“Hekima ya Vitu vya Asili”
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI JAPANI
HICHO ndicho kilichokuwa kichwa cha maonyesho ya Expo 2005 yaliyofanyika huko Aichi, Japani. Nchi 121 zilishiriki maonyesho hayo. Wageni walitiwa moyo kujifunza kutokana na uumbaji na “kuchukua hatua za kutafuta njia za kufaidika kiuchumi bila kuharibu mazingira.” Maonyesho hayo yaliyofanywa karibu na jiji la Nagoya liliko katikati mwa Japani, yalikuwa na misitu, vidimbwi, na maua. Jambo lenye kuvutia lilikuwa njia iliyoinuliwa yenye urefu wa kilomita 2.6 iliyoitwa Global Loop. Njia hiyo yenye upana wa mita 21 hivi, iliwawezesha watu kuona mandhari nzuri iliyokuwa chini na wakati huohuo kutoharibu mazingira.
Kuwa Katika Mazingira ya Asili
Mianzi 23,000 iliyosokotwa ilitumiwa kuzingira banda la maonyesho la Japani na kulikinga kutokana na jua. Banda hilo lilikuwa na urefu wa mita 7, kimo cha mita 19, upana wa mita 90, na kina cha mita 70, na hivyo kulifanya kuwa banda kubwa zaidi la mianzi kuwahi kutengenezwa duniani. Ndani ya banda hilo kulikuwa na kamera ya video iliyoweza kuonyesha picha kwa nyuzi 360. Ndani ya kamera hiyo ya duara yenye kipenyo cha mita 12.8, wageni walizungukwa na picha zinazosonga na kuwafanya wahisi kana kwamba wako katika mazingira ya asili yenye viumbe hai vingi.
Kwa kutumia video zenye sauti, banda la Malaysia lilionyesha misitu ya mvua na matumbawe ya nchi hiyo. Kwenye banda la Thailand kulikuwa na picha zenye kuhuzunisha sana kuhusu tsunami iliyotokea Desemba 26, 2004 (26/12/2004) ambazo ziliwakumbusha wageni kwamba mwanadamu hawezi “kudhibiti vitu vya asili.” Likionyesha jinsi wanyama fulani wametoweka, banda la Afrika Kusini lilikuwa na sanamu ya mtoto wa quagga. Huyo ni mnyama anayefanana na punda milia aliyekuwa anapatikana kwenye nyanda za Afrika Kusini kabla hajawindwa hadi kutoweka karne ya 19.
Katika banda lililokuwa kando ya banda kuu la maonyesho, kulikuwa na mabaki ya mnyama mkubwa sana anayefanana na tembo kwenye friji. Mabaki hayo yalifukuliwa kwenye theluji iliyoganda huko Siberia, Urusi, mwaka 2002. Mnyama huyo anaitwa Yukagir, jina la mahali alipofukuliwa. Yeye ni wa jamii ya tembo iliyotoweka, na alikuwa na pembe mbili kubwa zilizojipinda na alipokufa macho yake yalibaki nusu wazi. Kichwa chake bado kilikuwa na ngozi na manyoya. Mnyama huyo anayestaajabisha anatukumbusha wanyama wanaotoweka.
Je, Kutakuwa na Wakati Ujao Mzuri?
Wanadamu wanaweza kukabilianaje na mambo yanayohatarisha wakati ujao wa sayari yetu, kama vile uchafuzi na kuongezeka kwa kiwango cha joto? “Nembo ya maonyesho hayo ya Expo 2005” ilikuwa ukuta mkubwa wa mimea unaoitwa Bio-Lung (Pafu la Asili) uliokuwa na urefu wa mita 150 na kimo cha mita 15 hivi. Ukuta huo ulifanyizwa kwa mimea 200,000 kutoka spishi 200, kutia ndani maua. Ilipendekezwa kwamba mapafu kadhaa kama hayo, ambayo yanaweza kubadilishwa kwa kutegemea majira, yangekuwa kama mfumo wa jiji wa kupumua na wa kusafisha hewa, ukifyonza kaboni dioksidi na kutoa oksijeni.
Maonyesho hayo yalikuwa pia na usafiri uliotia ndani mabasi ya kipekee yaliyoendeshwa kwa umeme. Yalipowasafirisha watu, magari hayo yalitoa maji tu badala ya kutoa moshi. Kitu kingine kilichowafurahisha watu wanaopenda teknolojia ni treni ya kwanza ya abiria iitwayo Linimo, iliyoendeshwa kwa sumaku. Kwa kutumia sumaku zenye nguvu, Linimo iliendeshwa kwa unyamavu na utaratibu bila kugusa reli ikiacha mwanya wa milimita nane kati ya treni na reli. Pia kulikuwa na tramu zilizoendeshwa kwa betri, teksi za baiskeli, na mabasi ya aina fulani ambayo yangesonga bila kuongozwa au kuendeshwa na dereva. Magari hayo ambayo huenda yakatumiwa wakati ujao yalitumia gesi za asili, ambazo ni safi kuliko mafuta ya kawaida.
