Yohana
4 Basi, wakati Bwana alipojua kwamba Mafarisayo walikuwa wamesikia kwamba Yesu alikuwa akifanya na kubatiza wanafunzi zaidi kuliko Yohana— 2 ijapokuwa, kwa kweli, Yesu mwenyewe hakuwa akibatiza ila wanafunzi wake— 3 aliacha Yudea na kuondoka tena kwenda Galilaya. 4 Lakini ilikuwa lazima yeye apitie Samaria. 5 Basi akaja hadi jiji moja la Samaria liitwalo Sikari karibu na shamba ambalo Yakobo alimpa Yosefu mwana wake. 6 Kwa kweli, bubujiko la Yakobo lilikuwa hapo. Basi Yesu, akiwa amechoka kabisa kutokana na safari hiyo, alikuwa ameketi kwenye bubujiko kama vile alivyokuwa. Ilikuwa karibu saa ya sita.
7 Mwanamke mmoja wa Samaria alikuja kuteka maji. Yesu akamwambia: “Nipe kinywaji.” 8 (Kwa maana wanafunzi wake walikuwa wameenda katika jiji kununua vyakula.) 9 Kwa hiyo huyo mwanamke Msamaria akamwambia: “Ni jinsi gani kwamba wewe, ujapokuwa Myahudi, waniomba mimi kinywaji, wakati mimi ni mwanamke Msamaria?” (Kwa maana Wayahudi hawana shughuli pamoja na Wasamaria.) 10 Kwa kujibu Yesu akamwambia: “Kama ungalijua zawadi ya bure itokayo kwa Mungu na ni nani ambaye akuambia, ‘Nipe kinywaji,’ wewe ungalimwomba, naye angalikupa maji yaliyo hai.” 11 Akamwambia: “Bwana, huna hata ndoo ya kutekea maji, na kisima ni chenye kina kirefu. Kwa hiyo, ni kutoka chanzo gani unayo maji hayo yaliyo hai? 12 Wewe si mkubwa zaidi kuliko baba yetu wa zamani Yakobo, ambaye alitupa hiki kisima na ambaye yeye mwenyewe pamoja na wana wake na mifugo yake walikunywa kutokana nacho, ndivyo?” 13 Kwa kujibu Yesu akamwambia: “Kila mtu anayekunywa kutokana na maji haya atapatwa na kiu tena. 14 Yeyote yule anywaye kutokana na maji ambayo hakika mimi nitampa hatapatwa na kiu hata kidogo, lakini maji ambayo hakika mimi nitampa yatakuwa katika yeye bubujiko la maji linalobubujika ili kutoa uhai udumuo milele.” 15 Huyo mwanamke akamwambia: “Bwana, nipe maji hayo, ili nisipate kuwa na kiu wala kufuliza kuja mahali hapa kuteka maji.”
16 Akamwambia: “Nenda, ukamwite mume wako mje mahali hapa.” 17 Kwa kujibu huyo mwanamke akasema: “Sina mume.” Yesu akamwambia: “Umesema vema, ‘Mume sina.’ 18 Kwa maana umekuwa na waume watano, na mwanamume uliye naye sasa si mume wako. Hapo umesema kikweli.” 19 Huyo mwanamke akamwambia: “Bwana, nahisi wewe ni nabii. 20 Baba zetu wa zamani waliabudu katika mlima huu; lakini nyinyi watu husema kwamba katika Yerusalemu ndipo penye mahali ambapo watu wapaswa kuabudia.” 21 Yesu akamwambia: “Niamini mimi, mwanamke, Saa inakuja wakati ambapo wala si katika mlima huu wala katika Yerusalemu nyinyi watu mtamwabudu Baba. 22 Nyinyi mwaabudu kile msichojua; sisi twaabudu kile tujuacho, kwa sababu wokovu hutokana na Wayahudi. 23 Hata hivyo, saa inakuja, nayo ipo sasa, wakati waabudu wa kweli watakapomwabudu Baba kwa roho na kweli, kwa maana, kwa kweli, Baba anawatafuta wa namna hiyo wamwabudu yeye. 24 Mungu ni Roho, na wale wanaomwabudu yeye lazima waabudu kwa roho na kweli.” 25 Huyo mwanamke akamwambia: “Najua kwamba Mesiya anakuja, aitwaye Kristo. Wakati wowote ule huyo awasilipo, atatujulisha mambo yote waziwazi.” 26 Yesu akamwambia: “Mimi ninayesema nawe ndiye.”
27 Sasa kufikia hatua hii wanafunzi wake wakawasili, nao wakaanza kustaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke. Bila shaka, hakuna yeyote aliyesema: “Unatafuta nini?” au “Kwa nini unaongea na huyu mwanamke?” 28 Kwa hiyo, huyo mwanamke akaacha mtungi wake wa maji akaenda zake katika jiji na kuwaambia watu: 29 “Njoni hapa, mwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyofanya. Huyu labda ndiye Kristo, sivyo?” 30 Wakaenda kutoka jijini na kuanza kuja kwake.
31 Wakati huohuo wanafunzi walikuwa wakimhimiza, wakisema: “Rabi, kula.” 32 Lakini yeye akawaambia: “Mimi nina chakula ambacho nyinyi hamjui juu yacho.” 33 Kwa hiyo wanafunzi wakaanza kusemezana: “Hakuna ambaye amemletea kitu chochote cha kula, je, yuko?” 34 Yesu akawaambia: “Chakula changu ni kwamba mimi nifanye mapenzi yake aliyenituma na kumaliza kazi yake. 35 Je, nyinyi hamsemi kwamba bado kuna miezi minne kabla ya mavuno kuja? Tazama! Mimi nawaambia nyinyi: Inueni macho yenu mtazame mashamba, kwamba ni meupe kwa ajili ya kuvunwa. Tayari 36 mvunaji anapokea mshahara na kukusanya matunda kwa ajili ya uhai udumuo milele, ili mpanzi na mvunaji wapate kushangilia pamoja. 37 Katika habari hii, kwa kweli, huu usemi ni kweli, Mmoja ndiye mpanzi na mwingine ndiye mvunaji. 38 Mimi niliwatuma nyinyi mkavune ambacho hamkufanyia kazi ya jasho. Wengine wamefanya kazi ya jasho, nanyi mmeingia katika manufaa ya kazi yao.”
39 Sasa wengi wa Wasamaria kutoka jiji hilo waliweka imani katika yeye kwa sababu ya neno la mwanamke aliyesema hivi kwa ushahidi: “Yeye aliniambia mambo yote niliyofanya.” 40 Kwa hiyo Wasamaria walipokuja kwake, walianza kumwomba akae pamoja nao; naye akakaa huko siku mbili. 41 Kwa sababu hiyo wengi zaidi wakaamini kwa ajili ya aliyoyasema, 42 nao wakaanza kumwambia huyo mwanamke: “Hatuamini tena kamwe kwa sababu ya maongezi yako; kwa maana sisi tumejisikilia wenyewe nasi twajua kwamba mtu huyu kwa hakika ndiye mwokozi wa ulimwengu.”
43 Baada ya hizo siku mbili akaondoka huko kwenda Galilaya. 44 Hata hivyo, Yesu mwenyewe alitoa ushahidi kwamba katika nchi ya nyumbani mwake mwenyewe nabii hana heshima. 45 Kwa hiyo, alipowasili katika Galilaya, Wagalilaya walimpokea, kwa sababu walikuwa wameona mambo yote aliyofanya katika Yerusalemu kwenye msherehekeo, kwa maana wao pia walikuwa wameenda kwenye msherehekeo.
46 Basi akaja tena hadi Kana ya Galilaya, ambako alikuwa amegeuza maji kuwa divai. Basi kulikuwako hadimu fulani wa mfalme ambaye mwana wake alikuwa mgonjwa katika Kapernaumu. 47 Mtu huyu aliposikia kwamba Yesu alikuwa amekuja kutoka Yudea kuingia Galilaya, akamwendea na kuanza kumwomba ateremke amponye mwana wake, kwa maana alikuwa karibu kufa. 48 Hata hivyo, Yesu akamwambia: “Isipokuwa nyinyi watu mwone ishara na maajabu, hamtaamini kwa vyovyote.” 49 Hadimu wa mfalme akamwambia: “Bwana, teremka uje kabla mtoto wangu mchanga hajafa.” 50 Yesu akamwambia: “Shika njia uende zako; mwana wako yuko hai.” Huyo mtu akaamini neno ambalo Yesu alimwambia akashika njia kwenda zake. 51 Lakini tayari alipokuwa ameshika njia akishuka kwenda zake watumwa wake wakakutana naye ili kusema kwamba mvulana wake alikuwa yuko hai. 52 Kwa hiyo akaanza kuulizia habari kwao saa ambayo katika hiyo yeye alipata nafuu katika afya. Basi wakamwambia: “Jana kwenye saa ya saba homa ilimwacha.” 53 Kwa hiyo huyo baba akajua ilikuwa katika saa ileile ambayo Yesu alimwambia: “Mwana wako yuko hai.” Naye na watu wote wa nyumbani mwake wakaamini. 54 Tena hiyo ilikuwa ndiyo ishara ya pili aliyofanya Yesu alipokuja kutoka Yudea kuingia Galilaya.