Yohana
5 Baada ya mambo haya kulikuwa na msherehekeo wa Wayahudi, na Yesu akapanda kwenda Yerusalemu. 2 Sasa katika Yerusalemu kwenye lango la kondoo kuna dimbwi linaloitwa katika Kiebrania Bethzatha, lenye safu tano za nguzo. 3 Katika hizo umati wa wagonjwa, vipofu, vilema na wale wenye viungo vilivyonyauka, walikuwa wamelala chini. 4 —— 5 Lakini mtu fulani alikuwa hapo aliyekuwa amekuwa na ugonjwa wake kwa miaka thelathini na minane. 6 Alipomwona mtu huyu amelala chini, na akijua kwamba tayari alikuwa amekuwa mgonjwa muda mrefu, Yesu akamwambia: “Je, wataka kuwa timamu katika afya?” 7 Huyo mgonjwa akamjibu: “Bwana, sina mtu wa kuniweka ndani ya dimbwi wakati maji yatibuliwapo; lakini wakati ninapokuwa nikija mwingine huteremka mbele yangu.” 8 Yesu akamwambia: “Inuka, chukua kitanda chako utembee.” 9 Ndipo huyo mtu akawa timamu katika afya mara hiyo, naye akachukua kitanda chake akaanza kutembea.
Basi siku hiyo ilikuwa ya sabato. 10 Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kumwambia mtu huyo aliyeponywa: “Ni Sabato, na hairuhusiki kisheria ukichukue kitanda.” 11 Lakini yeye akawajibu: “Yuleyule aliyenifanya timamu katika afya aliniambia, ‘Chukua kitanda chako utembee.’” 12 Wakamuuliza: “Ni nani huyo mtu aliyekuambia, ‘Kichukue utembee’?” 13 Lakini mwanamume huyo aliyeponywa hakujua huyo alikuwa nani, kwa maana Yesu alikuwa amegeukia kando, mahali hapo pakiwa pana umati.
14 Baada ya mambo haya Yesu alimkuta hekaluni akamwambia: “Ona, umekuwa timamu katika afya. Usifanye dhambi tena kamwe, ili kitu fulani kibaya zaidi kisitukie kwako.” 15 Huyo mtu akaenda zake akawaambia Wayahudi kwamba alikuwa ni Yesu aliyemfanya timamu katika afya. 16 Kwa hiyo kwa sababu hiyo Wayahudi wakawa wanamnyanyasa Yesu, kwa sababu alikuwa akifanya mambo hayo wakati wa siku ya Sabato. 17 Lakini yeye akawajibu: “Baba yangu amefuliza kufanya kazi hadi sasa, na mimi nafuliza kufanya kazi.” 18 Kwa kweli, kwa sababu hiyo Wayahudi wakaanza kutafuta-tafuta hata zaidi kumuua, kwa sababu si kwamba tu alikuwa akiivunja Sabato bali pia alikuwa akimwita Mungu Baba yake mwenyewe, akijifanya mwenyewe kuwa sawa na Mungu.
19 Kwa hiyo, kwa kujibu, Yesu akaendelea kuwaambia: “Kwa kweli kabisa mimi nawaambia nyinyi, Mwana hawezi kufanya hata kitu kimoja kwa uanzisho wake mwenyewe, ila tu kile atazamacho Baba akifanya. Kwa maana mambo yoyote yale Huyo hufanya, mambo hayo Mwana pia hufanya kwa namna kama hiyo. 20 Kwa maana Baba ana shauku na Mwana na humwonyesha mambo yote afanyayo yeye mwenyewe, naye atamwonyesha kazi zilizo kubwa zaidi kuliko hizi, ili nyinyi mpate kustaajabu. 21 Kwa maana kama vile Baba huwafufua wafu na kuwafanya hai, ndivyo Mwana pia huwafanya hai wale atakao kuwafanya hai. 22 Kwa maana Baba hahukumu yeyote hata kidogo, bali amekabidhi kuhukumu kote kwa Mwana, 23 ili wote wapate kumheshimu Mwana kama vile wamheshimuvyo Baba. Yeye ambaye hamheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyemtuma. 24 Kwa kweli kabisa mimi nawaambia nyinyi, Yeye ambaye husikia neno langu na kumwamini yeye aliyenituma ana uhai udumuo milele, naye haji kuingia hukumuni bali amepita kuvuka kutoka kwenye kifo hadi kwenye uhai.
