Waebrania
7 Kwa maana Melkizedeki huyu, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu Aliye Juu Zaidi Sana, aliyekutana na Abrahamu akirudi kutoka kwenye machinjo ya wafalme akambariki yeye 2 na ambaye Abrahamu alimgawia sehemu ya kumi katika vitu vyote, yeye kwanza kabisa, kwa tafsiri, ni “Mfalme wa Uadilifu,” na kisha pia ni mfalme wa Salemu, yaani, “Mfalme wa Amani.” 3 Katika kuwa asiye na baba, asiye na mama, bila nasaba, akiwa hana mwanzo wa siku wala mwisho wa uhai, bali akiisha kufanywa kama Mwana wa Mungu, yeye adumu kuwa kuhani daima dawamu.
4 Oneni, basi, jinsi alivyokuwa mkubwa mtu huyu ambaye Abrahamu, kichwa cha familia, alimtolea sehemu ya kumi kutokana na nyara zilizo kuu. 5 Kweli, watu kutoka katika wana wa Lawi wapokeao cheo chao cha kikuhani wana amri kukusanya sehemu za kumi kutoka kwa watu kulingana na Sheria, yaani, kutoka kwa ndugu zao, hata ikiwa hawa wametoka katika viuno vya Abrahamu; 6 lakini mtu ambaye hakufuatisha nasaba yake kutoka kwao alichukua sehemu za kumi kutoka kwa Abrahamu na kumbariki yeye ambaye alikuwa na zile ahadi. 7 Basi bila bishano lolote, mdogo abarikiwa na mkubwa zaidi. 8 Na katika kisa kimoja ni watu wanaokufa ambao hupokea sehemu za kumi, bali katika kisa kingine ni mtu fulani ambaye juu yake ushahidi hutolewa kwamba yeye aishi. 9 Na, ikiwa naweza kutumia huu usemi, kupitia Abrahamu hata Lawi ambaye hupokea sehemu za kumi amelipa sehemu za kumi, 10 kwa maana alikuwa bado katika viuno vya baba yake wa zamani wakati Melkizedeki alipokutana naye.
11 Basi, kama kwa kweli ukamilifu ungekuwa ni kupitia ukuhani wa Kilawi, (kwa maana huo ukiwa sehemu kuu watu walipewa Sheria,) kungekuwa na uhitaji gani zaidi wa kuhani mwingine kuinuka kulingana na namna ya Melkizedeki na asiyesemwa kuwa alingana na namna ya Aroni? 12 Maana kwa kuwa ukuhani unabadilishwa, kwaja kuwa na uhitaji wa badiliko la sheria pia. 13 Kwa maana huyo mtu ambaye mambo haya yasemwa kwa habari yake amekuwa ni mshiriki wa kabila jingine, ambalo kutoka kwalo hakuna yeyote ambaye ametumikia rasmi kwenye madhabahu. 14 Kwa maana ni wazi kabisa kwamba Bwana wetu amechipuka kutokana na Yuda, kabila ambalo juu yalo Musa hakusema jambo lolote kuhusu makuhani.
15 Na bado ni wazi kwa wingi zaidi kwamba kwa ufanani na Melkizedeki kwainuka kuhani mwingine, 16 ambaye amekuwa wa namna hiyo, si kulingana na sheria ya amri ikitegemea mwili, bali kulingana na nguvu ya uhai usioharibika, 17 kwa maana kwa ushahidi yasemwa: “Wewe ni kuhani milele kulingana na namna ya Melkizedeki.”
18 Basi, hakika kwatokea kuwekwa kando kwa amri iliyotangulia kwa sababu ya udhaifu wayo na kutofaa kwayo. 19 Kwa maana Sheria haikufanya kitu chochote kiwe kikamilifu, bali zaidi ya hiyo kilichokamilisha ni kule kuingizwa kwa tumaini bora, ambalo kupitia kwalo tunakaribia Mungu. 20 Pia, kwa kadiri ambayo hiyo haikuwa bila kiapo kilichoapwa, 21 (kwa maana kwa kweli kuna watu ambao wamekuwa makuhani bila kiapo kilichoapwa, lakini kuna mmoja mwenye kiapo kilichoapwa na Yule aliyesema kwa habari yake: “Yehova ameapa (naye hatahisi juto lolote), ‘Wewe ni kuhani milele,’”) 22 kwa kadiri hiyo pia Yesu amekuwa yule aliyetolewa kuwa rehani ya agano bora. 23 Zaidi ya hilo, ilibidi wengi kuwa makuhani kwa mfuatano kwa sababu ya kuzuiwa na kifo wasiendelee kuwa hivyo, 24 lakini yeye kwa sababu ya kuendelea kuwa hai milele ana ukuhani wake bila kuwa na wafuataji wowote. 25 Kwa sababu hiyo aweza pia kuokoa kikamili wale wanaomkaribia Mungu kupitia yeye, kwa sababu yeye yuko hai sikuzote ili kuwaombea.
26 Kwa maana kuhani wa cheo cha juu wa namna kama hii alitufaa sisi, mwaminifu-mshikamanifu, asiye na hila, asiyetiwa unajisi, aliyetengwa na watenda-dhambi, na kuwa juu zaidi kuliko mbingu. 27 Yeye hahitaji kila siku, kama wale makuhani wa vyeo vya juu wafanyavyo, kuzitoa dhabihu, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe na kisha kwa ajili ya zile za watu: (kwa maana yeye alifanya hilo mara moja kwa wakati wote alipojitoa mwenyewe;) 28 kwa maana Sheria huweka rasmi watu kuwa makuhani wa vyeo vya juu walio na udhaifu, lakini neno la kiapo kilichoapwa lililokuja baada ya Sheria huweka rasmi Mwana, ambaye amekamilishwa milele.