Yohana
21 Baada ya mambo haya Yesu alijidhihirisha tena kwa wanafunzi kwenye bahari ya Tiberiasi; lakini alifanya huo udhihirisho katika njia hii. 2 Waliokuwa pamoja ni Simoni Petro na Tomasi, aliyeitwa Pacha, na Nathanaeli kutoka Kana ya Galilaya na wana wa Zebedayo na wengine wawili wa wanafunzi wake. 3 Simoni Petro akawaambia: “Ninaenda kuvua samaki.” Wakamwambia: “Sisi pia tunakuja pamoja nawe.” Wakatoka kwenda wakapanda ndani ya mashua, lakini usiku huo hawakuvua kitu.
4 Hata hivyo, ilipokuwa tu inapata kuwa asubuhi, Yesu alisimama ufuoni, lakini wanafunzi, bila shaka, hawakufahamu kwamba alikuwa Yesu. 5 Basi Yesu akawaambia: “Watoto wachanga, hamna kitu chochote cha kula, je, mnacho?” Wakamjibu: “La!” 6 Akawaambia: “Tupeni wavu upande wa kuume wa mashua nanyi mtapata baadhi yao.” Basi wakautupa, lakini hawakuweza tena kuuvuta ndani kwa sababu ya wingi mkubwa wa samaki. 7 Kwa sababu hiyo mwanafunzi ambaye Yesu alikuwa na kawaida ya kumpenda akamwambia Petro: “Ni Bwana!” Kwa hiyo Simoni Petro, aliposikia kwamba alikuwa Bwana, akajifunga mwenyewe kwa kujizungushia kiunoni vazi lake la juu, kwa maana alikuwa uchi, na kujitumbukiza ndani ya bahari. 8 Lakini wale wanafunzi wengine wakaja katika ile mashua ndogo, kwa maana hawakuwa mbali na nchi kavu, karibu umbali wa meta tisini tu, wakiukokota wavu wa samaki wengi.
9 Hata hivyo, wakati waliposhuka kwenye nchi kavu wakaona umewekwa hapo moto wa makaa na samaki wamewekwa juu yao na mkate. 10 Yesu akawaambia: “Leteni baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi.” 11 Kwa hiyo, Simoni Petro akapanda ndani na kuvuta wavu kwenye nchi kavu ukiwa umejaa samaki wakubwa, mia na hamsini na watatu. Lakini ijapokuwa kulikuwako wengi sana wavu haukupasuka. 12 Yesu akawaambia: “Njoni, twaeni kifungua-kinywa chenu.” Hakuna hata mmoja wa wanafunzi aliyekuwa na moyo wa kuulizia habari kwake: “Wewe ni nani?” kwa sababu walijua alikuwa Bwana. 13 Yesu akaja akachukua mkate na kuwapa, na samaki hivyohivyo. 14 Sasa hii ilikuwa ni mara ya tatu ambayo Yesu alionekana kwa wanafunzi baada ya kufufuliwa kwake kutoka kwa wafu.
15 Sasa, walipokuwa wamepata kifungua-kinywa, Yesu akamwambia Simoni Petro: “Simoni mwana wa Yohana, je, wanipenda mimi kuliko hawa?” Yeye akamwambia: “Ndiyo, Bwana, wajua nina shauku na wewe.” Akamwambia: “Lisha wana-kondoo wangu.” 16 Tena akamwambia, mara ya pili: “Simoni mwana wa Yohana, je, wanipenda mimi?” Yeye akamwambia: “Ndiyo, Bwana, wajua nina shauku na wewe.” Yeye akamwambia: “Chunga kondoo wangu wadogo.” 17 Akamwambia mara ya tatu: “Simoni mwana wa Yohana, je, una shauku na mimi?” Petro akatiwa kihoro kwamba alimwambia mara ya tatu: “Je, una shauku na mimi?” Kwa hiyo yeye akamwambia: “Bwana, wewe wajua mambo yote; wewe wajua kwamba mimi nina shauku na wewe.” Yesu akamwambia: “Lisha kondoo wangu wadogo. 18 Kwa kweli kabisa mimi nakuambia wewe, Ulipokuwa kijana zaidi, ulikuwa ukijifunga kiuno na kutembea huku na huku ulikotaka. Lakini wakati uzeekapo utanyoosha mikono yako na mtu mwingine atakufunga kiuno na kukuchukua usikotaka wewe.” 19 Hilo alisema ili kutoa ishara ni kwa kifo cha namna gani angemtukuza Mungu. Kwa hiyo, alipokuwa amesema hilo, akamwambia: “Endelea kunifuata mimi.”
20 Alipogeuka huku na huku Petro alimwona mwanafunzi ambaye Yesu alikuwa na kawaida ya kumpenda akifuata, yule ambaye kwenye mlo wa jioni alikuwa pia ameegama nyuma juu ya kifua chake akasema: “Bwana, ni nani anayekusaliti?” 21 Basi, alipomwona mara hiyo, Petro akamwambia Yesu: “Bwana, mtu huyu atafanya nini?” 22 Yesu akamwambia: “Ikiwa ni mapenzi yangu adumu hadi nije, hilo lakuhusu nini wewe? Wewe endelea kunifuata mimi.” 23 Kwa sababu hiyo, usemi huo ulitoka ukaenda miongoni mwa akina ndugu, kwamba huyo mwanafunzi hangekufa. Hata hivyo, Yesu hakumwambia kwamba hangekufa, bali: “Ikiwa ni mapenzi yangu adumu hadi nije, hilo lakuhusu nini wewe?”
24 Huyu ndiye mwanafunzi ambaye atoa ushahidi juu ya mambo haya na ambaye aliyaandika mambo haya, na sisi twajua kwamba ushahidi atoao ni wa kweli.
25 Kwa kweli, kuna mambo mengine mengi pia aliyofanya Yesu, ambayo, kama ingetukia wakati wowote yaandikwe kirefu kabisa, mimi nadhani ulimwengu wenyewe haungeweza kuwa na nafasi ya kuziweka hati-kunjo ambazo zingeandikwa.