Yohana
8 Lakini Yesu akaenda kwenye Mlima wa Mizeituni. 2 Hata hivyo, kwenye mapambazuko akajitokeza mwenyewe tena hekaluni, na watu wote wakaanza kuja kwake, naye akaketi na kuanza kuwafundisha. 3 Basi waandishi na Mafarisayo wakaleta mwanamke aliyefumaniwa kwenye uzinzi, na, baada ya kumsimamisha katikati yao, 4 wakamwambia: “Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa katika tendo la kufanya uzinzi. 5 Katika Sheria Musa aliagiza kwamba tuwapige kwa mawe wanawake wa namna hii. Kwa kweli, wewe wasema nini?” 6 Bila shaka, walikuwa wakisema hilo ili kumtia kwenye jaribu, kusudi wawe na jambo fulani la kumshtakia. Lakini Yesu akainama chini akaanza kuandika kwa kidole chake katika ardhi. 7 Walipodumu kumuuliza, alijinyoosha wima na kuwaambia: “Acheni yule kati yenu asiye na dhambi awe wa kwanza kumtupia jiwe.” 8 Na akiinama tena akafuliza kuandika katika ardhi. 9 Lakini wale waliosikia hilo wakaanza kuondoka wakienda, mmoja-mmoja, kuanza na wanaume wazee naye akaachwa peke yake, na mwanamke aliyekuwa katikati yao. 10 Akijinyoosha wima, Yesu akamwambia: “Mwanamke, wao wako wapi? Je, hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia?” 11 Mwanamke akasema: “Hakuna, bwana.” Yesu akasema: “ Wala mimi sikuhukumu kuwa na hatia. Shika njia uende zako; tangu sasa na kuendelea usizoee dhambi tena.”
12 Kwa hiyo Yesu akawaambia tena, akisema: “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Yeye anifuataye mimi hatatembea kwa vyovyote katika giza, bali atakuwa na nuru ya uhai.” 13 Kwa sababu hiyo Mafarisayo wakamwambia: “Wewe watoa ushahidi juu yako mwenyewe; ushahidi wako si kweli.” 14 Kwa kujibu Yesu akawaambia: “Hata ikiwa mimi natoa ushahidi juu yangu mwenyewe, ushahidi wangu ni kweli, kwa sababu najua mahali nilikotoka na mahali ninakoenda. Lakini nyinyi hamjui nilikuja kutoka wapi na ninaenda wapi. 15 Nyinyi mwahukumu kulingana na mwili; mimi sihukumu mtu yeyote hata kidogo. 16 Na bado ikiwa mimi nahukumu, hukumu yangu ni ya kweli, kwa sababu mimi siko peke yangu, bali Baba aliyenituma yuko pamoja nami. 17 Pia, katika Sheria yenu wenyewe imeandikwa, ‘Ushahidi wa watu wawili ni kweli.’ 18 Mimi ni mtu atoaye ushahidi juu yangu mwenyewe, na Baba aliyenituma hutoa ushahidi juu yangu.” 19 Kwa hiyo wakaendelea kumwambia: “Yuko wapi Baba yako?” Yesu akajibu: “Nyinyi hamnijui mimi wala Baba yangu. Kama mngenijua mimi, mngemjua Baba yangu pia.” 20 Semi hizi alizisema mahali pa hazina alipokuwa akifundisha katika hekalu. Lakini hakuna aliyemshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.
21 Kwa sababu hiyo akawaambia tena: “Mimi ninaenda zangu, nanyi mtanitafuta, na bado mtakufa katika dhambi yenu. Mahali ninakoenda hamwezi kuja.” 22 Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kusema: “Hatajiua mwenyewe, ndivyo? Kwa sababu asema, ‘Mahali ninakoenda hamwezi kuja.’” 23 Kwa hiyo akaendelea kuwaambia: “Nyinyi mwatoka kwenye makao ya chini; mimi natoka kwenye makao ya juu. Nyinyi mwatoka katika ulimwengu huu; mimi sitoki katika ulimwengu huu. 24 Kwa hiyo mimi niliwaambia nyinyi, Mtakufa katika dhambi zenu. Kwa maana ikiwa hamwamini kwamba mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu.” 25 Kwa hiyo wakaanza kumwambia: “Wewe ni nani?” Yesu akawaambia: “Kwa nini hata ninasema nanyi? 26 Nina mambo mengi ya kusema kuhusu nyinyi na kutoa hukumu juu yayo. Kwa hakika, yeye aliyenituma ni kweli, na mambo yaleyale niliyosikia kutoka kwake ninayasema ulimwenguni.” 27 Hawakufahamu kwamba alikuwa akiwaambia juu ya Baba. 28 Kwa hiyo Yesu akasema: “Mara mkiisha kumwinua Mwana wa binadamu, ndipo mtakapojua kwamba mimi ndiye, na kwamba sifanyi jambo lolote kwa uanzisho wangu mwenyewe; bali kama vile Baba alivyonifundisha nasema mambo haya. 29 Na yeye aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu mwenyewe, kwa sababu sikuzote mimi hufanya mambo yale yanayompendeza.” 30 Alipokuwa akisema mambo haya, wengi waliweka imani katika yeye.
31 Na kwa hiyo Yesu akaendelea kuwaambia Wayahudi waliokuwa wamemwamini: “Ikiwa nyinyi mwakaa katika neno langu, nyinyi kwa kweli ni wanafunzi wangu, 32 nanyi mtajua kweli, na kweli itawaweka nyinyi huru.” 33 Wakamjibu: “Sisi ni uzao wa Abrahamu nasi hatujapata kamwe kuwa watumwa wa yeyote. Ni jinsi gani wewe wasema, ‘Nyinyi mtakuwa huru’?” 34 Yesu akawajibu: “Kwa kweli kabisa mimi nawaambia, Kila mtendaji wa dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35 Zaidi ya hayo, mtumwa hakai katika watu wa nyumbani milele; mwana hukaa milele. 36 Kwa hiyo Mwana akiwaweka nyinyi huru, mtakuwa huru kikweli. 37 Mimi najua kwamba nyinyi ni uzao wa Abrahamu; lakini mnatafuta sana kuniua, kwa sababu neno langu halifanyi maendeleo miongoni mwenu. 38 Mambo ambayo nimeyaona pamoja na Baba yangu nayasema; na kwa hiyo, nyinyi fanyeni mambo ambayo mmesikia kutoka kwa baba yenu.” 39 Kwa kujibu wakamwambia: “Baba yetu ni Abrahamu.” Yesu akawaambia: “Ikiwa nyinyi ni watoto wa Abrahamu, fanyeni kazi za Abrahamu. 40 Lakini sasa mnatafuta sana kuniua, mtu ambaye amewaambia kweli ambayo nilisikia kutoka kwa Mungu. Abrahamu hakufanya hili. 41 Nyinyi hufanya kazi za baba yenu.” Wakamwambia: “Sisi hatukuzaliwa kutokana na uasherati; tuna Baba mmoja, Mungu.”
42 Yesu akawaambia: “Kama Mungu angekuwa ndiye Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilikuja kutoka kwa Mungu nami nipo hapa. Wala sikuja kwa uanzisho wangu mwenyewe hata kidogo, lakini Huyo alinituma. 43 Ni kwa nini hamjui kile ninachosema? Kwa sababu hamwezi kusikiliza neno langu. 44 Nyinyi mwatoka kwa baba yenu Ibilisi, nanyi mwataka kufanya tamaa za baba yenu. Huyo alikuwa muua-binadamu kikatili wakati alipoanza, naye hakusimama thabiti katika kweli, kwa sababu kweli haimo katika yeye. Wakati asemapo uwongo, yeye husema kulingana na mwelekeo wake mwenyewe, kwa sababu yeye ni mwongo na ndiye baba ya uwongo. 45 Kwa sababu mimi, kwa upande mwingine, nawaambia ile kweli, hamniamini. 46 Ni nani kati yenu anithibitishaye kuwa na hatia ya dhambi? Ikiwa nasema kweli, kwa nini hamniamini? 47 Yeye atokaye kwa Mungu husikiliza semi za Mungu. Hii ndiyo sababu hamsikilizi, kwa sababu nyinyi hamtoki kwa Mungu.”
48 Kwa kujibu, Wayahudi wakamwambia: “Je, sisi hatusemi sawasawa, Wewe ni Msamaria na una roho mwovu?” 49 Yesu akajibu: “Mimi sina roho mwovu, lakini namheshimu Baba yangu, nanyi mwanivunjia heshima. 50 Lakini mimi sitafuti utukufu kwa ajili yangu mwenyewe; kuna Mmoja ambaye anatafuta sana na anahukumu. 51 Kwa kweli kabisa mimi nawaambia, Yeyote akishika neno langu, hataona kifo kamwe hata kidogo.” 52 Wayahudi wakamwambia: “Sasa twajua una roho mwovu. Abrahamu alikufa, pia manabii; lakini wewe wasema, ‘Yeyote akishika neno langu, hataonja kifo kamwe hata kidogo.’ 53 Wewe si mkubwa kuliko Abrahamu baba yetu, ambaye alikufa, ndivyo? Pia, manabii walikufa. Wewe wadai kuwa nani?” 54 Yesu akajibu: “Ikiwa mimi najitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu. Ni Baba yangu ambaye hunitukuza, yeye ambaye nyinyi mwasema ni Mungu wenu; 55 na bado hamjamjua. Lakini mimi namjua. Na ikiwa ningesema simjui ningekuwa mwongo kama nyinyi. Lakini mimi namjua nami nalishika neno lake. 56 Baba yenu Abrahamu alishangilia sana katika tazamio la kuona siku yangu, naye aliiona na kushangilia.” 57 Kwa hiyo Wayahudi wakamwambia: “Wewe hujawa bado na miaka hamsini, na bado umemwona Abrahamu?” 58 Yesu akawaambia: “Kwa kweli kabisa mimi nawaambia, Kabla Abrahamu hajakuja kuwako, mimi nimekuwako.” 59 Kwa hiyo wakaokota mawe wamvurumizie; lakini Yesu akajificha na kwenda kutoka hekaluni.