja, sisi wanne tumetumia miaka 105 katika utumishi wa wakati wote na tumepata baraka nyingi, kama Yehova alivyoahidi.—Mal. 3:10.”

Katika Huduma Yetu ya Ufalme ya mwaka wa 1981, ofisi ya tawi ya Ufaransa ilitangaza kwamba kulikuwa na uhitaji wa wazee katika kisiwa cha Mooréa, kilicho umbali wa kilometa 19 kutoka Papeete. Ndugu wawili na wake zao waliitikia mwito huo. Alain na Eileen Raffaelli walikuwa kati yao, nao walitumikia huko Mooréa kwa muda wa miaka minane, na walisaidia kuanzisha kutaniko katika kisiwa hicho. Alain alifanya kazi pia katika Halmashauri ya Ofisi ya Tawi kuanzia mwaka wa 1987 hadi 1994.

Mwaka wa 1997, ofisi ya tawi ya Ufaransa iliwaalika ndugu waliokuwa wamestaafu wahamie visiwa vya mbali kwa muda wa miaka miwili au zaidi ili wasaidie makutaniko yaliyohitaji sana wazee. Gérard Balza, ambaye ni mratibu wa Halmashauri ya Ofisi ya Tawi ya Tahiti, anasema hivi: “Tulitarajia kwamba ndugu wawili au watatu pamoja na wake zao wangekuja. Tulishangaa kwelikweli tulipoona kwamba ndugu 11 pamoja na wake zao walijitolea! Isitoshe, ndugu wawili na wake zao waliamua kubaki hapa. Kwa sababu ndugu na dada hao wamekomaa kiroho na wana uzoefu mwingi, wamewasaidia sana wahubiri wetu. Na ijapokuwa wao si wamishonari, wamejionea maisha ya umishonari na magumu ya maisha kwenye kisiwa cha mbali.”

Ofisi ya Tawi Yafunguliwa

Kazi iliposonga mbele huko Pasifiki, mabadiliko ya kitengenezo yalifanywa kulingana na hali. Ofisi ya tawi ya Australia ilisimamia kazi huko Polinesia ya Ufaransa hadi mwaka wa 1958, kisha ofisi ya tawi ya Fiji iliyo karibu zaidi na Tahiti, ikapewa daraka hilo. Badiliko lingine lilifanywa mwaka wa 1975 wakati Nathan Knorr na Frederick W. Franz kutoka makao makuu ya ulimwengu walipotembelea Tahiti. Zaidi ya watu 700 walisikiliza hotuba zao zenye kutia moyo, na watu 500 hivi walikuwapo Ndugu Knorr alipotoa hotuba iliyoambatana na onyesho la picha katika Jumba moja la Ufalme.

Baada ya kuonyesha picha hizo, Ndugu Knorr alifanya mkutano pamoja na wazee na kupendekeza kwamba ofisi ya tawi ifunguliwe Tahiti. Ndugu walifurahia pendekezo hilo. Alain Jamet, mwangalizi wa mzunguko aliyejua Kiingereza, aliwekwa kuwa mwangalizi wa ofisi ya tawi. Ofisi ya tawi ilifunguliwa Aprili 1 mwaka huo, na hiyo ilikuwa hatua nzuri. Ijapokuwa ofisi ya tawi ya Fiji ilikuwa karibu na Tahiti kuliko Australia, bado kulikuwa na tatizo la lugha. Lakini sasa, ndugu wa Polinesia ya Ufaransa waliweza kuwasiliana moja kwa moja na kwa urahisi na ofisi yao ya tawi.

Ofisi hiyo ya tawi ilikuwa ndogo sana kwa sababu kulikuwa na wahubiri 300 tu katika eneo hilo lote. Ofisi hiyo ilikuwa chumba kimoja katika Jumba la Ufalme la Papeete. Katika chumba hicho kulikuwa na dawati upande mmoja na vitabu upande ule mwingine. Mwanzoni kazi ya mwangalizi wa ofisi ya tawi haikuwa nyingi, kwa hiyo, Ndugu Alain na mkewe Mary-Ann, waliweza kuendelea kufanya kazi ya mzunguko na kuhubiri kwenye visiwa vya mbali visivyokuwa na wahubiri.

Kuhubiri Kwenye Visiwa vya Tuamotu na vya Gambier

Baada ya ofisi ya tawi ya Tahiti kufunguliwa, ndugu walikazia fikira kuhubiri habari njema kwenye visiwa vya mbali. Nyakati nyingine ndugu walijipanga vikundi-vikundi na kusafiri hadi visiwa hivyo. Axel Chang, aliyefanya kazi katika Halmashauri ya Ofisi ya Tawi kwa muda, anakumbuka wakati ambapo ndugu na dada 20 walikodi ndege na kusafiri hadi Rangiroa, kisiwa kikubwa zaidi cha matumbawe cha Visiwa vya Tuamotu. Anasema hivi: “Baada ya kuwahubiria watu wote wa kisiwa hicho, tulifanya mpango wa kutoa hotuba ya watu wote. Meya wa sehemu hiyo alituruhusu kutumia jengo fulani lenye paa. Kwanza ilionekana kama ni sisi wenyewe tu ambao tungesikiliza hotuba hiyo! Tulifikiri, ‘Huenda watu wanawaogopa viongozi wao wa dini.’ Lakini baada ya hotuba kuanza, watu walingia mmoja baada ya mwingine, na jengo likajaa pole kwa pole.”

Ndugu Chang anaongeza hivi: “Hotuba ilipokuwa ikiendelea tulimwona kasisi wa Kanisa Katoliki akija kwa kasi kwa baiskeli kuelekea mahali tulipofanyia mkutano. Hata hivyo, alipokaribia, alipunguza mwendo huku akijaribu kuwatambua wafuasi wa kanisa lake waliohudhuria. Alipita kwa njia hiyo mara kadhaa. Tuliona jambo hilo kuwa lenye kuchekesha.”

Alain Raffaelli alifanya mpango ili kuhubiri kwenye Visiwa vya Gambier mwaka wa 1988. Visiwa hivyo vichache vyenye Wakatoliki wengi viko umbali wa kilometa 1,600 kutoka Tahiti, mbali zaidi kuliko visiwa vingine vya Polinesia ya Ufaransa. Watu wa visiwa hivyo walikuwa wamehubiriwa mara moja tu mwaka wa 1979, wakati Alain Jamet alipotembelea visiwa hivyo kwa muda wa siku tatu.

Kwanza ndugu hao walimtembelea meya ili wamweleze kuhusu shughuli zao na kumwomba mahali pa kufanyia Mkutano wa Watu Wote. Aliwaruhusu kulitumia jumba la arusi lakini akawaomba radhi kwa sababu hakuweza kuandamana nao walipowaalika watu, kwa kuwa alikuwa akifanya kampeni ya uchaguzi. Bila shaka ndugu walimwia radhi. Watu 30 walikuja kusikiliza hotuba hiyo, kutia ndani meya na polisi wa sehemu hiyo.

Katika hotuba yake, iliyozungumzia hali ya wafu, Alain alitaja kwamba kulingana na Biblia kuzimu (mahali ambapo inasemekana wafu huteseka) ni kaburi tu, na kwamba Kristo mwenyewe alienda kuzimu. Msikilizaji mmoja alipaaza sauti na kusema: “Haiwezekani kwamba Yesu alienda kuzimu.” Ndipo Alain akanukuu Kanuni ya Imani inayosema kwamba Kristo “akashukia kuzimu.” Wasikilizaji walishangaa waliposikia jambo hilo, kwa sababu waling’amua kwamba walikuwa wamekariri maneno hayo kwa miaka mingi bila kufikiria kile walichokuwa wakisema. Familia moja iliyohudhuria mkutano huo sasa ni Mashahidi.

Mara nyingi waangalizi wanaosafiri walihubiri kwenye maeneo yasiyokuwa na wahubiri katika majuma ambayo hawakuwa wamepangiwa kutembelea makutaniko. Ndivyo walivyofanya Mauri na Mélanie Mercier, mume na mke Watahiti. Walikuwa wa kwanza kuhubiri habari njema katika visiwa kadhaa vya matumbawe vya Tuamotu, yaani, Ahe, Anaa, Hao, Manihi, Takapoto, na Takaroa. Ilipowezekana, Mauri alitoa hotuba ya watu wote au hotuba yenye onyesho la picha. Anasema hivi: “Wenyeji wengi wa visiwa hivyo walikuwa wenye urafiki, isipokuwa wale wa kisiwa cha Anaa chenye Wakatoliki wengi. Wakati wa onyesho hilo la picha baadhi yao walianza kupaaza sauti na wengine wakataka kutupiga. Tulifurahi tulipofaulu kuwatuliza hatimaye.”

