Yohana
6 Baada ya mambo haya Yesu aliondoka kwenda ng’ambo ya bahari ya Galilaya, au Tiberiasi. 2 Lakini umati mkubwa ukafuliza kumfuata, kwa sababu ulikuwa ukiona ishara alizokuwa akifanya juu ya wale waliokuwa wakiugua. 3 Kwa hiyo Yesu akapanda kwenda kuingia mlimani, na hapo alikuwa ameketi pamoja na wanafunzi wake. 4 Sasa sikukuu ya kupitwa, msherehekeo wa Wayahudi, ilikuwa karibu. 5 Kwa hiyo, Yesu alipoinua macho yake na kuona kwamba umati mkubwa ulikuwa ukija kwake, alimwambia Filipo: “Tutainunua wapi mikate ili hawa wale?” 6 Hata hivyo, alikuwa akisema hilo amjaribu, kwa maana yeye mwenyewe alijua alilokuwa karibu kufanya. 7 Filipo akamjibu: “Mikate yenye thamani ya dinari mia mbili haiwatoshi, hata kwamba kila mmoja aweze kupata kidogo.” 8 Mmoja wa wanafunzi wake, Andrea ndugu ya Simoni Petro, akamwambia: 9 “Hapa yupo mvulana mdogo ambaye ana mikate mitano ya shayiri na samaki wadogo wawili. Lakini hivi ni nini miongoni mwa wengi sana hivi?”
10 Yesu akasema: “Wafanyeni watu waegame kama kwenye mlo.” Basi kulikuwa na nyasi nyingi mahali hapo. Kwa hiyo wanaume wakaegama, idadi yao karibu elfu tano. 11 Basi Yesu akachukua ile mikate na, baada ya kushukuru, akaigawanya kwa wale waliokuwa wameegama, hivyohivyo pia wale samaki wadogo kadiri walivyotaka. 12 Lakini walipokuwa wamepata kushiba akawaambia wanafunzi wake: “Kusanyeni pamoja vipande vidogo vinavyobakia, ili kitu kisipotee bure.” 13 Kwa hiyo wakavikusanya pamoja, nao wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vidogo kutokana na mikate mitano ya shayiri, ambavyo vilibakizwa na wale waliokuwa wamekula.
14 Kwa sababu hiyo watu hao walipoona ishara alizofanya, wakaanza kusema: “Kwa hakika huyu ndiye nabii aliyepaswa kuja ulimwenguni.” 15 Kwa hiyo Yesu, akijua walikuwa karibu kuja kumkamata wamfanye mfalme, akaondoka tena kwenda kuingia mlimani yeye mwenyewe peke yake.
16 Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake wakateremka kwenda baharini, 17 na, wakipanda mashua, wakaondoka kwenda ng’ambo ya bahari ili waende Kapernaumu. Basi, kufikia sasa ilikuwa imekuwa giza na Yesu alikuwa bado hajaja kwao. 18 Pia, bahari ikaanza kuchafuka kwa sababu upepo wenye nguvu ulikuwa ukivuma. 19 Hata hivyo, walipokuwa wamevuta makasia karibu kilometa tano au sita, wakamwona Yesu akitembea juu ya bahari akikaribia mashua; nao wakawa wenye hofu. 20 Lakini akawaambia: “Ni mimi; msiwe na hofu!” 21 Kwa hiyo walikuwa na nia ya kumchukua ndani ya mashua, na mara hiyo mashua ikawa kwenye nchi kavu walikokuwa wakijaribu kwenda.
22 Siku iliyofuata umati uliokuwa umesimama kwenye upande ule mwingine wa bahari ukaona kwamba palikuwa hapana mashua hapo ila moja ndogo, na kwamba Yesu hakuwa ameingia ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake bali kwamba ni wanafunzi wake tu waliokuwa wameondoka; 23 lakini mashua kutoka Tiberiasi ziliwasili karibu na mahali ambapo walikula mkate baada ya Bwana kuwa ameshukuru. 24 Kwa hiyo umati ulipoona kwamba Yesu hakuwa hapo wala wanafunzi wake, ukapanda mashua zao ndogo ukaja hadi Kapernaumu kumtafuta Yesu.
25 Kwa hiyo walipompata ng’ambo ya bahari wakamwambia: “Rabi, ulifika hapa lini?” 26 Yesu akawajibu na kusema: “Kwa kweli kabisa mimi nawaambia, Nyinyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula kutokana na mikate mkashiba.” 27 Fanyeni kazi, si kwa ajili ya chakula ambacho huharibika, bali kwa ajili ya chakula ambacho hudumu kwa uhai udumuo milele, ambacho Mwana wa binadamu atawapa nyinyi; kwa maana juu yake huyo, Baba, naam Mungu, ameweka muhuri wake wa kibali.”
28 Kwa hiyo wakamwambia: “Tutafanya nini ili tufanye kazi za Mungu?” 29 Kwa kujibu Yesu akawaambia: “Hii ndiyo kazi ya Mungu, kwamba mdhihirishe imani katika yeye ambaye Huyo alimtuma.” 30 Kwa hiyo wakamwambia: “Basi, wewe unafanya nini kuwa ishara, kusudi sisi tuione tukuamini? Ni kazi gani ambayo unafanya? 31 Baba zetu wa zamani walikula mana nyikani, kama vile imeandikwa, ‘Yeye aliwapa mkate kutoka mbinguni ili wale.’” 32 Kwa sababu hiyo Yesu akawaambia: “Kwa kweli kabisa mimi nawaambia, Musa hakuwapa nyinyi mkate kutoka mbinguni, lakini Baba yangu awapa nyinyi mkate wa kweli kutoka mbinguni. 33 Kwa maana mkate wa Mungu ni yeye ambaye huteremka kutoka mbinguni na huupa ulimwengu uhai.” 34 Kwa hiyo wakamwambia: “Bwana, utupe sikuzote mkate huu.”
