Yohana
16 “Mimi nimewaambia nyinyi mambo haya ili msipate kukwazika. 2 Watu watawafukuza nyinyi katika sinagogi. Kwa kweli, saa inakuja wakati kila mtu awauaye nyinyi atawazia amemtolea Mungu utumishi mtakatifu. 3 Lakini watafanya mambo haya kwa sababu hawajaja kumjua ama Baba ama mimi. 4 Hata hivyo, nimewaambia nyinyi mambo haya ili, saa ya haya iwasilipo, mpate kukumbuka niliwaambia nyinyi haya.
“Hata hivyo, mambo haya sikuwaambia nyinyi hapo kwanza, kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi. 5 Lakini sasa ninaenda kwake aliyenituma, na bado hakuna hata mmoja wenu aniulizaye, ‘Unaenda wapi?’ 6 Lakini kwa sababu nimewaambia mambo haya kihoro kimejaa mioyoni mwenu. 7 Hata hivyo, mimi ninawaambia nyinyi kweli, ni kwa manufaa yenu mimi ninaenda zangu. Kwa maana nisipoenda zangu, msaidiaji hatakuja kwenu kwa vyovyote; bali nikishika njia kwenda zangu, hakika nitamtuma yeye kwenu. 8 Na wakati huyo awasilipo ataupa ulimwengu uthibitisho wenye kusadikisha kuhusu dhambi na kuhusu uadilifu na kuhusu hukumu: 9 kwanza, kuhusu dhambi, kwa sababu hawadhihirishi imani katika mimi; 10 kisha kuhusu uadilifu, kwa sababu mimi ninaenda kwa Baba na hamtaniona tena; 11 kisha kuhusu hukumu, kwa sababu mtawala wa ulimwengu huu amehukumiwa.
12 “Bado nina mambo mengi ya kuwaambia nyinyi, lakini hamwezi kuyahimili wakati wa sasa. 13 Hata hivyo, wakati huyo awasilipo, roho ya ile kweli, atawaongoza nyinyi ndani ya kweli yote, kwa maana yeye hatasema kwa msukumo wake mwenyewe, bali mambo ayasikiayo atasema, naye atawatangazia mambo yanayokuja. 14 Huyo atanitukuza mimi, kwa sababu atapokea kutokana na lililo langu na atalitangaza kwenu. 15 Mambo yote aliyo nayo Baba ni yangu. Hiyo ndiyo sababu nilisema yeye hupokea kutokana na lililo langu na hulitangaza kwenu. 16 Baada ya muda kidogo hamtaniona tena, na, tena, baada ya muda kidogo mtaniona.”
17 Kwa hiyo baadhi ya wanafunzi wake wakaambiana: “Hili lamaanisha nini ambalo atuambia, ‘Baada ya muda kidogo hamtaniona, na, tena, baada ya muda kidogo mtaniona,’ na, ‘kwa sababu ninaenda kwa Baba’?” 18 Kwa sababu hiyo walikuwa wakisema: “Hili lamaanisha nini ambalo asema, ‘muda kidogo’? Sisi hatujui analoongea juu yalo.” 19 Yesu alijua walikuwa wanataka kumuuliza swali, kwa hiyo akawaambia: “Je, mnauliziana habari miongoni mwenu wenyewe juu ya hili, kwa sababu nilisema, Baada ya muda kidogo hamtaniona, na, tena, baada ya muda kidogo mtaniona? 20 Kwa kweli kabisa mimi nawaambia, Nyinyi mtatoa machozi na sauti za kuomboleza, bali ulimwengu utashangilia; nyinyi mtatiwa kihoro, lakini kihoro chenu kitageuzwa kiwe shangwe. 21 Mwanamke, anapokuwa akizaa, ana kihoro, kwa sababu saa yake imewasili; lakini wakati amekwisha zaa mtoto mchanga, yeye haikumbuki tena dhiki kwa sababu ya shangwe ya kwamba mtu amezaliwa ulimwenguni. 22 Kwa hiyo, nyinyi pia, sasa, kwa kweli, mna kihoro; lakini mimi nitawaona nyinyi tena na mioyo yenu itashangilia, na shangwe yenu hakuna atakayeichukua kutoka kwenu. 23 Na siku hiyo hamtaniuliza swali hata kidogo. Kwa kweli kabisa mimi nawaambia nyinyi, Mkimwomba Baba kitu chochote atawapa katika jina langu. 24 Hadi wakati huu wa sasa nyinyi hamjaomba hata jambo moja katika jina langu. Ombeni nanyi mtapokea, ili shangwe yenu ipate kujazwa.
25 “Nimewaambia nyinyi mambo haya kwa malinganisho. Saa inakuja wakati ambapo hakika sitasema nanyi tena kwa malinganisho, bali hakika nitaripoti kwenu waziwazi kuhusu Baba. 26 Siku hiyo mtaomba katika jina langu, nami siwaambii kwamba hakika nitafanya ombi kwa Baba kuwahusu nyinyi. 27 Kwa maana Baba mwenyewe ana shauku na nyinyi, kwa sababu nyinyi mmekuwa na shauku na mimi na mmeamini kwamba mimi nilitoka nikiwa mwakilishi wa Baba. 28 Mimi nilitoka kwa Baba na nimekuja ulimwenguni. Na zaidi, ninauacha ulimwengu nami ninashika njia yangu kwenda kwa Baba.”
29 Wanafunzi wake wakasema: “Waona! Sasa unasema waziwazi, na hutamki ulinganisho wowote. 30 Sasa twajua kwamba wajua mambo yote na huhitaji kuulizwa swali na yeyote. Kwa hili sisi twaamini kwamba ulitoka kwa Mungu.” 31 Yesu akawajibu: “Je, mwaamini kwa wakati wa sasa? 32 Tazameni! Saa inakuja, kwa kweli, imekuja, wakati mtakapotawanyika kila mmoja hadi kwenye nyumba yake mwenyewe nanyi mtaniacha peke yangu; na bado mimi siko peke yangu, kwa sababu Baba yuko pamoja nami. 33 Nimewaambia nyinyi mambo haya ili kupitia mimi mpate kuwa na amani. Ulimwenguni mnakuwa na dhiki, lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu.”