Wamishonari Wafika Visiwani

Kuanzia mwaka wa 1978, wamishonari kadhaa kutoka Ufaransa walitumwa hadi kwenye visiwa vya mbali. Michel na Babette Muller walifika Agosti 1978, nao wakatumwa Nuku Hiva, kisiwa kikubwa zaidi na chenye watu wengi zaidi kati ya Visiwa vya Marquesas. Ndugu walikuwa wametembelea visiwa hivyo vyenye Wakatoliki wengi mara kwa mara, lakini hakuna aliyefaulu kukaa huko kwa muda mrefu. Kwa kuwa hakukuwa na barabara, Michel na Babette walitembea kwa miguu au walitumia farasi. Mara nyingi wenyeji waliwakaribisha kulala nyumbani kwao. Usiku mmoja hata walilala juu ya buni zilizokuwa zinakaushwa!

Ndugu na Dada Muller walikaa Marquesas kwa muda wa miezi 18 kabla ya kuanza kufanya kazi ya mzunguko. Wengi walithamini ziara zao na kukubali vitabu. Michel na Babette waliwaachia watu nakala elfu moja za Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia katika mwaka mmoja! Kwa sababu ya jitihada za wamishonari kama hao, na vilevile mapainia na wahubiri wengine, kazi ya Ufalme huko Marquesas na katika eneo lote linalosimamiwa na ofisi ya tawi ya Tahiti ilisonga mbele vizuri. Rekodi zinaonyesha kwamba kulikuwa na mfululizo wa vilele 69 vya wahubiri!

Bila shaka, wapya hao wote walihitaji kuzoezwa. Lakini hakukuwa na ndugu na dada wa kutosha waliokomaa, ambao wangewazoeza moja kwa moja. Ndugu na Dada Muller walitatua tatizo hilo kwa kuhubiri pamoja na wahubiri wawili wapya kwa wakati mmoja. Mmoja aliandamana na Michel au Babette hadi mlangoni, huku yule mwingine akingoja barabarani. Sasa Ndugu na Dada Muller ni wamishonari huko Benin, barani Afrika.

‘Ilitubidi Kujua Maandiko Tulipohubiri’

Wamishonari Christian na Juliette Belotti waliwasili Polinesia ya Ufaransa mnamo Februari 1982. Kwanza walifanya kazi ya mzunguko, na baadaye wakafanya kazi ya umishonari kwa miaka mitano kwenye kisiwa cha Raïatéa. Sehemu fulani za kisiwa hicho zinaweza kufikiwa tu kwa mtumbwi. Christian anasema: ‘Ilitubidi kujifunza kutumia makasia na vilevile kujua Maandiko vizuri tulipohubiri kwenye eneo hilo.’ Anaongeza: “Mara nyingi tuliulizwa maswali kama vile: Watiwa-mafuta wanajuaje kwamba wataenda mbinguni? au Wanyama wa kitabu cha Ufunuo ni mfano wa nini?”

Kama ilivyo katika sehemu nyingi zenye watu wachache, watu wote walioishi Raïatéa walifahamiana. Christian anasema hivi: “Ndugu au dada alipoacha kuhubiri, mara nyingi mwenye nyumba alisema: ‘Sijamwona Fulani kwa muda mrefu. Je, amepoa?’ Au, ‘Fulani anapaswa kusaidiwa. Yaelekea ana tatizo la kiroho!’” Ndugu na Dada Belotti walipoondoka Raïatéa, Mashahidi wa Yehova walikuwa wamejifunza Biblia pamoja na angalau mtu mmoja katika karibu kila fare (“nyumba” katika Kitahiti) kwenye kisiwa hicho.

Ndugu na Dada Belotti waliishi Raïatéa lakini walihubiri pia kwenye kisiwa cha Maupiti. Wakati mmoja walipanga vitabu vitumwe moja kwa moja kwenye kisiwa hicho. Lakini havikufika kwa wakati. Christian na Juliette hawakuvunjika moyo, walitumia nakala zao za vitabu ambavyo walikuwa wamepanga kuwatolea watu. Karibu familia 30 ziliagiza vitabu hivyo, zikiwa na uhakika kwamba vingekuja. Vitabu hivyo vilipofika hatimaye, mtu mmoja aliyependezwa alijitolea kuvipeleka kwa wale walioviagiza.

Baadaye Ndugu na Dada Belotti walitumwa kwenye kisiwa cha Rangiroa, Tuamotu, ambako hakukuwa na Mashahidi wengine. Kisha wakatumwa Guiana ya Ufaransa, na hatimaye wakatumwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako Ndugu Belotti anafanya kazi katika Halmashauri ya Ofisi ya Tawi.

“Yehova Atakuzoeza”

Frédéric na Urminda Lucas kutoka Ufaransa walifika Aprili 1985, nao wakatumwa hadi kisiwa cha Tahaa, ambako kulikuwa na wahubiri watatu tu. Majuma mawili ya kwanza yalikuwa magumu kwa wenzi hao wa ndoa. Walifanya mikutano katika nyumba yao na ni wao tu waliohudhuria. Waliimba nyimbo za Ufalme na kulia; lakini hawakuvunjika moyo kiasi cha kuacha utumishi wao.

Hakukuwa na umeme kisiwani wala simu. Hata hivyo, Frédéric na Urminda walikuwa na redio ya mkononi ambayo walitumia kuwasiliana na wamishonari kwenye kisiwa jirani cha Raïatéa, ijapokuwa redio hiyo haikufanya kazi sikuzote! Walikuwa na friji ndogo pia, ambayo ilitumia jenereta ya jirani. Frédéric anasema: “Kwa kawaida, jenereta hiyo iliwashwa saa 12 jioni hadi saa 4 usiku. Siku moja tuliporudi nyumbani tulikuta kwamba nyanya zetu zote zilikuwa zimeganda kabisa. Jirani wetu alikuwa ameamua kutazama kipindi cha mchezo kwenye televisheni, hivyo alikuwa ameiwasha jenereta mapema.”

Pia iliwabidi Ndugu na Dada Lucas kujifunza Kitahiti. Wote ambao wamejifunza lugha mpya wanajua kwamba haikosi mtu anayejifunza lugha atafanya makosa yenye kuaibisha. Kwa mfano, Frédéric alipoenda nyumba kwa nyumba alifikiri alikuwa akisema, “roho takatifu,” yaani, varua mo’a. Lakini alishindwa kutamka vizuri neno mo’a, kwa hiyo alikuwa akisema “roho ya kuku.”

Ndugu na Dada Lucas walipofika Tahaa, Frédéric alikuwa na umri wa miaka 23 na alikuwa mtumishi wa huduma. Alimwambia Ndugu Alain Jamet, aliyekuwa mratibu wa Halmashauri ya Ofisi ya Tawi wakati huo, kwamba alihisi hana uwezo wa kutimiza madaraka aliyokabidhiwa. Alain alimwambia: “Usiwe na wasiwasi, Yehova atakuzoeza!” Na bila shaka Yehova alimzoeza. Miaka mitano baadaye, Ndugu na Dada Lucas walipotumwa Burkina Faso, kile kikundi kidogo huko Tahaa kilikuwa kimeongezeka na kuwa kutaniko lenye wahubiri 14, ambao walikuwa na Jumba lao la Ufalme, naye Frédéric alikuwa mzee wa kutaniko.

Ndugu na Dada hao wanafurahi sana kwamba hawakuacha utumishi wao kwa sababu ya kuvunjika moyo mwanzoni! Hivi majuzi walisema hivi: “Hiyo ndiyo miaka bora ya ujana wetu. Tulijifunza kuwa wenye subira na kumtegemea Yehova kabisa badala ya uwezo wetu. Tulipovunjika moyo sala ilitutia nguvu. Tulimfanya Yehova kuwa kimbilio letu, na hakutuacha kamwe. Ndiyo, alituzoeza kwelikweli.”

Wamishonari Waseja Watumwa Kwenye Maeneo Magumu

Wamishonari waseja pia kutoka Ufaransa walikwenda Polinesia ya Ufaransa ili kusaidia kuhubiri habari njema. Miongoni mwa wale wa kwanza kufika walikuwa Georges Bourgeonnier na Marc Montet. Wote wawili walifanya kazi kwenye ofisi ya tawi na pia kazi ya mwangalizi anayesafiri. Mzunguko wa Marc ulihusisha Visiwa vya Tubuaï, vya Gambier, vya Marquesas, na vya Tuamotu. Alihubiri peke yake kwenye visiwa fulani vya matumbawe; na nyakati nyingine aliandamana na mapainia wa pekee wenyeji. Kila ilipowezekana, alitoa hotuba ya watu wote, na katika visiwa fulani karibu watu wote walihudhuria. Baada ya kuoa, Marc aliendelea kufanya kazi ya mwangalizi anayesafiri kwa muda. Sasa Marc na mkewe Jessica wako katika Kutaniko la Bora Bora, na Marc ni painia na mzee katika kutaniko hilo.

Philippe Couzinet na Patrick Lemassif waliwasili kutoka Ufaransa mnamo Februari 1986. Walitumwa Visiwa vya Marquesas. Tofauti na visiwa vingine vya Polinesia ya Ufaransa, hakuna matumbawe yanayovilinda visiwa hivyo. Miamba mirefu ya visiwa hivyo inaingia moja kwa moja katika maji ya bluu ya Bahari ya Pasifiki, ambamo hupigwa-pigwa daima na mawimbi makubwa. Katikati ya milima myembamba kuna mabonde yenye rutuba na mito yenye maporomoko. Mabonde hayo ni makao mazuri sana kwa mbuzi, farasi, na ng’ombe-mwitu wanaoranda-randa kwenye visiwa hivyo.

