‘Desturi Hii Mbovu ya Kutumia Tumbako’
LENYE kuchukiza jicho, chukizo kwa pua, lenye kudhuru ubongo, hatari kwa mapafu.’
Maelezo hayo yaliyoandikwa karibu miaka mia nne iliyopita yamalizia taarifa ya kupinga kuvuta sigareti yenye kichwa A Counterblaste to Tobacco, iliyotangazwa si na mwingine ila Mfalme James 1 wa Uingereza, aliyedhamini tafsiri ya Biblia ya 1611 inayojulikana kuwa King James Version.
Ni nini kilichochochea hilo, na ni masomo gani tunayoweza kupata?
Matumizi ya Kitiba na Mengineyo
Wakati Christopher Columbus aliporejea Ulaya baada ya ziara yake Amerika katika 1492, alirudi na mbegu fulani za mmea uliokuwa wenye thamani kwa Wahindi Waamerika kwa ajili ya faida zao za kitiba. Baadaye, Nicholas Monardes alitambulisha mmea huo kuwa tabaco (au picielt, kulingana na Wahindi). Wahispania wenye kujitwalia milki walikuwa wamejifunza juu ya thamani yao katika kutunza majeraha waliyopata, ‘wakijiponya kwa faida kubwa.’—Joyful News Out of the New Found World, tafsiri ya Kiingereza ya John Frampton, 1577.
Hata hivyo, ni matumizi mengine ya mmea huo yaliyovuta fikira za wasafiri-wachunguzi. Monardes aeleza hivi:
‘Moja la maajabu ya mmea huu, na linalostaajabisha zaidi, ni jinsi Makuhani wa Wahindi waliutumia. Miongoni mwa Wahindi hao kulipokuwako namna yoyote ya shughuli, yenye umaana mkubwa, ambayo katika hiyo majumbe walipaswa kushauriana na makuhani, Kuhani mkuu wao alitwaa majani fulani ya Tabaco na kuyatupa katika moto, na akavuta moshi wayo kinywani mwake na puani mwake kwa mrija, na alipouvuta, alianguka chini, kama mtu aliyekufa, na akabaki hivyo, ikitegemea kiwango cha moshi aliovuta. Mmea huo ulipokuwa umemaliza kazi yao, alihuika na kuamka, akawapa majibu yao, kulingana na njozi na mizungu aliyoona. Hali moja na hiyo wale Wahindi wengine, kwa kujistarehesha, huvuta moshi wa Tabaco.’
Sir Walter Raleigh alimiliki Virginia katika 1584. Koloni hiyo ilipokuwa ikikua, desturi hiyo ya Kihindi ya kuvuta tumbako ikawa maarufu kwa walowezi huko pia. Kule Uingereza, ‘Raleigh ndiye aliyeanzisha na kutumia hasa mtindo huo,’ adai mwanahistoria A. L. Rowse.
“Counterblaste”
Hata hivyo, mwenye kupinga zoea hilo lililogunduliwa hakuwa mwingine ila James, mfalme wake. Aliandika ili kutahadharisha raia zake juu ya hatari za kuvuta tumbako.
‘Ili matumizi mengi mabaya ya desturi hiyo mbovu yaonekane vizuri, inafaa kwanza ufikirie kwanza awali yayo, na pia sababu ya mwingizo wayo wa kwanza katika nchi hii.’ Ndivyo inavyoanza Counterblaste ijulikanayo sana. Baada ya kufanya pitio la kile ambacho mfalme alikiita desturi ‘inayonuka na ya kuchukiza’ ya kutumia moshi wa tumbako ili kuponya maradhi, James anatoa orodha ya hoja nne walizotumia watu ili kutetea tabia yao:
1. Kwamba bongo za kibinadamu zina baridi ya mafua na chepechepe, na kwa hiyo, vitu vyote vikavu na vyenye moto (kama moshi wa tumbako) vyapasa kuwa vizuri kwazo.
