Waefeso
3 Kwa ajili ya hili mimi, Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu nyinyi, watu wa mataifa— 2 ikiwa, kwa kweli, mmesikia juu ya usimamizi-nyumba wa fadhili isiyostahiliwa ya Mungu ambao nilipewa kwa ajili yenu, 3 kwamba kwa njia ya ufunuo siri takatifu ilijulishwa kwangu, kama vile nilivyoandika hapo awali kwa ufupi. 4 Kuhusiana na hili nyinyi, mwisomapo hii, mwaweza kung’amua ufahamivu nilio nao katika siri takatifu ya Kristo. 5 Katika vizazi vingine siri hii hawakujulishwa wana wa watu kama ambavyo imefunuliwa sasa kwa mitume wake watakatifu na manabii kwa roho, 6 yaani, kwamba watu wa mataifa wawe warithi-washirika na viungo vyenzi vya mwili na washiriki pamoja nasi wa ahadi katika muungano na Kristo Yesu kupitia habari njema. 7 Mimi nikapata kuwa mhudumu wa hilo kulingana na zawadi ya bure ya fadhili isiyostahiliwa ya Mungu niliyopewa kulingana na njia ambayo nguvu yake hutenda.
8 Mimi, niliye mtu mdogo kuliko aliye mdogo zaidi sana kati ya watakatifu wote, nilipewa fadhili hii isiyostahiliwa, ili niwatangazie mataifa habari njema juu ya kina kisichofikilika cha utajiri wa Kristo 9 na kufanya watu waone jinsi siri takatifu inavyosimamiwa ambayo tangu wakati uliopita usio dhahiri imefichwa katika Mungu, aliyeviumba vitu vyote. 10 Hiyo ilikuwa kwa kusudi kwamba sasa serikali na mamlaka zilizo katika mahali pa kimbingu zipate kujulishwa kupitia kutaniko hekima ya Mungu ya namna nyingi, 11 kulingana na kusudi la milele alilofanyiza kuhusiana na Kristo, Yesu Bwana wetu, 12 ambaye kwa njia yake tuna uhuru huu wa usemi na ukaribiaji tukiwa na uhakika kupitia imani yetu katika yeye. 13 Kwa sababu hiyo nawaomba nyinyi msife moyo kwa sababu ya dhiki hizi zangu kwa niaba yenu, kwa maana hizi zamaanisha utukufu wenu.
14 Kwa sababu ya hili namkunjia Baba magoti yangu, 15 ambaye kwake kila familia mbinguni na duniani hupata jina layo, 16 kwa kusudi la kwamba apate kuwaruhusu nyinyi kulingana na utajiri wa utukufu wake ili mfanywe wenye uweza katika mtu mliye kwa ndani mkiwa na nguvu kupitia roho yake, 17 ili mpate kuwa na Kristo akikaa kupitia imani yenu katika mioyo yenu kwa upendo; ili mpate kutia mizizi na kuimarishwa juu ya ule msingi, 18 ili mpate kwa ukamili kuweza kufahamu kiakili pamoja na watakatifu wote ni nini ulio upana na urefu na kimo na kina, 19 na kuujua upendo wa Kristo uzidio ujuzi, ili mpate kujazwa ujao wote ambao Mungu hutoa.
20 Basi kwa yeye awezaye, kulingana na nguvu yake inayotenda ndani yetu, kufanya zaidi kwa wingi uzidio kupita mambo yote tuombayo au tuwazayo, 21 kwake kuwe utukufu kwa njia ya kutaniko na kwa njia ya Kristo Yesu kwa vizazi vyote milele na milele. Ameni.