Waefeso
5 Kwa hiyo, iweni waigaji wa Mungu, mkiwa watoto wapendwa, 2 na endeleeni kutembea katika upendo, kama vile Kristo pia alivyowapenda nyinyi na kujikabidhi mwenyewe kwa ajili yenu kuwa toleo na dhabihu kwa Mungu ili kuwa harufu yenye mnukio mtamu.
3 Acheni uasherati na ukosefu wa usafi wa kila namna au pupa hata visitajwe hata miongoni mwenu, kama vile ifaavyo watu watakatifu; 4 wala mwenendo wa aibu wala maongezi ya kipumbavu wala kufanya mzaha wenye aibu, mambo yasiyofaa, bali badala ya hivyo utoaji-shukrani. 5 Kwa maana mwajua hili, mkitambua wenyewe hilo, kwamba hakuna mwasherati au mtu asiye safi au mtu mwenye pupa—maana yake kuwa mwabudu-sanamu—aliye na urithi wowote katika ufalme wa Kristo na wa Mungu.
6 Msiache mtu yeyote awadanganye nyinyi kwa maneno matupu, kwa maana kwa sababu ya mambo yaliyotangulia kusemwa hasira ya kisasi ya Mungu inakuja juu ya wana wa kutotii. 7 Kwa hiyo msiwe washiriki pamoja nao; 8 kwa maana wakati mmoja nyinyi mlikuwa giza, bali sasa nyinyi ni nuru kuhusiana na Bwana. Endeleeni kutembea kama watoto wa nuru, 9 kwa maana matunda ya nuru huwa yana kila namna ya wema na uadilifu na kweli. 10 Fulizeni kuhakikisha ni nini lililo lenye kukubalika kwa Bwana; 11 na komeni kushiriki pamoja nao katika kazi zisizozaa matunda zilizo za giza, bali, badala ya hivyo, mwe hata mkizikaripia, 12 kwa maana mambo yatukiayo katika siri kupitia wao ni aibu hata kuyasimulia. 13 Basi mambo yote yanayokaripiwa yafanywa dhahiri na nuru, kwa maana kila kitu kinachofanywa dhahiri ni nuru. 14 Kwa sababu hii yeye asema: “Amka, Ee mlala-usingizi, na inuka kutoka kwa wafu, na Kristo atang’aa juu yako.”
15 Kwa hiyo fulizeni kuangalia sana kwamba jinsi mnavyotembea si kama wasio na hekima bali kama watu wenye hekima, 16 mkijinunulia kabisa wakati unaofaa, kwa sababu siku ni za uovu. 17 Kwa ajili ya hili acheni kuwa wenye kukosa akili, bali endeleeni kufahamu mapenzi ya Yehova ni nini. 18 Pia, msiwe mkilewa divai, ambayo katika hiyo mna ufasiki, bali fulizeni kujazwa roho, 19 mkijisemesha nyinyi wenyewe kwa zaburi na sifa kwa Mungu na nyimbo za kiroho, mkiimba na kufuatanisha sauti zenu wenyewe na muziki katika mioyo yenu kwa Yehova, 20 katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo mkimtolea shukrani sikuzote Mungu wetu na Baba kwa ajili ya mambo yote.
21 Iweni katika ujitiisho kuelekea mmoja na mwenzake katika hofu ya Kristo. 22 Acheni wake wawe katika ujitiisho kwa waume zao kama kwa Bwana, 23 kwa sababu mume ni kichwa cha mke wake kama vile Kristo pia alivyo kichwa cha kutaniko, yeye akiwa mwokozi wa mwili huu. 24 Kwa kweli, kama vile kutaniko lilivyo katika ujitiisho kwa Kristo, ndivyo wanawake pia na wawe kwa waume zao katika kila jambo. 25 Waume, endeleeni kuwapenda wake zenu, kama vile Kristo pia alivyolipenda kutaniko na kujikabidhi mwenyewe kwa ajili yalo, 26 ili apate kulitakasa, akilisafisha kwa mwosho wa maji kwa njia ya neno, 27 ili apate kujitokezea mwenyewe kutaniko likiwa katika fahari yalo, bila doa au kunyanzi au lolote la mambo ya namna hiyo, bali ili liwe takatifu na bila waa.
28 Katika njia hii waume wapaswa kuwa wakiwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Yeye apendaye mke wake ajipenda mwenyewe, 29 kwa maana hakuna mtu aliyepata wakati wowote kuuchukia mwili wake mwenyewe; bali huulisha na kuutunza sana, kama vile Kristo pia alifanyiavyo kutaniko, 30 kwa sababu sisi ni viungo vya mwili wake. 31 “Kwa sababu hii mwanamume ataacha baba yake na mama yake naye atashikamana na mke wake, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.” 32 Siri hii takatifu ni kubwa. Sasa ninasema kwa habari ya Kristo na kutaniko. 33 Hata hivyo, pia, acheni kila mtu mmoja-mmoja kati yenu ampende hivyo mke wake kama yeye mwenyewe; kwa upande mwingine, mke apaswa kuwa na staha yenye kina kirefu kwa mume wake.