Mapainia na wahubiri walikuwa wametembelea Visiwa vya Marquesas mara kwa mara. Kwa mfano, Ndugu na Dada Muller, waliishi kwenye kisiwa cha Nuku Hiva kwa mwaka mmoja na nusu hivi, kuanzia mwaka wa 1978 hadi 1979. Lakini habari njema haikuwa imehubiriwa kikamili kwenye visiwa vyote. Philippe na Patrick walipofika, walihubiri kikamili kwenye sehemu zote. Ni kweli kwamba maendeleo yalikuwa ya polepole, kwa kuwa watu walishikilia sana dini ya Katoliki na wengi waliwaogopa makasisi. Makasisi hata walifanya ndugu hao wawili watishwe. Pia, kikundi fulani cha Wakatoliki wanaoamini vipawa vya roho kilisitawi wakati huo, nacho kilichochea vitendo kadhaa vibaya katika jamii hiyo.

Mwanzoni Patrick na Philippe walihubiri pamoja, na walipozoea eneo kila mmoja alihubiri peke yake. Mmoja alibaki katika nyumba ya wamishonari kwenye kisiwa cha Hiva Oa, ambako aliongoza mikutano, huku yule mwingine akisafiri kwa mashua hadi visiwa vile vingine kwa muda wa majuma kadhaa. Hatimaye waliona ni afadhali watengane kabisa. Patrick alihubiri kwenye visiwa vya kaskazini, naye Philippe kwenye visiwa vya kusini.

Ili kuwasaidia wamishonari hao wawili, ofisi ya tawi iliwatuma mapainia wa pekee kutoka Tahiti kuhubiri pamoja nao. Mmoja wao ni Pascal Pater, ambaye sasa ni mzee wa kutaniko na yule mwingine ni Michel Bustamante, ambaye sasa ni mwangalizi wa mzunguko. Vijana hao wenye bidii walifurahi kutumia nguvu zao za ujana kumtumikia Yehova. (Met. 20:29) Na bila shaka walihitaji nguvu, kwa kuwa mtu dhaifu au mwoga hangefaulu kuhubiri kwenye Visiwa vya Marquesas. Hakukuwa na barabara. Ili kufika kwenye nyumba na vijiji vya mbali, walisafiri kwenye vijia vyenye mawe na vya matope na kwenye mabonde, katikati ya milima mirefu. Baadhi ya sehemu hizo zilifikika tu kwa kutumia pikipiki ndogo.

Philippe anakumbuka siku moja aliposafiri kwa pikipiki yake kwenye kijia chembamba. Ng’ombe-mwitu kadhaa waliokuwa wameshtushwa na gari walitimua mbio kumwelekea. Philippe hakuwa na mahali pa kutorokea, kwa kuwa kulikuwa na mteremko mkali upande mmoja na mwamba mkubwa upande ule mwingine. Kwa hiyo, alisimamisha pikipiki, akaishika, na kuegemea mwamba kabisa. Wale ng’ombe-mwitu walimpita kwa kishindo na kumwacha akiwa ameshtuka sana, lakini bila kumwumiza.

Michel Bustamante anasema: “Utumishi wangu kwenye visiwa hivyo ulikuwa wenye kusisimua na wenye kuvutia. Lakini tulipatwa na mambo yenye kutisha pia, hasa tulipokuwa peke yetu kwenye visiwa fulani. Pindi moja nilikaa katika nyumba iliyokuwa kwenye bonde lenye giza-giza, mbali na mahali nilipokuwa nimehubiri siku hiyo. Nilitafuta mahali pa kulala katika kijiji kilichokuwa karibu, lakini sikufaulu, kwa hiyo ikanibidi kurudi nyumbani. Giza lilikuwa limeingia na miamba mirefu ilionekana kuwa yenye kuogofya sana usiku. Nilianza kufikiria uchawi wa eneo hilo, na mashetani ambao bila shaka walisambaa kotekote. Kwa sababu ya woga, nilianza kusali na kuimba nyimbo za Ufalme zinazotaja jina la Yehova mara nyingi. Nilipoingia nyumbani kwangu hatimaye, nilifunga mlango, nikafungua Biblia, na kuanza kusoma. Polepole nilianza kujihisi salama.”

Baada ya kuhubiri kwa bidii kwa miaka mitatu, ndugu walifurahi sana wakati mwanafunzi wao wa kwanza wa Biblia kutoka Marquesas alipokubali kweli. Mwanafunzi huyo alikuwa mwanamume kijana anayeitwa Jean-Louis Peterano. Kasisi alimtembelea Jean-Louis ili “amrudishe zizini.” Ili kujaribu “kumwokoa” kijana huyo, kasisi alisema kwamba jina la Yehova lilitungwa na Mashahidi wa Yehova. Jean-Louis alijibu kwa kunukuu Zaburi 83:18 katika Biblia ya Kifaransa ya Kanisa Katoliki inayoitwa Crampon Bible (1905), inayotumia jina la Mungu. Kasisi aliduwaa, akatoka, na hakurudi tena. Yaelekea Jean-Louis ndiye mtu wa kwanza kutoka Marquesas kufaulu kumkabili kasisi kuhusu swali la kidini kwa kutumia Biblia ya Kikatoliki. Baadaye, hata karani wa askofu wa Kanisa Katoliki aliacha kanisa na kuwa Shahidi wa Yehova.

Wamishonari hao waliwatembelea Jean na Nadine Oberlin waliokuwa wamehamia kisiwa cha Hiva Oa kutoka Ulaya. Kama vile Paul Gauguin, yule msanii mashuhuri Mfaransa, walikuwa wamehamia Marquesas ili wajitenge na jamii. Waliishi mahali pagumu sana kufikika na hawakuwa na vitu vyovyote vya kisasa. Jean na Nadine walibatizwa baada ya kujifunza kwa muda wa miaka mitatu na kufanya mabadiliko mengi maishani mwao.

Philippe Couzinet na Patrick Lemassif walipofika Marquesas mwaka wa 1986, kulikuwa na mhubiri mmoja tu katika visiwa hivyo. Miaka minane baadaye, Philippe alipotumwa Kamerun (wakati huo Patrick alikuwa ameondoka) kulikuwa na wahubiri 36 kwenye visiwa hivyo, mhubiri 1 kati ya watu 210. Na kulikuwa na makutaniko matatu, moja kwenye kila kisiwa kikubwa, yaani, Hiva Oa, Nuku Hiva, na Ua Pou.

Wamishonari wa Mwisho Wafika

Wamishonari wa mwisho kufika kutoka Ufaransa ni Serge na Marie-Louise Gollin, waliofika Novemba 1990. Wao pia walitumwa Marquesas, ambako wamesaidia sana kuimarisha makutaniko. Ndugu na Dada Gollin wamejifunza lugha ya Marquesas, na jambo la kuvutia ni kwamba wametembelea kila jamaa kwenye visiwa sita vinavyokaliwa!

Ndugu na Dada Gollin wanaishi kwenye kisiwa cha Hiva Oa, ambako hakuna mzee mwingine isipokuwa Serge. Wanahubiri kwa ukawaida kwenye visiwa kadhaa, kutia ndani visiwa viwili visivyo na wahubiri. Walipotembelea kisiwa cha Fatu Hiva kwa mara ya kwanza, Serge alishangaa kwamba mashemasi wa Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiprotestanti waliwaunga mkono. Baada ya ibada katika makanisa yao, mashemasi hao waliwaalika watu wasikilize hotuba ya watu wote ya nusu saa ambayo Serge alitoa kwa kawaida kwenye shule ya eneo hilo. Isitoshe, shemasi wa Kanisa la Kiprotestanti alitafsiri hotuba ya Serge katika lugha ya Marquesasas, kwa kuwa wakati huo aliijua lugha hiyo vizuri kuliko Serge.

Ili kuwasaidia wasikilizaji wapate maandiko katika Biblia zao, Serge aliyaandika kwenye ubao. Pia alitoa sala, na wote wakasema “Amina.” Kesho yake, Ndugu na Dada Gollin waliiachia kila familia kwenye kisiwa cha Fatu Hiva vitabu. Tangu wakati huo, wamekaribishwa kwa uchangamfu kila wanapotembelea kisiwa hicho chenye watu 600 hivi.

Kweli ya Biblia Yahubiriwa Gerezani

Kama katika nchi nyingine nyingi, watu kadhaa huko Polinesia ya Ufaransa wamepata kujua kweli za Biblia wakiwa gerezani. Kwa mfano, Alexandre Tetiarahi alikuwa mhalifu tangu ujanani na alifungwa kwa miaka saba. Alitoroka angalau mara sita na hivyo akaitwa Butterfly (Kipepeo), jina la mfungwa mtoro anayesimuliwa katika hadithi fulani maarufu.

