Yohana
18 Akiisha kusema mambo haya, Yesu akatoka kwenda pamoja na wanafunzi wake ng’ambo ya mvo wa majira ya baridi kali wa Kidroni hadi mahali palipokuwa na bustani, na yeye na wanafunzi wake wakaingia ndani yayo. 2 Basi Yudasi, msaliti wake, alijua pia hapo mahali, kwa sababu nyakati nyingi Yesu alikuwa amekutana hapo pamoja na wanafunzi wake. 3 Kwa hiyo Yudasi akachukua kikosi cha askari-jeshi na maofisa wa makuhani wakuu na wa Mafarisayo nao wakaja hapo wakiwa na mienge na taa na silaha. 4 Kwa hiyo, Yesu akijua mambo yote yenye kuja juu yake, akatoka na kuwaambia: “Mnatafuta nani?” 5 Wakamjibu: “Yesu Mnazareti.” Akawaambia: “Mimi ndiye.” Basi Yudasi, msaliti wake, alikuwa pia amesimama pamoja nao.
6 Hata hivyo, alipowaambia: “Mimi ndiye,” wakarudi nyuma na kuanguka chini. 7 Kwa hiyo akawauliza tena: “Mnatafuta nani?” Wakasema: “Yesu Mnazareti.” 8 Yesu akajibu: “Niliwaambia mimi ndiye. Kwa hiyo, ikiwa ni mimi mnayetafuta, acheni hawa waende”; 9 ili neno lipate kutimizwa ambalo alisema: “Wa wale ambao umenipa sikupoteza hata mmoja.”
10 Ndipo Simoni Petro, kwa kuwa alikuwa na upanga, akaufuta na kumpiga mtumwa wa kuhani wa cheo cha juu akakatilia mbali sikio lake la kuume. Jina la mtumwa huyo lilikuwa ni Malko. 11 Hata hivyo, Yesu akamwambia Petro: “Tia upanga ndani ya ala yao. Kikombe ambacho Baba amenipa, je, sipaswi kukinywa kwa vyovyote?”
12 Basi kikosi cha askari-jeshi na kamanda wa kijeshi na maofisa wa Wayahudi wakamkamata Yesu na kumfunga, 13 nao wakamwongoza kwanza kwa Anasi; kwa maana alikuwa baba-mkwe wa Kayafa, ambaye alikuwa kuhani wa cheo cha juu mwaka huo. 14 Kwa kweli, Kayafa alikuwa ni yeye aliyewashauri Wayahudi kwamba ilikuwa kwa manufaa yao mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.
15 Sasa Simoni Petro na vilevile mwanafunzi mwingine alikuwa akimfuata Yesu. Mwanafunzi huyo alijulikana na kuhani wa cheo cha juu, naye aliingia pamoja na Yesu ndani ya ua wa kuhani wa cheo cha juu, 16 lakini Petro alikuwa amesimama nje kwenye mlango. Kwa hiyo yule mwanafunzi mwingine, ambaye alijulikana na kuhani wa cheo cha juu, akatoka nje na kusema na mtunza-mlango akamwingiza Petro ndani. 17 Basi msichana mtumishi, aliye mtunza-mlango, akamwambia Petro: “Wewe pia si mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu, ndivyo?” Akasema: “Mimi siye.” 18 Sasa wale watumwa na maofisa walikuwa wamesimama huku na huku, kwa kuwa walikuwa wamefanya moto wa makaa, kwa sababu kulikuwa na baridi, nao walikuwa wakijipasha moto. Petro pia alikuwa amesimama pamoja nao akijipasha mwenyewe moto.
