Yohana
11 Basi kulikuwako mtu fulani mgonjwa, Lazaro wa Bethania, wa kijiji cha Maria na cha Martha dada yake. 2 Kwa kweli, alikuwa ni Maria aliyempaka Bwana mafuta yenye marashi na kufuta miguu yake ili kuikausha kwa nywele zake, ambaye Lazaro ndugu yake alikuwa mgonjwa. 3 Kwa hiyo dada zake walipeleka neno kwake, wakisema: “Bwana, ona! yule ambaye una shauku naye ni mgonjwa.” 4 Lakini Yesu aliposikia hilo akasema: “Ugonjwa huu hauna kifo kikiwa lengo lao, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kupitia huo.”
5 Basi Yesu alimpenda Martha na dada yake na Lazaro. 6 Hata hivyo, aliposikia kwamba alikuwa mgonjwa, ndipo kwa kweli akakaa siku mbili mahali alipokuwa. 7 Kisha baada ya hili akawaambia wanafunzi: “Twendeni tuingie Yudea tena.” 8 Wanafunzi wakamwambia: “Rabi, juzijuzi tu Wayudea walikuwa wakitafuta sana kukupiga kwa mawe, na je, wewe unaenda huko tena?” 9 Yesu akajibu: “Kuna saa kumi na mbili za nuru ya mchana, sivyo? Ikiwa yeyote atembea katika nuru ya mchana hajigongi dhidi ya kitu chochote, kwa sababu yeye huona nuru ya ulimwengu huu. 10 Lakini ikiwa yeyote atembea usiku, yeye hujigonga dhidi ya kitu fulani, kwa sababu nuru haimo katika yeye.”
11 Alisema mambo hayo, na baada ya hilo akawaambia: “Lazaro rafiki yetu ameenda kupumzika, lakini ninafunga safari huko ili kumwamsha kutoka usingizini.” 12 Kwa hiyo wanafunzi wakamwambia: “Bwana, ikiwa ameenda kupumzika, atapata kupona.” 13 Hata hivyo, Yesu alikuwa amesema juu ya kifo chake. Lakini waliwazia alikuwa akisema juu ya kupumzika usingizini. 14 Kwa hiyo, wakati huo, Yesu akawaambia kwa kusema waziwazi: “Lazaro amekufa, 15 nami nashangilia kwa sababu yenu kwamba sikuwa huko, kusudi nyinyi mwamini. Lakini twendeni kwake.” 16 Kwa hiyo Tomasi, ambaye aliitwa Pacha, akawaambia wanafunzi wenzake: “Acheni sisi twende pia, ili tupate kufa pamoja naye.”
17 Kwa sababu hiyo Yesu alipowasili, alikuta tayari alikuwa amekuwa siku nne katika kaburi la ukumbusho. 18 Basi Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu umbali wa karibu kilometa tatu. 19 Basi wengi wa Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Maria kusudi wawafariji kuhusu ndugu yao. 20 Kwa hiyo Martha, aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, alienda kukutana naye; lakini Maria alifuliza kuketi nyumbani. 21 Kwa hiyo Martha akamwambia Yesu: “Bwana, kama ungalikuwa hapa ndugu yangu asingalikufa. 22 Na bado wakati wa sasa najua kwamba mambo mengi uombayo Mungu, Mungu atakupa.” 23 Yesu akamwambia: “Ndugu yako atainuka.” 24 Martha akamwambia: “Najua atafufuliwa katika ufufuo siku ya mwisho.” 25 Yesu akamwambia: “Mimi ndio ufufuo na uhai. Yeye ambaye hudhihirisha imani katika mimi, hata ingawa afa, atakuja kwenye uhai; 26 na kila mtu aliye hai na hudhihirisha imani katika mimi hatakufa hata kidogo kabisa. Je, unaamini hili?” 27 Yeye akamwambia: “Ndiyo, Bwana; mimi nimeamini kwamba wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu, Yule anayekuja ulimwenguni.” 28 Na alipokuwa amesema hilo, akaenda zake akamwita Maria dada yake, akisema kwa siri: “Mwalimu yupo naye anakuita wewe.” 29 Huyo wa mwisho, aliposikia hilo, akainuka upesi akawa ameshika njia yake kumwendea.
