Waefeso
2 Zaidi ya hilo, ni nyinyi [Mungu aliowafanya kuwa hai] ingawa mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu, 2 ambazo katika hizo wakati fulani nyinyi mlitembea kulingana na mfumo wa mambo wa ulimwengu huu, kulingana na mtawala wa mamlaka ya hewa, roho ambayo sasa hutenda katika wana wa kutotii. 3 Ndiyo, miongoni mwao sisi sote wakati fulani tulijiendesha wenyewe kwa kupatana na tamaa za mwili wetu, tukifanya mambo yanuiwayo na mwili na fikira, nasi kiasili tulikuwa watoto wa hasira ya kisasi sawa na wale wengine. 4 Lakini Mungu, aliye tajiri katika rehema, kwa upendo wake mkubwa aliotupenda, 5 alitufanya hai pamoja na Kristo, hata tulipokuwa wafu katika makosa—kwa fadhili isiyostahiliwa nyinyi mmeokolewa— 6 naye alituinua pamoja na kutuketisha pamoja katika mahali pa kimbingu katika muungano na Kristo Yesu, 7 ili katika mifumo ya mambo inayokuja upate kuonyeshwa utajiri uzidio wote wa fadhili yake isiyostahiliwa katika wema wake kutuelekea katika muungano na Kristo Yesu.
8 Kwa fadhili hii isiyostahiliwa, kwa kweli, nyinyi mmeokolewa kupitia imani; na hiyo si kwa sababu yenu, ni zawadi ya Mungu. 9 La, si kwa sababu ya kazi, ili mtu yeyote asiwe na sababu ya kujisifu. 10 Kwa maana sisi ni tokeo la kazi yake na tuliumbwa katika muungano na Kristo Yesu kwa ajili ya kazi zilizo njema, ambazo Mungu alitangulia kututayarishia ili tutembee katika hizo.
11 Kwa hiyo fulizeni kuzingatia akilini kwamba hapo zamani nyinyi mlikuwa watu wa mataifa kwa habari ya mwili; “kutotahiriwa” ndivyo mlivyoitwa na kile kiitwacho “kutahiriwa” kifanywacho katika mwili kwa mikono — 12 kwamba kwenye wakati huo maalumu mlikuwa bila Kristo, mkifanywa wageni kwa dola la Israeli na mkiwa watu wasiojulikana kwa maagano ya ahadi, nanyi mlikuwa hamna tumaini na mlikuwa bila Mungu katika ulimwengu. 13 Lakini sasa katika muungano na Kristo Yesu nyinyi ambao wakati mmoja mlikuwa mbali sana mmekuja kuwa karibu kupitia damu ya Kristo. 14 Kwa maana yeye ni amani yetu, yeye aliyefanya vile vikundi viwili vya watu kuwa kimoja na kuharibu ukuta wa katikati uliowatenganisha kwa ua. 15 Kwa njia ya mwili wake alibatilisha uadui, Sheria ya amri ambazo asili yazo ni katika maagizo, ili apate kuumba vile vikundi viwili vya watu katika muungano na yeye mwenyewe kuwa mtu mpya mmoja na kufanya amani; 16 na kwamba apate kuvipatanisha kikamili hivyo vikundi viwili vya watu katika mwili mmoja kwa Mungu kupitia mti wa mateso, kwa sababu alikuwa ameua uadui kabisa kwa njia ya yeye mwenyewe. 17 Naye alikuja na kuwatangazia nyinyi habari njema ya amani, nyinyi mliokuwa mbali sana, na pia amani kwa wale waliokuwa karibu, 18 kwa sababu kupitia yeye, sisi, vikundi vyote viwili vya watu, tunao ukaribio kwa Baba kwa roho moja.
19 Kwa hiyo, hakika nyinyi si watu wasiojulikana tena na wakazi wa kigeni, bali nyinyi ni raia wenzi wa watakatifu na ni washiriki wa watu wa nyumbani mwa Mungu, 20 nanyi mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, huku Kristo Yesu mwenyewe akiwa ndiye jiwe la pembeni la msingi. 21 Katika muungano na yeye, jengo lote likiungwa pamoja kwa upatano, linakua liwe hekalu takatifu kwa ajili ya Yehova. 22 Katika muungano na yeye, nyinyi pia mnajengwa pamoja mwe mahali pa Mungu ili akae kwa njia ya roho.