19 Na kwa hiyo kuhani mkuu akamuuliza Yesu maswali juu ya wanafunzi wake na juu ya fundisho lake. 20 Yesu akamjibu: “Mimi nimesema na ulimwengu hadharani. Sikuzote nilifundisha katika sinagogi na katika hekalu, ambapo Wayahudi wote huja pamoja; nami sikusema jambo lolote katika siri. 21 Kwa nini waniuliza maswali? Waulize maswali wale ambao wamesikia lile nililowaambia. Ona! Hawa wajua lile nililosema.” 22 Baada ya yeye kusema mambo hayo, mmoja wa maofisa aliyekuwa amesimama kando akampiga Yesu kofi usoni na kusema: “Je, hiyo ndiyo njia ambayo wamjibu kuhani mkuu?” 23 Yesu akamjibu: “Ikiwa nilisema kwa makosa, toa ushahidi kuhusu hilo kosa; lakini ikiwa ni sawasawa, kwa nini wanipiga?” 24 Basi Anasi akaagiza apelekwe kwa Kayafa kuhani wa cheo cha juu akiwa amefungwa.
25 Sasa Simoni Petro alikuwa amesimama akijipasha moto. Ndipo wakamwambia: “Wewe pia si mmoja wa wanafunzi wake, ndivyo?” Yeye akakana hilo na kusema: “Mimi siye.” 26 Mmoja wa watumwa wa kuhani wa cheo cha juu, akiwa ni jamaa ya mtu ambaye Petro alikatilia mbali sikio lake, akasema: “Mimi nilikuona wewe katika bustani pamoja naye, sivyo?” 27 Hata hivyo, Petro akakana hilo tena; na mara jogoo akawika.
28 Basi wakamwongoza Yesu kutoka kwa Kayafa hadi kwenye ikulu ya gavana. Sasa ilikuwa ni mapema katika siku. Lakini wao wenyewe hawakuingia ndani ya ikulu ya gavana, ili wasipate kutiwa unajisi bali wapate kula sikukuu ya kupitwa. 29 Kwa hiyo Pilato akawajia nje na kusema: “Ni shtaka gani ambalo mwaleta dhidi ya mtu huyu?” 30 Kwa kujibu wakamwambia: “Kama mtu huyu asingekuwa mkosaji, tusingalimkabidhi kwako.” 31 Kwa sababu hiyo Pilato akawaambia: “Mchukueni nyinyi wenyewe na kumhukumu kulingana na sheria yenu.” Wayahudi wakamwambia: “Hairuhusiki kisheria sisi kumuua mtu yeyote.” 32 Hili, kusudi neno la Yesu lipate kutimizwa alilosema ili kutoa ishara ni kifo cha namna gani alichokusudiwa kufa.
33 Kwa hiyo Pilato akaingia tena ndani ya ikulu ya gavana naye akamwita Yesu na kumwambia: “Je, wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” 34 Yesu akajibu: “Je, ni kwa ubuni wako mwenyewe kwamba wasema hilo, au wengine walikuambia juu yangu?” 35 Pilato akajibu: “Mimi si Myahudi, je, ni hivyo? Taifa lako mwenyewe na makuhani wakuu walikukabidhi kwangu. Wewe ulifanya nini?” 36 Yesu akajibu: “Ufalme wangu si sehemu ya ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa sehemu ya ulimwengu huu, mahadimu wangu wangalipigana ili nisikabidhiwe kwa Wayahudi. Lakini, kama ilivyo, ufalme wangu si kutoka chanzo hiki.” 37 Kwa hiyo Pilato akamwambia: “Hivyo, basi, je, wewe ni mfalme?” Yesu akajibu: “Wewe mwenyewe unasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa ajili ya hili mimi nimezaliwa, na kwa ajili ya hili nimekuja kuingia ulimwenguni, ili nitoe ushahidi juu ya ile kweli. Kila mtu aliye upande wa ile kweli husikiliza sauti yangu.” 38 Pilato akamwambia: “Kweli ni nini?”
Na baada ya kusema hili, akatoka tena kwenda kwa Wayahudi na kuwaambia: “Mimi sipati kosa lolote katika yeye. 39 Zaidi ya hayo, nyinyi mna desturi kwamba mimi napaswa kuwafungulia mtu kwenye sikukuu ya kupitwa. Kwa hiyo, je, mwataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi?” 40 Basi wakapaaza sauti tena, wakisema: “Si mtu huyu, bali Baraba!” Basi Baraba alikuwa mpokonyaji.