Yohana
17 Yesu alisema mambo haya, na, akiinua macho yake mbinguni, akasema: “Baba, saa imekuja; mtukuze mwana wako, ili mwana wako apate kukutukuza wewe, 2 kulingana na ambavyo umempa yeye mamlaka juu ya mwili wote, ili, kwa habari ya idadi yote ambao umempa yeye, apate kuwapa uhai udumuo milele. 3 Hii yamaaanisha uhai udumuo milele, wao kuendelea kutwaa ujuzi juu yako wewe, Mungu pekee wa kweli, na juu ya yule uliyemtuma, Yesu Kristo. 4 Mimi nimekutukuza duniani, nikiwa nimemaliza kazi ambayo umenipa kufanya. 5 Kwa hiyo sasa wewe, Baba, nitukuze kando yako mwenyewe kwa utukufu niliokuwa nao kando yako kabla ya ulimwengu kuwa.
6 “Nimefanya jina lako kuwa dhahiri kwa watu ulionipa kutoka ulimwenguni. Walikuwa wako, nawe ukanipa wao, nao wameshika neno lako. 7 Sasa wamekuja kujua kwamba vitu vyote vile ulivyonipa ni kutoka kwako; 8 kwa sababu semi ulizonipa nimewapa wao, nao wamezipokea na hakika wamekuja kujua kwamba nilitoka nikiwa mwakilishi wako, nao wameamini kwamba wewe ulinituma. 9 Mimi nafanya ombi kuwahusu wao; nafanya ombi, si kuhusu ulimwengu, bali kuhusu wale ambao umenipa; kwa sababu wao ni wako, 10 na vitu vyangu vyote ni vyako na vyako ni vyangu, nami nimetukuzwa miongoni mwao.
11 “Pia, mimi simo tena ulimwenguni, bali wao wamo ulimwenguni nami ninakuja kwako. Baba Mtakatifu, walinde kwa sababu ya jina lako mwenyewe ambalo umenipa, ili wawe mmoja kama vile sisi tulivyo. 12 Wakati nilipokuwa pamoja nao nilikuwa na kawaida ya kuwalinda kwa sababu ya jina lako mwenyewe ambalo umenipa; nami nimewatunza, na hata mmoja wao hakuangamizwa ila mwana wa uangamizo, ili andiko lipate kutimizwa. 13 Lakini sasa ninakuja kwako, nami ninasema mambo haya ulimwenguni ili wao wapate kuwa na shangwe yangu katika wao wenyewe kwa ukamili. 14 Nimewapa wao neno lako, lakini ulimwengu umewachukia, kwa sababu wao si sehemu ya ulimwengu, kama vile mimi si sehemu ya ulimwengu.
15 “Nakuomba wewe, si uwachukue kutoka ulimwenguni, bali uwalinde kwa sababu ya yule mwovu. 16 Wao si sehemu ya ulimwengu, kama vile mimi si sehemu ya ulimwengu. 17 Watakase kwa njia ya ile kweli; neno lako ni kweli. 18 Kama vile ulivyonituma mimi kuingia ulimwenguni, mimi pia niliwatuma wao kuingia ulimwenguni. 19 Nami ninajitakasa kwa ajili yao, ili wao pia wapate kutakaswa kwa njia ya ile kweli.
20 “Nafanya ombi, si kuhusu hawa tu, bali pia kuhusu wale wanaoweka imani katika mimi kupitia neno lao; 21 ili wote wapate kuwa mmoja, kama vile wewe, Baba, umo katika muungano na mimi na mimi nimo katika muungano na wewe, ili wao pia wapate kuwa katika muungano na sisi, ili ulimwengu upate kuamini kwamba ulinituma mimi. 22 Pia, nimewapa wao utukufu ambao umenipa, ili wapate kuwa mmoja kama vile sisi tulivyo mmoja. 23 Mimi katika muungano na wao na wewe katika muungano na mimi, ili wapate kukamilishwa kuwa mmoja, ili ulimwengu upate kuwa na ujuzi kwamba wewe ulinituma na kwamba uliwapenda wao kama vile ulivyonipenda mimi. 24 Baba, kwa habari ya ambacho umenipa, nataka kwamba, mahali nilipo mimi, wao pia wapate kuwa pamoja nami, kusudi waone utukufu wangu ambao umenipa, kwa sababu ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi wa ulimwengu. 25 Baba Mwadilifu, kwa kweli, ulimwengu haujaja kukujua wewe; lakini mimi nimekuja kukujua, na hawa wamekuja kujua kwamba wewe ulinituma. 26 Nami nimelifanya jina lako lijulikane kwao na hakika nitalifanya lijulikane, ili upendo ulionipenda nao upate kuwa katika wao nami katika muungano na wao.”