Mabadiliko Makubwa
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UJERUMANI
“KUONDOKA nyumbani kulimhuzunisha sana mke wangu,” akasema Dieter. “Michaela, binti yetu mwenye umri wa miaka 11 alisononeka pia. Lakini hatukuwa na la kufanya.” Je, hiyo ni familia ya wakimbizi, inayotoroka eneo la vita? Hapana, familia hiyo inaishi katika mojawapo ya maeneo ya kuchimba migodi ya Ujerumani.
Kwa muda wa miaka 55 iliyopita, watu wapatao 33,000 katika eneo la Rhineland huko Ujerumani wamekumbwa na hali ileile kama Dieter na familia yake. Walihamishwa ili kuruhusu uchimbuaji wa liginaiti au makaa ya mawe ya kahawia. Kwa sababu ya uhitaji mkubwa wa nishati viwandani, tani milioni 180 hivi za liginaiti huchimbuliwa kila mwaka nchini Ujerumani pekee. Inakadiriwa kwamba uzito huo unazidi uzito wa Piramidi ya Cheops huko Misri kwa mara 25 hivi.
Hilo limeathirije ardhi na watu wanaoishi katika eneo hilo? Kulingana na kitabu Brockhaus Enzyklopädie, “Mara nyingi kuchimba migodi kwa kadiri kubwa hufanya watu wengi wahame makwao na kusababisha mabadiliko makubwa.”a Acheni tuchunguze uchimbaji wa migodi huko Rhineland na jinsi watu wamekuwa wakiathiriwa nao.
Kuchimbua Liginaiti
Eneo lililo kati ya Cologne na Aachen kwenye upande wa chini wa Mto Rhine ndilo eneo kubwa zaidi lenye liginaiti barani Ulaya. Eneo hilo linakaribiana kwa ukubwa na eneo la Luxembourg au Mbuga ya Kitaifa ya Yosemite huko California, Marekani. Liginaiti inapatikana chini ya ardhi, ikiwa imefunikwa kwa matabaka ya changarawe, mchanga, au udongo wa mfinyanzi ambayo yanapaswa kuondolewa kwanza.
Ili kufikia liginaiti, mashine za kuchimba zenye ndoo hutumiwa kukwangua matabaka ya juu. Mashine moja ya aina hiyo hukwangua kila siku matabaka yanayoweza kujaza trela 16,000. Ili kuzuia kuta za migodi zisiporomoke inapozidi kuchimbwa, migodi huchimbwa kama ngazi. Hebu tazama mashine zenye ndoo za kuchimba migodi ambazo zimeonyeshwa juu. Hizo ni baadhi ya mashine kubwa zaidi duniani. Mashine hizo zina urefu wa meta 95, urefu unaokaribia mara mbili ya ule wa Sanamu ya Liberty huko New York.
Baada ya matabaka hayo kukwanguliwa, yanasafirishwa kwa kutumia ukanda-safirishi. Jaribu kuwazia kiasi cha liginaiti na matabaka ambacho kinahitaji kusafirishwa. Kwa kila meta moja ya mraba ya liginaiti inayochimbuliwa katika eneo la Rhineland nchini Ujerumani, zaidi ya meta 6 za mraba za matabaka hukwanguliwa. Ukanda-safirishi huzunguka kwa mwendo wa kasi sana kuliko hata mwendo wa baiskeli. Kanda-safirishi hizo hukutana mahali pa kukusanya liginaiti na matabaka hayo ya juu. Kisha kwa kutumia magari-moshi, liginaiti hupelekwa kwenye ghala la makaa au vituo vya umeme nayo matabaka hupelekwa kwenye eneo la takataka. Liginaiti nyingi hupelekwa kwenye vituo vya umeme ili kuzalisha umeme.
Matabaka hayo ya juu hutumiwa kujaza mahali ambapo liginaiti imechimbuliwa. Mashine humwaga udongo hatua kwa hatua hadi shimo linapojaa. Udongo unaosalia hupelekwa kwenye maeneo ya takataka. Takataka hizo zinaweza kurundamana kufikia urefu wa meta 200. Watunzaji wa bustani huwa na kazi ngumu ya kutandaza marundo hayo katika maeneo ya mashambani na kuyafanya yafae kilimo na upandaji wa miti.
Kushusha Tabaka la Maji
Uchimbaji wa migodi huathiri sana mandhari na mifumo ya kiasili. Ili kuudumisha mgodi bila maji, tabaka la maji hushushwa hadi sehemu ya chini sana ya mgodi. Kiasi cha maji kinachoondolewa nchini Ujerumani kila mwaka, kinaweza kuwatosheleza wakaaji wa Berlin, jiji kuu la Ujerumani, kwa miaka mitatu na nusu hivi. Kuondolewa kwa maji mengi hivyo kunawahangaisha wanamazingira ambao wanahofia jinsi Mbuga ya Maas-Schwalm-Nette iliyo kwenye mpaka wa Ujerumani na Uholanzi inavyoathiriwa. Hilo ni eneo lenye umajimaji ambalo lina mimea mingi na ndege.
Wasimamizi wa migodi wamesema kwamba hakuna sababu ya kuhangaika. Kwa kuwa maji yaliondolewa wakati wa kuchimba migodi, maji mengine hurudishwa ardhini mwendo mfupi kutoka kwenye mgodi. Maji hayo hurudishwa kupitia visima. Kwa kufanya hivyo inatumainiwa kuwa eneo hilo halitakauka.
