Waebrania
5 Kwa maana kila kuhani wa cheo cha juu aliyechukuliwa kutoka miongoni mwa wanadamu huwekwa rasmi kwa niaba ya wanadamu juu ya mambo yanayohusiana na Mungu, ili atoe zawadi na dhabihu kwa ajili ya dhambi. 2 Yeye aweza kushughulika kwa kiasi na wasio na ujuzi na wanaokosea kwa kuwa yeye pia ni mwenye kuzingirwa na udhaifu wake mwenyewe, 3 na kwa sababu ya huo ana wajibu wa kutoa matoleo ya dhambi kadiri ileile kwa ajili yake mwenyewe kama kwa ajili ya watu.
4 Pia, mtu achukua heshima hii, si kwa hiari yake mwenyewe, ila tu aitwapo na Mungu, kama vile Aroni pia alivyoitwa. 5 Ndivyo pia Kristo hakujitukuza mwenyewe kwa kuwa kuhani wa cheo cha juu, bali alitukuzwa na yeye aliyesema kumhusu: “Wewe ni mwana wangu; mimi, leo, nimekuwa baba yako.” 6 Kama vile asemavyo pia mahali pengine: “Wewe ni kuhani milele kulingana na namna ya Melkizedeki.”
7 Katika siku za mwili wake [Kristo] alitoa dua na pia maombi ya bidii kwa Yule aliyekuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka katika kifo, pamoja na vilio vyenye kupaazwa kwa nguvu na machozi, naye akasikiwa kwa kupendelewa kwa sababu ya hofu yake ya kimungu. 8 Ijapokuwa yeye alikuwa Mwana, alijifunza utii kutokana na mambo aliyoteseka; 9 naye baada ya kuwa amefanywa mkamilifu akawa ndiye mwenye daraka la wokovu udumuo milele kwa wale wote wanaomtii yeye, 10 kwa sababu ameitwa kihususa na Mungu kuwa kuhani wa cheo cha juu kulingana na namna ya Melkizedeki.
11 Kumhusu yeye tuna mengi ya kusema na yaliyo magumu kufafanuliwa, kwa kuwa mmekuwa wazito katika kusikia kwenu. 12 Kwa maana, kwa kweli, ijapokuwa mwapaswa kuwa walimu kwa kufikiria wakati, nyinyi mwahitaji tena mtu fulani awafundishe tangu mwanzo mambo ya msingi ya matamko matakatifu ya Mungu; nanyi mmekuwa kama wahitajio maziwa, si chakula kigumu. 13 Kwa maana kila mtu ashirikiye maziwa halijui sana neno la uadilifu, kwa maana yeye ni kitoto. 14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wakomavu, cha wale ambao kupitia utumizi, nguvu zao za ufahamu zimezoezwa kutofautisha lililo sahihi na lililo kosa pia.