Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 6/14 kur. 10-11
  • Joseph Priestley

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Joseph Priestley
  • Amkeni!—2014
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • ALITAFUTA UKWELI KATIKA SAYANSI
  • ALITAFUTA UKWELI KATIKA DINI
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2014
  • 1914 Ni Historia Tu? Au Una Matokeo Juu Yako?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
  • Waweza Kuitumaini Sayansi Kadiri Gani?
    Amkeni!—1998
  • Kutoka Maumivu Makali Hadi Unusukaputi
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2014
g 6/14 kur. 10-11
Sanamu ya Joseph Priestley

TUNAYOJIFUNZA KUTOKANA NA HISTORIA

Joseph Priestley

“Ujuzi wake mwingi, msisimko, matendo, na huruma; udadisi wake mwingi kuhusiana na viumbe, maadili, au jamii; mchango wake kwa sayansi, theolojia, falsafa, na siasa; jinsi alivyojihusisha na Mapinduzi [ya Ufaransa], na mateso ya kusikitisha ambayo hakustahili, huenda hayo yote yanamfanya awe shujaa wa karne ya 18.”—Frederic Harrison, mwanafalsafa.

NI JAMBO gani muhimu ambalo Joseph Priestley alitimiza? Mambo aliyovumbua na kuandika yamechochea maoni ya watu kuhusu serikali, jinsi Mungu alivyo, na hata kuhusu hewa tunayopumua.

Alipoandika kuhusu sayansi au dini, Priestley alikataa nadharia na mapokeo na akakubali mambo yaliyothibitishwa na ya kweli. Alifanyaje hivyo?

ALITAFUTA UKWELI KATIKA SAYANSI

Baada ya kukutana na mwanasayansi Mmarekani Benjamin Franklin, mwaka wa 1765, Joseph Priestley—ambaye alijishughulisha na sayansi ili kujifurahisha tu—alianza kuchunguza umeme. Mwaka uliofuata, wanasayansi wenzake walivutiwa sana na uvumbuzi wake hivi kwamba wakamteua ajiunge na shirika maarufu la Royal Society huko London.

Kisha Priestley akaanza kushughulika na kemia. Baada ya muda mfupi aligundua gesi kadhaa mpya kutia ndani amonia na nitrasi oksidi. Hata alichanganya maji na kaboni dioksidi na hivyo kuvumbua maji yenye kaboni

Mwaka wa 1774, alipokuwa akifanya utafiti kusini mwa Uingereza, Priestley alivumbua gesi ya kipekee iliyofanya mishumaa iangaze zaidi. Baadaye, aliweka mililita 60 za gesi hiyo katika glasi na akamtia panya humo. Panya alikaa humo muda mrefu mara mbili zaidi ya jinsi alivyokaa katika glasi yenye hewa ya kawaida! Priestley mwenyewe alipumua hewa hiyo na akasema kwamba “ilikuwa rahisi zaidi kupumua.”

Joseph Priestley alikuwa amevumbua oksijeni.a Hata hivyo, aliita gesi hiyo hewa isiyo na flojistoni akidhania kwamba alikuwa amevumbua hewa ya kawaida isiyo na flojistoni, kitu cha kuwaziwa ambacho ilidhaniwa kilizuia vitu kuchomeka. Mkataa aliofikia Priestley haukuwa sahihi, hata hivyo wengi bado wanaona uvumbuzi huo kuwa “jambo muhimu zaidi alilotimiza maishani.”

ALITAFUTA UKWELI KATIKA DINI

Kama Priestley alivyoamini kwamba nadharia huzuia ukweli wa kisayansi, pia aliamini kuwa mapokeo na itikadi huzuia ukweli wa kidini. Jambo la kushangaza ni kwamba, ingawa alitafuta ujuzi wa Biblia kwa miaka mingi, Priestley aliamini mambo yaliyopingana na mafundisho ya kweli ya Biblia. Kwa mfano, pindi moja hakuamini kwamba Biblia iliongozwa kimuujiza na roho ya Mungu. Pia, alikataa fundisho la Biblia kwamba Yesu aliishi mbinguni kabla ya kuja duniani.

“Ikiwa sayansi ndiyo njia ya kutafuta ukweli, basi Priestley alikuwa mwanasayansi wa kweli.”—Katherine Cullen, mwanabiolojia

Kwa upande mwingine, Priestley alipinga mafundisho ya uwongo ya kidini yaliyokubaliwa siku hizo, na ambayo bado yanafuatwa katika dini nyingi. Aliandika kwamba ukweli ambao Yesu aliwafundisha wafuasi wake ulipotoshwa na uwongo—kutia ndani fundisho la uwongo la Utatu, fundisho lenye kosa kwamba nafsi haiwezi kufa, na ibada ya sanamu, ambayo kwa kweli imeshutumiwa katika Biblia.

Mawazo ya kidini ya Priestley na pia msimamo wake wa kuunga mkono mapinduzi ya Ufaransa na Marekani kuliwakasirisha Waingereza wenzake. Mwaka wa 1791, umati wenye ghasia uliharibu nyumba na maabara yake na hatimaye Priestley akakimbilia Marekani. Ingawa Joseph Priestley anakumbukwa hasa kwa sababu ya uvumbuzi wake wa kisayansi, aliamini kwamba kujifunza kumhusu Mungu na kusudi lake ndilo jambo lenye “kuheshimika na muhimu zaidi.”

a Mapema, mwanakemia kutoka Sweden Carl Scheele alikuwa amevumbua oksijeni lakini hakuchapisha uvumbuzi wake. Baadaye, mwanakemia Mfaransa Antoine-Laurent Lavoisier aliita gesi hiyo oksijeni.

TAARIFA FUPI

  • Joseph Priestley alizaliwa mwaka wa 1733 karibu na Leeds, Uingereza.

  • Akiwa mwanasayansi, alivumbua gesi kadhaa.

  • Akiwa mtaalamu wa kisiasa, alitetea uhuru wa kusema, ibada, na elimu.

  • Akiwa kasisi, alipinga mafundisho ya kanisa, kutia ndani Utatu na kutokufa kwa nafsi.

  • Mwaka wa 1794, Priestley alikimbilia Marekani ambako alikufa miaka kumi hivi baadaye.

UKWELI AU MAPOKEO?

Wafanya ghasia wakiharibu nyumba na maabara ya Priestley

Mwaka wa 1791 umati wenye ghasia uliharibu nyumba na maabara ya Priestley

Priestley aligundua kwamba mafundisho mengi ya kidini yanapingana na mafundisho ya Biblia. Chunguza mifano ifuatayo:

  • Mapokeo: Yesu ni sawa na Mungu.

    Ukweli wa Biblia: Kristo Yesu alisema hivi: “Baba ni mkuu kuliko mimi.”—Yohana 14:28.

  • Mapokeo: Nafsi haiwezi kufa.

    Ukweli wa Biblia: “Nafsi inayotenda dhambi—hiyo yenyewe itakufa.”—Ezekieli 18:4.

  • Mapokeo: Sanamu zinaweza kutumiwa kumwabudu Mungu.

    Ukweli wa Biblia: “Mimi ni Yehova. Hilo ni jina langu; nami sitampa mwingine yeyote utukufu wangu mwenyewe, wala sitazipa sanamu za kuchongwa sifa yangu.”​—Isaya 42:8.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki