Yohana
7 Basi baada ya mambo haya Yesu akaendelea kutembea huku na huku katika Galilaya, kwa maana hakutaka kutembea huku na huku katika Yudea, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta sana kumuua. 2 Hata hivyo, msherehekeo wa Wayahudi, msherehekeo wa matabenakulo, ulikuwa karibu. 3 Kwa hiyo ndugu zake wakamwambia: “Pita mbele uvuke kutoka hapa uende kuingia Yudea, ili wanafunzi wako pia wapate kuona kazi ufanyazo. 4 Kwa maana hakuna mtu afanyaye jambo lolote katika siri huku yeye mwenyewe akitafuta sana kujulikana hadharani. Ikiwa wafanya mambo hayo, jidhihirishe mwenyewe kwa ulimwengu.” 5 Kwa kweli, ndugu zake walikuwa hawadhihirishi imani katika yeye. 6 Kwa hiyo Yesu akawaambia: “Wakati wangu upasao haujakuwapo bado, lakini wakati wenu upasao uko karibu sikuzote. 7 Ulimwengu hauna sababu ya kuwachukia nyinyi, lakini huo wanichukia mimi, kwa sababu natoa ushahidi kuhusu huo kwamba kazi zao ni mbovu. 8 Nyinyi pandeni kwenda kwenye msherehekeo; mimi bado sipandi kwenda kwenye msherehekeo huu, kwa sababu wakati wangu upasao bado haujaja kikamili.” 9 Kwa hiyo baada ya kuwaambia mambo haya, akabaki Galilaya.
10 Lakini ndugu zake walipokuwa wamepanda kwenda kwenye msherehekeo, ndipo yeye mwenyewe pia akapanda kwenda, si waziwazi bali kama katika siri. 11 Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kumtafuta kwenye msherehekeo na kusema: “Yuko wapi mtu yule?” 12 Na kulikuwako maongezi mengi ya kunong’oneza juu yake miongoni mwa umati. Baadhi yao wakawa wakisema: “Yeye ni mtu mwema.” Wengine wakawa wakisema: “Sivyo, bali yeye huongoza umati vibaya.” 13 Bila shaka, hakuna aliyekuwa akisema juu yake hadharani kwa sababu ya kuhofu Wayahudi.
14 Wakati kufikia sasa msherehekeo ulipokuwa umeisha nusu, Yesu akapanda kwenda ndani ya hekalu na kuanza kufundisha. 15 Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kustaajabu, wakisema: “Ni jinsi gani mtu huyu ana ujuzi wa maandishi, wakati yeye hajajifunza kwenye mashule?” 16 Yesu, naye, akawajibu na kusema: “Kile nifundishacho si changu, bali ni chake yeye aliyenituma. 17 Ikiwa yeyote atamani kufanya mapenzi Yake, atajua kuhusu fundisho kama ni la kutoka kwa Mungu au mimi nasema kwa ubuni wangu mwenyewe. 18 Yeye ambaye husema kwa ubuni wake mwenyewe anatafuta sana utukufu wake mwenyewe; bali yeye atafutaye utukufu wake aliyemtuma, huyu ni wa kweli, na hakuna ukosefu wa uadilifu katika yeye. 19 Musa aliwapa nyinyi Sheria, sivyo? Lakini hakuna hata mmoja wenu atiiye Sheria. Kwa nini mnatafuta sana kuniua?” 20 Umati ukajibu: “Wewe una roho mwovu. Ni nani anayetafuta sana kukuua?” 21 Kwa kujibu Yesu akawaambia: “Kitendo kimoja nilifanya, nanyi nyote mnastaajabu. 22 Kwa sababu hiyo Musa amewapa tohara—si kwamba yatoka kwa Musa, bali kwamba yatoka kwa baba wa zamani—nanyi mwatahiri mtu siku ya sabato. 23 Ikiwa mtu apokea tohara siku ya sabato ili sheria ya Musa isipate kuvunjwa, je, mwanikasirikia vikali kwa sababu nilifanya mtu awe timamu kikamili katika afya siku ya sabato? 24 Komeni kuhukumu kutokana na kuonekana kwa nje, bali hukumuni kwa hukumu ya uadilifu.”
25 Kwa hiyo baadhi ya wakaaji wa Yerusalemu wakaanza kusema: “Huyu ndiye mtu ambaye wanatafuta sana kuua, sivyo? 26 Na bado, oneni! yeye anasema na watu wote, nao hawamwambii jambo lolote. Watawala hawajaja kujua kwa hakika kwamba huyu ndiye Kristo, je, wamejua? 27 Kinyume chake, sisi twajua mtu huyu atoka wapi; lakini Kristo ajapo, hakuna atakayejua yeye atoka wapi.” 28 Kwa hiyo Yesu akapaaza kilio alipokuwa akifundisha katika hekalu na kusema: “Nyinyi mwanijua mimi tena mwajua natoka wapi. Pia, sikuja kwa uanzisho wangu mwenyewe, lakini yeye aliyenituma ni halisi, nanyi hammjui yeye. 29 Mimi namjua yeye, kwa sababu mimi ni mwakilishi kutoka kwake, na Huyo alinituma.” 30 Kwa sababu hiyo wakaanza kutafuta sana kumshika, lakini hakuna aliyemwekea mkono amshike, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado. 31 Bado, wengi wa umati waliweka imani katika yeye; nao wakaanza kusema: “Kristo awasilipo, hatafanya ishara zaidi ya zile ambazo mtu huyu amefanya, je, atafanya?”
32 Mafarisayo walisikia umati ukinong’ona mambo hayo juu yake, na makuhani wakuu na Mafarisayo wakatuma maofisa wamshike. 33 Kwa hiyo Yesu akasema: “Mimi naendelea kuwa pamoja nanyi muda kidogo zaidi kabla ya kwenda kwake aliyenituma. 34 Nyinyi mtanitafuta, lakini hamtanipata, na mahali nilipo hamwezi kuja.” 35 Kwa hiyo Wayahudi wakasema miongoni mwao wenyewe: “Ni wapi mwanamume huyu akusudia kwenda, hivi kwamba hatutampata? Yeye hakusudii kwenda kwa Wayahudi waliotawanyika miongoni mwa Wagiriki na kufundisha Wagiriki, je, akusudia? 36 Wamaanisha nini usemi huu aliosema kwamba, ‘Nyinyi mtanitafuta, lakini hamtanipata, na mahali nilipo hamwezi kuja’?”
37 Basi siku ya mwisho, siku kubwa ya msherehekeo, Yesu alikuwa amesimama naye akapaaza kilio, akisema: “Ikiwa yeyote ni mwenye kiu, acheni aje kwangu na kunywa. 38 Yeye ambaye huweka imani katika mimi, kama vile Andiko limesema, ‘Kutoka katika sehemu yake ya ndani kabisa vijito vya maji yaliyo hai vitatiririka.’” 39 Hata hivyo, alisema hilo kuhusu ile roho ambayo wale walioweka imani katika yeye walikuwa karibu kupokea; kwa maana hadi hapo hakukuwako roho, kwa sababu Yesu hakuwa ametukuzwa bado. 40 Kwa hiyo baadhi ya umati ambao ulisikia maneno hayo ukaanza kusema: “Kwa hakika huyu ni Yule Nabii.” 41 Wengine walikuwa wakisema: “Huyu ndiye Kristo.” Lakini baadhi walikuwa wakisema: “Hakika Kristo haji kutoka Galilaya, ndivyo? 42 Je, Andiko halijasema kwamba Kristo anakuja kutokana na uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu kijiji ambako Daudi alikuwa kwa kawaida?” 43 Kwa hiyo mgawanyiko juu yake ukatokea miongoni mwa umati. 44 Ingawa hivyo, baadhi yao walikuwa wanataka kumshika, lakini hakuna aliyeweka mikono yake juu yake.
45 Kwa hiyo maofisa wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo, na hao wa mwisho wakawaambia: “Ni kwa nini hamkumleta?” 46 Maofisa wakajibu: “Hajasema kamwe mtu mwingine kama hivi.” 47 Nao Mafarisayo wakajibu: “Nyinyi hamjaongozwa vibaya pia, ndivyo? 48 Hakuna hata mmoja wa watawala au wa Mafarisayo ambaye ameweka imani katika yeye, ndivyo? 49 Lakini umati huu usiojua Sheria ni watu waliolaaniwa.” 50 Nikodemo, aliyekuwa amekuja kwake hapo awali, na aliyekuwa mmoja wao, akawaambia: 51 “Sheria yetu haimhukumu mtu isipokuwa kwanza iwe imesikia kutoka kwake na kuja kujua analofanya, ndivyo?” 52 Kwa kujibu wakamwambia: “Wewe pia si wa kutoka Galilaya, ndivyo? Chunguza uone kwamba hakuna nabii atakayeinuliwa kutoka Galilaya.”*
*Hati-mkono אBSys zaondoa mstari wa 53 hadi sura ya 8, mstari wa 11, ambayo husomwa (kukiwa na kubadilika-badilika fulani katika maandishi-awali mbalimbali na tafsiri za Kigriki) kama ifuatavyo:
53 Kwa hiyo wakaenda kila mmoja nyumbani kwake.