Waefeso
4 Kwa hiyo, mimi, niliye mfungwa katika Bwana, nawasihi nyinyi sana mtembee kwa kustahili wito ambao kwa huo mliitwa, 2 mkiwa na hali kamili ya akili ya kujishusha chini na upole, mkiwa na ustahimilivu, mkichukuliana mtu na mwenzake katika upendo, 3 mkijitahidi sana kwa bidii kushika umoja wa roho katika kifungo chenye kuunganisha cha amani. 4 Kuna mwili mmoja, na roho moja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja mliloitiwa; 5 Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja; 6 Mungu mmoja na Baba wa watu wote, ambaye yuko juu ya wote na kupitia wote na katika wote.
7 Basi kila mmoja wetu alipewa fadhili isiyostahiliwa kulingana na jinsi Kristo alivyopima hiyo zawadi ya bure. 8 Kwa sababu hii yeye asema: “Alipopaa juu alichukua mateka; alitoa zawadi [zikiwa] wanadamu.” 9 Basi usemi “alipopaa juu,” wamaanisha nini ila kwamba alishuka pia katika mikoa ya chini zaidi, yaani, dunia? 10 Yuleyule aliyeshuka ndiye pia aliyepaa juu zaidi sana kuliko mbingu zote, ili apate kuvipa vitu vyote ujao.
11 Naye alitoa wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa waeneza-evanjeli, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwarekebisha upya watakatifu, kwa ajili ya kazi ya huduma, kwa ajili ya kuujenga mwili wa Kristo, 13 mpaka sisi sote tuufikie umoja katika imani na katika ujuzi sahihi wa Mwana wa Mungu, kufikia kuwa mwanamume aliyekua kabisa, kufikia kipimo cha kimo ambacho ni cha ujao wa Kristo; 14 ili tusiwe tena vitoto, tukirushwa huku na huku kama vile na mawimbi na kuchukuliwa huku na huku na kila upepo wa fundisho kwa njia ya mbinu ya hadaa ya watu, kwa njia ya ujanja katika kutunga kosa. 15 Lakini tukisema kweli, na tukue kwa upendo katika mambo yote katika yeye aliye kichwa, Kristo. 16 Kutoka katika yeye mwili wote, kwa kuunganishwa pamoja kwa upatano na kufanywa ushirikiane kupitia kila kiungo ambacho hupa kile kihitajiwacho, kulingana na utendaji wa kila kiungo kimoja-kimoja katika kipimo kipasacho, hutokeza ukuzi wa mwili ili kujijenga huo wenyewe katika upendo.
17 Kwa hiyo, nasema hili na kutoa ushahidi katika Bwana, kwamba nyinyi msiendelee tena kutembea kama vile mataifa watembeavyo pia katika ukosefu wa faida wa akili zao, 18 huku wao wakiwa katika giza kiakili, na kufanywa wageni kwa uhai ambao ni wa Mungu, kwa sababu ya kule kutokuwa na ujuzi ambako kumo ndani yao, kwa sababu ya ukosefu wa hisi wa mioyo yao. 19 Wakiisha kuishiwa na hisia zote za adili, walijikabidhi wenyewe kwenye mwenendo mlegevu ili wafanye ukosefu wa usafi wa kila namna pamoja na pupa.
20 Lakini nyinyi hamkujifunza Kristo kuwa hivyo, 21 kwa kweli, mradi mlimsikia yeye na mlifundishwa kupitia yeye, kama vile kweli ilivyo katika Yesu, 22 ili mweke mbali utu wa hapo zamani unaofuatana na njia yenu ya kwanza ya mwenendo na ambao unafisidiwa kulingana na tamaa zake za udanganyifu; 23 bali ili mfanywe upya katika kani inayotendesha akili yenu, 24 na mvae utu mpya ulioumbwa kulingana na mapenzi ya Mungu katika uadilifu wa kweli na uaminifu-mshikamanifu.
25 Kwa sababu hii, sasa kwa kuwa mmeweka mbali ukosefu wa lililo kweli, semeni kweli kila mmoja wenu pamoja na jirani yake, kwa sababu sisi ni viungo vya mtu na mwenzake. 26 Iweni na hasira ya kisasi, na bado msifanye dhambi; msiache jua litue mkiwa katika hali ya kuchokozeka, 27 wala msiruhusu mahali kwa ajili ya Ibilisi. 28 Mwibaji na asiibe tena, bali acheni afanye kazi ya bidii, akifanya kwa mikono yake kazi iliyo njema, ili apate kuwa na kitu fulani cha kugawa kwa mtu aliye katika uhitaji. 29 Msiache usemi uliooza utoke kinywani mwenu, bali usemi wowote ule ulio mwema kwa ajili ya kujenga kama vile kuwezavyo kuwa na uhitaji, ili huo upate kuwapa wasikiaji lililo la kupendeleka. 30 Pia, msiwe mkiitia kihoro roho takatifu ya Mungu, ambayo kwayo mmetiwa muhuri kwa ajili ya siku ya kuachiliwa kupitia fidia.
31 Acheni uchungu wote wenye nia ya kudhuru na hasira na hasira ya kisasi na kupiga kelele na usemi wenye kuudhi viondolewe mbali kutoka kwenu pamoja na ubaya wote. 32 Bali iweni wenye fadhili nyinyi kwa nyinyi, wenye huruma kwa njia nyororo, mkisameheana kwa hiari mtu na mwenzake kama vile Mungu pia kupitia Kristo alivyowasamehe nyinyi kwa hiari.