2. Kwamba moshi huo, kupitia joto, nguvu, na wema wao wa asili, wapaswa kuondoa baridi ya mafua na mivurugo ya kichwa na tumbo.
3. Kwamba watu hawangalitia desturi hiyo moyoni mno kama isingewafaidi kwa matumizi.
4. Kwamba wengi hupata faraja kutokana na ugonjwa na kwamba hakuna mtu aliyewahi kupata dhara kutokana na kuvuta tumbako.
Kulingana na maarifa ya sayansi ya ki-siku-hizi, bila shaka utakubaliana sana na hoja zenye kupinga za James. Si kwamba tu moshi wa tumbako ni wenye joto na ni mkavu, bali, pia, una ‘kitu fulani chenye sumu kilichoungana na joto lao.’ ‘Hakuna faida ya kuvuta moshi huo kuponya baridi ya mafua kama kusivyokuwako katika kula nyama na vinywaji vya kulevya vinavyokuvimbisha tumbo ili uzuie maumivu ya kuvimbiwa!’ Huenda watu wengine wakadai wamevuta sigareti kwa miaka mingi bila ya madhara yoyote, lakini je! hilo lafanya kuvuta sigareti kuwe na faida?
Kwa mkazo James alitoa sababu kwamba ‘ingawa malaya wenye umri mkubwa huenda wakasema sababu ya maisha yao marefu ni mazoea yao yasiyo ya adili, wanapuuza uhakika wa kwamba malaya wengi hufa mapema mno’ kutokana na magonjwa yanayowapata ya kuambukizwa kingono. Na vipi juu ya walevi wanaoamini wanarefusha siku zao ‘kwa ulaji ulio kama wa nguruwe’ lakini wasifikirie kamwe juu ya ni wangapi wengine hufa ‘wakiwa wamezama ndani ya kinywaji kabla hawajafikia nusu ya umri’?
Dhambi na Ubatili
Baada ya kubomoa hoja zinazopendelea uvutaji sigareti, kisha James avuta fikira kwenye ‘dhambi na ubatili’ unaofanywa na wale wanaovuta sigareti. Iliyo mashuhuri kati yazo, yeye ashikilia, ni ile dhambi ya tamaa mbaya. Kwa kutoridhika na kuvuta tumbako kidogo, wengi hutamani zaidi. Kwa kweli, uzoevu wa nikotini (tumbako-sumu) umekuwa tukio la kawaida.
Na vipi juu ya ‘ubatili’? James anawamaliza wavutaji tumbako kwa hoja hii: ‘Je! si ubatili mkubwa na uchafu kwamba mezani, mahali pa staha, unavuta moshi mchafu na harufu mbaya, ukipumua nje moshi huo, ukitia viini hewani, wakati wengine waliopo wanachukia sana zoea hilo?’
Kama kwamba akijua juu ya hatari nyingi za afya wanazokabili wavutaji sigareti, James atoa sababu hivi: ‘Hakika moshi huwa jiko kwa kufaa zaidi ya chumba cha kulia chakula, na hali mara nyingi hufanya sehemu za ndani za wanaume kuwa jiko, ukichafua na kuwaambukiza, kwa masizi ya aina ya kuvutia na yenye mafuta, kama ambavyo imepatikana katika baadhi ya watumiaji wakubwa wa Tobacco ambao walipasuliwa baada ya kifo chao.’
Katika kumalizia hoja yake, James aendelea hivi: ‘Humu hamna ubatili mkubwa tu bali pia chukizo kubwa sana kwa zawadi njema za Mungu, kwamba ladha nzuri ya pumzi ya mtu, ikiwa ni zawadi nzuri ya Mungu, yapasa kuchafuliwa kimakusudi na moshi huo unaonuka vibaya sana!’
[Picha katika ukurasa wa 14]
King James I
[Hisani]
Ashmolean Museum, Oxford
[Picha katika ukurasa wa 14]
Sir Walter Raleigh
[Hisani]
Courtesy of the Trustees of The British Museum