Kanisa Katoliki Katika Afrika
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA ITALIA
KANISA Katoliki lina makumi ya mamilioni ya waambatani katika Afrika, na matatizo yalo huko ni makubwa. Mapema kidogo mwaka huu zaidi ya viongozi 300 wa kanisa walikutana katika Vatikani katika Roma kuzungumzia baadhi ya matatizo haya wakati wa mkutano mkuu wa mashauriano ya mwezi mmoja.
Akifungua vipindi hivyo papa alisema, kama ilivyoripotiwa katika L’Osservatore Romano: “Leo kwa mara ya kwanza kunatukia Mkutano Mkuu wa Kanisa la Kiafrika unaohusisha kontinenti nzima. . . . Afrika yote ipo leo katika St Peter’s Basilica. Askofu wa Roma aisalimu Afrika kwa shauku ya kina kirefu.”
Vita ya Kikabila
Kama vile wengi walivyo na habari, matatizo ya Kanisa Katoliki ni makubwa hususa katika nchi za Kiafrika za Burundi na Rwanda, ambazo kwa sehemu kubwa ni za Kikatoliki. Vita ya kikabila huko ilipata kusambazwa katika habari za kimataifa masika haya wakati mamia ya maelfu walipochinjwa na jirani zao. Shahidi mmoja aliyejionea kwa macho aliripoti hivi: “Tuliona wanawake walioeleka watoto wadogo migongoni wakiua. Tuliona watoto wakiua watoto.”
National Catholic Reporter lilieleza juu ya taabu kubwa ya uongozi wa Kikatoliki. Lilisema kwamba papa ‘alihisi “maumivu makubwa sana” juu ya ripoti mpya za mapigano katika lile taifa dogo sana la Afrika [la Burundi], ambalo kwa sehemu kubwa idadi yalo ni ya Kikatoliki.’
Yale machinjo ya ovyoovyo katika Rwanda yalikuwa na madhara kwa uongozi wa Kikatoliki hata zaidi. “Papa Ashutumu Mauaji ya Jamii Katika Taifa Lililo la Kikatoliki kwa Asilimia 70,” kikatangaza kichwa kikuu kimoja katika gazeti hilohilo. Makala hiyo ilionelea hivi: “Upiganaji huo katika taifa hilo la Afrika wahusisha ‘mauaji ya kijamii yaliyo halisi na ya kweli ambayo, kwa kusikitisha, hata Wakatoliki wana daraka kwayo,’ papa akasema.”
Kwa kuwa matendo ya kinyama katika Rwanda yalikuwa yakifanywa wakati ule mkutano mkuu wa Kikatoliki ulio wa kihistoria ulipokuwa ukifanywa katika Roma, kwa wazi uangalifu wa maaskofu ulikazwa juu ya hali katika Rwanda. National Catholic Reporter lilionelea hivi: “Pambano hilo la Rwanda lafunua jambo fulani la kugutusha: Imani ya Kikristo haijaimarisha mizizi vya kutosha katika Afrika ili kushinda ukabila.”
Kwa kuona hangaikio la maaskofu waliokusanyika, National Catholic Reporter liliendelea kusema: “Kichwa hiki [cha ukabila] kilishughulikiwa na Albert Kanene Obiefuna, askofu wa Awka, Nigeria, akihutubia mkutano mkuu huo.” Katika hotuba yake, Obiefuna alieleza hivi: “Mwafrika halisi huishi maisha ya kifamilia na pia maisha yake ya Kikristo kufuatana na kazi yake ya kikabila.”
Halafu, bila shaka akiifikiria Rwanda, Obiefuna aliendeleza hotuba yake kwa ule mkutano mkuu: “Njia hii ya kufikiri imeenea sana hivi kwamba kuna usemi miongoni mwa Waafrika kwamba mambo yakiumana, lile wazo la Kikristo kwamba Kanisa ni familia silo hutawala bali ni ule msemo wa kale kwamba ‘damu ni nzito kuliko maji.’ Na kwa kutaja maji hapa mtu aweza kujitanguliza kutia na yale maji ya Ubatizo ambayo kupitia hayo mtu huzaliwa kuingia katika familia ya Kanisa. Uhusiano wa damu ni wa maana zaidi hata kwa Mwafrika ambaye amekuwa Mkristo.”
Hivyo askofu huyo alikiri kwamba katika Afrika imani ya Kikatoliki ilikuwa imekosa mafanikio ya kufanyiza udugu wa Kikristo ambamo waamini hupendana kikweli kama vile Yesu Kristo alivyofundisha yawapasa kufanya. (Yohana 13:35) Badala ya hivyo, “uhusiano wa damu ni wa maana zaidi” kwa Wakatoliki Waafrika. Hii imefanya tokeo liwe ni kutanguliza kwao chuki za kikabila mbele ya mafikirio mengine yote. Kama vile papa alivyokubali, Wakatoliki katika Afrika ni lazima wabebe daraka la baadhi ya matendo ya kinyama ambayo ndiyo mabaya kupita yote yawezayo kukumbukwa nyakati za majuzi.
Kuendelea Kuwako Kwasemwa Kumo Hatarini
Maaskofu Waafrika kwenye mkutano mkuu huo walionyesha hofu juu ya kuendelea kuwako kwa Ukatoliki katika Afrika. “Ikiwa twataka Kanisa liendelee kuwako katika nchi yangu,” akasema Bonifatius Haushiku, askofu Mnamibia, “ni lazima tufikirie kwa uzito lile suala la kutamadunisha.”
Likieleza maoni kama hayo, shirika la habari Adista la Italia la Kikatoliki lilisema: “Kuongea juu ya ‘kutamadunisha’ Gospeli katika Afrika kwamaanisha kuongea juu ya tamati halisi ya Kanisa la Kikatoliki katika kontinenti hiyo, juu ya fursa zalo za kuendelea kuwako.”
Maaskofu wamaanisha nini hasa kwa kusema “kutamadunisha”?
Kanisa na “Kutamadunisha”
John M. Waliggo alieleza kwamba “utohozi ndio mtajo ambao umetumiwa kwa muda mrefu kumaanisha uhalisi huohuo.” Kwa usahili zaidi, “kutamadunisha” kwamaanisha kutwaa ndani mapokeo na mawazo ya dini za kikabila kuyaingiza katika sherehe rasmi na ibada ya Kikatoliki, kuzipa desturi za kidini, vyombo, ishara, na mahali pa kale jina jipya na maana mpya.
Kutamadunisha huruhusu Waafrika wawe Wakatoliki wenye msimamo mwema na bado washikilie mazoea, sherehe rasmi, na imani za dini zao za kikabila. Je, kwapaswa kuwe na katao lolote juu ya jambo hili? Kwa kielelezo, gazeti la Kiitalia La Repubblica liliuliza hivi: “Je, si kweli kwamba katika Ulaya Krismasi ilitiwa nanga kwenye msherehekeo wa Solis Invicti, uliotukia katika Desemba 25?”
Kwa kweli, kama vile Josef Cardinal Tomko, kadinali wa Kutaniko la Ueneza-Evanjeli kwa Vikundi vya Watu, alivyosema: “Kanisa la kimishonari lilizoea ile kazi ya kuingiza utamaduni muda mrefu kabla mtajo huo haujaanza kutumiwa.” Mwadhimisho wa Krismasi hutoa kielezi cha jambo hilo vizuri, kama vile La Repubblica lilivyoandika. Hapo awali huo ulikuwa mwadhimisho wa kipagani. “Tarehe ya Desemba 25 hailingani na kuzaliwa kwa Kristo,” yakubali New Catholic Encyclopedia, “bali na sikukuu ya Natalis Solis Invicti, ule msherehekeo wa jua wa Kiroma wakati wa kituo cha mbali zaidi cha jua.”
Krismasi ni mojapo tu ya desturi nyingi za kanisa zilizotiwa nanga katika upagani. Ndivyo na imani kama Utatu, kutokufa kwa nafsi, na mateso ya milele ya nafsi za kibinadamu baada ya kifo. John Henry Cardinal Newman wa karne ya 19 aliandika kwamba “watawala wa Kanisa kuanzia nyakati za mapema walikuwa tayari, ikiwa fursa ingetokea, kukubali au kuiga, au kuidhinisha kawaida za kidini na desturi zilizokuwako za halaiki ya watu, iwapo fursa ingetokea.” Akiorodhesha mazoea na sikukuu nyingi za kanisa, alisema zilikuwa “zote za asili ya kipagani, na zilitakaswa kwa kukubaliwa ndani ya Kanisa.”
Wakati Wakatoliki waingiapo maeneo yasiyo ya Kikristo, kama sehemu za Afrika, mara nyingi wao hukuta kwamba tayari watu wana mazoea na imani za kidini kama zile za kanisa. Hii ni kwa sababu katika karne zilizotangulia, kanisa lilikubali kufuata mazoea na mafundisho kutokana na vikundi vya watu wasio Wakristo na kuziingiza katika Ukatoliki. Mazoea na mafundisho kama hayo, alidai Cardinal Newman, ‘yalitakaswa kwa kukubaliwa ndani ya Kanisa.’
Hivyo, wakati Papa John Paul 2 alipozuru vikundi vya watu wasio Wakristo katika Afrika mwaka uliopita, alinukuliwa katika L’Osservatore Romano kuwa akisema hivi: “Katika Cotonou [Benin, Afrika] niliwakuta waambatani wa dini ya ulozi, na kutokana na walivyosema ilionekana wazi kwamba katika akili yao tayari wana kadiri fulani ya desturi za kidini, itikadi na mielekeo ifananayo kidogo na ile ambayo Kanisa lataka kuwatolea. Wanangojea tu wakati ufike mtu fulani aje kuwavuta mkono wauvuke mpaka ili kupitia Ubatizo waishi maisha yale waliyokuwa tayari wakiyaishi na kuyazoea kwa njia fulani kabla ya Ubatizo.”
Wewe Wapaswa Kufanya Nini?
Kushindwa kwa kanisa kufundisha vikundi vya watu wa Afrika Ukristo wa kweli, usioghoshiwa kumekuwa na matokeo yenye msiba. Ukabila umeendelea, hali moja na utaifa kwingineko kote, ukitokeza kuchinjana kwa Wakatoliki. Lo, ni kumvunjia Kristo heshima kama nini! Biblia husema kwamba kuuana huko hutambulisha watu kuwa “watoto wa Ibilisi,” na Yesu asema hivi juu yao: “Ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”—1 Yohana 3:10-12; Mathayo 7:23.
Hivyo basi, ni lazima Wakatoliki wenye mioyo ya kufuata haki wafanye nini? Biblia huhimiza Wakristo wajikinge dhidi ya kuridhiana na mazoea au imani zozote ambazo zingefanya ibada yao isiwe safi machoni pa Mungu. “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini,” Biblia yasema. Ili kufurahia upendeleo wa Mungu, mwahitaji ‘mtengwe nao msiguse kitu kilicho kichafu machoni pa Mungu.’—2 Wakorintho 6:14-17.
[Blabu katika ukurasa wa 20]
Ile vita katika Rwanda ni mauaji ya kweli ya kijamii ambayo hata Wakatoliki wana daraka kwayo,’ akasema papa
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]
Picha: Jerden Bouman/Sipa Press