Alexandre alipata Biblia na kitabu “Mambo Mawili Yasiyobadilika Asiyoweza Mungu Kusema Uongo” mahali alipokuwa akijificha kwenye kisiwa cha Raïatéa. Alisoma Biblia nzima na akasoma kitabu hicho mara kadhaa. Alisadikishwa kwamba amepata kweli, kwa hiyo, dhamiri yake ikaanza kumsumbua. Alifanya nini?

Ingawa hakuwasiliana moja kwa moja na Mashahidi wa Yehova ambao ni wachapishaji wa kitabu hicho, Alexandre alijisalimisha kwa polisi, nao wakamrudisha gerezani Tahiti. Colson Deane alikuwa mlinzi kwenye gereza alimofungwa Alexandre. Muda mfupi baada ya kufika, Alexandre alimsikia Colson akimhubiria mfanyakazi mwenzake na mara moja akayatambua mafundisho hayo. Hivyo, alimwendea Colson faraghani na kumwomba amfundishe mengi zaidi.

Ndugu Deane alimwomba msimamizi wa gereza ruhusa ya kumfundisha Alexandre. Punde si punde, wafungwa wengine pia walitaka kujifunza. Msimamizi wa gereza alimruhusu Colson kujifunza na wafungwa wakati wa mapumziko ya mchana pia. Baadaye ilionwa kuwa afadhali wazee wengine wawili waongoze funzo hilo. Kwa muda wa miaka kadhaa, wafungwa 30 hadi 50 hivi walisikiliza hotuba ya Biblia kila juma, kisha ndugu waliongoza funzo la Biblia pamoja na kila mmoja aliyetaka.

Alexandre alifanya maendeleo kwa haraka na maafisa wa gereza wakatambua jambo hilo. Kwa hiyo, walimpa mtoro huyo bingwa ruhusa ya kipekee ya kuhudhuria kusanyiko lake la kwanza la wilaya, chini ya usimamizi wa Ndugu Deane. Alexandre alibatizwa kwenye kusanyiko hilo. Sasa ameachiliwa na anaendelea kumtumikia Yehova.

Makusanyiko ya Kimataifa Huko Tahiti

Kusanyiko la kimataifa la kwanza lilifanywa Tahiti mwaka wa 1969. Kulikuwa na wahubiri 124 tu kwenye visiwa hivyo wakati huo. Unaweza kuwazia jinsi walivyofurahi kuwakaribisha ndugu 210 kutoka nchi 16, kutia ndani Ndugu Frederick W. Franz, ndugu wa kwanza wa Baraza Linaloongoza kutembelea Tahiti. Kusanyiko hilo lililohudhuriwa na watu 610 liliwachochea sana ndugu, na mwaka uliofuata kulikuwa na ongezeko la asilimia 15. Kisha, mwaka wa 1978, Kusanyiko la Kimataifa la “Imani Yenye Ushindi” likafanywa huko Tahiti. Kusanyiko hilo lilikuwa na hudhurio la watu 985!

Kutafsiri Katika Kitahiti

Kadiri idadi ya wahubiri ilivyoongezeka, ndivyo kazi kwenye ofisi ya tawi ilivyoongezeka pia, hasa kazi ya kutafsiri vichapo vya Biblia katika Kitahiti, lugha kuu ya wenyeji wa Polinesia. Hata kabla ya ofisi ya tawi kufunguliwa, wahubiri wazee wachache waliojua Kitahiti vizuri walitafsiri vichapo kadhaa katika Kitahiti, wakitumia vichapo vya Kifaransa. Kwa mfano, walianza kutafsiri Huduma Yetu ya Ufalme mwaka wa 1963. Kisha, mwaka wa 1971, wakamaliza kutafsiri kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele.

Kazi ya kutafsiri ilisonga mbele ofisi ya tawi ya Tahiti ilipofunguliwa mwaka wa 1975. Watafsiri wengi wapya walijua Kiingereza, kwa kuwa lugha hiyo inafundishwa shuleni. Kwa hiyo, waliweza kutafsiri moja kwa moja kutoka Kiingereza badala ya tafsiri za Kifaransa. Gazeti la Mnara wa Mlinzi limetolewa mara mbili kwa mwezi katika Kitahiti tangu mwaka wa 1976, nalo gazeti la Amkeni! pia lilitafsiriwa katika lugha hiyo kwa muda. Pia, kitabu “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa,” Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko, na kitabu cha nyimbo vilitafsiriwa. Mashahidi wa Yehova ndio wamechapisha vitabu vingi zaidi vya Kitahiti kuliko kikundi kingine chochote!

Hata hivyo, kwa muda wa miaka 30 iliyopita, watu wengi wameanza kuongea sana Kifaransa badala ya Kitahiti na lugha nyingine za Polinesia. Kifaransa hupendelewa kwa kuwa ni lugha yenye maneno mengi, nacho hutumiwa kwenye vyombo vya habari na shuleni, kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu.

Wenyeji wengi wa Polinesia wanakiona Kitahiti kuwa sehemu ya utamaduni wao, kwa hiyo mara nyingi ndugu hutumia lugha hiyo katika kazi ya kuhubiri. Kati ya makutaniko 26 katika eneo linalosimamiwa na ofisi ya tawi, makutaniko 5 hutumia Kitahiti. Asilimia 20 hivi ya wahubiri huhudhuria makutaniko hayo matano. Kwa hiyo, bado vichapo vya lugha hiyo vinahitajika.

Mradi wa Ujenzi Waanzishwa

Ofisi ya tawi ilikuwa katika kile chumba kidogo kilichopakana na Jumba la Ufalme huko Papeete kuanzia mwaka wa 1975 hadi 1983, lakini mwaka wa 1983 ofisi mpya ya tawi ilijengwa mjini Paea, umbali wa kilometa 25 hivi kutoka Papeete. Betheli hiyo mpya ilijengwa na ndugu wenyeji, na ilikuwa na vyumba vinne kwa ajili ya familia ya Betheli, ofisi tatu, sehemu ya kuhifadhia vitabu, na Jumba la Ufalme. Ndugu Lloyd Barry wa Baraza Linaloongoza, aliyaweka wakfu majengo hayo mapya Aprili 15, 1983. Watu 700 walihudhuria mkutano huo.

Lakini baada ya muda hata ofisi hiyo haikutosha. Kwa hiyo, Baraza Linaloongoza liliidhinisha ujenzi wa ofisi kubwa ya tawi pamoja na Jumba la Kusanyiko, huko Toahotu, wilaya yenye mashamba-mashamba karibu na sehemu nyembamba ya nchi inayounganisha sehemu mbili za kisiwa hicho. Ujenzi huo ulikamilishwa na ndugu kutoka Australia, Kanada, Marekani, New Zealand, na Ufaransa. Ndugu na dada wenyeji walisaidia pia. Ndugu wa Baraza Linaloongoza, Milton G. Henschel, aliyaweka wakfu majengo hayo mapya Desemba 11, 1993.

Wakati huohuo, mradi mkubwa wa ujenzi wa Majumba ya Ufalme ulianzishwa pia. Chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Ujenzi ya Mkoa, ndugu walijenga majumba mapya 16 katika muda wa miaka kumi hivi. Kwa hiyo, karibu kila kutaniko lina Jumba la Ufalme.

Mabadiliko Kwenye Ofisi ya Tawi na Mazoezi Zaidi

Alain Jamet alikuwa mratibu wa Halmashauri ya Ofisi ya Tawi kwa miaka 20 hivi, lakini mwaka wa 1995 ikambidi kuacha kazi hiyo kwa sababu ya madaraka ya familia. Hata hivyo, alibaki kwenye Halmashauri ya Ofisi ya Tawi, naye anafanya kazi ya mwangalizi wa wilaya mara kwa mara. Kwa hiyo, mnamo Septemba mwaka huo, Baraza Linaloongoza liliwatuma Gérard na Dominique Balza kutoka Betheli ya Ufaransa hadi Tahiti. Gérard aliwekwa kuwa mratibu wa Halmashauri ya Ofisi ya Tawi.

Luc Granger ndiye ndugu wa tatu katika Halmashauri ya Ofisi ya Tawi. Yeye na mkewe Rébecca, walihamia Tahiti mwaka wa 1991 ili kusaidia kuhubiri kwenye eneo hilo lenye uhitaji mkubwa. Baada ya kutumikia kama mapainia kwa muda mfupi, walifanya kazi ya mzunguko na ya wilaya kwa miaka minne, na mwaka wa 1995 wakaombwa kufanya kazi kwenye ofisi ya tawi.

Ofisi ya tawi ya Tahiti ilipanga darasa la kwanza la Shule ya Mazoezi ya Kihuduma lifanywe Mei 1997. Wengi wa wale wanafunzi 20 waliohudhuria walipata mapendeleo ya kipekee ya utumishi. Kwa mfano, Félix Temarii sasa ni mmojawapo wa waangalizi wawili wa mzunguko kwenye visiwa hivyo. Gérard Balza anasema hivi: “Tunasali kwamba ndugu wengi zaidi wajitahidi kukuza sifa za kustahili na kujitolea, ili tuweze kuwa na darasa lingine. Bado kuna uhitaji mkubwa katika visiwa kadhaa, ambavyo baadhi yake havina wahubiri wowote mpaka leo. Katika visiwa vingine, ndugu wanaostahili wanahitajika ili kushughulikia majukumu mbalimbali kutanikoni. Na habari njema inahubiriwa mara chache sana kwenye visiwa 58, ambako asilimia 7 hivi ya watu wote wa Polinesia ya Ufaransa wanaishi. Ndugu na dada wenye uraia wa Ufaransa ambao wamekomaa kiroho na ambao wamestaafu, wangeweza kusaidia sana katika visiwa fulani. Ikiwa kuna ndugu na dada kama hao ambao wangetaka kusaidia, hata kwa miaka miwili tu, ndugu kwenye ofisi ya tawi wangependa ndugu hao wawasiliane nao.”

Magumu ya Jamii Inayobadilika Haraka

Kisiwani Tahiti kuna maendeleo makubwa ya kiuchumi. Watu wengi hawaoni umuhimu wa dini, na wengi hupendelea maisha ya mjini. Mambo hayo yamewafanya watu wengi wahamie Tahiti kutoka visiwa vingine. Hali ya uchumi inapozidi kuwa bora watu hukazia sana anasa na ukusanyaji wa mali.

Inasikitisha kwamba baadhi ya watu wa Yehova wamenaswa na vishawishi hivyo visivyotambulika kwa urahisi. Vijana hasa wanaona ni vigumu kutanguliza mambo ya kiroho na kubaki safi kiadili. Hata hivyo, ni wazi kwamba Yehova anabariki kazi kwa kuwa katika eneo hilo sasa kuna mhubiri 1 kati ya watu 141.

Jambo hilo linaonyesha kwamba watu wengi huko Polinesia ya Ufaransa wamekuja kuthamini paradiso bora, yaani, paradiso ya kiroho, ambayo inamilikiwa na watu wanaoitwa kwa jina la Mungu. (Yoh. 6:44; Mdo. 15:14) Zaidi ya hayo, paradiso hiyo inatangulia paradiso halisi itakayokuja hivi karibuni na kuondoa maumivu, huzuni, na hata kifo, mambo ambayo yamewaathiri watu wote kotekote duniani.—Ayu. 14:1; Ufu. 21:3, 4.

Wapolinesia wa zamani walikuwa wajasiri, mabaharia hodari, na waliamini kwamba wangepata nchi bora. Hawakukosea. Vivyo hivyo, waabudu waaminifu wa Yehova leo, kama wale waliotajwa katika masimulizi haya, wanajitahidi kupata zawadi bora ambayo Yehova amewaahidi. Wao pia, watapata kile wanachotafuta. Naam, Yehova atawaongoza, vizuri kuliko nyota za angani, wote wanaomtumaini hadi Paradiso itakayokuja hivi karibuni.—Zab. 73:23, 24; Luka 23:43.

[Maelezo ya Chini]

a Ijapokuwa masimulizi haya yanazungumzia Polinesia ya Ufaransa kwa ujumla, yameitwa “Tahiti” kwa sababu Tahiti ndicho kisiwa kikuu cha eneo hilo na watu wengi wanalijua jina hilo. Hata hivyo, jina “Tahiti” linapotumiwa katika masimulizi yenyewe kisiwa cha Tahiti ndicho kinachozungumziwa.

b Gazeti la Mnara wa Mlinzi la Julai 1, 2003, ukurasa wa 26-29, linazungumzia jinsi Biblia ya Kitahiti ilivyotafsiriwa.

[Sanduku katika ukurasa wa 72]

Maelezo Mafupi Kuhusu Polinesia ya Ufaransa

Nchi: Visiwa hivyo 130 vina ukubwa wa kilometa 4,000 za mraba, navyo vimetawanyika kwenye eneo la bahari lenye ukubwa wa kilometa milioni 5 za mraba. Visiwa hivyo 130 viko katika makundi matano ya visiwa, yaani, Visiwa vya Tubuaï (Austral), vya Gambier, vya Marquesas, vya Society, na vya Tuamotu. Asilimia 85 ya watu wa eneo hilo wanaishi katika vile visiwa 14 vinavyoitwa Visiwa vya Society.

Watu: Watu wengi ni Wapolinesia au Wapolinesia machotara. Pia kuna idadi ndogo ya Wachina, Wazungu wa Ulaya, na Wamarekani.

Lugha: Kifaransa na Kitahiti ndizo lugha kuu, lakini Kifaransa ndiyo lugha rasmi na ya biashara.

Kazi: Watu wengi hufanya kazi ya serikali, na pia kazi kama vile ualimu, utalii, biashara, na kadhalika. Wengine hufanya kazi ya kukuza lulu, kilimo, au kazi ya viwanda. Asilimia 80 ya bidhaa zinazopelekwa nchi za nje kuuzwa ni lulu.

Chakula: Vyakula vingi huingizwa kutoka nchi za nje. Mazao kama vile ndizi, mihogo, nazi, mboga, mapapai, mananasi, myugwa, nyanya, na matikiti-maji hulimwa visiwani humo. Chakula cha kawaida ni nyama ya samaki, chaza, uduvi, na vilevile ya ng’ombe, mbuzi, na nguruwe.

Hali ya hewa: Hali ya hewa ni yenye joto na unyevunyevu, lakini inatofautiana kidogo kati ya visiwa mbalimbali. Majira ya mvua huanza Novemba na huisha Aprili. Eneo la katikati la kisiwa cha Tahiti linaweza kupata meta tisa za mvua kila mwaka.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 74]

Visiwa Vyenye Milima, Visiwa Tambarare, na Motu

Visiwa vyote vya Polinesia ya Ufaransa vimetokea kwa sababu ya milipuko ya volkeno. Baadhi ya visiwa hivyo ni tambarare na vingine ni vyenye mawemawe na milima. Milima fulani ina urefu wa maelfu ya meta juu ya usawa wa bahari. Tahiti ni kimojawapo cha visiwa vyenye milima.

Visiwa vyote vyenye milima, isipokuwa Marquesas, vimezungukwa na miamba ya matumbawe. Kwenye miamba mingi ya matumbawe, kama ile inayozunguka Bora Bora, kuna visiwa vidogo vyenye mimea inayositawi ambavyo vinaitwa motu. Watalii huvipenda sana visiwa hivyo.

Vile visiwa tambarare ni vya miamba ya matumbawe, navyo ni vyenye urefu wa meta moja hivi tu juu ya usawa wa bahari. Kwa kawaida miamba hiyo ya matumbawe huwa na umbo la mviringo na katikati yake kuna kidimbwi chenye maji maangavu. Visiwa vya Tuamotu ni vya aina hiyo. Vidimbwi fulani ni vikubwa mno. Kwa mfano, kile cha Rangiroa kina urefu wa kilometa 70 na upana wa zaidi ya kilometa 20.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 77]

Alikuwa Shemasi wa Kanisa, Sasa Ni Mhubiri wa Ufalme

Manuari Tefaatau

Alizaliwa: 1913

Alibatizwa: 1959

Maisha yake: Manuari, aliyekuwa shemasi katika Kanisa la Kiprotestanti, alifundishwa kweli na baadhi ya wanafunzi wa kwanza wa Biblia kisiwani Makatéa.

Baada ya Mashahidi Jean-Marie na Jeanne Félix kufika kisiwani Makatéa mwaka wa 1956, wanafunzi wao wa kwanza wa Biblia, Maui Piirai na Germaine Amaru, walinihubiria. Muda si muda nikaanza kuwahubiria watu wa kanisa langu, jambo ambalo lilisababisha mgogoro kanisani. Hata, kasisi aliniamuru niache kuzungumza na Mashahidi wa Yehova.

Bila kusita niliacha kanisa na kuanza kuhudhuria mikutano iliyofanywa nyumbani kwa familia ya Félix. Wafuasi wengine wachache wa kanisa langu la zamani walianza pia kujifunza na kuhudhuria mikutano. Ninafurahia sana kuwa miongoni mwa wale wanafunzi wachache wa kwanza wa Biblia katika eneo la Polinesia ya Ufaransa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 83, 84]

Yehova Alinisaidia Nilipopungukiwa

Leonard (Len) Helberg

Alizaliwa: 1930

Alibatizwa: 1951

Maisha yake: Ndugu Helberg alianzisha kazi ya kuhubiri kisiwani Tahiti alipokuwa mseja, baada tu ya kuwekwa kuwa mwangalizi wa mzunguko. Sasa yeye na mkewe Rita wanaishi Australia.

Mwaka wa 1955, nilipowekwa na ofisi ya tawi ya Australia kuwa mwangalizi wa mzunguko huko Pasifiki Kusini, kulikuwa na makutaniko mawili tu katika eneo hilo kubwa, moja kisiwani Fiji na lingine huko Samoa. Pia kulikuwa na vikundi sita. Hakukuwa na wahubiri wowote kisiwani Tahiti.

Niliamua kwenda Tahiti kwa mara ya kwanza mnamo Desemba mwaka wa 1956, na kukaa huko mwezi huo wote. Nilisafiri kwa siku sita kutoka Fiji hadi Tahiti kwa meli iitwayo Southern Cross. Kutoka chumba nilichopanga niliweza kuiona bandari maridadi ya Papeete. Asubuhi iliyofuata, nilipokuwa nikijitayarisha kwenda katika utumishi wa shambani, niliona meli ya Southern Cross ikipita karibu na dirisha langu. Nilikuwa peke yangu katika nchi ya kigeni, umbali wa kilometa 3,000 kutoka kwa ndugu zangu, miongoni mwa watu walioongea lugha ambayo sikuelewa, yaani, Kifaransa. Nilikuwa na anwani ya mwanamke mmoja tu aliyekuwa akipata gazeti la Amkeni! kwa njia ya posta.

Ghafula nililemewa sana na hisia za upweke hivi kwamba nilianza kulia. Sikuweza kuacha kulia, kwa hiyo, nikawaza, ‘Potelea mbali, sitahubiri leo, nitarudi kulala. Nitaanza kuhubiri kesho.’ Baada ya kusali sana usiku huo, niliamka asubuhi iliyofuata nikiwa mchangamfu. Alasiri hiyo nilimpata yule mwanamke Mwalgeria aliyekuwa akipokea gazeti la Amkeni! kwa njia ya posta. Kama Lidia anayetajwa katika kitabu cha Matendo, mwanamke huyo na mwanawe mwenye umri wa miaka 34 walinikaribisha kwa moyo wote, nao wakasisitiza nikae pamoja nao. (Mdo. 16:15) Upweke wangu ukatoweka mara moja! Nilimshukuru Yehova, ambaye bila shaka alinisikia nilipomlilia katika sala.

Ninapofikiria mambo haya ninatambua vizuri zaidi kwamba Yehova ni Baba mwenye upendo mwingi sana! Naam, tunapojitolea ili kumtumikia, yeye hutusaidia sana tunapopungukiwa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 87, 88]

Mapainia wa Kwanza

Alexis Tinorua alihudhuria mikutano ambayo Len Helberg alipanga mwishoni mwa miaka ya 1950. Alexis alisema hivi: “Nilisikiliza Ndugu Helberg alipozungumzia Biblia pamoja na mashemasi kadhaa wa kanisa la Kiprotestanti. Papo hapo, nilitambua kwamba mafundisho ya Mashahidi wa Yehova ni ya kweli, nami nikaanza kujifunza nao. Nilibatizwa mwaka wa 1960. Baadaye nilifurahia kuwa painia kwa miaka tisa. Mnamo mwaka wa 1965, nilikuwa Shahidi wa kwanza kuhubiri kwenye kisiwa cha Huahine, kimojawapo cha Visiwa vya Society. Ninamshukuru sana Yehova kwa pendeleo la kuwasaidia watu 80 kupata ujuzi sahihi wa kweli ya Biblia.” Alexis alimtumikia Yehova hadi alipokufa mnamo Mei 2002.

Hélène Mapu alianza utumishi wa painia kisiwani Tahiti mwaka wa 1963, muda mfupi tu baada ya kujifunza kweli. Mumewe alimwunga mkono sana, ijapokuwa hakuwa Shahidi. Kazi ya mume huyo ilihusisha kusafiri kwa mashua kati ya Tahiti na Raïatéa. Kwa hiyo, hakukataa wakati Hélène alipowekwa kuwa painia wa pekee kwenye kisiwa cha Raïatéa. Dada huyo alikuwa Shahidi wa kwanza kuhubiri habari njema kwenye kisiwa hicho. Baadaye Hélène alirudi Tahiti na kukaa kwenye ile sehemu ndogo ya kisiwa cha Tahiti inayoitwa Tahiti Iti. (Kisiwa cha Tahiti kina sehemu mbili zilizounganishwa.) Hakukuwa na Mashahidi wengine katika sehemu hiyo, isipokuwa yeye na dada mwingine aitwaye Mereani Tefaaroa. Hélène anasema hivi: “Watu wengi walipendezwa, na muda si muda tukaanzisha mafunzo mengi ya Biblia.”

Bila shaka Yehova aliwabariki dada hao waaminifu, kwa kuwa baadaye kutaniko lilianzishwa katika mji wa Vairao kwenye eneo hilo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 101]

“Chagua Kati Yangu na Yehova”

Yvette Gillot

Alizaliwa: 1932

Alibatizwa: 1968

Maisha yake: Amekuwa painia kwa muda mrefu kuliko painia mwingine yeyote yule huko Polinesia ya Ufaransa.

Nilipomwambia mume wangu kwamba nilitaka kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova alinilazimisha kufanya uamuzi. Alisema: “Chagua kati yangu na Yehova.” Nilijaribu kuongea naye, lakini wapi. Aliniacha na watoto wetu watatu. Hata hivyo, alirudi baada ya miaka kadhaa.

Katika miaka hiyo nilifaulu kujiruzuku na kuwaruzuku watoto wangu na kufanya utumishi wa painia wa kawaida. Nilienda kazini mapema asubuhi, kisha nikaongoza mkutano wa utumishi. Mwishoni mwa miaka ya 1960 kulikuwa na wahubiri mia moja tu visiwani, kwa hiyo mara nyingi tulikosa ndugu wa kuongoza mikutano hiyo.

Ninamshukuru Yehova kwa kunipa pendeleo la kuwasaidia watu 50 hivi kujiweka wakfu kwake. Mmoja wao ni Richard Wong Foo ambaye amefanya kazi katika Betheli ya Tahiti tangu 1991. Ninafurahi kwamba wana wangu wawili ni wazee wa kutaniko.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 105]

Mazishi ya Binti Mfalme wa Mwisho

Michel Gelas ambaye ni mzee wa kutaniko huko Papeete alihusika katika tukio lisilo la kawaida linalohusu Binti Mfalme Takau Pomare wa Tahiti, aliyekufa mwaka wa 1976 akiwa na umri wa miaka 89. Binti mfalme huyo alikuwa mtu wa mwisho wa ukoo wa wafalme wanaoitwa Pomare, ambao walitawala Tahiti na visiwa kadhaa vya karibu kwa muda fulani. Binti yake ambaye ni Shahidi wa Yehova alimwomba Michel atoe hotuba ya mazishi ingawa binti mfalme huyo, aliyekuwa mama yake mlezi, hakuwa Shahidi.

Michel alikubali kutoa hotuba hiyo, kwa kuwa aliiona pindi hiyo kuwa nafasi nzuri ya kuwaeleza watu kadhaa kama vile viongozi wa kisiasa na wa dini, na waandishi wa habari juu ya tumaini la ufufuo. Siku moja baada ya mazishi, gazeti la eneo hilo lilikuwa na picha ya Ndugu Gelas alipotoa hotuba, jeneza likiwa mbele yake. Kati ya wale waliohudhuria ni gavana, rais wa Polinesia, maafisa mbalimbali, na askofu mkuu wa Kanisa Katoliki aliyekuwa amevalia kanzu nyeupe.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 109, 110]

Kasisi Mmoja Alituazima Pikipiki Yake; Mwingine Akateketeza Vitabu Vyetu

Jacques Inaudi

Alizaliwa: 1944

Alibatizwa: 1965

Maisha yake: Jacques na mkewe Paulette walikuwa mapainia wa pekee nchini Ufaransa. Huko Pasifiki walitumikia pamoja, Jacques alipokuwa mwangalizi anayesafiri.

Mimi na Paulette tuliwaaga familia na marafiki wetu huko Ufaransa mwaka wa 1969, na tukafunga safari ya kwenda Tahiti ambako tulikuwa tumetumwa. Safari yetu haikuwa shwari kwani tulipokuwa katikati ya bahari ya Pasifiki moto ulitokea melini, na mawimbi yakatupeleka huku na huku kwa muda wa siku nne! Tulipofika Tahiti, niliwekwa kuwa mwangalizi wa mzunguko.

Mzunguko wetu ulitia ndani New Caledonia, Vanuatu, na Polinesia ya Ufaransa. Wakati huo kulikuwa na kutaniko moja na vikundi viwili tu huko Polinesia ya Ufaransa. Mwaka wa 1971 mzunguko wetu ulipunguzwa na tukabaki tu na Polinesia ya Ufaransa, hivyo tulipata nafasi ya kutembelea visiwa kadhaa vya mbali. Ujumbe wa Ufalme haukuwa umehubiriwa kamwe katika baadhi ya visiwa hivyo. Mimi na Paulette tulikaa pia Huahine kwa muda wa miezi tisa, na kwa muda mfupi kwenye kisiwa kidogo cha Maupiti. Tulipokuwa Huahine tulikuwa na pendeleo la kuongoza mafunzo 44 ya Biblia.

Tulikula samaki ambao mara nyingi nilivua kwa kutumia bunduki inayorusha mkuki majini. Hatukuwa na chakula kingi, lakini hatukulala njaa kamwe; tulipata mahitaji yetu ya kimwili sikuzote. Tulipokuwa tukihubiri kwenye kisiwa cha Tubuaï, tulishangaa na kufurahi wakati padri fulani alipotuazima pikipiki yake. Huenda alituhurumia kwa sababu hatukuwa na gari wala pikipiki.

Mwaka wa 1974 tulitembelea visiwa vinne kati ya Visiwa vya Marquesas, yaani, Hiva Oa, Nuku Hiva, Ua Huka, na Ua Pou. Ndugu kwenye ofisi ya tawi walituomba tumtembelee Kalina Tom Sing Vien, dada mwuguzi aliyekuwa amehamia kisiwa cha Ua Pou mwaka wa 1973. Alikaa huko kwa muda wa miezi 13, naye ndiye mhubiri wa kwanza wa Ufalme aliyetoa ripoti ya utumishi katika Visiwa vya Marquesas.

Tofauti na kasisi mwenye urafiki wa Tubuaï, kasisi wa Ua Pou alipinga kazi yetu. Alitufuata kisiri tulipohubiri, na kuwaamuru wafuasi wa kanisa lake wampe vitabu vyovyote tulivyokuwa tumewaachia. Kisha akaviteketeza vyote nje ya nyumba ya Kalina. Jambo hilo lilitushtua na pia likawashtua Wakatoliki wengi!

Licha ya upinzani kama huo, kazi ya Ufalme ilisonga mbele huko Marquesas, na lilikuwa pendeleo kwetu kushiriki kidogo katika kazi hiyo. Kwa sababu ya afya ya Paulette ilitubidi kuacha utumishi wa wakati wote. Hata hivyo, tumeazimia kuendelea kumpa Yehova kilicho bora.

[Sanduku katika ukurasa wa 113]

Kutembelea Kisiwa kwa Mara ya Kwanza

Ebu wazia kwamba umefika kwenye kisiwa cha mbali au kisiwa cha matumbawe kwa mara ya kwanza. Umepanga kukaa huko kwa juma moja au mawili ili kuwahubiria watu. Hata hivyo, hakuna Shahidi mwingine kisiwani, na hakuna hoteli wala usafiri wa umma. Utafanya nini? Utakaa wapi? Marc Montet na Jacques Inaudi, ambao wamekuwa mapainia na waangalizi wa mzunguko, wamepatwa na matatizo hayo mara kadhaa.

Marc anasema hivi: “Kwa kawaida nilianza kuhubiri mara niliposhuka katika ndege au mashua, na nilipohubiri niliuliza-uliza juu ya mahali pa kulala. Haikuwa rahisi kwa mwanamume mseja kupata mahali pa kukaa, lakini kwa kawaida mtu alinikaribisha nyumbani kwake na kuniandalia chakula na mahali pa kulala. Niliporudi tena ilikuwa rahisi zaidi kupata mahali pa kulala, kwa sababu watu walinijua. Ilikuwa rahisi pia baada ya kuoa. Watu hawakuwa na wasiwasi sana kuwakaribisha mume na mke nyumbani.”

Jacques anaeleza jinsi alivyofanya: “Mara nyingi nilitembelea meya na kumwuliza ikiwa alimjua mtu yeyote ambaye angeweza kunipa mahali pa kulala kwa muda ambao nilitaka kukaa kisiwani. Kwa kawaida alipendekeza mahali pazuri. Katika visiwa vingi, watu humheshimu mtu ambaye wanamwona kuwa mtu wa Mungu, nao hujitahidi kumsaidia. Hivyo, kwa kawaida nilipata mahali pa kulala bila malipo.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 117, 118]

Tunafurahia Sana Kazi ya Kuhubiri

Alain Jamet

Alizaliwa: 1946

Alibatizwa: 1969

Maisha yake: Yeye na mkewe Mary-Ann wamefanya utumishi wa wakati wote nchini Ufaransa na huko Polinesia ya Ufaransa.

Nilipokuwa na umri wa miaka 13 familia yetu ilihamia Tahiti kutoka Ufaransa. Baada ya shule ya upili nilirudi Ufaransa ili kusomea udaktari. Nilipokuwa huko nilikutana na Mary-Ann, mwanafunzi wa biolojia kutoka Tahiti, na tukaoana. Mashahidi wa Yehova walitutembelea mwaka wa 1968, tukakubali kweli.

Tulijitahidi kuwaeleza wazazi wetu kuhusu imani yetu mpya, lakini hawakuitikia. Niliandika barua na kuomba jina langu lifutwe katika kanisa langu huko Tahiti, naye Mary-Ann akaliandikia kanisa lake. Kanisa la Mary-Ann huko Papeete hata walichukua hatua ya kumtenga na kanisa mbele ya watu. Padri aliwaalika wazazi wake wahudhurie pindi hiyo.

Tulibatizwa mwaka wa 1969 na kuanza utumishi wa painia. Tulipokuwa Marseilles, Ufaransa, niliitwa kujiunga na jeshi na nilifungwa kwa miezi miwili kwa sababu ya kukataa. Nilipoachiliwa, mimi na Mary-Ann tuliwekwa kuwa mapainia wa pekee na tulitumwa Marseilles na Bordeaux. Halafu, mwaka wa 1973, wazazi wetu wazee walituomba turudi Tahiti, na tukafundisha katika shule ya msingi kwa mwaka mmoja.

Kisha mwangalizi wa ofisi ya tawi ya Fiji akatuuliza kama lengo letu lilikuwa kuanza utumishi wa wakati wote tena, kwa kuwa kulikuwa na uhitaji wa mwangalizi wa mzunguko huko New Caledonia na Polinesia ya Ufaransa. Kwa sababu wazazi wetu hawakuhitaji utunzaji wetu tena, tulikubali mwaliko huo na tulianza kazi ya mzunguko Agosti 1974. Ndugu N. H. Knorr alipotembelea eneo hilo mwaka wa 1975 niliwekwa kuwa mwangalizi wa kwanza wa ofisi ya tawi ya Tahiti.

Mwana wetu Rauma alizaliwa mwaka wa 1986, na mke wangu akaacha utumishi wa wakati wote. Tunashukuru kwamba Rauma ni ndugu yetu wa kiroho leo. Tunapofikiria maisha yetu, tunathamini sana mapendeleo yetu yote ya utumishi. Lakini tunafurahia hasa kazi ya kuhubiri.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 123-125]

Yehova Anawajali Kondoo Zake

Michel Bustamante

Alizaliwa: 1966

Alibatizwa: 1987

Maisha yake: Yeye pamoja na mkewe Sandra, anafanya kazi ya mzunguko huko Polinesia ya Ufaransa, ambako kuna mizunguko miwili.

Mzunguko wetu unatia ndani vikundi vyote vitano vya visiwa vya Polinesia ya Ufaransa na kwa ukubwa unalingana na Ulaya. Katika baadhi ya visiwa vya mbali kuna mhubiri mmoja tu au wawili. Ijapokuwa wanaishi katika eneo la mbali sana, bado tunawatembelea. Kwa mfano, Rosita, anaishi Takapoto, kimoja cha Visiwa vya Tuamotu. Dada huyo mwaminifu hutayarisha mikutano yote kila juma, na mumewe ambaye si Shahidi, hujiunga naye mara nyingi. Kila Jumapili, wakati ambapo watu wengi huenda kuogelea au kuvua samaki, Rosita huvalia nguo za mkutano na kujifunza somo la Mnara wa Mlinzi la juma hilo. Pia anatoa ripoti ya utumishi kwa ukawaida. Mara nyingi ripoti yake inayopokewa kwa simu kwenye ofisi ya tawi huwa ndiyo ya kwanza kufika! Dada huyo anastahili pongezi kwa jambo hilo hasa kwa sababu inambidi kusafiri kwa dakika 45 kwa mashua hadi mahali ambapo simu inapatikana.

Watu humiminika kwenye uwanja ndege inapofika. Kwa hiyo, tunapofika ili kumtembelea dada yetu, karibu watu wote wanaoishi kwenye ujirani wa uwanja wa ndege huja ili waone ni nani watakaoshuka. Siku moja mwanamke fulani alimwuliza Rosita hivi: “Wewe umekuja kumkaribisha nani?” Rosita alijibu: “Ndugu na dada yangu wa kiroho. Wanakuja kwa ajili yangu tu, ili kunitia moyo.” Kwa kawaida sisi hukaa siku tatu pamoja na Rosita, tukihubiri pamoja naye, na kumtia moyo kiroho. Mara nyingi sisi hulala baada ya saa sita usiku, kwa sababu ana hamu kubwa sana ya mazungumzo ya kiroho.

Katika kisiwa kingine, mtu wa kanisa la Wasabato alituona tulipomtembelea jirani yake ambaye ni Shahidi. Baadaye alimwambia ndugu yetu hivi: “Nimekaa kwenye kisiwa hiki kwa muda wa miaka saba, lakini hakuna hata mtu mmoja wa kanisa langu ambaye amekuja kunitia moyo.” Mtu huyo ni padri ambaye hajawekwa rasmi wa kikundi kidogo cha Wasabato kwenye kisiwa hicho.