35 Yesu akawaambia: “Mimi ndio mkate wa uhai. Yeye ambaye huja kwangu hataona njaa hata kidogo, naye adhihirishaye imani katika mimi hatapatwa na kiu kamwe kabisa. 36 Lakini nimewaambia, Nyinyi hata mmeniona mimi na bado hamwamini. 37 Kila kitu anipacho Baba kitakuja kwangu, naye ajaye kwangu sitamwondoshea mbali kwa vyovyote; 38 kwa sababu nimeteremka kutoka mbinguni kufanya, si mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenituma. 39 Haya ndiyo mapenzi yake aliyenituma, kwamba nisipoteze kitu chochote kutokana na vyote ambavyo amenipa bali kwamba nikifufue kwenye siku ya mwisho. 40 Kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Baba yangu, kwamba kila mtu ambaye hutazama Mwana na kudhihirisha imani katika yeye awe na uhai udumuo milele, nami hakika nitamfufua siku ya mwisho.”
41 Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kumnung’unikia kwa sababu alisema: “Mimi ndio mkate ambao uliteremka kutoka mbinguni”; 42 nao wakaanza kusema: “Je, huyu si Yesu mwana wa Yosefu, ambaye baba na mama yake sisi twawajua? Ni jinsi gani kwamba sasa asema, ‘Mimi nimeteremka kutoka mbinguni’?” 43 Kwa kujibu Yesu akawaambia: “Komeni kunung’unika miongoni mwenu wenyewe. 44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa Baba, aliyenituma, amvute yeye; nami hakika nitamfufua siku ya mwisho. 45 Imeandikwa katika Manabii, ‘Na wote watafundishwa na Yehova.’ Kila mtu ambaye amesikia kutoka kwa Baba na ambaye amejifunza huja kwangu. 46 Si kwamba mtu yeyote amemwona Baba, ila yeye aliyetoka kwa Mungu; yeye huyo amemwona Baba. 47 Kwa kweli kabisa mimi nawaambia, Yeye ambaye huamini ana uhai udumuo milele.
48 “Mimi ndio mkate wa uhai. 49 Baba zenu wa zamani walikula mana nyikani na bado wakafa. 50 Huu ndio mkate ambao huteremka kutoka mbinguni, ili yeyote apate kula kutokana nao na asife. 51 Mimi ndio mkate ulio hai ulioteremka kutoka mbinguni; yeyote akila kutokana na mkate huu ataishi milele; na, kwa kweli, mkate ambao nitatoa ni mwili wangu kwa ajili ya uhai wa ulimwengu.”
52 Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kushindana, wakisema: “Mtu huyu awezaje kutupa mwili wake tule?” 53 Basi Yesu akawaambia: “Kwa kweli kabisa mimi nawaambia, Nyinyi msipoula mwili wa Mwana wa binadamu na kunywa damu yake, hamna uhai katika nyinyi wenyewe. 54 Yeye ambaye hula mwili wangu na kunywa damu yangu ana uhai udumuo milele, nami nitamfufua kwenye siku ya mwisho; 55 kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56 Yeye ambaye hula mwili wangu na kunywa damu yangu hukaa katika muungano nami, na mimi katika muungano naye. 57 Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi nami naishi kwa sababu ya Baba, yeye ambaye pia hunila mimi, hata huyo ataishi kwa sababu yangu. 58 Huu ndio mkate ulioteremka kutoka mbinguni. Si kama wakati baba zenu wa zamani walipokula na bado wakafa. Yeye ambaye hula mkate huu ataishi milele.” 59 Mambo haya aliyasema alipokuwa akifundisha katika kusanyiko la watu wote katika Kapernaumu.
60 Kwa hiyo wengi wa wanafunzi wake, waliposikia hilo, wakasema: “Usemi huu unashtua; ni nani ambaye aweza kuusikiliza?” 61 Lakini Yesu, akijua katika yeye mwenyewe kwamba wanafunzi wake walikuwa wakinung’unika juu ya hili, akawaambia: “Je, hili lawakwaza nyinyi? 62 Kwa hiyo, namna gani ikiwa mtamwona Mwana wa binadamu akipaa kwenda alikokuwa kabla ya hapo? 63 Ni roho ndiyo ipayo uhai; mwili hauna mafaa hata kidogo. Semi ambazo nimewaambia ni roho na ni uhai. 64 Lakini kuna baadhi yenu ambao hawaamini.” Kwa maana kutoka mwanzo Yesu alijua ni nani wale waliokuwa hawaamini na ni nani angemsaliti. 65 Kwa hiyo akaendelea kusema: “Hii ndiyo sababu nimewaambia nyinyi, Hakuna awezaye kuja kwangu isipokuwa aruhusiwe na Baba.”
66 Kwa sababu ya hili wengi wa wanafunzi wake wakaenda zao kwenye mambo yaliyo nyuma wakawa hawatembei tena pamoja naye. 67 Kwa hiyo Yesu akawaambia wale kumi na wawili: “Nyinyi hamtaki kwenda pia, je, mwataka?” 68 Simoni Petro akamjibu: “Bwana, tutaenda zetu kwa nani? Wewe una semi za uhai udumuo milele; 69 na sisi tumeamini na tumekuja kujua kwamba wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.” 70 Yesu akawajibu: “Mimi niliwachagua nyinyi kumi na wawili, sivyo? Lakini mmoja wenu ni mchongezi.” 71 Kwa kweli, alikuwa akisema juu ya Yudasi mwana wa Simoni Iskariote; kwa maana huyu alikuwa akielekea kumsaliti, ajapokuwa mmoja wa wale kumi na wawili.