Waebrania
6 Kwa sababu hiyo, kwa kuwa sasa tumeacha fundisho la msingi juu ya Kristo, acheni tuzidi kusonga mbele kwenye ukomavu, si kuweka msingi tena, yaani, wa toba juu ya kazi zilizokufa, na imani kuelekea Mungu, 2 fundisho juu ya mabatizo na kule kuwekwa kwa mikono, ufufuo wa wafu na hukumu idumuyo milele. 3 Na hili hakika tutalifanya, ikiwa kwa kweli Mungu aruhusu.
4 Kwa maana haiwezekani kwa habari ya wale ambao wametiwa nuru mara moja kwa wakati wote, na ambao wameonja zawadi ya bure ya kimbingu, na ambao wamekuwa washiriki wa roho takatifu, 5 na ambao wameonja neno bora la Mungu na nguvu za mfumo wa mambo unaokuja, 6 lakini ambao wameanguka, kuwarudisha tena kwenye toba, kwa sababu wao wamtundika mtini upya Mwana wa Mungu kwa ajili yao wenyewe na kumweka yeye wazi kwenye aibu ya hadharani. 7 Kwa kielelezo, nchi inywayo mvua ambayo huja mara nyingi juu yayo, na ambayo kisha hutokeza mimea ifaayo kwa wale ambao hiyo hulimwa kwa ajili yao pia, hupokea malipo ya baraka kutoka kwa Mungu. 8 Lakini ikitoa miiba na michongoma, hukataliwa na huwa karibu kulaaniwa; nayo mwisho wayo huwa ni kuchomwa.
9 Hata hivyo, katika kisa chenu, wapendwa, twasadikishwa juu ya mambo yaliyo bora na mambo yenye kuandamana na wokovu, ijapokuwa tunasema katika njia hii. 10 Kwa maana Mungu si asiye mwadilifu ili asahau kazi yenu na upendo mlioonyesha kwa ajili ya jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu na mwaendelea kuhudumu. 11 Lakini twatamani kila mmoja wenu aonyeshe bidii ileile ya kazi ili kuwa na uhakikisho kamili wa tumaini hadi mwisho, 12 ili nyinyi msipate kuwa goigoi, bali mwe waigaji wa wale ambao kupitia imani na subira huzirithi ahadi.
13 Kwa maana Mungu alipotoa ahadi yake kwa Abrahamu, kwa kuwa hangeweza kuapa kwa yeyote aliye mkubwa zaidi, aliapa kwa yeye mwenyewe, 14 akisema: “Kwa kweli katika kubariki hakika nitakubariki wewe, na katika kuzidisha hakika nitakuzidisha wewe.” 15 Na hivyo baada ya Abrahamu kuwa ameonyesha subira, yeye alipata ahadi hii. 16 Kwa maana watu huapa kwa aliye mkubwa zaidi, na kiapo chao ndio mwisho wa kila bishano, kwa kuwa hicho ni uhakikisho wa kisheria kwao. 17 Katika namna hii Mungu, wakati alipokusudia kuwaonyesha kwa wingi zaidi warithi wa ahadi kule kutobadilika kwa shauri lake, aliingia kwa kiapo, 18 ili, kupitia mambo mawili yasiyobadilika ambayo katika hayo haiwezekani Mungu kusema uwongo, sisi ambao tumekimbia hadi kwenye kimbilio tupate kuwa na kitia-moyo chenye nguvu tukishikilia tumaini lililowekwa mbele yetu. 19 Tumaini hili tunalo kama nanga ya nafsi, likiwa hakika na imara, nalo huingia katika pazia, 20 ambapo mtangulizi ameingia kwa ajili yetu, Yesu, ambaye amekuwa kuhani wa cheo cha juu kulingana na namna ya Melkizedeki milele.