25 “Kwa kweli kabisa mimi nawaambia nyinyi, Saa inakuja, nayo ipo sasa, wakati wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu na wale ambao wamemsikiliza wataishi. 26 Kwa maana kama vile Baba alivyo na uhai katika yeye mwenyewe, ndivyo pia amemruhusu Mwana kuwa na uhai katika yeye mwenyewe. 27 Naye amempa mamlaka kufanya kazi ya kuhukumu, kwa sababu Mwana wa binadamu ndiye. 28 Msistaajabie hili, kwa sababu saa inakuja ambayo katika hiyo wote wale waliomo ndani ya makaburi ya ukumbusho watasikia sauti yake 29 na kutoka, wale waliofanya mambo mema kwenye ufufuo wa uhai, wale waliozoea kufanya mambo maovu kwenye ufufuo wa hukumu. 30 Mimi siwezi kufanya kitu chochote kwa uanzisho wangu mwenyewe; kama vile nisikiavyo, ndivyo nihukumuvyo; na hukumu nitoayo ni ya uadilifu, kwa sababu natafuta sana, si mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake aliyenituma mimi.
31 “Ikiwa mimi peke yangu natoa ushahidi juu yangu mwenyewe, ushahidi wangu si wa kweli. 32 Kuna mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba ushahidi ambao yeye hutoa juu yangu ni wa kweli. 33 Nyinyi mmetuma watu kwa Yohana, naye ametoa ushahidi kwa ile kweli. 34 Hata hivyo, mimi siukubali ushahidi kutoka kwa mtu, bali nasema mambo hayo ili nyinyi mpate kuokolewa. 35 Mtu huyo alikuwa taa yenye kuwaka na yenye kung’aa, nanyi kwa wakati mfupi mlikuwa na nia ya kushangilia sana katika nuru yake. 36 Lakini mimi nina ushahidi ulio mkubwa zaidi kuliko ule wa Yohana, kwa maana kazi zilezile ambazo Baba yangu alinigawia kutimiza, kazi hizo zenyewe ambazo ninafanya, hutoa ushahidi juu yangu kwamba Baba alinituma mimi. 37 Pia, Baba aliyenituma yeye mwenyewe ametoa ushahidi juu yangu. Nyinyi hamjasikia sauti yake wakati wowote wala kuona umbo lake; 38 nanyi hamna neno lake likikaa katika nyinyi, kwa sababu yuleyule ambaye yeye alimtuma nyinyi hammwamini.
39 “Nyinyi mnayachunguza Maandiko, kwa sababu mwafikiri kwamba kwa njia yayo mtakuwa na uhai udumuo milele; na hayo yenyewe ndiyo yatoayo ushahidi juu yangu. 40 Na bado hamtaki kuja kwangu ili mpate kuwa na uhai. 41 Mimi sikubali utukufu kutoka kwa watu, 42 lakini najua vizuri kwamba nyinyi hammpendi Mungu katika nyinyi. 43 Mimi nimekuja katika jina la Baba yangu, lakini nyinyi hamnipokei; ikiwa mtu fulani mwingine angewasili katika jina lake mwenyewe, mngempokea huyo. 44 Mtawezaje kuamini, wakati nyinyi mnakubali utukufu kutoka kwa mtu na mwenzake na hamtafuti sana utukufu ambao ni kutoka kwa Mungu pekee? 45 Msifikiri kwamba hakika mimi nitawashtaki kwa Baba; kuna mmoja ambaye huwashtaki nyinyi, Musa, ambaye katika yeye mmetia tumaini lenu. 46 Kwa kweli, ikiwa mngalimwamini Musa mngaliniamini mimi, kwa maana huyo aliandika juu yangu. 47 Lakini ikiwa hamwamini maandishi ya huyo, mtaaminije semi zangu?”