Wakolosai
2 Kwa maana nataka nyinyi mng’amue jinsi lilivyo kubwa shindano nililo nalo kwa niaba yenu na ya hao walio katika Laodikia na ya wale wote ambao hawajaona uso wangu katika mwili wenye nyama, 2 ili mioyo yao ipate kufarijiwa, kwa kusudi la kupata kuunganishwa pamoja kwa upatano katika upendo na kwa kusudi la kupata utajiri wote wa uhakikisho kamili wa uelewevu wao, kwa kusudi la kupata ujuzi sahihi wa siri takatifu ya Mungu, yaani, Kristo. 3 Zenye kusitiriwa kwa uangalifu ndani yake ni hazina zote za hekima na za ujuzi. 4 Ninasema hili ili mtu yeyote asipate kuwapotosha nyinyi kwa hoja zenye kushawishi. 5 Kwa maana ingawa sipo katika mwili, hata hivyo mimi nipo pamoja nanyi katika roho, nikishangilia na kuona utaratibu wenu mzuri na imara ya imani yenu kuelekea Kristo.
6 Kwa hiyo, kama ambavyo mmempokea Kristo Yesu Bwana, endeleeni kutembea katika muungano na yeye, 7 mkiwa wenye kutia mizizi na kujengwa katika yeye na kuimarishwa katika imani, kama vile mlivyofundishwa, mkifurikwa na imani katika utoaji-shukrani.
8 Jihadharini: labda huenda kukawa na mtu fulani ambaye atawachukua nyinyi kama windo lake kupitia falsafa na udanganyo mtupu kulingana na mapokeo ya wanadamu, kulingana na mambo ya msingi ya ulimwengu na si kulingana na Kristo; 9 kwa sababu ni katika yeye kwamba ujao wote wa sifa ya kimungu hukaa kimwili. 10 Na kwa hiyo nyinyi ni wenye kuwa na ujao kwa njia yake, ambaye ni kichwa cha serikali yote na mamlaka. 11 Kwa uhusiano pamoja naye nyinyi pia mlitahiriwa kwa tohara iliyofanywa bila mikono kwa kuuvua mwili wenye nyama, kwa tohara ambayo ni ya Kristo, 12 kwa maana mlizikwa pamoja naye katika ubatizo wake, na kwa uhusiano pamoja naye mliinuliwa pia pamoja kupitia imani yenu katika utendaji wa Mungu, aliyemfufua yeye kutoka kwa wafu.
13 Zaidi ya hilo, ingawa nyinyi mlikuwa wafu katika makosa yenu na katika hali ya kutotahiriwa ya mwili wenu, Mungu aliwafanya nyinyi kuwa hai pamoja naye. Yeye alitusamehe kwa fadhili makosa yetu yote 14 na kufuta kabisa hati iliyoandikwa kwa mkono dhidi yetu, iliyokuwa na maagizo na iliyokuwa yenye upinzani kwetu; na Yeye ameiondoa njiani kwa kuipigilia misumari kwenye mti wa mateso. 15 Kwa kuzivua na kuziacha utupu serikali na mamlaka, alizionyesha wazi hadharani kuwa zilizoshindwa, akiziongoza katika mwandamano wenye shangwe ya ushindi kwa njia ya huo.
16 Kwa hiyo msiache mtu yeyote awahukumu nyinyi katika kula na kunywa au kwa habari ya msherehekeo au mwadhimisho wa mwezi mpya au wa sabato; 17 kwa maana mambo haya ni kivuli cha mambo yajayo, bali uhalisi ni wa Kristo. 18 Msiache mtu yeyote awazuilie nyinyi tuzo ambaye hupendezwa na unyenyekevu wa dhihaka na namna ya ibada ya malaika, “akichukua msimamo wake juu ya” mambo ambayo ameona, akijitutumua bila sababu ifaayo kwa hali yake ya akili ya kimwili, 19 lakini yeye hashiki kwa imara kile kichwa, yeye ambaye kutoka kwake mwili wote, ukiandaliwa na kuungwa pamoja kwa upatano kwa njia ya viungo vyao na kano, huendelea kukua kwa ukuzi ambao Mungu hutoa.
20 Ikiwa mlikufa pamoja na Kristo kuelekea mambo ya msingi ya ulimwengu, kwa nini nyinyi, kama kwamba mnaishi katika ulimwengu, mwajitiisha wenyewe zaidi kwenye hayo maagizo: 21 “Usishike, wala usionje, wala usiguse,” 22 kwa habari ya mambo ambayo yote yamekusudiwa uharibifu kwa kutumiwa na kwisha kabisa, kwa kupatana na amri na mafundisho mbalimbali ya wanadamu? 23 Kwa kweli, mambo hayahaya yana mwonekano wa kuwa na hekima katika namna ya ibada ya kujitwika na unyenyekevu wa dhihaka, kutendea mwili kwa ukali; lakini hayana thamani yoyote katika kupigana na utoshelezaji wa mwili wenye nyama.