Yohana
19 Kwa hiyo, wakati huo Pilato akamchukua Yesu na kumpiga mijeledi. 2 Nao askari-jeshi wakasuka taji la miiba na kuliweka juu ya kichwa chake nao wakampamba kwa vazi la nje la kizambarau; 3 nao wakaanza kumjia na kusema: “Siku njema, wewe Mfalme wa Wayahudi!” Pia wakawa wakimpiga makofi usoni. 4 Naye Pilato akaenda nje tena na kuwaambia: “Oneni! Namleta nje kwenu kusudi nyinyi mjue kwamba sipati kosa lolote katika yeye.” 5 Basi Yesu akaja nje, amevaa taji lenye miiba na vazi la nje la kizambarau. Naye akawaambia: “Tazameni! Mwanamume!” 6 Hata hivyo, wakati makuhani wakuu na maofisa walipomwona, wakapaaza sauti, wakisema: “Mtundike mtini! Mtundike mtini!” Pilato akawaambia: “Mchukueni nyinyi wenyewe mmtundike mtini, kwa maana mimi sipati kosa lolote katika yeye.” 7 Wayahudi wakamjibu: “Sisi tuna sheria, na kulingana na sheria yeye apaswa kufa, kwa sababu alijifanya mwenyewe mwana wa Mungu.”
8 Kwa hiyo, Pilato aliposikia usemi huu, akawa mwenye hofu zaidi; 9 naye akaingia ndani ya ikulu ya gavana tena na kumwambia Yesu: “Wewe ni wa kutoka wapi?” Lakini Yesu hakumpa jibu. 10 Kwa sababu hiyo Pilato akamwambia: “Je, husemi nami? Je, hujui mimi nina mamlaka ya kukufungua na nina mamlaka ya kukutundika mtini?” 11 Yesu akamjibu: “Wewe hungekuwa na mamlaka hata kidogo dhidi yangu isipokuwa uwe ulikuwa umepewa hiyo kutoka juu. Hii ndiyo sababu mtu aliyenikabidhi kwako ana dhambi kubwa zaidi.”
12 Kwa sababu hii Pilato akafuliza kutafuta sana jinsi ya kumfungua. Lakini Wayahudi wakapaaza sauti, wakisema: “Ukimfungua mtu huyu, wewe si rafiki ya Kaisari. Kila mtu anayejifanya mwenyewe mfalme asema vibaya dhidi ya Kaisari.” 13 Kwa hiyo Pilato, baada ya kusikia maneno haya, akamleta Yesu nje, naye akaketi juu ya kiti cha hukumu mahali paitwapo Sakafu ya Jiwe, lakini, katika Kiebrania, Gabatha. 14 Sasa ilikuwa ni matayarisho ya sikukuu ya kupitwa; ilikuwa karibu saa ya sita. Naye akawaambia Wayahudi: “Oneni! Mfalme wenu!” 15 Hata hivyo, wakapaaza sauti: “Mwondolee mbali! Mwondolee mbali! Mtundike mtini!” Pilato akawaambia: “Je, nitamtundika mtini mfalme wenu?” Makuhani wakuu wakajibu: “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.” 16 Kwa hiyo, wakati huo akamkabidhi kwao atundikwe mtini.
Basi wakamchukua Yesu. 17 Naye, akijichukulia mti wa mateso, akatoka kwenda pale paitwapo kwa kawaida Mahali pa Fuvu la Kichwa, paitwapo Golgotha katika Kiebrania; 18 na huko wakamtundika mtini, na watu wengine wawili pamoja naye, mmoja upande huu na mmoja upande huu, lakini Yesu katikati. 19 Pilato akaandika pia tangazo na kuliweka juu ya huo mti wa mateso. Liliandikwa: “Yesu Mnazareti Mfalme wa Wayahudi.” 20 Kwa hiyo wengi wa Wayahudi walisoma hili tangazo, kwa sababu mahali ambapo Yesu alitundikwa mtini palikuwa karibu na jiji; nalo liliandikwa katika Kiebrania, katika Kilatini, katika Kigiriki. 21 Hata hivyo, makuhani wakuu wa Wayahudi wakaanza kumwambia Pilato: “Usiandike ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali kwamba yeye alisema, ‘Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.’” 22 Pilato akajibu: “Lile ambalo nimeandika nimeandika.”
