Yohana
2 Basi siku ya tatu karamu ya ndoa ilikuwa katika Kana ya Galilaya, na mama ya Yesu alikuwa huko. 2 Yesu na wanafunzi wake walialikwa pia kwenye karamu ya ndoa.
3 Divai ilipopungua mama ya Yesu alimwambia: “Hawana divai.” 4 Lakini Yesu akamwambia: “Nina jambo gani na wewe, mwanamke? Saa yangu haijaja bado.” 5 Mama yake akawaambia wale wenye kuhudumia: “Lolote lile awaambialo nyinyi, fanyeni.” 6 Kama ilivyokuwa, kulikuwako mitungi sita ya maji ikiwa imekaa hapo kama ilivyotakwa na kanuni za utakaso za Wayahudi, kila mmoja ukiwa waweza kuchukua vipimo viwili au vitatu vya maji. 7 Yesu akawaambia: “Ijazeni maji mitungi ya maji.” Nao wakaijaza pomoni. 8 Naye akawaambia: “Choteni baadhi yayo sasa na kumpelekea mwelekezi wa karamu.” Kwa hiyo wakayapeleka. 9 Basi, wakati mwelekezi wa karamu alipoyaonja maji yaliyokuwa yamegeuzwa kuwa divai, lakini hakujua chanzo chayo kilikuwa nini, ijapokuwa wale wenye kuhudumia waliokuwa wamechota hayo maji walijua, mwelekezi wa karamu alimwita bwana-arusi 10 na kumwambia: “Kila mtu mwingineye hutoa divai bora kwanza, na hafifu wakati watu waingiwapo na kileo. Wewe umeweka akiba divai bora hadi sasa.” 11 Yesu alifanya hilo katika Kana ya Galilaya likiwa mwanzo wa ishara zake, naye akafanya utukufu wake kuwa dhahiri; na wanafunzi wake wakaweka imani katika yeye.
12 Baada ya hilo, yeye na mama na ndugu zake na wanafunzi wake waliteremka kwenda Kapernaumu, lakini hawakukaa huko siku nyingi.
13 Basi sikukuu ya kupitwa ya Wayahudi ilikuwa karibu, na Yesu alipanda kwenda Yerusalemu. 14 Naye alikuta katika hekalu wale wanaouza ng’ombe na kondoo na njiwa na wavunja-fedha katika viti vyao. 15 Kwa hiyo, baada ya kufanya mjeledi wa kamba, aliondosha nje ya hekalu wale wote wenye kondoo na ng’ombe, naye akamwaga sarafu za wabadili-fedha na kupindua meza zao. 16 Naye akawaambia wale wenye kuuza njiwa: “Ondoleeni mbali vitu hivi kutoka hapa! Komeni kufanya nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya bidhaa za biashara!” 17 Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba imeandikwa: “Bidii kwa ajili ya nyumba yako itanila mimi kabisa.”
18 Kwa hiyo, kwa kujibu, Wayahudi wakamwambia: “Una ishara gani ya kutuonyesha, kwa kuwa unafanya mambo haya?” 19 Kwa kujibu Yesu akawaambia: “Vunjeni hekalu hili, na hakika katika siku tatu nitaliinua.” 20 Kwa hiyo Wayahudi wakasema: “Hekalu hili lilijengwa kwa miaka arobaini na sita, nawe je, utaliinua katika siku tatu?” 21 Lakini yeye alikuwa akiongea juu ya hekalu la mwili wake. 22 Ingawa hivyo, wakati alipofufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka kwamba alikuwa na kawaida ya kusema hilo; nao wakaamini Andiko na usemi ambao Yesu alisema.
23 Hata hivyo, wakati alipokuwa Yerusalemu kwenye sikukuu ya kupitwa, kwenye msherehekeo wayo, watu wengi waliweka imani yao katika jina lake, wakitazama ishara zake alizokuwa akifanya. 24 Lakini Yesu mwenyewe hakuwa akijitumainisha mwenyewe kwao kwa sababu ya kuwajua wote 25 na kwa sababu yeye hakuwa na uhitaji wa yeyote kutoa ushahidi juu ya binadamu, kwa maana yeye mwenyewe alijua kile kilichokuwa katika binadamu.