Yohana
9 Basi alipokuwa akipita aliona mtu aliye kipofu tangu kuzaliwa. 2 Na wanafunzi wake wakamuuliza: “Rabi, ni nani aliyefanya dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hivi kwamba akazaliwa kipofu?” 3 Yesu akajibu: “Mtu huyu hakufanya dhambi wala wazazi wake, bali ilikuwa ili kazi za Mungu zipate kufanywa dhahiri katika kisa chake. 4 Lazima sisi tuzifanye kazi za aliyenituma wakati ni mchana; usiku unakuja wakati hakuna mtu awezaye kufanya kazi. 5 Maadamu nimo ulimwenguni, mimi ndiyo nuru ya ulimwengu.” 6 Baada ya kusema mambo haya, alitema mate chini akafanya udongo wa mfinyanzi kwa hayo mate, akaweka udongo wake wa mfinyanzi juu ya macho ya mtu huyo 7 na kumwambia: “Nenda kajioshe katika dimbwi la Siloamu” (linalotafsiriwa ‘Aliyetumwa’). Na kwa hiyo akaenda na kujiosha, akarudi akiona.
8 Kwa hiyo majirani na wale ambao hapo zamani walikuwa na kawaida ya kumwona akiwa mwombaji wakaanza kusema: “Huyu ndiye mtu ambaye alikuwa na kawaida ya kuketi na kuombaomba, sivyo?” 9 Baadhi yao wakawa wakisema: “Huyu ndiye.” Wengine wakawa wakisema: “Sivyo hata kidogo, lakini yuko kama yeye.” Huyo mtu akawa akisema: “Mimi ndiye.” 10 Kwa sababu hiyo wakaanza kumwambia: “Basi, macho yako yalifunguliwaje?” 11 Yeye akajibu: “Mtu aitwaye Yesu alifanya udongo wa mfinyanzi akaupaka juu ya macho yangu na kuniambia, ‘Nenda hadi Siloamu ukajioshe.’ Kwa hiyo nikaenda nikajiosha na kupata kuona.” 12 Ndipo wakamwambia: “Yuko wapi mtu huyo?” Akasema: “Mimi sijui.”
13 Wakamwongoza mtu mwenyewe aliyekuwa kipofu wakati mmoja kwa Mafarisayo. 14 Ikatukia kwamba ilikuwa Sabato siku ambayo Yesu aliufanya udongo wa mfinyanzi na kuyafungua macho yake. 15 Kwa hiyo, wakati huo Mafarisayo pia wakazidi kumuuliza jinsi alivyopata kuona. Akawaambia: “Yeye aliweka udongo wa mfinyanzi juu ya macho yangu, nami nikajiosha na ninaona.” 16 Basi baadhi ya Mafarisayo wakaanza kusema: “Huyu si mtu atokaye kwa Mungu, kwa sababu haishiki Sabato.” Wengine wakaanza kusema: “Mtu aliye mtenda-dhambi awezaje kufanya ishara za namna hiyo?” Basi kukawa na mgawanyiko miongoni mwao. 17 Kwa sababu hiyo wakamwambia tena huyo mtu aliye kipofu: “Wewe wasema nini juu yake, kwa kuwa alifungua macho yako?” Huyo mtu akasema: “Yeye ni nabii.”
18 Hata hivyo, Wayahudi hawakuamini kuhusu yeye kwamba alikuwa amekuwa kipofu na alikuwa amepata kuona, mpaka walipowaita wazazi wa mtu aliyepata kuona. 19 Nao wakawauliza: “Je, huyu ni mwana wenu ambaye mwasema alizaliwa kipofu? Basi, ni jinsi gani aona sasa?” 20 Ndipo kwa kujibu wazazi wake wakasema: “Sisi twajua kwamba huyu ni mwana wetu na kwamba alizaliwa kipofu. 21 Lakini jinsi aona sasa hatujui, au nani aliyemfungua macho yake sisi hatujui. Muulizeni yeye. Ana umri wa kutosha. Lazima ajisemee mwenyewe.” 22 Wazazi wake walisema mambo hayo kwa sababu walikuwa wakihofu Wayahudi, kwa maana Wayahudi walikuwa tayari wamefikia patano kwamba, ikiwa yeyote angemuungama kuwa ndiye Kristo, angepaswa kufukuzwa katika sinagogi. 23 Hii ndiyo sababu wazazi wake walisema: “Ana umri wa kutosha. Muulizeni yeye.”
24 Kwa hiyo mara ya pili wakamwita mtu aliyekuwa amekuwa kipofu na kumwambia: “Mpe Mungu utukufu; sisi twajua kwamba mtu huyu ni mtenda-dhambi.” 25 Naye akajibu: “Kama yeye ni mtenda-dhambi mimi sijui. Jambo moja mimi najua, kwamba, ingawa nilikuwa kipofu, naona sasa.” 26 Kwa hiyo wakamwambia: “Alifanya nini kwako? Alifunguaje macho yako?” 27 Yeye akawajibu: “Tayari nimewaambia, na bado hamkusikiliza. Kwa nini mwataka kusikia hilo tena? Nyinyi hamtaki kuwa wanafunzi wake pia, je, mwataka?” 28 Ndipo wakamtukana na kusema: “Wewe ni mwanafunzi wa mwanamume huyo, lakini sisi ni wanafunzi wa Musa. 29 Sisi twajua kwamba Mungu amesema na Musa; lakini kwa habari ya mtu huyu, sisi hatujui anakotoka.” 30 Kwa kujibu huyo mtu akawaambia: “Hakika hili ni staajabu, kwamba nyinyi hamjui anakotoka, na bado alifungua macho yangu. 31 Twajua kwamba Mungu hawasikilizi watenda-dhambi, bali ikiwa yeyote ni mwenye kuhofu Mungu na hufanya mapenzi yake, yeye humsikiliza huyu. 32 Kutoka zamani za kale haijasikiwa kamwe kwamba yeyote alifungua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu. 33 Kama mtu huyu hangekuwa atoka kwa Mungu, hangeweza kufanya lolote hata kidogo.” 34 Kwa kujibu wakamwambia: “Wewe ulizaliwa katika dhambi kabisa, na bado je, unatufundisha sisi?” Nao wakamfukuza nje!
35 Yesu akasikia kwamba walikuwa wamemfukuza nje, na, alipompata, akasema: “Je, wewe unaweka imani katika Mwana wa binadamu?” 36 Huyo mtu akajibu: “Na yeye ni nani, bwana, ili nipate kuweka imani katika yeye?” 37 Yesu akamwambia: “Wewe umemwona na, mbali na hilo, yeye anayesema nawe ndiye huyo.” 38 Ndipo akasema: “Mimi naweka imani katika yeye, Bwana.” Naye akamsujudia. 39 Na Yesu akasema: “Kwa ajili ya hukumu hii mimi nilikuja katika ulimwengu huu: ili wale wanaokuwa hawaoni wapate kuona na wale wanaoona wapate kuwa vipofu.” 40 Wale wa Mafarisayo waliokuwa pamoja naye wakasikia mambo haya, nao wakamwambia: “Sisi si vipofu pia, ama ndivyo?” 41 Yesu akawaambia: “Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi. Lakini sasa mwasema, ‘Sisi twaona.’ Dhambi yenu yadumu.”