Ngiri-Mwenye Ucheshi
MOJAWAPO tamasha zenye kuchekesha zaidi katika misitu ya Afrika ni familia ya ngiri wanaokimbia polepole. Wao waweza kuonwa wakikimbia kwa mwendo wa haraka katika njia ya ngiri yenye adhama, kila mmoja wao akiwa na mkia mwembamba wenye kishungu cha manyoya ukiwa umeinuliwa juu wima kama waya ya kupokea habari ya redio.[1] Bila shaka, madhumuni ya ngiri si kuchekesha watazamaji. Kulingana na kitabu Maberly’s Mammals of Southern Africa, “labda tabia hiyo husaidia wanyama hao waonane katika nyasi ndefu wanapotoroka, hasa katika hali ya wachanga wenye uwezo mdogo sana wa kuona.”[2]
Jambo linalochekesha hata zaidi ni namna waingiavyo “nyumbani” mwao, hasa wakifanya hivyo kwa mwendo wa kasi. “Nyumbani” kwa ngiri laweza kuwa shimo lililopanuliwa ardhini la mhanga au la nungunungu,[3] na ngiri wana njia ya pekee ya kuingia humo. Wale wachanga, ambao bado hawajajifunza adabu nzuri za ngiri, wataingia kwenye tundu wakitanguliza kichwa kama mnyama mwingine yeyote mwenye kujistahi. Wazazi ni tofauti! Wakiwa katika mwendo wa kasi kabisa, wao hugeuka kwa we-pesi kwenye kiingilio cha tundu lao kwa usahihi kabisa—na kuingia kinyume-nyume katika usalama wa makao yao! Kitendo hicho hakifanywi ili kuchekesha watazamaji. Waona, ngiri sasa kwa kufaa aweza kukabili maadui wake ana kwa ana na kukinza mashambulizi yoyote zaidi kwa pembe zake hatari.[4]
Bila shaka, nyakati nyingine marejeo hayo ya haraka yaweza kuwa na magumu yasiyotazamiwa. Tatizo ni kwamba si ngiri pekee wanaoweza kuishi katika mapango hayo yenye mavumbi yaliyoko chini ya ardhi. Fisi, nyegere, mbweha, na nungunungu waweza kutafuta makao katika mapango hayo.[5] “Ikiwa tayari mashimo hayo yana mkazi, mara kwa mara [ngiri] waweza kupata maono yasiyopendeza,” laripoti gazeti Custos. “Katika pindi kadhaa ngiri wameonwa mishale [ya nungunungu] ikiwa imetokeza kwenye makalio yao.”[6] Kwa kweli, hilo haliwezi kuwa lenye kuchekesha maskini ngiri.
Akiwa mwenye pembe zake zenye kutisha, ngiri huonekana kama adui mkatili anayetafuta mawindo. Lakini sivyo. Ngiri amefafanuliwa kuwa “mnyama ambaye kwa kawaida si mchokozi.”[8a] Uhakika ni kwamba ngiri ni mla nyasi, na yeye ni mteuzi sana kwa kile alacho! Yeye hula nyasi fupi pekee, akila tu ncha nyororo za nyasi chipukizi; yeye huepuka magugu, nyasi ndefu, au mimea mingineyo.[10a] Isitoshe, ngiri huwa tayari kuingia hata katika mahali pasipopendeza zaidi ili kupata chakula chake. Na anaposukumiza sura yake katika sehemu zenye vichaka vyenye miiba ili kutafuta nyasi mpya zenye ladha ambazo zaweza kuwa zaota chini yazo, pembe zake hulinda uso wake.[11a]
Wakati wa saa za mchana zilizo na joto jingi zaidi, mara nyingi ngiri waweza kupatikana “nyumbani” katika shimo la mhanga lililoachwa ambalo limepanuliwa kwa pembe zao.[4a] Ikiwa hawapumziki, huenda ukawaona wakigaagaa na kunywa maji kwenye chanzo cha maji kilicho karibu.[5a] Unapokuwa wakati wa kula, wao waweza kuonwa wakikimbia polepole kwenye nyanda zenye nyasi. (Wao hawapendi kukimbia mbio isipokuwa wakilazimishwa kufanya hivyo.)[6a] Wao huenda kwa adhama, wote pamoja—kuanzia wale wazima hadi wale wachanga kabisa—wakiinua mikia yao myembamba wima.[7a]
Ngiri si washiriki wenye sura ya kupendeza katika familia ya nguruwe.[7] Lakini, jina lao la Kiingereza “warthog” lafaa sana, ambalo latokana na “chunjua” zenye kutokeza za sura zao mstatili. Hizo hasa si chunjua za kweli bali ni vimelea vya ngozi ngumu,[8] na vyaweza kutumika sana. Vyaweza kusaidia kulinda macho ya ngiri anapolima au kula.[9] Vyaweza pia kutumika wakati wale wa kiume wanapopigana, vikitumika kama ngao dhidi ya pembe zenye kukata za mpinzani.[10]
Nyuma ya uso huo wenye kuchekesha kuna mpiga vita hodari.[11] Ngiri wa kike wenye watoto huwa wenye uangalifu na wenye kulinda sana watoto wao. Washiriki wengine wakubwa wa kikundi hicho watawalinda watoto vivyo hivyo, hata hiyo ikimaanisha kujihatarisha. Kwa kielelezo, duma akijaribu kuchukua mtoto wa ngiri, ngiri mkubwa atamshambulia adui huyo. Mara nyingi mwono tu wa mnyama huyo mkubwa mwenye hasira na pembe kali utafanya duma atoroke. Wakati uo huo, watoto watakimbia huku na kule, wakijaribu kubaki kwa usalama chini ya tumbo la mama yao. Bila shaka, ikiwa tisho ni kubwa zaidi, kama vile simba au chui, basi kwa busara ngiri hutoroka, mikia yao ikiwa bado imeinuliwa juu kabisa. Hata hivyo, wale wakubwa watafuata nyuma, wakiwaruhusu wachanga wafikie usalama kwanza.[14a]
Hata hivyo, Dakt. Darryl Mason asema katika gazeti Custos, “Ngiri wakubwa waweza kuwa wakinzani wakali kwa duma, chui na fisi.”[12] Ngiri wa kike alionwa akilinda mmoja wa watoto wake dhidi ya chui mkubwa wa kiume. Yeye alimshambulia chui huyo, akimkimbiza kwa meta thelathini kabla ya chui huyo kurudi upesi na kupanda mti. Katika pindi nyingine ngiri wawili walionwa wakikinza mashambulio ya kikundi cha mbwa mwitu 16.[13]
Yasisimua kama nini kutazama vichekesho vya mcheshi huyu mwenye nguvu wa misitu ya Afrika!