Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 11/12 kur. 16-17
  • “Common Loon”—Ndege Mwenye Milio Yenye Kustajabisha

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Common Loon”—Ndege Mwenye Milio Yenye Kustajabisha
  • Amkeni!—2012
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Milio ya Aina Mbalimbali
  • Anavutia, Ni Stadi, na Mzembe
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2012
  • Cock-of-the-Rock—Mrembo wa Msitu wa Amazon
    Amkeni!—1998
  • Kuwatazama Ndege—Je, Kwavutia Kila Mtu?
    Amkeni!—1998
  • Jinsi Wanyama Wanavyowalisha na Kuwatunza Watoto Wao
    Amkeni!—2005
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2012
g 11/12 kur. 16-17
[Picha katika ukurasa wa 16 na 17]

“Common Loon”​—Ndege Mwenye Milio Yenye Kustajabisha

RAHISI kusahau kilio chenye kuogopesha cha ndege anayeitwa common loon. Kilio hicho kinachoashiria upweke wa nyikani, kinaweza kusikika katika maeneo ya maziwa ya maji baridi nchini Kanada, barani Ulaya, na hata kaskazini mwa nchi ya Marekani.

Ndege huyo maridadi wa majini, ni alama ya nembo ya jimbo la Minnesota, nchini Marekani, na pia mchoro wa ndege huyo huonekana kwenye sarafu ya dola ya Kanada. Ndege huyo ni mhamaji, na kwa kawaida wakati wa majira ya baridi kali hupatikana maeneo ya pwani kusini mwa Marekani. Kwa nini anasemwa kuwa ndege mwenye milio yenye kustaajabisha?

Milio ya Aina Mbalimbali

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ndege anayeitwa “common loon” akitoa sauti

Ndege huyo anayeitwa loon ana milio ya pekee. Kilio chake kinachofanana na sauti ya kuomboleza, husikika pindi za jioni au usiku na kinaweza kusikiwa umbali wa kilomita kadhaa. Ana kilio kingine kinachofanana na kile cha bundi, ambacho yeye hutumia kuwaita vifaranga wake au wenzake kwenye ziwa. Ana kilio kingine kinachofanana na sauti ya vigelegele ambacho yeye hutumia kama king’ora. Kilio hicho ambacho kimefafanuliwa kuwa “kicheko cha kichaa,” ndiyo sauti pekee ambayo ndege huyu hutoa anaporuka.

Kilio kingine aina ya yodel hutolewa na ndege wa kiume pekee na “inaonekana kwamba yeye hutoa kilio hicho anapolinda maeneo yake,” linasema jarida BirdWatch Canada. “Kila ndege wa kiume ana aina tofauti za kilio hicho,” na “kadiri ndege huyo alivyo mzito ndivyo sauti yake inavyozidi kuwa nzito.” Zaidi ya hayo, ndege wa kiume “anapohama, yeye hubadili pia yodel yake,” na “kwa kadiri anavyoweza ndege huyo hufanya yodel yake iwe tofauti kabisa na ya yule wa awali,” jarida hilo linasema.

Anavutia, Ni Stadi, na Mzembe

Ndege huyo ana kichwa chenye rangi nyeusi iliyochangamana na kijani, na macho mekundu na mdomo mweusi uliochongoka. Manyoya yake hubadilika kwa kutegemea msimu.

Kwa kuwa ndege hao wana miguu mikubwa yenye utando, wao ni wawindaji stadi, wana uwezo mkubwa wa kuogelea, nao ni wapiga-mbizi stadi. Kwa kweli, wanaweza kuzama chini ya maji kufikia kina cha mita 60, na mara kwa mara wanaweza kubaki ndani ya maji kwa dakika kadhaa!

Hata hivyo, ndege huyo hupaa na kutua kwa njia ya ajabu! Kwa sababu ya uzito wake, ndege huyo anahitaji nafasi kubwa ya kumwezesha kupaa, na nyakati nyingine anaweza kukimbia akipigapiga mabawa yake kwa umbali wa mita nyingi ili tu apate msukumo wa kumwezesha kupaa. Kwa sababu hiyo, ndege hao hupendelea zaidi maeneo yenye maji mengi. Anapotua, yeye huja kwa kasi sana huku miguu yake ikiwa imenyooshwa kuelekea nyuma kana kwamba imeshindwa kufanya kazi. Kwa sababu hiyo, yeye hupiga maji kwa tumbo lake na kuteleza mpaka atakaposimama kabisa.

Licha ya kwamba miguu yake inafaa sana katika kuogelea, inamletea shida anapojaribu kutembea​—au hata kusimama—​kwa kuwa iko karibu na sehemu ya nyuma ya mwili. Kwa hiyo, wao hujenga viota vyao karibu na maji ili iwe rahisi kwao kuingia ndani ya maji.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kifaranga kikiwa kinapumzika juu ya mgongo wa mama yake

Ndege wa kiume na wa kike husaidiana kuatamia mayai (kwa kawaida huwa mawili), ambayo huwa na rangi nzito ya kijani kibichi na madoa meusi. Mayai hayo huanguliwa baada ya wastani wa siku 29. Vifaranga hao wanapokuwa na umri wa siku mbili tu, wanaweza kuogelea au hata kupiga mbizi kidogo. Wanapohitaji kupumzika, wanapanda juu ya mgongo wa mzazi wao. Baada ya miezi miwili au mitatu, wakati ndege hao wadogo wanapokuwa na uwezo wa kupaa, wao huwaacha wazazi.

Adui wakubwa wa ndege huyo ni tai, shakwe, mnyama anayeitwa raccoon, na mwanadamu—ambaye ndiye adui hatari zaidi. Ndege huyo hufa kutokana na sumu ya vyuma vya risasi vinavyofungwa kwenye nyavu na mafuta yanayomwagika majini. Mvua ya asidi humwaga kemikali na kuchafua maji na hivyo kupunguza idadi ya samaki ambacho ndicho chakula kikuu cha ndege hao. Mawimbi yanayotokezwa na boti zinazoenda kwa kasi huharibu viota vyao. Shughuli zinazofanywa na binadamu kwenye ufuo huchangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya ndege hao wahame kutoka kwenye maeneo yao ya kutagia mayai.

Licha ya hatari hizo zote, bado kuna idadi kubwa ya ndege hao. Kwa hiyo, ndege huyo maridadi aliye na milio ya pekee ataendelea kuwavutia watu wote wanaopenda ndege kwa miaka mingi ijayo.

MAMBO HAKIKA KUHUSU “LOON”

Urefu: Karibu mita moja kutoka kwenye ncha ya mdomo hadi kwenye mguu ulionyooshwa

Upana kutoka bawa hadi bawa: Sentimita 140 hivi

Uzito: Kwa wastani ana uzito wa kilogramu 4 lakini anaweza kufikia kilogramu 6.3

Muundo wa mfupa: Wana mifupa migumu (tofauti na mifupa ya ndege wengine ambayo huwa na uwazi kwa ndani), ambayo huongeza uzito wao lakini huwasaidia kupiga mbizi

Mwendo anaporuka: Anaweza kusonga kwa kasi ya kilomita 120 kwa saa wakati wa kuhama

Chakula: Anapendelea zaidi kula samaki lakini pia hula kambamto, vyura, ruba, salamanda, uduvi, konokono, na viumbe wengine wanaoishi kwenye maji

Page 16, loon landing: Spectrumphotofile; page 17, loon chick: © All Canada Photos/SuperStock; loon vocalizing: © Roberta Olenick/age fotostock

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki