Waefeso
6 Watoto, iweni watiifu kwa wazazi wenu katika muungano na Bwana, kwa maana hili ni lenye uadilifu: 2 “Heshimu baba yako na mama yako”; ambayo ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi: 3 “Ili ipate kuwa vema kwako nawe upate kudumu muda mrefu juu ya dunia.” 4 Nanyi, akina baba, msiwe mkiwasumbua watoto wenu, bali endeleeni kuwalea katika nidhamu na rekebisho la akilini la Yehova.
5 Nyinyi watumwa, iweni watiifu kwa wale ambao ni mabwana-wakubwa wenu katika maana ya kimwili, kwa hofu na kutetemeka katika weupe wa mioyo yenu, kama vile kwa Kristo, 6 si kwa njia ya utumishi wa macho kama wapendeza-wanadamu, bali kama watumwa wa Kristo, mkifanya mapenzi ya Mungu kwa nafsi yote. 7 Iweni watumwa mkiwa na maelekeo mema, kama vile kwa Yehova, wala si kwa wanadamu, 8 kwa maana nyinyi mwajua kwamba kila mmoja, uwapo wema wowote apatao kufanya, ataupokea kwa kurudishiwa na Yehova, kama yeye ni mtumwa au mtu huru. 9 Pia, nyinyi mabwana-wakubwa, fulizeni kuwafanyia mambo yaleyale, mkiacha kutisha, kwa maana nyinyi mwajua kwamba Bwana-mkubwa wao na wenu pia yumo katika mbingu, na kwake hakuna ubaguzi wowote.
10 Mwishowe, endeleeni kujipatia nguvu katika Bwana na katika uwezaji wa nguvu yake. 11 Vaeni suti kamili ya silaha kutoka kwa Mungu ili mpate kuweza kusimama imara dhidi ya mbinu za Ibilisi; 12 kwa sababu tuna kushindana mwereka, si dhidi ya damu na mwili, bali dhidi ya serikali, dhidi ya mamlaka, dhidi ya watawala wa ulimwengu wa giza hili, dhidi ya majeshi ya roho waovu katika mahali pa kimbingu. 13 Kwa sababu hiyo chukueni suti kamili ya silaha kutoka kwa Mungu, ili mpate kuweza kukinza katika siku ya uovu na, baada ya nyinyi kuwa mmefanya mambo yote kikamili, kusimama imara.
14 Kwa hiyo, simameni imara mkiwa na viuno vyenu vimefungiwa kweli, na mkiwa mmevaa bamba la kifuani la uadilifu, 15 na miguu yenu ikiwa imevishwa kama viatu vifaa vya habari njema ya amani. 16 Juu ya mambo yote, chukueni ngao kubwa ya imani, ambayo kwayo mtaweza kuzima vishale vyote vinavyowaka moto vya yule mwovu. 17 Pia, pokeeni kofia ya chuma ya wokovu, na upanga wa roho, yaani, neno la Mungu, 18 huku kwa kila namna ya sala na dua mkiendeleza sala kila wakati katika roho. Na kwa lengo hilo fulizeni kuwa macho kwa udumifu wote na kwa dua kwa niaba ya watakatifu wote, 19 pia kwa ajili yangu, ili nipate kupewa uwezo wa kusema kwa kufungua kinywa changu, kwa uhuru wa usemi kujulisha siri takatifu ya habari njema, 20 ambayo kwa ajili yayo ninatenda nikiwa balozi katika minyororo; ili nipate kusema kuhusiana nayo kwa ujasiri kama nipasavyo kusema.
21 Basi ili nyinyi mpate kujua pia juu ya mambo yangu, kuhusu hali yangu ilivyo, Tikiko, ndugu mpendwa na mhudumu mwaminifu katika Bwana, atawajulisha nyinyi kila jambo. 22 Ninamtuma kwenu kwa kusudi hilohilo, ili mpate kuyajua mambo yanayohusiana nasi na kwamba yeye apate kufariji mioyo yenu.
23 Akina ndugu na wawe na amani na upendo pamoja na imani kutoka kwa Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo. 24 Fadhili isiyostahiliwa na iwe pamoja na wote wale wanaompenda Bwana wetu Yesu Kristo katika hali ya kutofisidika.