Yohana
13 Sasa, kwa sababu alijua kabla ya msherehekeo wa sikukuu ya kupitwa kwamba saa yake ilikuwa imekuja ya kuhama kutoka katika ulimwengu huu kwenda kwa Baba, Yesu, akiisha kuwa amependa walio wake mwenyewe waliokuwa ulimwenguni, aliwapenda hadi mwisho. 2 Kwa hiyo, mlo wa jioni ulipokuwa ukiendelea, Ibilisi akiwa tayari amekwisha kuweka ndani ya moyo wa Yudasi Iskariote, mwana wa Simoni, amsaliti, 3 yeye, akijua kwamba Baba alikuwa ametia vitu vyote mikononi mwake na kwamba alikuja kutoka kwa Mungu na alikuwa akienda kwa Mungu, 4 aliinuka kutoka penye mlo wa jioni na kuweka kando mavazi yake ya nje. Na, akichukua taulo, akajifunga mwenyewe kiuno. 5 Baada ya hilo akatia maji ndani ya beseni akaanza kuosha miguu ya wanafunzi na kuikausha kwa taulo ambayo kwayo alikuwa amefungwa kiuno. 6 Na kwa hiyo akaja kwa Simoni Petro. Yeye akamwambia: “Bwana, je, wewe unaosha miguu yangu?” 7 Kwa kujibu Yesu akamwambia: “Kile ninachofanya wewe hukielewi wakati wa sasa, bali utaelewa baada ya mambo haya.” 8 Petro akamwambia: “Hakika wewe hutaosha kamwe miguu yangu.” Yesu akamjibu: “Isipokuwa nikuoshe, wewe huna sehemu pamoja na mimi.” 9 Simoni Petro akamwambia: “Bwana, si miguu yangu tu, bali pia mikono yangu na kichwa changu.” 10 Yesu akamwambia: “Yeye ambaye ameoga hahitaji kuoshwa zaidi ya miguu yake, bali ni safi kotekote. Nanyi watu ni safi, lakini si nyinyi nyote.” 11 Kwa kweli, yeye alimjua mtu anayemsaliti. Hii ndiyo sababu alisema: “Si wote kati yenu walio safi.”
12 Basi, alipokuwa ameosha miguu yao akawa amevaa mavazi yake ya nje na kujiegemeza mezani tena, akawaambia: “Je, mwalijua ambalo nimewafanyia nyinyi? 13 Nyinyi huniita, ‘Mwalimu,’ na, ‘Bwana,’ nanyi mwasema sawasawa, kwa maana mimi ni wa namna hiyo. 14 Kwa hiyo, ikiwa mimi, nijapokuwa Bwana na Mwalimu, niliosha miguu yenu, nyinyi pia mwapaswa kuoshana miguu. 15 Kwa maana mimi niliweka kiolezo kwa ajili yenu, ili, kama vile nilivyowafanyia nyinyi, nyinyi mpaswe kufanya pia. 16 Kwa kweli kabisa mimi nawaambia nyinyi, Mtumwa si mkubwa zaidi kuliko bwana-mkubwa wake, wala yeye aliyetumwa si mkubwa zaidi kuliko yeye aliyemtuma. 17 Ikiwa mwajua mambo haya, wenye furaha ni nyinyi ikiwa mwayafanya. 18 Mimi siongei juu ya nyinyi nyote; mimi nawajua wale ambao nimewachagua. Lakini ni ili Andiko lipate kutimizwa, ‘Yeye aliyekuwa na kawaida ya kujilisha mkate wangu ameinua kisigino chake dhidi yangu.’ 19 Kuanzia dakika hii na kuendelea mimi ninawaambia nyinyi kabla ya hilo kutukia, ili wakati litukiapo mpate kuamini kwamba mimi ndiye. 20 Kwa kweli kabisa mimi nawaambia, Yeye apokeaye yeyote nitumaye hunipokea mimi pia. Naye ambaye hunipokea mimi, humpokea pia yeye aliyenituma mimi.”
21 Baada ya kusema mambo haya, Yesu akawa mwenye kutaabika katika roho, naye akatoa ushahidi na kusema: “Kwa kweli kabisa mimi nawaambia nyinyi, Mmoja wenu atanisaliti.” 22 Wanafunzi wakaanza kutazamana, wasijue kabisa alikuwa akisema hilo kuhusu yupi. 23 Kulikuwa kumeegama mbele ya kifua cha Yesu mmoja wa wanafunzi wake, na Yesu alimpenda. 24 Kwa hiyo Simoni Petro akamtolea huyo ishara ya kichwa na kumwambia: “Sema ni kuhusu nani anasema hilo.” 25 Kwa hiyo huyo wa mwisho akaegemea nyuma juu ya kifua cha Yesu na kumwambia: “Bwana, ni nani?” 26 Kwa hiyo Yesu akajibu: “Ni yule ambaye mimi nitampa tonge ambalo nachovya.” Na kwa hiyo, akiisha kuchovya tonge, akalichukua na kumpa Yudasi, mwana wa Simoni Iskariote. 27 Na baada ya hilo tonge ndipo Shetani akaingia katika huyo. Kwa hiyo, Yesu akamwambia: “Lile unalofanya lifanye upesi zaidi.” 28 Hata hivyo, hakuna hata mmoja wa wale wenye kuegama mezani aliyejua ni kwa kusudi gani alimwambia hili. 29 Kwa kweli, baadhi yao walikuwa wakiwazia, kwa kuwa Yudasi alikuwa akilishika sanduku la fedha, kwamba Yesu alikuwa akimwambia: “Nunua vitu ambavyo twahitaji kwa ajili ya msherehekeo,” au kwamba apaswa kuwapa maskini kitu fulani. 30 Kwa hiyo, baada ya yeye kulipokea tonge, mara akatoka akaenda. Na ilikuwa usiku.
31 Kwa sababu hiyo alipokuwa ametoka kwenda, Yesu akasema: “Sasa Mwana wa binadamu ametukuzwa, na Mungu ametukuzwa kwa kuhusiana na yeye. 32 Na Mungu mwenyewe atamtukuza yeye, naye atamtukuza mara hiyo. 33 Watoto wadogo, mimi nipo pamoja nanyi muda kidogo zaidi. Nyinyi mtanitafuta; na kama vile nilivyowaambia Wayahudi, ‘Ninakoenda nyinyi hamwezi kuja,’ mimi nawaambia pia wakati wa sasa. 34 Mimi ninawapa nyinyi amri mpya, kwamba mpendane; kama vile nimewapenda nyinyi, kwamba nyinyi pia mpendane. 35 Kwa hilo wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo miongoni mwenu wenyewe.”
36 Simoni Petro akamwambia: “Bwana, unaenda wapi?” Yesu akajibu: “Ninakoenda wewe huwezi kunifuata sasa, lakini utafuata baadaye.” 37 Petro akamwambia: “Bwana, ni kwa nini siwezi kukufuata wewe kwa wakati wa sasa? Hakika mimi nitatoa nafsi yangu kwa ajili yako.” 38 Yesu akajibu: “Je, wewe utaitoa nafsi yako kwa ajili yangu? Kwa kweli kabisa nakuambia wewe, Jogoo hatawika kwa vyovyote mpaka uwe umenikana mimi mara tatu.”