Matendo
Matendo ya Mitume
1 Simulizi la kwanza, Ee Theofilo, nilitunga juu ya mambo yote ambayo Yesu alianza kuyafanya na pia kuyafundisha, 2 hadi siku aliyochukuliwa juu, alipokuwa ametoa amri kupitia roho takatifu kwa mitume aliowachagua. 3 Kwa hawa pia kwa ithibati zilizo hakika alijionyesha yeye mwenyewe kuwa hai alipokuwa ameteseka, akionwa nao wakati wote wa siku arobaini na kusema mambo juu ya ufalme wa Mungu. 4 Naye alipokuwa akikutana pamoja nao aliwapa haya maagizo: “Msiondoke Yerusalemu, bali fulizeni kungojea kile ambacho Baba ameahidi, ambacho mlisikia juu yacho kutoka kwangu; 5 kwa sababu Yohana, kwa kweli, alibatiza kwa maji, lakini nyinyi mtabatizwa katika roho takatifu si siku nyingi baada ya hili.”
6 Basi, wakati walipokuwa wamekusanyika, wakaanza kumuuliza: “Bwana, je, wakati huu unarudishia Israeli ufalme?” 7 Akawaambia: “Si juu yenu kupata ujuzi wa nyakati au majira ambayo Baba ameweka katika mamlaka yake mwenyewe; 8 lakini mtapokea nguvu wakati roho takatifu iwasilipo juu yenu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu na pia katika Yudea yote na Samaria na hadi sehemu ya mbali zaidi sana ya dunia.” 9 Na alipokuwa amesema mambo haya, huku walipokuwa wakitazama, aliinuliwa na wingu likamchukua juu kutoka machoni pao. 10 Nao walipokuwa wakikodoa macho angani alipokuwa ameshika njia yake kwenda, pia, tazama! wanaume wawili wenye mavazi meupe wakasimama kandokando yao, 11 nao wakasema: “Wanaume wa Galilaya, kwa nini mwasimama mkitazama angani? Yesu huyu aliyepokewa juu angani kutoka kwenu atakuja hivyo namna ileile kama vile mmemwona akienda angani.”
12 Ndipo wakarudi Yerusalemu kutoka katika mlima uitwao Mlima wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, ukiwa ni umbali wa safari ya siku ya sabato. 13 Kwa hiyo, walipokuwa wameingia, wakapanda kwenda kuingia katika chumba cha juu, ambamo walikuwa wakikaa, Petro vilevile Yohana na Yakobo na Andrea, Filipo na Tomasi, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo na Simoni mwenye bidii, na Yudasi mwana wa Yakobo. 14 Kwa umoja wote hawa walikuwa wakidumu katika sala, pamoja na wanawake fulani na Maria mama ya Yesu na pamoja na ndugu zake.
15 Sasa katika siku hizo Petro akainuka katikati ya akina ndugu na kusema (umati wa watu ulikuwa wote pamoja karibu mia na ishirini): 16 “Wanaume, akina ndugu, ilikuwa lazima andiko litimizwe, ambalo roho takatifu ilisema kimbele kwa kinywa cha Daudi juu ya Yudasi, aliyekuja kuwa kiongozi kwa wale waliomkamata Yesu, 17 kwa sababu alikuwa amehesabiwa miongoni mwetu naye alipata fungu katika huduma hii. 18 (Kwa hiyo, mtu huyuhuyu alinunua shamba kwa mshahara wa ukosefu wa uadilifu, na akianguka kasi kichwa kwanza akapasuka kwa kelele katikati na matumbo yake yote yakamwagwa nje. 19 Pia ikapata kujulikana kwa wakaaji wote wa Yerusalemu, hivi kwamba shamba hilo likaitwa katika lugha yao Akeldama, yaani, Shamba la Damu.) 20 Kwa maana imeandikwa katika kitabu cha Zaburi, ‘Acha mahali pake pa kukaa pawe ukiwa, na acha pasiwe na mkaaji ndani yapo,’ na, ‘Cheo chake cha uangalizi acha mtu mwingine achukue.’ 21 Kwa hiyo ni lazima kwamba kati ya wanaume waliokusanyika pamoja nasi wakati wote ambao Bwana Yesu aliingia na kutoka miongoni mwetu, 22 kuanza na ubatizo wake uliofanywa na Yohana hadi siku aliyopokewa juu kutoka kwetu, mmoja wa watu hao apaswa kuwa shahidi pamoja nasi juu ya ufufuo wake.”
23 Kwa hiyo wakasimamisha wawili, Yosefu aitwaye Barsaba, aliyeitwa jina la ziada Yustasi, na Mathiasi. 24 Nao wakasali na kusema: “Wewe, Ee Yehova, ambaye wajua mioyo ya wote, onyesha ni yupi kati ya watu wawili hawa ambaye umemchagua, 25 achukue mahali pa huduma na utume huu, ambao kutoka kwao Yudasi alikengeuka kwenda mahali pake mwenyewe.” 26 Kwa hiyo wakapiga kura juu yao, na kura ikamwangukia Mathiasi; naye akahesabiwa pamoja na wale mitume kumi na mmoja.