Yohana
10 “Kwa kweli kabisa nawaambia nyinyi, Yeye asiyeingia ndani ya zizi la kondoo kupitia mlango bali hupanda juu mahali pengine, huyo ni mwizi na mporaji. 2 Lakini yeye aingiaye kupitia mlango ni mchungaji wa kondoo. 3 Mtunza-mlango humfungulia huyu, nao kondoo husikiliza sauti yake, naye huita kondoo wake mwenyewe kwa jina na huwaongoza watoke nje. 4 Wakati amewatoa nje wote walio wake mwenyewe, yeye huenda mbele yao, nao kondoo humfuata, kwa sababu wajua sauti yake. 5 Mgeni hawatamfuata kwa vyovyote bali watamkimbia, kwa sababu hawaijui sauti ya wageni.” 6 Yesu aliwaambia ulinganisho huu; lakini hawakujua mambo aliyokuwa akiwaambia yalimaanisha nini.
7 Kwa hiyo Yesu akasema tena: “Kwa kweli kabisa mimi nawaambia nyinyi, mimi ndimi mlango wa kondoo. 8 Wote wale ambao wamekuja mahali pangu ni wezi na waporaji; lakini kondoo hawajawasikiliza. 9 Mimi ndimi mlango; yeyote yule aingiaye kupitia mimi ataokolewa, naye ataingia na kutoka nje na kupata malisho. 10 Mwizi haji isipokuwa iwe ni kuiba na kuua kikatili na kuharibu. Mimi nimekuja ili wapate kuwa na uhai na wapate kuwa nao kwa wingi. 11 Mimi ndiye mchungaji mwema; mchungaji mwema hutoa nafsi yake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtu aliyeajiriwa, ambaye si mchungaji na ambaye kondoo si wake mwenyewe, hutazama mbwa-mwitu akija na huacha kondoo na hukimbia—na mbwa-mwitu huwanyakua na huwatawanya— 13 kwa sababu yeye ni mtu aliyeajiriwa na hajali kondoo. 14 Mimi ndiye mchungaji mwema, nami najua kondoo wangu na kondoo wangu wanijua mimi, 15 kama vile Baba anijuavyo mimi nami namjua Baba; nami naisalimisha nafsi yangu kwa ajili ya kondoo.
16 “Na nina kondoo wengine, ambao si wa zizi hili; hao pia lazima niwalete, nao watasikiliza sauti yangu, nao watakuwa kundi moja, mchungaji mmoja. 17 Hiyo ndiyo sababu Baba hunipenda, kwa sababu mimi naisalimisha nafsi yangu, ili nipate kuipokea tena. 18 Hakuna mtu ambaye ameiondoa kwangu, bali mimi naisalimisha kwa uanzisho wangu mwenyewe. Nina mamlaka ya kuisalimisha, nami nina mamlaka ya kuipokea tena. Amri kuhusu hili niliipokea kutoka kwa Baba yangu.”
19 Tena mgawanyiko ukatokea miongoni mwa Wayahudi kwa sababu ya maneno haya. 20 Wengi wao walikuwa wakisema: “Yeye ana roho mwovu na ana kichaa. Kwa nini mwamsikiliza?” 21 Wengine wakawa wakisema: “Hizi si semi za mtu mwenye roho mwovu. Roho mwovu hawezi kufungua macho ya vipofu, je, aweza?”
22 Wakati huo msherehekeo wa wakfu ulitukia katika Yerusalemu. Ulikuwa wakati wa majira ya baridi kali, 23 na Yesu alikuwa akitembea katika hekalu katika safu ya nguzo ya Solomoni. 24 Kwa hiyo Wayahudi wakamzunguka na kuanza kumwambia: “Ni kwa muda gani utaweka nafsi zetu katika hali ya kukosa uhakika? Ikiwa wewe ndiwe Kristo, tuambie kwa kusema waziwazi.” 25 Yesu akawajibu: “Mimi niliwaambia, na bado hamwamini. Kazi ninazofanya katika jina la Baba yangu, hizi zatoa ushahidi juu yangu. 26 Lakini hamwamini, kwa sababu nyinyi si miongoni mwa kondoo wangu. 27 Kondoo wangu husikiliza sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata mimi. 28 Nami nawapa hawa uhai udumuo milele, na hawataharibiwa kwa vyovyote, na hakuna atakayewanyakua mkononi mwangu. 29 Kile ambacho Baba yangu amenipa ni kitu kikubwa zaidi kuliko vitu vingine vyote, na hakuna awezaye kuwanyakua mkononi mwa Baba. 30 Mimi na Baba ni mmoja.”
31 Kwa mara nyingine tena Wayahudi wakaokota mawe ili wampige kwa mawe. 32 Yesu akawajibu: “Mimi niliwaonyesha kazi nyingi bora kutoka kwa Baba. Ni kwa sababu ya ipi kati ya kazi hizi mnanipiga kwa mawe?” 33 Wayahudi wakamjibu: “Sisi tunakupiga kwa mawe, si kwa sababu ya kazi bora, bali kwa sababu ya kukufuru, naam, kwa sababu wewe, ijapokuwa wewe ni binadamu, wajifanya mwenyewe kuwa mungu.” 34 Yesu akawajibu: “Je, haikuandikwa katika Sheria yenu, ‘Mimi nilisema: “Nyinyi ni miungu”’? 35 Ikiwa yeye aliwaita ‘miungu’ wale ambao dhidi yao neno la Mungu lilikuja, na bado Andiko haliwezi kutanguka, 36 je, mwaniambia mimi ambaye Baba alitakasa na kutuma niingie ulimwenguni, ‘Wewe wakufuru,’ kwa sababu nilisema, Mimi ni Mwana wa Mungu? 37 Ikiwa mimi sifanyi kazi za Baba, msiniamini. 38 Lakini ikiwa ninazifanya, hata ingawa hamniamini mimi, aminini hizi kazi, ili mpate kuja kujua na mpate kuendelea mkiwa mnajua kwamba Baba yuko katika muungano na mimi nami katika muungano na Baba.” 39 Kwa hiyo wakajaribu tena kumkamata; lakini akatoka kwenye mfikio wao.
40 Kwa hiyo akaenda tena ng’ambo ya Yordani hadi mahali ambako Yohana alikuwa akibatizia hapo kwanza, naye akakaa huko. 41 Na watu wengi wakaja kwake, nao wakaanza kusema: “Yohana, kwa kweli, hakufanya hata ishara moja, lakini mambo mengi ambayo Yohana alisema juu ya mtu huyu yote yalikuwa kweli.” 42 Na wengi wakaweka imani katika yeye huko.