Daniel na Doris ndio Mashahidi pekee kwenye kisiwa kimoja cha Tubuaï kinachoitwa Raevavae. Wanaishi katika eneo la mbali sana, na tulipowapata hatimaye tuliwaomba ruhusa kufanya mkutano nyumbani kwao alasiri hiyo. Walifurahi sana, na sote tukatoka ili kuwaalika watu. Tulipofika kwa ajili ya mkutano, wafanyakazi saba wa mashamba ambao walikuwa wametoka tu kazini, walingoja barabarani, karibu na nyumba ya ndugu huyo. Baadhi yao walibeba magunia ya myugwa begani.

Tuliwaambia: “Karibuni, msiwe na wasiwasi kwa sababu ya nguo zenu.” Walikuja, lakini wakaketi sakafuni, ijapokuwa kulikuwa na viti. Walifurahia mkutano, na kutuuliza maswali mengi baadaye. Bila shaka, mambo hayo yalimtia moyo sana ndugu na dada yetu, na hilo ndilo lililokuwa kusudi kuu la ziara yetu.

Nyakati nyingine ni vigumu kuwatembelea wahubiri wanaoishi kwenye visiwa vya mbali kwa kuwa hakuna uwanja wa ndege kwenye visiwa vyao. Siku moja, baada ya kushuka katika ndege, tulisafiri kwa mashua kwa muda wa saa mbili hadi kisiwa fulani ambamo wahubiri wawili waliishi. Mashua tuliyotumia ilikuwa yenye urefu wa meta nne tu na haikuwa na paa. Bila shaka tulimwuliza mwenye mashua kama chombo chake kilikuwa salama na kama alikuwa na injini ya ziada. Kupelekwa huku na huku na mikondo na mawimbi ya bahari si jambo linalofurahisha hata kidogo!

Tulipofika tulikuwa tumelowa, na migongo yetu iliuma kwa sababu ya mawimbi yaliyoipiga-piga mashua. Ndivyo ilivyokuwa tuliporudi. Sandra anasema: “Tuliporudi kwenye kisiwa kikubwa alasiri hiyo, nilipanda baiskeli yangu ili niende kuhubiri. Lakini, nilikuwa nimechoka sana kwa sababu ya kuyumbishwa katika mashua hivi kwamba sikuweza kudhibiti baiskeli, na nikaanguka papo hapo!”

Ukifikiria mambo ambayo tumesimulia, unaweza kuona kwamba kila tunapowatembelea ndugu na dada zetu wanaoishi mbali, tunatambua upendo mkubwa ambao ndugu hao wanaonyeshwa na Yehova na tengenezo lake. Bila shaka sisi sote ni sehemu ya familia ya kipekee ya kiroho.—Yoh. 13:35.

[Blurb]

“Wanakuja kwa ajili yangu tu, ili kunitia moyo”

[Chati/Picha katika ukurasa wa 80, 81]

POLINESIA YA UFARANSA—MFUATANO WA MATUKIO

1835: Tafsiri ya Biblia ya Kitahiti yakamilishwa.

Miaka ya 1930: Sydney Shepherd na Frank Dewar watembelea Tahiti na labda visiwa vingine.

1940

1956: Ujumbe wa Ufalme wahubiriwa kwa bidii kwenye kisiwa cha Makatéa na cha Tahiti.

1958: Vipindi viwili vya ubatizo, ambavyo ndivyo vya kwanza kabisa huko Polinesia ya Ufaransa.

1959: Kutaniko la kwanza la Polinesia ya Ufaransa laanzishwa mjini Papeete.

1960

1960: Shirika la Mashahidi wa Yehova laandikishwa kisheria.

1962: Jumba la Ufalme la kwanza visiwani lajengwa Papeete.

1969: Kusanyiko la kwanza la kimataifa lafanywa Tahiti.

1975: Ofisi ya tawi yafunguliwa kisiwani Tahiti.

1976: Kazi ya kutafsiri gazeti la Mnara wa Mlinzi katika Kitahiti yaanza.

1980

1983: Betheli ya kwanza yawekwa wakfu.

1989: Kilele cha wahubiri 1,000.

1993: Jumba la Kusanyiko na Betheli mpya yawekwa wakfu.

1997: Darasa la kwanza la Shule ya Mazoezi ya Kihuduma.

2000

2004: Wahubiri 1,746 huko Polinesia ya Ufaransa.

[Grafu]

(See publication)

Jumla ya Wahubiri

Jumla ya Mapainia

2,000

1,000

1940 1960 1980 2000

[Ramani katika ukurasa wa 73]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

POLINESIA YA UFARANSA

POLINESIA YA UFARANSA

VISIWA VYA MARQUESAS

Nuku Hiva

Ua Pou

Ua Huka

Hiva Oa

Fatu Hiva

VISIWA VYA TUAMOTU

Manihi

Ahe

Rangiroa

Takaroa

Takapoto

Makatéa

Anaa

Hao

VISIWA VYA SOCIETY

Maupiti

Tahaa

Raïatéa

Bora Bora

Huahine

Mooréa

Tahiti

VISIWA VYA TUBUAÏ (AUSTRAL)

Rurutu

Rimatara

Tubuaï

Raevavae

VISIWA VYA GAMBIER

MOORÉA

TAHITI

PAPEETE

Punaauia

Paea

Toahotu

Vairao

[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 66]

[Picha katika ukurasa wa 70]

Jeanne na Jean-Marie Félix walikuwa kati ya Mashahidi wa kwanza kuhubiri kikamili kwenye eneo la Polinesia ya Ufaransa

[Picha katika ukurasa wa 71]

Katika mwaka wa 1958, Jean-Marie Félix alimbatiza Maui Piirai, Mpolinesia wa kwanza katika eneo hilo kujiweka wakfu kwa Yehova

[Picha katika ukurasa wa 79]

Clyde na Ann Neill (chini) walijiunga na Agnès Schenck (kulia) kisiwani Tahiti ili kusaidia kuhubiri habari njema

[Picha katika ukurasa wa 85]

John na Ellen Hubler walianza kufanya kazi ya mzunguko mwaka wa 1960

[Picha katika ukurasa wa 86]

Jumba la Ufalme la kwanza la Kutaniko la Papeete lilijengwa mwaka wa 1962. Jumba hilo ambalo halikuwa na kuta, lilikuwa na paa lililoezekwa kwa makuti

[Picha katika ukurasa wa 89]

Toleo la Aprili 15, 1965, la Mlinzi (“La Sentinelle”) lenye makala za “Mnara wa Mlinzi”

[Picha katika ukurasa wa 92]

Ili kufanya maendeleo ya kiroho, Taina Rataro alijifunza kusoma na kuandika Kitahiti

[Picha katika ukurasa wa 92]

Elisabeth Avae (ambaye ameketi) na mjukuu wake Diana Tautu

[Picha katika ukurasa wa 95]

Anna na Antonio Lanza

[Picha katika ukurasa wa 96]

Vaieretiai na Marie-Medeleine Mara

[Picha katika ukurasa wa 97]

Ato Lacour

[Picha katika ukurasa wa 98]

Rudolphe Haamarurai

[Picha katika ukurasa wa 99]

Vahinerii na Edmond Rai (kushoto) pamoja na Taaroa na Catherine Terii (kulia)

[Picha katika ukurasa wa 100]

Auguste na Stella Temanaha

[Picha katika ukurasa wa 102]

Christiane na Jean-Paul Lassalle (kushoto) na Lina na Colson Deane (kulia)

[Picha katika ukurasa wa 103]

Roger Sage (kushoto) akitafsiri hotuba ya Francis Sicari katika Kitahiti kwenye kusanyiko la wilaya katika miaka ya 1970

[Picha katika ukurasa wa 107]

Eileen na Alain Raffaelli

[Picha katika ukurasa wa 108]

Mauri na Mélanie Mercier

[Picha katika ukurasa wa 120]

Marie-Louise na Serge Gollin ni mishonari huko Marquesas

[Picha katika ukurasa wa 122]

Alexandre Tetiarahi pamoja na mkewe Elma, na binti zao, Rava (kushoto) na Riva

[Picha katika ukurasa wa 126]

Watafsiri wa Kitahiti

[Picha katika ukurasa wa 127]

Kusanyiko la Kimataifa la “Amani Duniani” la mwaka wa 1969, ndilo la kwanza kufanywa Tahiti

[Picha katika ukurasa wa 128]

Jumba hili la Ufalme kwenye kisiwa cha Bora Bora ndilo la karibuni zaidi kujengwa huko Polinesia ya Ufaransa

[Picha katika ukurasa wa 130]

Christine na Félix Temarii

[Picha katika ukurasa wa 131]

Halmashauri ya Ofisi ya Tawi, kuanzia kushoto kuelekea kulia: Alain Jamet, Gérard Balza, na Luc Granger

[Picha katika ukurasa wa 132, 133]

(1) Ofisi ya tawi ya Tahiti

(2) Gérard Balza alipotangaza kitabu “Mkaribie Yehova,” katika Kitahiti, Julai 2002

(3) Familia ya Betheli ya Tahiti

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki