Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 6/15 kur. 10-11
  • Galileo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Galileo
  • Amkeni!—2015
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • SAYANSI NA DINI
  • “Hata Hivyo Imo Katika Mwendo!”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Mgogoro Kati ya Galileo na Kanisa
    Amkeni!—2003
  • Sayansi na Dini Mwanzo wa Ubishi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
  • Kitabu Kinachowakilishwa Vibaya
    Kitabu kwa Ajili ya Watu Wote
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2015
g 6/15 kur. 10-11
Galileo

TUNAYOJIFUNZA KUTOKANA NA HISTORIA

Galileo

Kati ya karne ya 14 na 16, wanasayansi na wanafalsafa wa Ulaya walianza kuelewa ulimwengu katika njia ambayo ilipingana na mafundisho ya Kanisa Katoliki. Mtu mmoja aliyechunguza upya mbingu ni Galileo Galilei.

KABLA ya kuwapo kwa Galileo, watu wengi waliamini kwamba jua, sayari, na nyota zilizunguka dunia. Imani hiyo ilikuwa miongoni mwa mafundisho rasmi ya Kanisa Katoliki.

Akitumia darubini yake, Galileo alipata ushahidi unaopingana na mafundisho ya kisayansi yaliyokubaliwa na wengi. Kwa mfano, alipotazama madoa meusi yaliyoonekana katika uso wa jua yakihama, alitambua kwamba jua linazunguka katika mhimili. Utafiti kama huo umemsaidia mwanadamu kuongeza ujuzi wake kuhusu ulimwengu kwa kiasi kikubwa, ijapokuwa uchunguzi huo ulikuwa chanzo cha ugomvi kati ya Galileo na Kanisa Katoliki.

SAYANSI NA DINI

Galileo akieleza kuhusu utafiti wake

Miaka mingi mapema, mtaalamu wa nyota kutoka Poland, Nicolaus Copernicus, alianzisha nadharia ya kwamba dunia inazunguka jua. Galileo alichunguza utafiti wa Copernicus kuhusu mwendo wa vitu vilivyo angani na kukusanya ushahidi akitegemea nadharia hiyo. Mwanzoni, Galileo alisita kusema kuhusu utafiti wake kwa sababu ya kuhofu kwamba atadhihakiwa na kupuuzwa. Akiwa ameshindwa kuzuia msisimuko wake kutokana na yale aliyoona kupitia darubini yake, Galileo alianza kusema kuhusu utafiti wake. Baadhi ya wanasayansi waliona utafiti wake kuwa chanzo cha ubishi, na baada ya muda mfupi, makasisi walianza kutumia majukwaa ya kanisa kumpinga Galileo.

Katika mwaka wa 1616, Kadinali Bellarmine, “mwanatheolojia maarufu wakati huo,” alimweleza Galileo kuhusu amri mpya iliyowekwa na Kanisa Katoliki dhidi ya mawazo ya Copernicus. Alimsisitiza sana Galileo kukubaliana na amri hiyo, na kwa miaka mingi baadaye, Galileo hakupinga waziwazi kwamba dunia inazunguka jua.

Katika mwaka 1623, Papa Urban wa Nane, aliyekuwa rafiki wa Galileo, alianza kutawala. Hivyo, katika mwaka wa 1624, Galileo alimwomba papa aondoe amri iliyowekwa mwaka 1616. Badala ya kufanya hivyo, Urban alimsihi Galileo kufafanua nadharia zinazopingana za Copernicus na Aristotle katika njia ambayo haitapendelea yeyote kati ya hizo.

Hivyo, Galileo akaandika kitabu chenye kichwa Dialogue on the Great World Systems. Ingawa papa alimwagiza Galileo kutopendelea upande wowote, kitabu hicho kilipendelea mawazo ya Copernicus. Baada ya muda mfupi tu, maadui wa Galileo walianza kudai kwamba kitabu chake kinamdhihaki papa. Akiwa ameshitakiwa kuwa mzushi wa kidini na kutishiwa kuteswa, Galileo alilazimishwa kukataa mafundisho ya Corpenicus. Katika mwaka wa 1633, Baraza la Kikatoliki la Kuhukumu Wazushi, lilimhukumu kifungo cha kudumu cha nyumbani, na kupiga marufuku vitabu vyake. Galileo alikufa akiwa nyumbani kwake katika mji wa Arcetri, karibu na Florence, Januari 8, 1642.

Papa John Paul wa Pili, alikubali kwamba Kanisa Katoliki lilimhukumu kimakosa Galileo

Kwa mamia ya miaka, baadhi ya utafiti wa Galileo uliendelea kuwa katika orodha ya vitabu ambavyo Wakatoliki hawakuruhusiwa kusoma. Hata hivyo, katika mwaka wa 1979, kanisa hilo lilichunguza tena hatua iliyochukuliwa na Baraza la Kikatoliki la Kuhukumu Wazushi miaka 300 iliyopita. Mwishowe, katika mwaka wa 1992, Papa John Paul wa Pili, alikubali kwamba Kanisa Katoliki lilimhukumu kimakosa Galileo.

TAARIFA FUPI

  • Galileo Galilei alizaliwa mwaka wa 1564, katika Pisa, Italia, jiji maarufu kutokana na kuwa na mnara unaoegama. Alifundisha katika Chuo Kikuu cha Padua na baadaye akaishi na kufanya kazi katika jiji la Florence.

  • Ingawa Galileo hakuvumbua darubini, aliboresha sana uwezo wake wa kukuza na hivyo kufanya iwe yenye kufaa hata zaidi.

  • Kwa sababu ya maoni yake kuhusu ulimwengu, Galileo aliitwa mara mbili mbele ya Baraza la Kikatoliki la Kuhukumu Wazushi, ambalo lilikuwa na jukumu la kutoa adhabu kali kwa wale ambao waliacha kufuata mafundisho ya kanisa.

Je, Baraza la Kikatoliki la Kuhukumu Wazushi Lilimtesa Galileo?

Baadhi ya wanahistoria wamesema kwamba huenda Baraza la Kikatoliki la Kuhukumu Wazushi lilimtesa kimwili Galileo. Nakala ya hukumu aliyopewa inasema kwamba ili kujua nia ya Galileo, ilikuwa lazima kufanya “mahoji makali.” Usemi huo ambao hutumiwa katika mambo ya kihukumu mara nyingi humaanisha “kutesa,” huenda ukamaanisha “maneno ya vitisho au kutesa kimwili.”

Wataalamu husema kwamba kuna hatua na viwango vya mateso. Huenda ikatia ndani kumwonyesha anayeteswa vifaa vinavyotumiwa kutesa, kumfunga, au hata kumsababishia maumivu makali kwa kuendelea. Aina ya “mahoji makali,” aliyofanyiwa Galileo haijulikani mpaka leo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki