Yohana
12 Basi, siku sita kabla ya sikukuu ya kupitwa, Yesu aliwasili Bethania, alikokuwa Lazaro ambaye Yesu alikuwa amefufua kutoka kwa wafu. 2 Kwa hiyo wakamwandalia mlo wa jioni huko, na Martha alikuwa akihudumu, lakini Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa wanaegama mezani pamoja naye. 3 Kwa hiyo, Maria akachukua ratili moja ya mafuta yenye marashi, nardo halisi, ghali sana, na kupaka miguu ya Yesu naye akaifuta miguu yake kwa nywele zake ili kuikausha. Nyumba ikawa yenye kujawa na mnukio wa mafuta yenye marashi. 4 Lakini Yudasi Iskariote, mmoja wa wanafunzi wake, aliyekuwa karibu kumsaliti, akasema: 5 “Kwa nini mafuta haya yenye marashi hayakuuzwa kwa dinari mia tatu na kupewa kwa maskini?” 6 Ingawa hivyo, alisema hilo si kwa sababu alihangaikia maskini, bali kwa sababu alikuwa mwizi na alikuwa na sanduku la fedha na alikuwa na kawaida ya kuchukua fedha zilizowekwa ndani yalo. 7 Kwa hiyo Yesu akasema: “Mwacheni, ili ashike mwadhimisho huu kwa kufikiria siku ya maziko yangu. 8 Kwa maana mna maskini pamoja nanyi sikuzote, lakini mimi hamtakuwa nami sikuzote.”
9 Kwa hiyo umati mkubwa wa Wayahudi ukapata kujua kwamba alikuwa huko, nao ukaja, si kwa sababu ya Yesu tu, bali pia kuona Lazaro, aliyemfufua kutoka kwa wafu. 10 Sasa makuhani wakuu wakafanya shauri kumuua Lazaro pia, 11 kwa sababu kwa ajili yake wengi wa Wayahudi walikuwa wakienda huko na kuweka imani katika Yesu.
12 Siku iliyofuata umati mkubwa uliokuwa umekuja kwenye msherehekeo, uliposikia kwamba Yesu alikuwa akija Yerusalemu, 13 ulichukua matawi ya mitende ukatoka kwenda nje kukutana naye. Nao ukaanza kupaaza sauti: “Okoa, twakusihi! Mbarikiwa ni yeye ajaye katika jina la Yehova, naam, mfalme wa Israeli!” 14 Lakini Yesu alipokuwa amempata punda mchanga, akaketi juu yake, kama vile imeandikwa: 15 “Usiwe na hofu, binti wa Zayoni. Tazama! Mfalme wako anakuja, akiwa ameketi juu ya mwana wa punda.” 16 Mambo haya wanafunzi wake hawakuyajali hapo kwanza, lakini Yesu alipopata kutukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba mambo haya yalikuwa yameandikwa kwa habari yake na kwamba walimfanya mambo haya.
17 Basi umati uliokuwa pamoja naye alipomwita Lazaro kutoka katika kaburi la ukumbusho na kumfufua kutoka kwa wafu ukafuliza kutoa ushahidi. 18 Kwa ajili ya hili huo umati, kwa sababu ulisikia alikuwa amefanya ishara hii, ukakutana naye pia. 19 Kwa hiyo Mafarisayo walisema miongoni mwao wenyewe: “Nyinyi mwaona kwamba hamfanikiwi kamwe. Oneni! Ulimwengu umemfuata.”
20 Sasa kulikuwa na baadhi ya Wagiriki miongoni mwa wale waliopanda kuabudu kwenye msherehekeo. 21 Kwa hiyo, hawa walimkaribia Filipo ambaye alikuwa wa kutoka Bethsaida ya Galilaya, nao wakaanza kumwomba, wakisema: “Bwana, twataka kumwona Yesu.” 22 Filipo akaja akamwambia Andrea. Andrea na Filipo wakaja wakamwambia Yesu.
23 Lakini Yesu akawajibu, akisema: “Saa imekuja kwa Mwana wa binadamu kutukuzwa. 24 Kwa kweli kabisa mimi nawaambia nyinyi, Punje ya ngano isipoanguka kuingia katika ardhi na kufa, hiyo hubaki punje moja tu; lakini ikifa, ndipo hiyo huzaa matunda mengi. 25 Yeye apendaye sana nafsi yake huiangamiza, bali yeye ambaye huchukia nafsi yake katika ulimwengu huu atailinda kwa uhai udumuo milele. 26 Ikiwa yeyote angenihudumia, acha anifuate mimi, na nilipo mimi ndipo mhudumu wangu atakuwa pia. Ikiwa yeyote angenihudumia mimi, Baba atamheshimu yeye. 27 Sasa nafsi yangu yataabika, nami nitasema nini? Baba, niokoe kutoka katika saa hii. Hata hivyo, hii ndiyo sababu nimekuja kwenye saa hii. 28 Baba, tukuza jina lako.” Kwa hiyo sauti ikaja kutoka mbinguni: “Mimi nimelitukuza na pia hakika nitalitukuza tena.”
29 Kwa sababu hiyo umati uliosimama huku na huku na kusikia hilo ukaanza kusema kulikuwa kumenguruma. Wengine wakaanza kusema: “Malaika amesema naye.” 30 Kwa kujibu Yesu akasema: “Sauti hii imetokea, si kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu. 31 Sasa kuna kuhukumu ulimwengu huu; sasa mtawala wa ulimwengu huu atatupwa nje. 32 Na bado mimi, nikiinuliwa juu kutoka duniani, hakika nitavuta watu wa namna zote kwangu.” 33 Kwa kweli hili alikuwa akilisema ili kutoa ishara ni kifo cha namna gani alikuwa karibu kufa. 34 Kwa hiyo umati ukamjibu: “Sisi tulisikia kutoka Sheria kwamba Kristo hudumu milele; nawe ni jinsi gani wasema kwamba lazima Mwana wa binadamu ainuliwe juu? Huyu Mwana wa binadamu ni nani?” 35 Kwa hiyo Yesu akawaambia: “Nuru itakuwa miongoni mwenu kwa muda kidogo zaidi. Tembeeni wakati nyinyi mna nuru, ili giza lisiwazidi nguvu; naye ambaye hutembea katika giza hajui anakoenda. 36 Wakati nyinyi mna nuru, dhihirisheni imani katika nuru, kusudi mwe wana wa nuru.”
Yesu alisema mambo hayo akaenda zake na kujificha kutoka kwao. 37 Lakini ijapokuwa alikuwa amefanya ishara nyingi sana mbele yao, hawakuwa wakiweka imani katika yeye, 38 hivi kwamba neno la Isaya nabii likatimizwa ambalo alisema: “Yehova, ni nani ambaye ameweka imani katika jambo lililosikiwa na sisi? Na kwa habari ya mkono wa Yehova, umefunuliwa kwa nani?” 39 Sababu kwa nini wao hawakuweza kuamini ni kwamba tena Isaya alisema: 40 “Yeye amepofusha macho yao na amefanya mioyo yao iwe migumu, ili wasione kwa macho yao na kulielewa wazo kwa mioyo yao na kugeuka kabisa niwaponye.” 41 Isaya alisema mambo haya kwa sababu aliona utukufu wake, naye alisema juu yake. 42 Hata hivyo, wengi hata wa watawala kwa kweli waliweka imani katika yeye, lakini kwa sababu ya Mafarisayo wakawa hawamuungami, kusudi wasifukuzwe katika sinagogi; 43 kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu zaidi ya hata utukufu wa Mungu.
44 Hata hivyo, Yesu akapaaza kilio na kusema: “Yeye ambaye huweka imani katika mimi huweka imani, si katika mimi tu, bali pia katika yeye aliyenituma; 45 na yeye ambaye hunitazama mimi humtazama pia yeye aliyenituma. 46 Mimi nimekuja nikiwa nuru ulimwenguni, ili kila mtu anayeweka imani katika mimi asipate kukaa katika giza. 47 Lakini ikiwa yeyote asikia semi zangu na hazishiki, mimi simhukumu; kwa maana nilikuja, si kuhukumu ulimwengu, bali kuokoa ulimwengu. 48 Yeye ambaye hunipuuza mimi na hapokei semi zangu ana mmoja wa kumhukumu. Neno ambalo nimesema ndilo litakalomhukumu katika siku ya mwisho; 49 kwa sababu mimi sijasema kutokana na msukumo wangu mwenyewe, bali Baba mwenyewe aliyenituma amenipa amri kuhusu lile la kunena na lile la kusema. 50 Pia najua kwamba amri yake yamaanisha uhai udumuo milele. Kwa hiyo mambo nisemayo, kama vile Baba ameniambia hayo, ndivyo nisemavyo [hayo].”