Hebu wazia kubadili takataka kama vile mabaki ya chakula, kuwa umeme na mbolea. Ili kufanya hivyo, kituo fulani cha kuzalisha nishati katika eneo la maonyesho hayo kilitumia mbinu ya kuchachisha methani. Badala ya kuchoma takataka, kituo hicho kilichachisha takataka hizo na kuzibadili kuwa gesi ya methani, ambayo ilitumiwa kutokeza hidrojeni. Vifaa vingine vilichanganya hidrojeni hiyo na oksijeni na kutokeza umeme. Uchafu uliotokezwa ni maji na mbolea pekee. Kituo hicho kilitumia takataka zote zilizotupwa katika maonyesho hayo kuzalisha umeme uliotumiwa katika mabanda mbalimbali.
Utafiti mwingi unafanywa katika taaluma ya kutokeza roboti, kukiwa na lengo la kutokeza mashine nyepesi zinazoweza kutumika kama watumishi wa wanadamu. Ili kuonyesha maendeleo ya teknolojia ya roboti, roboti saba zilitembea hadi katikati ya jukwaa la banda moja na kuwavutia watu kwa kupiga muziki. Roboti kadhaa zilipiga kwa ustadi vyombo vya kupuliza, huku moja ikipiga ngoma. “Zilisonga kwa utaratibu na wepesi hivi kwamba mtu angefikiri ni wanadamu,” akasema mtazamaji mmoja.
Uvumbuzi mwingine wa kiteknolojia wa hali ya juu ni plastiki zinazoweza kuoza zilizotengenezwa kwa wanga wa mahindi na bidhaa nyingine za aina hiyo, na pia mapovu madogo sana ya gesi yenye kipenyo cha chini ya nanomita 200. Unywele wa mwanadamu una kipenyo cha nanomita 50,000 hivi. Kwa kawaida, mapovu madogo hivyo hutoweka haraka. Lakini watafiti huko Japani wamevumbua teknolojia ya kutokeza mapovu madogo sana ya oksijeni, ambayo huboresha “uwezo wa samaki na samaki-gamba kujipatanisha na mabadiliko katika mazingira.” Hata samaki wa maji baridi na maji ya chumvi waliishi pamoja katika kidimbwi kilichojazwa mapovu madogo sana ya oksijeni! Watafiti wanatumaini kwamba watapata njia za kutumia teknolojia hiyo mpya katika ufugaji wa samaki, ukulima, na katika mambo mengine.
Je, Ulimwengu Unasikiliza?
Ingawa maonyesho hayo yalikazia umuhimu wa kusikiliza “hekima ya vitu vya asili,” ulimwengu kwa ujumla haujafanya hivyo. Maoni ya watu wanaotetea “hekima ya vitu vya asili” yanakandamizwa kwa sababu ya watu kupuuza mambo, kuwa na pupa, na ufisadi. Kwa sababu hiyo, dunia imekuwa “Sayari Iliyojeruhiwa,” kama kichwa cha banda moja kilivyosema. Lakini hata watu wenye nia nzuri wafanye nini, hawawezi kuwapa wanadamu masuluhisho ya kudumu kwa matatizo yao na kuharibiwa kwa mazingira. Kulingana na Biblia, ujuzi na hekima ya mwanadamu haiwezi kusuluhisha matatizo hayo. (Yeremia 10:23) Hata hivyo, bado kuna matumaini. Kwa nini tunasema hivyo?
Biblia inatuambia kwamba Chanzo kikuu zaidi cha hekima, yaani Muumba wetu, ataingilia mambo ya dunia kabla wanadamu hawajaharibu kazi yake. (Ufunuo 4:11; 11:18) “Bado muda kidogo tu, na mtu mwovu hatakuwako tena . . . Bali wapole wataimiliki dunia, nao watapata furaha yao tele katika wingi wa amani,” inasema Zaburi 37:10, 11. Kwa kweli, ni jambo la hekima kusikiliza vitu vya asili, lakini ni jambo la hekima zaidi kumsikiliza Muumba kwa kusoma na kufuata Neno lake, Biblia Takatifu. (2 Timotheo 3:16) Wote wanaofanya hivyo wataona sayari yetu iliyojeruhiwa ikiponywa kabisa na kufanywa kuwa paradiso.—Luka 23:43.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kidimbwi chenye mapovu madogo sana
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mabasi yasiyoendeshwa na madereva
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Kifaa kilichoweza kuonyesha picha kwa nyuzi 360
[Picha katika ukurasa wa 25]
“Bio-Lung” iliyofanyizwa kwa mimea 200,000 kutoka spishi 200
[Picha katika ukurasa wa 25]
Roboti ziliwatumbuiza watazamaji kwa muziki