Yohana
15 “Mimi ndio mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mlimaji. 2 Kila tawi katika mimi lisilozaa matunda yeye huliondolea mbali, na kila linalozaa matunda yeye hulisafisha, lipate kuzaa matunda zaidi. 3 Tayari nyinyi ni safi kwa sababu ya neno ambalo nimewaambia. 4 Kaeni katika muungano nami, na mimi katika muungano nanyi. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda likiwa pekee isipokuwa likae katika mzabibu, katika njia hiyohiyo wala nyinyi hamwezi, isipokuwa mkae katika muungano nami. 5 Mimi ndio mzabibu, nyinyi ndiyo matawi. Yeye ambaye hukaa katika muungano nami, na mimi katika muungano naye, huyu huzaa matunda mengi; kwa sababu bila mimi hamwezi kufanya lolote hata kidogo. 6 Ikiwa yeyote hakai katika muungano na mimi, yeye hutupwa nje kama tawi na hukauka kabisa; na watu hukusanya matawi hayo na kuyatupa ndani ya moto nayo yanachomwa. 7 Ikiwa nyinyi mwakaa katika muungano nami na semi zangu zakaa katika nyinyi, ombeni lolote lile mtakalo nalo litatukia kwenu. 8 Baba yangu hutukuzwa katika hili, kwamba mfulize kuzaa matunda mengi na kujithibitisha wenyewe kuwa wanafunzi wangu. 9 Kama vile Baba amenipenda mimi nami nimewapenda nyinyi, kaeni katika upendo wangu. 10 Mkishika amri zangu, mtakaa katika upendo wangu, kama vile mimi nimeshika amri za Baba na kukaa katika upendo wake.
11 “Mambo haya nimewaambia, ili shangwe yangu ipate kuwa katika nyinyi na shangwe yenu ipate kufanywa yenye kujaa. 12 Hii ndiyo amri yangu, kwamba mpendane kama vile mimi nimewapenda nyinyi. 13 Hakuna aliye na upendo mkubwa zaidi kuliko huu, kwamba mtu fulani aisalimishe nafsi yake kwa niaba ya marafiki wake. 14 Nyinyi ni marafiki wangu ikiwa mwafanya lile ninalowaamuru nyinyi. 15 Siwaiti nyinyi tena watumwa, kwa sababu mtumwa hayajui yale afanyayo bwana-mkubwa wake. Lakini nimewaita nyinyi marafiki, kwa sababu mambo yote ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu nimewajulisha nyinyi. 16 Nyinyi hamkunichagua mimi, bali mimi niliwachagua nyinyi, nami niliwaweka nyinyi rasmi mwendelee na kufuliza kuzaa matunda na kwamba matunda yenu yapate kukaa; ili hata liwe ni nini mwombalo Baba katika jina langu apate kuwapa nyinyi hilo.
17 “Mambo haya nawaamuru nyinyi, kwamba mpendane. 18 Ikiwa ulimwengu wawachukia nyinyi, mwajua kwamba huo umenichukia mimi kabla ya huo kuwachukia nyinyi. 19 Kama mngekuwa sehemu ya ulimwengu, ulimwengu ungependa sana kilicho chao wenyewe. Sasa kwa sababu nyinyi si sehemu ya ulimwengu, bali nimewachagua nyinyi kutoka ulimwenguni, kwa ajili ya hili ulimwengu huwachukia nyinyi. 20 Zingatieni akilini neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa zaidi kuliko bwana-mkubwa wake. Ikiwa wameninyanyasa mimi, watawanyanyasa nyinyi pia; ikiwa wameshika neno langu, watashika lenu pia. 21 Lakini watafanya mambo yote haya dhidi yenu kwa ajili ya jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma. 22 Kama nisingalikuja na kuwaambia, wasingekuwa na dhambi; lakini sasa hawana sababu ya kujitetea kwa ajili ya dhambi yao. 23 Yeye anichukiaye mimi humchukia Baba yangu pia. 24 Kama nisingalifanya miongoni mwao kazi ambazo hakuna mwingine aliyezifanya, wasingekuwa na dhambi; lakini sasa wameniona na pia wamenichukia mimi na vilevile Baba yangu. 25 Lakini ni ili neno lililoandikwa katika Sheria yao lipate kutimizwa, ‘Walinichukia bila sababu.’ 26 Wakati msaidiaji awasilipo ambaye hakika nitawapelekea nyinyi kutoka kwa Baba, roho ya ile kweli, ambayo yatoka kwa Baba, hiyo itatoa ushahidi juu yangu; 27 nanyi, mtapaswa kutoa ushahidi, kwa sababu mmekuwa pamoja nami kutoka wakati nilipoanza.