Waebrania
4 Kwa hiyo, kwa kuwa ahadi imebaki ya kuingia ndani ya pumziko lake, acheni sisi tuhofu kwamba wakati fulani mtu fulani kati yenu asije akaonekana kuwa amepungukiwa na hiyo. 2 Kwa maana tumetangaziwa habari njema pia, kama vile wao pia walivyokuwa wametangaziwa; lakini neno lililosikiwa halikuwa na manufaa kwao, kwa sababu hawakuunganishwa kwa imani pamoja na wale waliosikia. 3 Kwa maana sisi ambao tumedhihirisha imani twaingia katika pumziko, kama vile yeye amesema: “Kwa hiyo niliapa katika hasira yangu, ‘Hakika wao hawataingia katika pumziko langu,’” ijapokuwa kazi zake zilimalizwa tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu. 4 Kwa maana katika mahali pamoja yeye amesema juu ya siku ya saba kama ifuatavyo: “Na Mungu akapumzika siku ya saba kutokana na kazi zake zote,” 5 na tena katika mahali hapa: “Hakika wao hawataingia katika pumziko langu.”
6 Kwa hiyo, kwa kuwa kwabaki kwa wengine kati yao kuingia katika hilo, na wale waliotangaziwa kwanza habari njema hawakuingia kwa sababu ya kutotii, 7 yeye atia tena alama siku fulani kwa kusema baada ya wakati mrefu sana katika zaburi ya Daudi “Leo”; kama vile imesemwa juu: “Leo ikiwa nyinyi watu mtaisikiliza sauti yake mwenyewe, msifanye mioyo yenu kuwa migumu.” 8 Kwa maana kama Yoshua angalikuwa amewaongoza kuingia katika mahali pa pumziko, Mungu hangalikuwa amesema baadaye juu ya siku nyingine. 9 Kwa hiyo kumebaki pumziko la sabato kwa watu wa Mungu. 10 Kwa maana mtu ambaye ameingia ndani ya pumziko la Mungu amepumzika pia mwenyewe kutokana na kazi zake mwenyewe, kama vile Mungu alivyofanya kutokana na zake mwenyewe.
11 Kwa hiyo acheni sisi tufanye yote kabisa tuwezayo ili kuingia ndani ya pumziko hilo, kwa kuhofu yeyote asije akaanguka katika kiolezo kilekile cha kutotii. 12 Kwa maana neno la Mungu liko hai na hukazia nguvu na ni lenye makali zaidi kuliko upanga wowote wenye makali kuwili na hudunga hata kufikia kugawanya nafsi na roho, na viungo na uloto wavyo, na ni lenye kuweza kufahamu fikira na makusudio ya moyo. 13 Na hakuna kiumbe kisichokuwa dhahiri machoni pake, bali vitu vyote viko uchi na vikiwa vimefunuliwa wazi machoni pake ambaye kwake sisi tuna kutoa hesabu.
14 Kwa hiyo, kwa kuwa tuna kuhani wa cheo cha juu aliye mkubwa ambaye amepita katika mbingu, Yesu Mwana wa Mungu, acheni tushikilie ungamo letu juu yake. 15 Kwa maana tuna kuhani wa cheo cha juu, si mmoja asiyeweza kushiriki hisia za udhaifu wetu mbalimbali, bali mmoja ambaye amejaribiwa katika mambo yote kama sisi wenyewe, lakini asiye na dhambi. 16 Kwa hiyo, acheni tukaribie kwa uhuru wa usemi kwenye kiti cha ufalme cha fadhili isiyostahiliwa, ili tuweze kupokea rehema na kupata fadhili isiyostahiliwa kwa msaada katika wakati ufaao.