Wakolosai
Kwa Wakolosai
1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu kupitia mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu 2 kwa watakatifu na akina ndugu waaminifu katika muungano na Kristo walioko Kolosai:
Na mwe na fadhili isiyostahiliwa na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu.
3 Sikuzote twamshukuru Mungu Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo tusalipo kwa ajili yenu, 4 kwa kuwa tulisikia juu ya imani yenu kuhusiana na Kristo Yesu na upendo mlio nao kwa watakatifu wote 5 kwa sababu ya tumaini ambalo linawekwa akiba kwa ajili yenu katika mbingu. Tumaini hili mlisikia juu yalo hapo mbele kwa kuelezwa kweli ya habari njema hiyo 6 ambayo imejitokeza yenyewe kwenu, kama inavyozaa matunda na kuongezeka katika ulimwengu wote kama vile inavyofanya pia miongoni mwenu, tangu siku mliposikia na kujua kwa usahihi fadhili isiyostahiliwa ya Mungu katika kweli. 7 Hivyo ndivyo mmejifunza kutoka kwa Epafrasi mtumwa mwenzetu mpendwa, aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa niaba yetu, 8 ambaye pia alitufunulia upendo wenu katika njia ya kiroho.
9 Hiyo ndiyo sababu pia sisi, tangu siku tuliposikia juu ya hilo, hatujaacha kusali kwa ajili yenu na kuomba ili nyinyi mpate kujazwa ujuzi sahihi wa mapenzi yake katika hekima yote na ufahamivu wa kiroho, 10 kusudi mtembee kwa kumstahili Yehova kwa madhumuni ya kumpendeza yeye kikamili mnapoendelea kuzaa matunda katika kila kazi njema na kuongezeka katika ujuzi sahihi wa Mungu, 11 mkifanywa wenye nguvu nyingi kwa nguvu zote kwa kadiri ya uweza wake wenye utukufu ili kuvumilia kikamili na kuwa wenye ustahimilivu pamoja na shangwe, 12 mkimshukuru Baba aliyewafanya nyinyi mfae kushiriki urithi wa watakatifu katika nuru.
13 Yeye alitukomboa kutoka katika mamlaka ya giza na kutuhamisha kuingia katika ufalme wa Mwana wa upendo wake, 14 ambaye kwa njia yake tuna kuachiliwa kwetu kwa njia ya fidia, ule msamaha wa dhambi zetu. 15 Yeye ndio mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa uumbaji wote; 16 kwa sababu kwa njia yake vitu vingine vyote viliumbwa katika mbingu na juu ya dunia, vitu vinavyoonekana na vitu visivyoonekana, hata iwe hivyo ni viti vya ufalme au ubwana au serikali au mamlaka. Vitu vingine vyote vimeumbwa kupitia yeye na kwa ajili yake. 17 Pia, yeye ni wa kabla ya vitu vingine vyote na kwa njia yake vitu vingine vyote vilifanywa viweko, 18 naye ndiye kichwa cha mwili, kutaniko. Yeye ndiye mwanzo, mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili apate kuwa aliye wa kwanza katika vitu vyote; 19 kwa sababu Mungu aliona vema ujao wote ukae katika yeye, 20 na kupitia yeye apatanishe tena kwake mwenyewe vitu vingine vyote kwa kufanya amani kupitia damu aliyoimwaga juu ya mti wa mateso, kwamba ni vitu vilivyo juu ya dunia au vitu vilivyo katika mbingu.
21 Kwa kweli, nyinyi mliokuwa wakati mmoja mmefanywa wageni na mkiwa maadui kwa sababu akili zenu zilikuwa juu ya kazi zilizokuwa zenye uovu, 22 yeye sasa amewapatanisha tena kwa njia ya mwili wenye nyama wa yeye huyo kupitia kifo chake, kusudi awatoe nyinyi mkiwa watakatifu na wasio na waa na bila lawama yoyote mbele yake, 23 mradi, bila shaka, mwaendelea katika imani, mkiwekwa imara juu ya msingi na mkiwa thabiti na bila kuondoshwa mbali kutoka kwenye tumaini la habari njema mliyoisikia, na iliyohubiriwa katika viumbe vyote chini ya mbingu. Juu ya habari njema hii mimi Paulo nikawa mhudumu.
24 Ninashangilia sasa katika mateso yangu kwa ajili yenu, nami, najazia kinachokosekana cha dhiki za Kristo katika mwili wangu kwa niaba ya mwili wake, ambao ni kutaniko. 25 Mimi nikawa mhudumu wa kutaniko hili kwa kupatana na usimamizi-nyumba kutoka kwa Mungu niliopewa kwa faida yenu ili kulihubiri neno la Mungu kikamili, 26 siri takatifu iliyokuwa imefichwa tangu mifumo ya mambo iliyopita na tangu vizazi vilivyopita. Lakini sasa imefanywa dhahiri kwa watakatifu wake, 27 ambao kwao Mungu amependezwa kujulisha ni nini ulio utajiri wenye utukufu wa siri takatifu hii miongoni mwa mataifa. Ni Kristo katika muungano nanyi, tumaini la utukufu wake. 28 Yeye ndiye sisi tunatangaza, tukionya kwa upole kila mtu na kufundisha kila mtu katika hekima yote, ili tupate kumtoa kila mtu akiwa kamili katika muungano na Kristo. 29 Kwa madhumuni haya kwa kweli ninafanya kazi kwa bidii, nikijikakamua mwenyewe kwa kupatana na utendaji wake na unaofanya kazi ndani yangu kwa nguvu.