Mandhari Mpya Yasitawi
Dunia inabadilika daima. Tani milioni 25,000 za takataka husukumwa baharini kila mwaka bila sisi kujua. Hata hivyo, mabadiliko ya mandhari huonekana waziwazi kwa mtu anayesimama kando ya mgodi. Mandhari mpya husitawi. Hilo limeathirije eneo la migodi ya liginaiti huko Rhineland?
Maeneo ya migodi yaliyokuwa yamechimbuliwa katika bonde lililoko kati ya Cologne na Aachen yamebadilishwa na kutumiwa kwa ajili ya kilimo, misitu, na mbuga. Isitoshe, mikondo ya maji, barabara, na reli imegeuzwa na kuelekezwa kwingine. Kitabu Lignite Mining in the Rhineland kinasema: “[Marekebisho] hayo hayakusudiwi kuigiza asili. Mwanadamu anaweza kutimiza sehemu ndogo tu. Sehemu kubwa hutukia kiasili.” Kufikia sasa, zaidi ya asilimia 65 ya ardhi iliyoathiriwa imeanza kutumiwa hasa kwa kilimo. Ili kutimiza kusudi hilo, udongo wenye rutuba ulitandazwa vizuri kufikia meta mbili juu ya udongo unaoweza kupenyeza maji. Kwa miaka mingi maeneo hayo yalilimwa na makampuni yenye mashamba ambayo baadaye yaliyaacha ili yatumiwe kwa ajili ya kilimo cha kawaida.
Sehemu ndogo ya misitu iliyositawi karibuni na maziwa yaliyotengenezwa na wanadamu yamekuwa hifadhi zinazolindwa na serikali. Hata viumbe fulani walio hatarini wamepata makao katika maeneo hayo. Kipepeo mmoja maridadi na ndege fulani aina ya shoro wamepata makao. Isitoshe mimea kama vile bladderwort na aina fulani ya okidi hupatikana huko. Wakaaji wa majiji ya Cologne na Bonn hufurahia kupumzika katika maeneo yaliyokuwa na migodi.
Maisha Mapya Katika Makao Mapya
Mojawapo ya kazi ngumu zinazohusiana na kuchimba migodi ni kuwahamisha watu wanaoishi katika maeneo yenye liginaiti. Lazima jamii nzima-nzima zihamishwe kabla ya uchimbaji kuanza.
Kuhamisha watu kunahitaji mipango mingi inayoanza miaka 10 hadi 15 kabla ya kazi hiyo kuanza. Jitihada hufanywa ili kuhakikisha kwamba jamii hazitenganishwi zinapohamia eneo jipya. Inaonekana kwamba nusu ya watu wanaohamishwa hutaka kuishi katika eneo lilelile na majirani wao, hali wengine huona hiyo kuwa nafasi ya kuanza maisha mapya katika eneo jipya. Watu wanaolazimika kuhama hulipwa, lakini haiwezekani kulipia mambo fulani. Kwa mfano, ikiwa ulikuwa ukifurahia kutazama mandhari yenye kupendeza ukiwa sebuleni kwako au ulikuwa na uhusiano mzuri na majirani wako, huwezi kurudishiwa hali hizo. Huenda kila kitu kikawa tofauti mahali unapohamia.
Kuhamishwa kunahusisha mengi zaidi ya kuhamia nyumba nyingine, kwani uchimbaji wa migodi hubadili mazingira kabisa. Wazazi hawawezi kuwaonyesha watoto wao mahali walipokulia na kwenda shule. Mahali ambapo mtu alikulia hubadilika kabisa. Watu hukabilianaje na hali hiyo? Amkeni! liliwahoji baadhi yao.
Friedhelm anaishi katika kijiji ambacho kitahamishwa karibuni. Hafurahii wazo la kujenga nyumba mpya, kwani hiyo ni mara ya pili kufanya hivyo. Inge, mke wake anasema: “Tulipojenga nyumba ya kwanza, tulijifunza mambo mengi muhimu, lakini hatuna nguvu za kufanya hivyo tena.” Kujenga nyumba mpya ni kazi ngumu sana, na huenda kukahusisha kuishi kwenye eneo la ujenzi kwa miaka kadhaa.
Werner na Margarethe wanafikiri kwamba watu wengi hufaidika kifedha wanapohamishwa. Lakini watu fulani kama vile wazee, wakulima, na wafanyabiashara huathiriwa zaidi. Baadhi ya watu wanaofanya biashara huona kwamba inagharimu pesa nyingi sana kuanzisha biashara tena katika eneo jipya. Mkulima mmoja aliyehamishwa na kulima kwa zaidi ya miaka 20 shamba lililogeuzwa anasema kwamba anafikiri mambo si mabaya. Anaonelea hivi: “Ni afadhali kujitahidi uwezavyo katika hali hiyo kwani haiwezi kubadilishwa.”
Hilo ni kweli kabisa! Hatimaye, Dieter na familia yake waliotajwa mwanzoni waliyazoea makao yao mapya. Hao ni watu watatu tu kati ya wengi wanaoweza kuelezea hali hiyo. Kuchimba migodi hubadili sana ardhi na maisha ya watu.
[Maelezo ya Chini]
a Katika maeneo fulani suala la kuchimba migodi na athari yake kwa mazingira linabishaniwa sana. Gazeti la Amkeni! haliungi mkono upande wowote.
[Picha katika ukurasa wa 21]
Mashine ya kuchimba yenye ndoo yachimbua liginaiti
[Hisani]
Rheinbraun AG
[Picha katika ukurasa wa 23]
Mashine ya kutandaza yajaza mgodi kwa udongo wenye rutuba
Eneo lililokuwa na mgodi lageuzwa
[Hisani]
All photos: Rheinbraun AG