23 Sasa wakati askari-jeshi walipokuwa wamemtundika Yesu mtini, walichukua mavazi yake ya nje na kufanya sehemu nne, kwa kila askari-jeshi sehemu moja, na vazi la ndani. Lakini lile vazi la ndani lilikuwa halina mshono, likiwa limefumwa kutoka juu hadi urefu walo wote. 24 Kwa hiyo wakaambiana: “Tusilirarue, bali na tuamue kwa kura juu yalo litakuwa la nani.” Hii ilikuwa ili andiko lipate kutimizwa: “Waligawana mavazi yangu ya nje miongoni mwao wenyewe, na juu ya vao langu walipiga kura.” Ndivyo hasa hao askari-jeshi walivyofanya mambo haya.
25 Hata hivyo, kando ya mti wa mateso wa Yesu, palikuwa pamesimama mama yake na dada ya mama yake; Maria mke wa Klopasi, na Maria Magdalene. 26 Kwa hiyo Yesu, kwa kuona mama yake na mwanafunzi ambaye yeye alimpenda wamesimama kando, akamwambia mama yake: “Mwanamke, ona! Mwana wako!” 27 Halafu akamwambia mwanafunzi huyo: “Ona! Mama yako!” Na tangu saa hiyo na kuendelea huyo mwanafunzi akampeleka nyumbani kwake mwenyewe.
28 Baada ya hili, Yesu alipojua kwamba kufikia sasa mambo yote yalikuwa yametimizwa, ili andiko lipate kutimizwa akasema: “Nina kiu.” 29 Chombo kimoja kilikuwa hapo chenye kujaa divai iliyochacha. Kwa hiyo wakaweka sponji yenye kujaa divai iliyochacha juu ya shina la hisopo na kulileta kwenye kinywa chake. 30 Sasa, alipokuwa amepokea divai iliyochacha, Yesu akasema: “Imetimizwa!” na, akiinamisha kichwa chake, akaikabidhi roho yake.
31 Basi Wayahudi, kwa kuwa yalikuwa ni Matayarisho, ili miili hiyo isipate kukaa juu ya miti ya mateso siku ya Sabato, (kwa maana siku ya Sabato hiyo ilikuwa kubwa,) wakamwomba Pilato aagize miguu yao ivunjwe na miili iondolewe. 32 Kwa hiyo, askari-jeshi wakaja na kuvunja miguu ya mtu wa kwanza na ile ya yule mtu mwingine aliyekuwa ametundikwa mtini pamoja naye. 33 Lakini walipokuja kwa Yesu, kwa kuwa waliona kwamba tayari alikuwa amekufa, hawakuvunja miguu yake. 34 Lakini mmoja wa hao askari-jeshi alichoma ubavu wake kwa mkuki, na mara damu na maji vikatoka. 35 Na yeye ambaye ameona hilo ametoa ushahidi, nao ushahidi wake ni wa kweli, na mtu huyo ajua yeye husema mambo ya kweli, ili nyinyi pia mweze kuamini. 36 Kwa kweli, mambo haya yalitendeka kusudi andiko litimizwe: “Hakuna hata mfupa wake mmoja utakaopondwa.” 37 Na, tena, andiko tofauti lasema: “Watatazama Kwake waliyemdunga.”
38 Basi baada ya mambo haya Yosefu kutoka Arimathea, aliyekuwa mwanafunzi wa Yesu lakini wa siri kutokana na kuhofu kwake Wayahudi, alimwomba Pilato kwamba apate kuondoa mwili wa Yesu; naye Pilato akampa ruhusa. Kwa hiyo akaja na kuuondoa mwili wake. 39 Nikodemo pia, yule mtu aliyemjia usiku mara ya kwanza, alikuja akileta kikuto cha manemane na udi, karibu ratili mia zayo. 40 Basi wakauchukua mwili wa Yesu na kuufunga kwa mabendeji pamoja na manukato, sawa na jinsi Wayahudi walivyo na desturi ya kutayarisha kwa ajili ya maziko. 41 Ilitukia kwamba, mahali alipotundikwa mtini palikuwa na bustani, na katika hiyo bustani kaburi jipya la ukumbusho, ambalo bado hakuna yeyote aliyekuwa amelazwa ndani yalo. 42 Humo, basi, kwa ajili ya matayarisho ya Wayahudi, ndimo walimlaza Yesu, kwa sababu kaburi la ukumbusho lilikuwa hapo karibu.