30 Kwa kweli, Yesu alikuwa bado hajaja ndani ya kijiji, lakini alikuwa bado mahali ambapo Martha alikuwa amekutana naye. 31 Kwa hiyo Wayahudi waliokuwa pamoja naye katika nyumba na waliokuwa wakimfariji, walipomwona Maria akiinuka upesi na kuondoka aende, wakamfuata, wakidhani kwamba alikuwa akienda kwenye kaburi la ukumbusho ili kutolea machozi huko. 32 Na kwa hiyo Maria, alipowasili mahali ambapo Yesu alikuwa na kumwona mara hiyo, alijiangusha penye miguu yake, akimwambia: “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu asingalikufa.” 33 Kwa hiyo, Yesu alipomwona akitoa machozi na Wayahudi waliokuja pamoja naye wakitoa machozi, akapiga kite katika roho na kuwa mwenye kutaabika; 34 naye akasema: “Mmemlaza wapi?” Wakamwambia: “Bwana, njoo uone.” 35 Yesu akatokwa na machozi. 36 Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kusema: “Ona, jinsi alivyokuwa na shauku naye!” 37 Lakini baadhi yao walisema: “Je, mtu huyu aliyefungua macho ya mtu aliye kipofu hakuweza kuzuia huyu asife?”
38 Kwa sababu hiyo Yesu, baada ya kupiga kite tena ndani yake mwenyewe, akaja kwenye hilo kaburi la ukumbusho. Kwa kweli, lilikuwa pango, na jiwe lilikuwa limelilalia. 39 Yesu akasema: “Liondoeni mbali jiwe.” Martha, dada ya aliyekufa, akamwambia: “Bwana, kufikia sasa lazima awe anuka, kwa maana ni siku nne.” 40 Yesu akamwambia: “Je, sikukuambia kwamba kama ungeamini ungeona utukufu wa Mungu?” 41 Kwa hiyo wakaliondolea mbali jiwe. Basi Yesu akainua macho yake kuelekea mbinguni na kusema: “Baba, nakushukuru kwamba umenisikia. 42 Kweli, nilijua kwamba sikuzote wewe hunisikia; lakini kwa sababu ya umati uliosimama kuzunguka nilisema, ili wapate kuamini kwamba wewe ulinituma.” 43 Na alipokuwa amekwisha kusema mambo hayo, akapaaza kilio kwa sauti kubwa: “Lazaro, njoo huku nje!” 44 Huyo mtu aliyekuwa amekuwa mfu akatoka miguu na mikono yake ikiwa imefungwa vitambaa, na sura yake ilifungwa-fungwa kwa nguo. Yesu akawaambia: “Mfungueni mmwache aende.”
45 Kwa hiyo wengi wa Wayahudi waliokuwa wamekuja kwa Maria na walioona lile alilofanya wakaweka imani katika yeye; 46 lakini baadhi yao wakaenda zao kwa Mafarisayo na kuwaambia mambo aliyofanya Yesu. 47 Kwa sababu hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakaikusanya pamoja Sanhedrini na kuanza kusema: “Twapaswa kufanya nini, kwa sababu mtu huyu hufanya ishara nyingi? 48 Tukimwacha hivyo, wao wote wataweka imani katika yeye, na Waroma watakuja na kuondolea mbali mahali petu na taifa letu pia.” 49 Lakini mtu fulani kati yao, Kayafa, aliyekuwa kuhani wa cheo cha juu mwaka huo, akawaambia: “Nyinyi hamjui lolote hata kidogo, 50 nanyi hamwoni kwamba ni kwa manufaa yenu mtu mmoja afe kwa ajili ya watu kuliko taifa lote liangamizwe.” 51 Ingawa hivyo, hilo hakulisema kwa ubuni wake mwenyewe; lakini kwa sababu alikuwa kuhani wa cheo cha juu mwaka huo, alitoa unabii kwamba Yesu alikusudiwa kufa kwa ajili ya taifa, 52 na si kwa ajili ya hilo taifa tu, bali ili watoto wa Mungu waliotawanyika huku na huku apate pia kuwakusanya pamoja katika mmoja. 53 Kwa hiyo tangu siku hiyo na kuendelea walifanya shauri kumuua.
54 Kwa sababu hiyo Yesu hakutembea tena huku na huku hadharani miongoni mwa Wayahudi, bali aliondoka huko hadi kwenye nchi iliyo karibu na nyika, akaingia katika jiji liitwalo Efraimu, na humo akakaa pamoja na wanafunzi. 55 Sasa sikukuu ya kupitwa ya Wayahudi ilikuwa karibu, na watu wengi walipanda kwenda kutoka hiyo nchi hadi Yerusalemu kabla ya sikukuu ya kupitwa kusudi wajisafishe wenyewe kisherehe. 56 Kwa hiyo wakaenda wakimtafuta Yesu nao wakawa wakiambiana huku wamesimama kuzunguka katika hekalu: “Kauli yenu ni nini? Kwamba hatakuja kwenye msherehekeo hata kidogo?” 57 Ilivyokuwa ni kwamba, makuhani wakuu na Mafarisayo walikuwa wametoa maagizo kwamba ikiwa yeyote angepata kujua alikokuwa, angepaswa kufunua hilo, ili waweze kumkamata.