Yohana
20 Siku ya kwanza ya juma Maria Magdalene alikuja mapema kwenye kaburi la ukumbusho, wakati kulipokuwa bado giza, naye akaona jiwe likiwa tayari limeondolewa mbali kutoka kwenye kaburi la ukumbusho. 2 Kwa hiyo akakimbia na kuja kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine, ambaye Yesu alikuwa na shauku naye, naye akawaambia: “Wamemwondoa Bwana kutoka katika kaburi la ukumbusho, nasi hatujui ni wapi wamemlaza.”
3 Ndipo Petro na yule mwanafunzi mwingine wakatoka kwenda na kuanza kuliendea kaburi la ukumbusho. 4 Ndiyo, hao wawili pamoja wakaanza kukimbia; lakini yule mwanafunzi mwingine alikimbia mbele ya Petro kwa kasi zaidi naye akalifikia kaburi la ukumbusho kwanza. 5 Naye, akiinama mbele, akaona mabendeji yamelala, lakini hakuingia. 6 Ndipo Simoni Petro pia akaja akimfuata, naye akaingia ndani ya kaburi la ukumbusho. Naye akaona mabendeji yamelala, 7 pia nguo iliyokuwa imekuwa juu ya kichwa chake ikiwa haipo pamoja na mabendeji bali imebiringwa mahali pamoja ikiwa pekee. 8 Kwa hiyo, wakati huo mwanafunzi yule mwingine aliyekuwa amefika kwanza kwenye kaburi la ukumbusho akaingia pia, naye akaona na kuamini. 9 Kwa maana bado hawakufahamu andiko kwamba lazima afufuliwe kutoka kwa wafu. 10 Na kwa hiyo wanafunzi wakarudi nyumbani kwao.
11 Hata hivyo, Maria alifuliza kusimama nje karibu na kaburi la ukumbusho, akitoa machozi. Ndipo, alipokuwa akitoa machozi, akainama mbele kutazama ndani ya kaburi la ukumbusho 12 naye akaona malaika wawili waliovaa meupe wameketi mmoja penye kichwa na mmoja penye miguu ambapo mwili wa Yesu ulikuwa umekuwa umelala. 13 Nao wakamwambia: “Mwanamke, kwa nini unatoa machozi?” Yeye akawaambia: “Wamemwondoa Bwana wangu, nami sijui wamemlaza wapi.” 14 Baada ya kusema mambo haya, akageuka nyuma na kumwona Yesu amesimama, lakini hakufahamu alikuwa ni Yesu. 15 Yesu akamwambia: “Mwanamke, kwa nini unatoa machozi? Unatafuta nani?” Yeye, akiwaza alikuwa ni mtunza-bustani, akamwambia: “Bwana, ikiwa umemchukua, niambie ni wapi umemlaza, na hakika nitamwondoa.” 16 Yesu akamwambia: “Maria!” Alipogeuka kabisa, Maria akamwambia, katika Kiebrania: “Raboni!” (ambalo lamaanisha “Mwalimu!”) 17 Yesu akamwambia: “Acha kuniambatia. Kwa maana bado sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini shika njia yako uende kwa ndugu zangu nawe uwaambie, ‘Mimi ninapaa kwenda kwa Baba yangu na Baba yenu na kwa Mungu wangu na Mungu wenu.’” 18 Maria Magdalene akaja na kuleta hizo habari kwa wanafunzi: “Mimi nimemwona Bwana!” na kwamba alimwambia mambo haya.
19 Kwa hiyo, ilipokuwa jioni-jioni siku hiyo, siku ya kwanza ya juma, na, ijapokuwa milango ilikuwa imefungwa kwa kufuli mahali ambamo wanafunzi walikuwa kwa kuhofu Wayahudi, Yesu alikuja na kusimama katikati yao na kuwaambia: “Na mwe na amani.” 20 Na baada ya kusema hayo akawaonyesha mikono yake miwili na ubavu wake. Basi hao wanafunzi wakashangilia kwa kumwona Bwana. 21 Kwa hiyo, Yesu akawaambia tena: “Na mwe na amani. Kama vile Baba amenituma, mimi pia ninawatuma nyinyi.” 22 Na baada ya kusema hili akapuliza juu yao na kuwaambia: “Pokeeni roho takatifu. 23 Mkisamehe dhambi za watu wowote, zadumu wakiwa wamesamehewa hizo; msiposamehe zile za watu wowote, zadumu bila kusamehewa.”
24 Lakini Tomasi, mmoja wa wale kumi na wawili, aliyeitwa Pacha, hakuwa pamoja nao wakati Yesu alipokuja. 25 Kwa sababu hiyo wanafunzi wengine wakawa wamwambia: “Tumemwona Bwana!” Lakini yeye akawaambia: “Isipokuwa nione katika mikono yake chapa ya misumari na nitie kidole changu ndani ya chapa ya misumari na kutia mkono wangu ndani ya ubavu wake, hakika kabisa mimi sitaamini.”
26 Basi, siku nane baadaye wanafunzi wake walikuwa tena ndani ya nyumba, naye Tomasi alikuwa pamoja nao. Yesu akaja, ijapokuwa milango ilikuwa imefungwa kwa kufuli, naye akasimama katikati yao akasema: “Na mwe na amani.” 27 Halafu akamwambia Tomasi: “Weka kidole chako hapa, uone mikono yangu, na chukua mkono wako utie ndani ya ubavu wangu, na koma kuwa asiyeamini bali uwe mwenye kuamini.” 28 Kwa kujibu Tomasi akamwambia: “Bwana wangu na Mungu wangu!” 29 Yesu akamwambia: “Kwa sababu umeniona mimi je, umeamini? Wenye furaha ni wale ambao hawaoni na bado waamini.”
30 Kwa hakika, Yesu alifanya pia ishara nyingine nyingi mbele ya hao wanafunzi, ambazo hazikuandikwa katika hati-kunjo hii. 31 Lakini haya yameandikwa ili mpate kuamini kwamba Yesu ndiye Kristo Mwana wa Mungu, na kwamba, kwa sababu ya kuamini, nyinyi mpate kuwa na uhai kwa njia ya jina lake.